Tuesday, 31 May 2016

LHRC wamshughulikia Naibu Spika

Hellen Bisimba , Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
KITENDO cha Bunge kusimamisha wabunge saba wa upinzani kuhudhuria vikao vyake kimepingwa vikali na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), anaandika Aisha Amran.
Pia LHRC wamelaani hatua ya Dk. Tulia Ackson, Naibu Spika kukataa hoja ya dharura ya kuahirisha Bunge kujadili mustakabali wa wanafunzi 7,802 wa Chuo Kikuu cha Dododma (UDOM) waliosimamishwa masomo yao.
Helen Bisimba, Mkurungenzi Mtendaji wa LHRC amesema, kitendo cha kuwasimamisha baadhi ya wabunge ambao walikuwa wanatimiza wajibu wao kwa kutetea wananchi hasa wanafunzi hao kutolewa nje ya ukimbi wa Bunge kwa ubabe na katika hali ya kudhalilisha kama waalifu, hakikubaliki.
“Jana tumeshuhudia Bunge likivunjwa na baadhi ya wabunge kutolewa nje ya ukumbi wa Bunge kwa ubabe, nguvu na katika hali ya udhalilishaji wakati walikuwa wakitimiza wajibu wao wa kuwatetea wananchi na wanafunzi ili kupata suluhu ya matatizo yanayowakabili,” amesema Bisimba.
Amesema kuwa, inapofikia wakati ambapo Dk. Tulia anashindwa majukumu yake ya kusimamia, kuishauri na kuiwajibisha serikali na badala yake kusimamia upande wa serikali kuilinda na kuitetea, kunaleta mashaka na kukiuka ibara ya 8 ya Katiba.
“Haingii akilini hata kidogo kuona Naibu Spika akikataa hoja ya dharura ili kuahirisha Bunge kwa muda kujadili mustakabali wa wanafunzi na kutamka waziwazi haoni dharura katika hilo,” amesema Bisimba na kuongeza;
“Kwa hiyo, kwa maana nyingine hajali kuona wale vijana wakishinda njaa, wakikosa pa kulala , wakidhalilishwa kijinsia na hata kuuwawa kwake hilo sio dharura na halihitaji kutengewa muda na kujadiliwa maana ni wazi kosa la serikali kupitia wizara ya elimu.”
Amesema kuwa, ni ukiukwaji na ukandamizwaji wa haki za binadamu na wazi inaonesha kwamba Naibu Spika hajali maslahi ya wananchi ambao ni taifa la kesho na ndio walioiweka serikali hiyo ya awamu ya tano madarakani na kusababisha yeye kuwa kwenye kiti hicho.
Bisimba amesema kuwa, Naibu Spika na wenyeviti wameshindwa kuendana na kasi ya Bunge la 11 na kuwa, ndani ya miezi sita kumekuwa na ubabe katika kuwanyima wabunge kutimiza wajibu wao kama Katiba inavyowataka.
“Mbunge yeyote ambaye ataonekana anamuelekeo wa kuibaini serikali basi watahakikisha wanambana kwa njia yoyote ile ili kumzimisha, kiasi cha kuingiza mbwa na askari kuwakabili,” amesema.
Kwa niaba ya LHRC amesema, wanaishauri wabunge waliosimamishwa bunge kuwarejesha ili kuwawakilisha wananchi kama wajibu wao unavyowaelekeza.

No comments: