Friday 13 May 2016

Tafakuri ya Muungano wetu.

Gavana wa sasa (Bank of England) ambae ni raia wa Canada mwenye asili ya jamhuri ya kiairish, leo ametoa nae hoja nne kuu za kuwaeleza wananchi athari ya kujitoa katika muungano wa Ulaya. La mwanzo alisema na kupunguza kwa nguvu za kiuchumi, la pili kuzidi kwa watu wasio na ajira, tatu ni kuongezeka kwa Inflation na nne ni kuanguka kwa thamani ya sarafu yao (pound).

Waliompinga wamekuja nao na hoja muhimu zenye mvuto. Kwanza wanasema kwamba Himaya hii ya mflame wa kiingereza ni miongoni mwa mataifa matano yenye uchumi mkubwa duniani. Kusema kwamba kujitoa katika muungano wao kutapunguza kasi ya ukuwaji wa uchumi ni utabiri usio na mashiko. Wanauliza iweje Norway na Switzerland ambao si miongoni mwa mchi wanachama wa EU zikawa na uchumi imara hata iwe ngumu kwa Uingereza?

Mwengine katika kambi ya kujitoa anasema kwamba tafiti zinaonyesha kwamba Uingereza ni nchi pekee yenye uchumi usioweza kutikisa kirahisi kuliko nchi nyengine yoyote duniani. Na ndio maana athari ya anguko la uchumi duniani wa mwaka 2009, halikuiathiri  nchi yao kama ilivyoathirika nchi nyengine, zikiwamo nchi zenye uchumi mkubwa.

Kuhusu inflation na ukosefu wa ajira, wanasema mifano ipo mingi ya nchi nje ya EU zenye kujiendesha vizuri zaidi kuliko Uingereza iliomo katika EU. Wanamuuliza Gordon Brown, aliekuwa Waziri Mkuu aliepita, pamoja na kushika nafasi ya Waziri wa Fedha kipindi cha Blair, kwa nini kama kweli EU ni imara hakukubali kuiondosha sarafu ya Pound na kuiweka Euro hata leo awe mtetezi anaeuona Uchumi wa Muingereza kuwa tegemezi kwa EU?

Spain na Portugal ni miongoni mwa nchi zenye wananchi wasio na ajira katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya. Wanauliza kama kweli kuwemo katika umoja huu kunazuia nchi ukosefu wa ajira mbona Spain, Portugal, Ugiriki na hata Ufaransa zinahangaika? Kwa nini nchi hizi ni miongoni mwa nchi zenye inflation kubwa? Wanajiuliza vile vile waingereza kwamba kuanguka kwa thamani ya Sarafu si jambo baya kwa wananchi pamoja na sekta ya "export".

Wanatoa mfano Japan, kwamba Toyota imeweza kuweka rekodi kubwa ya faida kwa sababu ya kuanguka kwa thamani ya sarafu yao ya Yen. China inafaidika zaidi kwa kuangusha sarafu yao kiasi kwamba Marekani imeilalamikia mara kwa mara kwa vile inaathiri uchumi wa Marekani kutokana na bidhaa za China kuwa rahisi kuliko za Marekani na hivyo kuuwa soko la ndani la nchi yao.

Mgogoro huu wa Himaya hii ya malkia wa Kiingereza kutishia kujitoa unatokana na kitu kimoja kikubwa, suala la Uhamiaji. Kwa vile kisiwa kidogo lakini chenye nguvu ya Uchumi (pamoja na ongezeko la nchi wanachama kutoka Umoja wa Ulaya kama Poland, Romania na nchi za Mashariki ya Ulaya) kimefanywa kuwa kimbilio la wengi kutoka nchi wanachama kiasi ya kwamba wanakosa uhuru wa mamlaka ya kusimamia uhamiaji kulingana na mahitaji ya kiuchumi au usalama wa nchi.

Jengine kubwa ni Umoja wa Ulaya kuwa na mamlaka makubwa zaidi katika masuala madogo madogo lakini ya msingi yanayoonekana kupora mamlaka za kidemokrasia kama vile Mabunge ya nchi husika na mahakama zao. Kwa mfano masuala ya uvuvi ambayo Umoja wa Ulaya, kwa kulinda mazingira imeweka kiasi maalum cha wavuvi kuvuwa, na kikizidi inabidi wamwage baharini kukimbia adhabu. Au karibuni tu kulikuwa na agizo la mahakama ya Ulaya iliotaka wafungwa wawe na haki ya kupiga kura kitu ambacho hakikubaliwi na mahakama za Uingereza pamoja na Bunge lao.

Nini tunasoma kutoka katika mgogoro huu? Kwamba kuungana ni kwa maslahi ya nchi washirika na si suala la udogo au ukubwa wa nchi. Uingereza ni ndogo kuliko Ujarumani, au Ufaransa, lakini inaheshimika sawa na nchi kubwa au nchi ndogo kabisa kama Leichtenstein (160km^2), Malta (316km^2), au hata Monaco (1.95km^2) inayoingia kwa mgongo wa Mfaransa lakini yenye ushiriki kamili kwa mambo maalum yanayowahusu.

Vatican kwa mfano, kijinchi kidogo kwa tafsiri ya mamlaka kamili (sovereign entity), inayojengwa kwa dayosis kiuongozi (Ecclesiastical Jurisdiction) na kiti cha Papa mtakatifu (Episcopal See of the Pope). Nchi hii haijakubaliwa kujiunga na Umoja wa Ulaya kwa sababu ya sharti moja kwamba ili uwe mwanachama lazima uwe na mfumo wa demokrasia wa soko huria wakati Vatican ni yenye kufuata mfumo wa kiimani (theocracy). Heshima yake kwa vile iko katika mipaka ya Umoja wa Ulaya inalindwa na kupewa haki nyingi kama nchi mwanachama ikiwamo matumizi ya sarafu ya Euro na mipaka huru, uwepo wa kiti cha muwakilishi wao na hata katika masuala ya misamaha ya kodi. Hivyo udogo wetu katika muungano huu isizuwie hoja ya uwepo wa heshima, usawa na haki baina yetu.

Vile katika kura hii ya maoni, ni hoja zilizojengewa ushahidi na kuachiwa wananchi uhuru wa maamuzi. Hakuna na vitisho vya kuingia msituni, au matusi kwa wenye kuupinga, kebehi kwa wenye maoni tafauti au vitisho kwa wabunge wa vyama vyao wenye maoni tafauti na misimamo ya vyama. Na ndio maana katika Baraza la Mawaziri suala hili limeachiwa uhuru kiasi kwamba mawaziri wametafautiana hata na bosi wao katika kambi mbili ya kubaki au kujitoa.

Mwisho nilikuwa nafikiri jee haya manne yaliotajwa na Gavana wa Benki Kuu ya Uingereza Mark Carney, yanaweza pia kutumika kwa upande wetu kama hoja ya kuudadisi muungano na faida zake kiuchumi kwa upande wetu? Kwa mfano Jee Zanzibar inaweza nayo kuambiwa kujitoa katika muungano kutaathiri ukuaji wa Uchumi wake? Au kuongezeka kwa wasio na ajira? Au kuongezeka kwa inflation? Au kwamba sarafu ya Tanzania itatetereka?

Kwa haraka haraka yote hayo hayako katika mamlaka ya Muungano kasoro Sarafu. Ila yote hayo ni sehemu inayopelekea kuwapo kwa kero zinazohatarisha uwepo wa Muungano. Japo kuwa kimamlaka ya uchumi kuna uhuru, lakini kisera zinategemea zaidi upande wa pili katika "fiscal policies" zinazosimamisha uchumi na ukuwaji wake, ajira, inflation na sarafu.

Kuweka mamlaka ya kiuchumi kujiongoza lakini ukakosa nyenzo za kisera ni sawa kuwa na daktari aliekosa stethoscope akabaki kusikiliza kifua kwa sikio. Kinachofurahisha ni kwamba kwa Waingereza hayo yanatajwa kuwa yataathirika pindipo wakijitoa katika Muungano wa Ulaya lakini kwa upande wa Zanzibar ni miongoni mwa kero (au tuite majipu?) zinazotamkwa kuiathiri Zanzibar ikiwa katika muungano. Ni kweli huu wa kwetu ni wa aina ya kipekee.

No comments: