Thursday, 28 March 2019

TANZANIA YANG'ARA BENKI YA DUNIA



Edward  Edmund Kinabo (akiwa Makao Makuu ya Benki ya Dunia, akiwasilisha  mada Washington DC, Marekani.

TANZANIA YANG'ARA BENKI YA DUNIA

Na. Dira Yetu Blog, Washington DC Marekani

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazopiga hatua kubwa katika kutatua tatizo la makazi holela duniani.

Watu bilioni 1 kati ya bilioni 7.4 duniani wanaishi katika makazi holela hususan katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania

Makazi hayo yaliyoendelezwa bila wahusika kuwa na umiliki halali wa kisheria, mengi yana hali duni ya miundombinu na upungufu mkubwa wa huduma za kijamii. 

Hata hivyo, hatua ya Serikali ya Tanzania kushirikisha sekta binafsi katika kupangilia miji, kupima viwanja na kumilikisha ardhi kwa hatimiliki imeleta tija na kuongeza kasi kubwa katika kurasimisha na kuboresha makazi holela nchini.

Hayo yameelezwa na Mratibu Mwandamizi wa Miradi wa Kampuni ya Mipango Miji ya HUSEA, Bwana Edward Kinabo, katika Mkutano Mkuu wa Benki ya Dunia unaohusu Ardhi na Umaskini, unaoendelea jijini Washington nchini Marekani.

Akiwasilisha mada jana, kwa niaba ya Kampuni ya HUSEA iliyohusu

"Uzoefu wa Ubia baina ya Sekta Binafsi na Jamii katika Kurasimisha Makazi kwa kutumia fedha zinazochangwa na Wananchi wenyewe"

Kinabo alisema kwa miaka mingi ongezeko kubwa la idadi ya watu na ukuaji wa kasi wa miji dhidi ya uhaba wa bajeti za serikali, nguvu kazi na vitendea kazi, vilifanya kuwe na kasi ndogo ya upangaji miji na hivyo kusababisha kukithiri kwa makazi holela. 

Alisema asilimia 70 hadi 80 ya wakazi wa mijini nchini Tanzania wanaishi kwenye makazi holela ambayo hayajapangwa wala kupimwa licha ya baadhi yao kuwa ni watu wenye kipato kizuri na nyumba nzuri.

Hata hivyo, alifafanua kuwa kupitia mazoezi shirikishi ya urasimishaji makazi yanayotekelezwa na kampuni binafsi kwa mfumo wa wananchi kuchangia gharama nafuu kwa pamoja, sasa maelfu ya Watanzania wamepata fursa kubwa ya kumiliki maeneo yao kisheria.

"Hatua ya Wizara ya Ardhi kushirikisha kampuni binafsi imeleta tija kubwa. Nampongeza Mhe Waziri wetu wa Ardhi kwa uamuzi sahihi wa kutumia Kampuni binafsi ...na kwa kweli Waziri Lukuvi ndiye amekuwa mhamasishaji mkuu wa urasimishaji wa makazi", alisema Kinabo

Mkutano huo wa Benki ya Dunia unashirikisha wadau wa maendeleo  kutoka nchi mbalimbali duniani, wakiwemo viongozi na maafisa wa serikali, Asasi za Kiraia na wawakilishi kutoka sekta binafsi wakiwemo watoa mada walioalikwa kutoa uzoefu juu ya namna bora ya kushughulikia masuala yahusuyo ardhi na umasikini.

Akifafanua zaidi kuhusu kasi ya urasimishaji makazi, Kinabo alisema Tanzania hivi sasa ina kampuni nyingi za mipango miji na upimaji na nyingi zimeenea kwenye majiji na miji mbalimbali zikifanya urasimishaji wa makazi. 

Alisema kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Ardhi hadi kufikia mwezi Mei 2017 Tanzania ilikuwa na Kampuni za mipango miji 40 na za upimaji 67, idadi ambayo kwasasa imeongezeka zaidi.

"Kampuni ya HUSEA pekee imeweza kuandaa ramani za mipango miji na kuratibu upimaji wa zaidi ya viwanja 30,000 katika miradi inayoendelea katika mitaa ya Manispaa za Ubungo, Kinondoni na Kigamboni jijini Dar es Salaam. Kampuni hii pia  ipo katika hatua za awali za kufanya kazi kubwa zaidi katika Jiji la Mbeya, Arusha na mkoa wa Songwe.

"Kwa kuzingatia wingi wa kampuni na kazi kubwa ya urasimishaji inayoendelea nchini ni dhahiri kuwa kasi yetu kama nchi kwasasa ni kubwa pengine kuliko ya miongo minne iliyopita", alisema Kinabo

"Kwa kasi hii, tunaamini ndani ya miaka michache ijayo tathmini zitaonyesha kupungua kwa makazi holela Tanzania", aliongeza Kinabo

Alisema urasimishaji makazi ni jitihada muhimu katika kufufua mitaji mfu ya ardhi, kuongeza usalama na thamani za viwanja na makazi ya wananchi na hivyo kuwawezesha kuvutia mitaji, kupunguza umaskini na kuchochea maendeleo yao.

Alisema jitihada hizo pia zitaongeza wigo wa ardhi yenye umiliki rasmi na makusanyo ya kodi ya ardhi kwaajili ya kuharakisha utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo. 

"Hapa Marekani kwa mfano kodi inayotokana na umiliki wa ardhi na majengo ndiyo chanzo kikuu cha mapato yanayotumika kutekeleza miradi ya maendeleo. Kwa hiyo, urasimishaji makazi Tanzania ni kipaumbele muhimu sio tu katika kuboresha maisha ya mtu mmoja mmoja bali pia kuipa nchi wigo mpana wa mapato ambayo yakitumika vizuri yanaweza kupunguza umaskini kwa kiasi kikubwa sana", alisema Kinabo 

"Tunaifanya kazi hii bila kutegemea fedha za wafadhili wa nje wala bajeti ya serikali. Tunaifanya kazi hii kwa nguvu ya wananchi wenyewe… kwa kuwaelimisha, kuwashirikisha na kuwahamasisha kuchangia gharama nafuu za kurasimisha maeneo yao", aliongeza Kinabo ambaye kitaaluma ni mchambuzi wa sera na mtaalam wa miradi ya kijamii. 

Alisema mfumo wa uchangiaji gharama za kupanga na kupima viwanja vya wananchi wanaofikiwa katika mitaa yao kwa pamoja umesaidia sana kumpunguzia mwananchi mzigo wa gharama kwa zaidi ya asilimia 90, kitu ambacho wananchi wengi wasingeweza kumudu kama kila mmoja angepima ardhi yake peke yake.

Awali, akichambua takwimu za hali halisi ya nchi kuhusu ongezeko la watu na makazi holela, Kinabo alisema Ripoti ya Hali ya Maendeleo ya Binadamu Tanzania iliyotolewa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) mwaka 2017, inaonyesha idadi ya watu nchini inaongezeka kwa zaidi ya asilimia 2.7, sawa na ongezeko la watu milioni 1.2 kwa mwaka. 

Alisema kwa kasi hiyo Tanzania yenye takribani watu Milioni 55 hivi sasa inakadiriwa kuwa itafikisha watu milioni 67 ifikapo mwaka 2025 na watu milioni 89.2 ifikapo mwaka 2035.

Aliueleza mkutano huo kuwa Tanzania ina kasi kubwa ya ongezeko la watu mijini ambayo ni asilimia 5.2 kwa mwaka, kiwango ambacho ni zaidi ya mara mbili ya wastani wa dunia ambao ni asilimia 2.1 na zaidi ya wastani wa Afrika ambao ni asilimia 3.5.

Aidha, akinukuu Ripoti ya Shirika la Makazi Duniani (UN Habita) ya mwaka 2016 kuhusu Ukuaji wa Majiji, alisema wakati theluthi mbili ya watu wote duniani watakuwa wanaishi mijini ifikapo mwaka 2050, huku asilimia 90 wakitarajiwa kutokea ndani ya Bara la Afrika na Asia, Tanzania itakuwa ni nchi ya tisa kwa kuwa na watu wengi waishio mijini, ikitanguliwa na India, China, Indonesia, Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.  

"Kwa kadri idadi ya watu inavyozidi kuongezeka mijini kuliko vijijini ndivyo   umaskini wa dunia unavyozidi kuhamia mijini kutoka vijijini. Ile dhana iliyozoeleka kuwa umaskini umekithiri vijijini tu sasa imepitwa na wakati", alisema Kinabo

Mbali na urasimishaji wa makazi holela, Mtaalam huyo amezishauri nchi zinazoendelea kufanya mageuzi makubwa ya mwelekeo wa kisera ili kutatua changamoto mpya ya umaskini unaozidi kukithiri zaidi mijini hivi sasa kuliko vijijini.

"Ukuaji wa miji si tatizo, ni fursa. Ni rahisi na nafuu zaidi kubuni na kutekeleza sera za kuboresha maisha ya wananchi wengi walio pamoja. Kwa wimbi hili la ongezeko la watu mijini, nchi zetu zinazoendelea zinahitaji kubadili sana mwelekeo wa kisera....upangaji, uendelezaji na usimamizi wa miji katika mfumo jumuishi ni kipaumbele muhimu sana hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote ule katika historia ya nchi za dunia ya tatu", alisema Kinabo.

Kinabo alisisitiza kuwa mageuzi ya kisera yenye kuzingatia mahitaji makubwa ya sasa ya miji yana nafasi kubwa ya kuharakisha jitihada za kutimiza lengo la kutokomeza umaskini wa namna zote duniani ifikapo mwaka 2030, kama ilivyoazimiwa katika Shabaha za Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ikiwemo Tanzania. 

Mkutano huo  umehudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Kampuni ya Mipangomiiji ya HUSEA na Makamu wa Rais wa Chama cha Wataalam wa Mipango Miji nchini, Bwana Renny Chiwa, ambaye pia alipata fursa ya kutoa mawazo kuhusu nafasi ya taaluma ya mipango miji katika kutatua changamoto za miji inayokua kwa kasi duniani.

Mkutano huo ulioanza Tarehe 25 unatarajiwa kumalizika Tarehe 29 Machi mwaka 2019.



Edward  Edmund Kinabo (kushoto) Mratibu wa Miradi wa Kampuni ya Mipangomiji ya Human Settlements Action (HUSEA) na Mwenyekiti wa Kampuni hiyo, Renny Chiwa, wakiwa Makao Makuu ya Benki ya Dunia, Washington DC, Marekani.













No comments: