Friday 4 March 2016

WAZANZIBARI NA MUUNGANO WA MKUBWA NA MDOGO

Tafauti kubwa kati ya wananchi washirika wa Muungano bara na visiwani ni ideology. Wazanzibari wengi ni waumini wa liberalism wakati ujamaa una mizizi mikubwa upande wa pili wa muungano. Ndio maana hata ASP haikuwa ikiufahamu au hata ukiuamini ujamaa wa Mwalimu au hata wa babu. Kumbuka Azimio la Arusha lilikuwa mwisho Chumbe. Mmoja wa marafiki zangu wa kifaransa aliekaa miaka mingi Zanzibar hufika hadi akasema Zanzibar ni ya waliberali zaidi kuliko kwao anapotoka.
Na hata Mzee Mwinyi na mabadiliko yake ya kiuchumi yalijengwa zaidi na "influence" ya siasa za liberalism za Zanzibar na azimio jengine la Zanzibar lililobeba uhuru wa kiuchumi wa kiliberali lakini utawala wa mkono wa chuma wa authoritarian socialism. Matokeo yake ni hii huu utawala usio na dira katika suala la itikadi. Ukitazama kwa upande mkubwa hata kukataliwa kwa watawala visiwani au kupata ushindani mkubwa sana kunachangiwa zaidi na itikadi.
Kwa upande wa wazanzibari wengi ujamaa kwao ni kutoufahamu zaidi ya uimla na maonevu yaliokuja nayo miaka ya 70. Na hulinganisha uhuru wa kiuchumi kabla ya uhuru hata kama kulikuwa na mgawanyiko wa kimapato kutokana na sera za ubepari wa muingereza pamoja na uimla wa kiuchumi katika miaka ya sabini na kuutazama ujamaa wa Mwalimu hasa kama tatizo. Hata Babu hakuweza kuwa maarufu bila ya kujenga mahaba na ima ASP au hizbu kwa sababu sera za kijamaa hazikuwa na mvuto kwa Zanzibar ya asilimia 99 waislam.
Bado naamini laiti Umma party ingeliungana na Hizbu baada ya uhuru na kuleta serikali ya kitaifa ya msingi wa maridhiano na maslahi kwanza ya nchi leo hii tungekuwa na muungano lakini si huu usio na mipaka ya haki, heshima na usawa. Wala sifikirii kama mapinduzi hasa msingi wa wanamgambo wa Sakura au Kipumbwi ungelifanikiwa. Mfano mzuri ni Maldives ambayo ufalme uliondolewa si kwa mapinduzi bali mabadiliko katika bunge lao baada ya uhuru.
Nakumbuka wakati wa waliberali wa kiingereza walipoungana na mabepari wa Conservative kuitoa Labour katika utawala. Halikuwa jambo rahisi maana tafauti ya kisera ni kubwa mno baina yao, lakini walifanya kwa maslahi ya nchi na "influence" ya maliberali iliweza kuonekana katika masuala ya sheria, haki na hata masuala ya ugawaji wa fedha za serikali kwa wasiojiweza. Maliberali walijitoa muhanga wakiamini wananchi watawafahamu lakini walipigwa vibaya katika uchaguzi kwa wapiga kura wa kibepari na wale wa ujamaa wa kati kwa kuwaona ima ni wazushi wa kuzuia maendeleo ya kibepari au wasaliti wa "civil liberities" walizosimama nazo. Kwa vyovyote miaka mitano ya serikali ya pamoja ilikuwa na afuweni kubwa kuliko hii ya sasa ya mabepari wanaoegemea kulia zaidi kila kukicha.
Na kwetu hivyo hivyo, mgawanyiko na ushindani wa pande mbili ni mkubwa mno kukataa uhalisia wa serikali ya pamoja huku mshindi akiongoza sera. Na ndio maana nashindwa kufahamu hasa msimamo wa walioshindwa katika uchaguzi uliosifika kwa uhuru kuurejea tena na kuapa kwamba sasa wakishindwa wataachia kinyume na kabla ya tarehe 25 Oktoba walipokataa kata kata kukiri wataposhindwa kuacha mshindi halali aongoze. Maslahi ya nchi yanapochezewa na vichochezi vya mabom ya kutegana na kulaumiana yataturudisha nyuma sote hasa kwa utalii kuwa ndio msingi mkubwa wa maendeleo yetu.
BY FARELL 

No comments: