Monday, 30 May 2016

WABUNGE SABA WAZUIWA KUHUDHURIA VIKAO VYA BUNGE


Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge limepitisha azimio la kuwasimamisha kuhudhuria vikao vya Bunge baadhi ya wabunge wa Kambi ya Upinzani waliohusika katika kufanya vitendo vya vurugu ndani ya ukumbi na kudharau Mamlaka ya Spika Januari, 27, 2016.
Wabunge waliosimamishwa kuhudhuria vikao hivyo ni Mhe. Kabwe Zubeir Ruyangwa Kabwe, Mhe. John Heche, Mhe. Halima Mdee, Mhe. Tundu Lissu, Mhe. Godbless Lema, Mhe. Pauline Gekul na Mhe. Esther Bulaya. Azimio la adhabu kwa wabunge hao limetolewa na Bunge chini ya Kifungu cha 30A (1) cha sheria ya Haki Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na kanuni ya 74 (4) na (6).
Akisoma adhabu hizo Mwenyekiti wa kamati hiyo yenye wajumbe 15 Mhe.George Huruma Mkuchika amesema kuwa uchunguzi uliofanywa na Kamati hiyo kwa kuwaita na kuwahoji wahusika ulibaini kuwa wabunge hao walitenda kosa kwa kukiuka kanuni zinazoliongoza bunge hilo.


Imebainishwa kuwa Mhe.Zitto Kabwe alivunja masharti ya Kifungu cha 24(c), (d) na (e) cha Sheria ya Haki na Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na Kanuni ya 60(2) na (12) , 74(1) na (b) kwa kusimama na kuzungumza bila kufuata utaratibu na kudharau mamlaka ya Spika.

Kamati hiyo ilibaini kuwa Mhe.Godbless Lema, Mbunge wa Arusha alivunja Masharti ya kifungu cha 24 (c),(d) na (e) cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 pamoja na Kanuni ya 74(1) (a) na (b) ya kanun hiyo Kudharau Mamlaka ya Spika.

Kwa upande wa Mhe.John Heche alivunja kanuni ya 72 (1) na 68(10) ya kanuni za Bunge kwa kuendelea kusimama na kuomba mwongozo kwa jambo ambalo limekwishatolewa mwongozo na kuongeza kuwa vitendo hivyo vilivuruga shughuli za Bunge.

Kwa mujibu wa maelezo ya kamati hiyo Mhe.Halima Mdee, Mhe.Tundu Lissu,Mhe Pauline Gekul na Mhe.Ester Bulaya walivunja masharti ya kifungu cha 24 (c), (d) na (e) cha sheria ya Haki,Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na Kanuni ya 72 (1)68 (10), 60(2) na 12 na 74(1) (a) na (b) kwa kusimama na kuendelea kuomba mwongozo kwa jambo ambalo limekwishatolewa uamuzi, kuzungumza bila kufuata utaratibu na kudharau Mamlaka ya Spika.

Kufuatia uchunguzi huo Bunge kupitia kamati hiyo limeazimia kuwa Mhe. Ester Bulaya na Mhe.Tundu Lisu wasihudhurie vikao vyote vya mkutano wa tatu wa Bunge la Kumi na Moja vilivyobaki kuanzia tarehe 30 Mei , 2016 pamoja na vikao vyote vya Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi na Moja kwa kuwa walipatikana na makosa ya ukiukwaji wa Kanuni na kuonyesha dharau kubwa kwa mamlaka ya Spika.

Aidha, Bunge limeazimia kuwa Mhe. Pauline Gekul, Mhe.Godbless Lema, Mhe.Zitto Kabwe na Mhe Halima Mdee wasihudhurie vikao vyote vya mkutano wa tatu wa Bunge kuanzia tarehe 30 Mei 2016.

Adhabu hizo Bunge limeazimia Mhe.John Heche asihudhurie vikao kumi mfululizo vya Mkutano wa Tatu wa Bunge hilo kuanzia Mei, 30, 2016 kwa kuwa alipatikana na kosa moja na pia kwa kuwa alitoa ushirikiano kwa kamati kwa kufika na kujibu maswali yote kama alivyoulizwa pamoja na kuheshimu vikao vya kamati na Mwenyekiti aliyeongoza vikao hivyo.

Pamoja na adhabu hizo Kamati hiyo imetoa maoni na mapendekezo kuwa Bunge liandae mafunzo ya kutosha kwa wabunge wote kuhusu matumizi ya uzingatiaji sahihi wa kanuni sahihi wa kanuni za Kudumu za Bunge hasa kanuni za majadiliano ndani ya Bungeni.

Aidha, Kamati hiyo imesema kuwa ipo haja ya kutungwa kwa kanuni za maadili kwa wabunge wote kama kifungu cha 12 A Cha Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kinavyoelekeza ili kuweza kudhibiti nidhamu kwa wabunge kwa kuhakikisha heshima na hadhi ya Bunge inadumishwa.

Kwa upande wao baadhi ya wabunge wakichangia kwa nyakati tofauti kuhusu suala hilo wamesema kuwa ipo haja ya Bunge kurudisha heshima yake kwa wabunge wote kuheshimiana na kutoa michango yenye staha kwa kuzingatia nafasi walizonazo katika jamii.

Wamesema kuwa michango wanayoitoa ndani ya Bunge hilo lazima ijikite katika masuala yanayowahusu wananchi wanaowawakilisha badala ya mambo yanayochochea vurugu na kulifanya Bunge lipoteze heshima yake katika jamii.

Aidha, wabunge hao wamekubali kwa kauli moja kuanza upya kuzingatia kanuni zinazoendesha vikao vya Bunge huku wakimtaka Spika wa Bunge au Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kutosita kuchukua hatua za haraka kwa mbunge yeyote atakayekiuka utaratibu na kanuni zilizowekwa.

No comments: