Wednesday 29 June 2016

Tumchambue Tindu Lisu na kauli ya Dictator Uchwara.


Udikteta ni nini?

Udikteta ni mfumo wa utawala wa nchi ambapo mtu mmoja asiyebanwa na sheria wala katiba anashika madaraka ya serikali na ana uwezo wa kuyatumia jinsi anavyoamua mwenyewe.  Kwa upande mwingine kuna Udikteta wa mtu mmoja au wa kundi, Mtu huyu anaitwa "dikteta" ingawa cheo rasmi mara nyingi ni "rais" au "kiongozi wa taifa". Wakati mwingine neno "udikteta" unataja pia hali ambayo kundi la watu linashika madaraka yake kwa pamoja kwa mfano kamati ya wanajeshi waliochukua madaraka ya serikali.

Kila nchi inahitaji sheria na pia udikteta hauwezi kuongoza bila sheria. Lakini tabia muhimu ya udikteta ni ya kwamba dikteta ana nafasi au uwezo wa kupuuza sheria au kufanya maazimio nje ya sheria na hakuna njia ya kumlazimisha kutii sheria.

Mara nyingi uhuru na haki za wananchi zimepungukiwa sana au kuondolewa kabisa kwenye mfumo wa udikteta. Tabia muhimu ya demokrasia ni uhuru wa mahakama. Katika udikteta serikali inateua mahakimu na kuingilia kati katika maazimio ya kesi. Kama kesi inaangaliwa na serikali ni kawaida ya kwamba hukumu huamuliwa nje ya mahakama.

Matumizi mabaya ya vyombo vya Dola.

Polisi inapewa nafasi ya kuibaka demokrasia, kuwatesa watu na hii ni aina ya adhabu bila sheria wala mahakama. Mara nyingi polisi zinapewa pia nafasi ya kuua watu hovyo au kuwafunga ndani bila kesi kusikilizwa mahakamani.

Uchaguzi Bandia.

Utaratibu wa uchaguzi huru haufuatwi. Tume ya uchaguzi inaundwa kwa matakwa ya mtu au chama tawala. Katika nchi kadhaa uchaguzi hufutwa kabisa kwa miaka mingi. Lakini mara nyingi kuna uchaguzi bandia badala ya uchaguzi huru. Kati ya njia mbalimbali za kuathiri matokeo ya uchaguzi ni:

Kuteuliwa kwa wagombea na serikali na kukataliwa kwa wote ambao serikali haipendezwi nao. Mfumo wa chama kimoja au mfumo wa vyama Vinci lakini wenye tabia ya chama kimoja ambako viongozi wana nafasi ya kufukuza watu ambao hawapendezi katika chama na kuwatenga na siasa. Kutawala usimamizi wa uchaguzi na kutangaza matokeo kufuatana na mipango ya uongozi si kutokana na kura yake, ama uchaguzi hautokei au serikali inateua wagombea ikiondoa wapinzani wote au uchaguzi unaamuliwa awali na serikali ya kidikteta.

Uhuru wa maoni.

Uhuru wa maoni unabanwa au hata kupigwa marufuku kabisa. Serikali inasimamia vyombo vya habari kama magazeti, redio na televisheni. Kutolewa kwa maoni yasiyopendwa na serikali ni vigumu. Hata hivyo kuna tofauti kwa sababu kuna udikteta ambako kuna kiwango fulani cha nafasi ya kupinga maazimio ya serikali kwenye ngazi za chini kwa mfano mjini au wilayani, hali za barabara au rushwa ya watumishi wadogo wa serikali. Lakini udikteta hauruhusu upinzani unaoendelea kueleza uhusiano kati ya makosa madogo na muundo wa serikali. Upinzani dhidi ya viongozi wa juu haukubaliwi kabisa.

Spika au mwenyekiti wa bunge kutumika kuikingia kifua serikali na kuwabana wapinzani hususani wale wanaoonekana wakiikosoa sana serikali au mfumo kandamizi uliopo na wakati huohuo ikitoa Uhuru wa maoni uliopitiliza kwa wabunge au wawakilishi wanaotokana na utawala au chama kilichoko madarakani. Mara nyingine serikali au utawala wa kidikteta huweza kwenda mbali zaidi na kuzuia hata wananchi wasiweze kufuatilia au kuona vikao vya Bunge na jinsi wawakilishi wao wanavyo wawakilisha Bungeni.

Jambo la kawaida ni uteuzi wa habari zitakazoonekana kwenye vyombo vya habari. Nchi kadhaa zinajaribu pia kukataza habari za nje kufika. Katika Ujerumani ya Mashariki kwa miaka kadhaa antena za Tv zilizoelekea magharibi zilipigwa marufuku kwa sababu serikali ilitaka kuzuia upatikanaji wa Tv yaUjerumani ya Magharibi. Katika Korea ya Kaskazini wananchi wa kawaida hawana nafasi ya kuangalia intaneti. China inatumia mitambo mingi inayojaribu kuzuia habari fulani kupitia intaneti; kuna programu ambazo zinazuia kuangalia kurasa zenye jina la “Dalai Lama” anayehofiwa kama mpinzani wa serikali.

Kwa kipande hiki kidogo natumai kwa wale watakaoweza kukisoma na kukielewa wataweza kupima na kutafakari kwa mapana na kupata kufahamu tabia ya serikali inayojiongoza kwa kufuata mfumo wa kidikteta kinyume na serikali inayojiongoza kwa kufuata mfumo wa demokrasia na kupima aina ya mfumo wa serikali tuliyonayo.

No comments: