Tuesday 28 June 2016

Mkutano wa Wabunge wa UKAWA kwa Waandishi wa Habari kuhusu Kadhiya na Mateso ya Police na Vukosi vya Mazombi yanayoendelea Zanzibar dhidi ya Wafuasi wa CUF.


Ndugu Wana habari,

Tokea kumalizika kwa Uchaguzi Haramu wa marudio huko Zanzibar Machi 20, 2016 hali ya kiusalama ya Zanzibar haijatulia. Tulia shuhudia ushushwaji wa kiwango kikubwa cha Wanajeshi, Polisi na silaha kipindi cha kuelekea uchaguzi huo kote Unguja na Pemba katika mbinu ya kuwatisha raia.

Wananchi wa Zanzibar kwa wingi wao walikataa kushiriki uchaguzi huo uliolazimishwa baada ya kufutwa ule uliofanyika Oktoba 25,2015 ambapo CUF iliibuka mshindi dhidi ya CCM, lakini CCM kwa mara nyengine tena ikaendeleza ubabe na kukataa kusalimu amri kwa njia ya kidemokrasia.

Kwa sababu ya hasira ya kukatliwa vikosi vya ulinzi na hasa Jeshi la Polisi vimekuwa vikishiriki katika vitendo kadhaa wa kadhaa vya kuonea raia huko Pemba ambapo kwa zaidi ya miezi miwili sasa wamekuwa wakipita vijiji kadhaa vya Wilaya zote nne za Pemba hasa nyakati za usiku.

Wamekuwa wakipiga risasi ovyo, kukamata raia ovyo, kuwatesa na kuwafungulia mashtaka bandia ambayo hadi leo hakuna yaliosimama seuze yaliokamilishwa kwa mtu yeyote kutiwa hatiani.

Visingizio kadhaa vimetumika dhidi ya raia ikiwa na pamoja kudai kufanywa kwa hujuma kwa taasisi za Serikali na hata mali za watu binafsi. Ukamataji unaofanywa na Polisi haufuati utaratibu wa kisheria unaoeleweka. Tunaamini pia vikosi maarufu kwa uonevu vya Mazombie nao pia hivi sasa wako huko Pemba kuendeleza ubababe huo.

Kuna ushahidi wa watu kuteswa wakiwa mikononi mwa Polisi na hivi sasa kuna watu wanakimbia sehemu wanazoishi wakisakwa na Polisi na wao kuhofia usalama wao. Wabunge wa Pemba wa Chama cha CUF wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kufuatilia kadhia za wapiga kura wao.

Vijiji ambavyo vimeathirika na kadhia hiyo huko Pemba ni pamoja na vijiji kadhaa katika majimbo ya Mgogoni, Mtambwe, Wingwi, Kiwani, Ziwani, Tumbe na Chonga.



Ndugu Wana habari

Nako Unguja mambo si shwari ambavyo hivi karibuni kutokana na amri ya Dk. Ali Muhammed Shein ya kusafishwa mifugo ndani ya mji wa Zanzibar nguvu kubwa imekuwa ikitumika kutaifisha wanyama hao na risasi za moto kutumika.

Watu 5 wamepigwa risasi na kujeruhiwa vibaya katika kadhia hio. Pamoja na kufikishwa Kituo cha Polisi cha Mwanakwerekwe, watu hao hajawapewa  RB Namba katika kile kinachookena Polisi kukwepa kuwajibishwa na matukio hayo.

Vitendo vya Mazombi navyo pia vimekuwa vikiendelea.





Ndugu Wana habari



 UKAWA inaamini kabisa kuwa nguvu na jeuri ya Polisi kufanya matendo hayo inatokana na Rais wa Jamhuri ya Muunagano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli ambaye ndie Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama.

Hatuamini kabisa kuwa Dk Magufuli hajui kinachoendelea huko Pemba kwa sababu ni matukio ya muda mrefu sasa, na kama hajui kutakuwa hakuna msamaha maana atakuwa amekoseshwa taarifa na vyombo vyake. Matukio yote ya Unguja na Pemba yamekuwa yakiarifiwa katika vyombo vya habari.

Pia UKAWA inaamini kuwa Mkuu wa Polisi Tanzania IGP Mangu anajua kila kinachotokea na kunyamazia kwake matukio hayo ambayo wanfanyiwa raia ni kuunga mkono na hata kwamba kuna baraka zake na ndio maana yamekuwa yakiendelea.

Bila ya shaka vitendo hivyo vinafurahiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo inafaidika na matukio ya kuonewa kwa raia ili hasa kuwatoa wanachama wa CUF katika kuendeleza dhamira yao ya kuikataa Serikali iliyojiweka madarakani kwa njia ya ghilba, nguvu na kinyme cha ridhaa ya Wazanzibari.



Ndugu Wana Habari

UKAWA inatoa wito kwa Rais Magufuli kutimiza wajibu wake mkuu wa kwanza kikatiba nao ni kuhakikisha usalama wa raia wa Jamhuri ya Muungano. Pia kuhakikisha kuwa vikosi vya usalama vinatimiza kazi yao kuu ya kuwalinda na sio kuwaonea raia.

UKAWA itapenda kusikia kauli ya wazi kabisa ya Rais Magufuli juu ya maonevu yaliodumu kwa muda mrefu dhidi ya Wazanzibari na kuheshimiwa haki zao za binaadamu ikiwa ni pamoja na zile za kujikusanya, kujiunga na maoni.

UKAWA inamtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba afanye ziara ya haraka Pemba na kisha Unguja na apate first hand information juu ya matendo hayo ya Polisi kwa kukutana na wananchi walioathirika katika matukio tuliyoyataja na UKAWA iko tayari kumsaidia kuwapata watu hao.


UKAWA pia inamtaka IGP Mangu kwanza atue amri ya kusitishwa kwa matendo hayo, lakini pili achukue hatua dhidi ya Polisi ambao wamekuwa wakionea na kutesa raia ili kurudisha imani ya jeshi hilo kwa wananchi hasa wa Pemba


Mwisho UKAWA inawataka wananchi wa Unguja na Pemba kuikataa Serikali haramu iliopo madarakani huko Zanzibar kwa njia za amani  na pia wadumishe utaratibu walionao hivi sasa wa kuheshimu sheria na kujizuia kufana vitendo vya kukinzana na sheria.


UKAWA inaamini Usiku Hauwezi kuwa mrefu wa kuzuia Alfajiri na Asubuhi Isifike.

press --

No comments: