Tuesday, 11 October 2016

Maalim Seif Amuandikia barua Msajili

Image result for Maalim seif Pictures

Our Ref: CUF/HQ/KM/2016/21        Date: 4 Oktoba, 2016

Msajili wa Vyama vya Siasa
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
Kivukoni Ilala CBD
1 Mtaa wa Shaaban Robert
P.O. Box 63010
11101 DAR ES SALAAM


Yah: MAAMUZI YA KIKAO CHA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA LA CHAMA CHA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF) KILICHOFANYIKA
TAREHE 27 SEPTEMBA, 2016


Tafadhali rejea barua yako yenye Kumbukumbu Nam. HA.322/362/14/93 ya tarehe 30 Septemba, 2016 kuhusu mada iliotajwa hapo juu.

Tumebaini kwamba pamoja na kukuandikia mara kadhaa kwamba Ofsi ya Msajili wa Vyama vya Siasa haina mamlaka, uwezo wala wajibu wa kuingilia maamuzi ya vikao halali vya Chama, bado umekuwa ukituandikia na kututaka tujibu malalamiko ya watu waliowasilisha malalamiko kwako kuhusiana na maamuzi ya vikao halali vya Chama.

Uzoefu tulioupata kupitia barua yako Kumb. Nam. HA.322/362/14/85 ya tarehe 23 Septemba, 2016 iliyokuwa na kichwa cha maneno, “MSIMAMO NA USHAURI WA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA KUHUSU UONGOZI WA KITAIFA WA CHAMA CHA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF)” umetuonesha kuwa baada ya kukuandikia maelezo umekuwa ukijipa mamlaka ya Mahakama na kutoa uamuzi (judgment) kuhusiana na malalamiko hayo, jambo ambalo ni nje ya uwezo wa Msajili wa Vyama vya Siasa. Tunasikitishwa sana kwamba mtu wa hadhi na elimu yako ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu unashindwa kulielewa hili.

Tunapenda kukukumbusha tena, iwapo umeghafilika, kwamba majukumu ya Ofisi yako kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha ofisi hiyo, Sheria ya Vyama Vya Siasa Sura ya 258, haikupi mamlaka ya kutoa msimamo na muongozo wala “kujiridhisha kuwa kikao hicho na mamuzi yake ni halali kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Chama” kama ulivyoeleza katika barua yako. Hayo ni mamlaka ya Mahakama. Badala yake, unapewa mamlaka ya kuhifadhi kumbukumbu na taarifa za vyama vya siasa. Tafadhali rejea tena maamuzi ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam katika Shauri la Madai Na. 6 la mwaka 2003 baina ya Emmanuel Nyenyemela and Another Versus Registrar of Political Parties and Others mbele ya Mheshimiwa Jaji Mihayo ambapo ilielezwa kama ifuatavyo kwenye ukurasa wa pili wa hukumu:

“The reliefs sought in this matter do not fall under section 20 of the Political Parties Act. They cannot therefore be sought by way of judicial review. In the same vein, I do not see anywhere in the Political Parties Act where the Registrar has power to bless or condemn meetings of political parties or decisions that they make”.

Tunakukumbusha tena na kukutaka utambue kuwa uamuzi na muongozo huo wa Mahakama Kuu ya Tanzania haukuwahi kutenguliwa na mahakama yoyote ile na hivyo tunaamini wewe ukiwa na weledi katika taaluma ya sheria na Jaji wa Mahakama Kuu, unafahamu uamuzi huo na nafassi yake kisheria.

Katika barua yako umetaja na kutumia Kanuni ya 13 na 16 ya Kanuni za Usajili wa Vyama vya Siasa [Tangazo la Serikali Namba 111 la mwaka 1992] kututaka tuwasilishe maelezo ya upande wetu kuhusiana na malalamiko ya Profesa Ibrahim Lipumba aliyoyawasilisha kwako kupinga uhalali wa kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa cha tarehe 27 Septemba, 2016. Kanuni ya 13 na 16 ulizozitaja hazikupi mamlaka hayo na wala hazihusiani na kupokea na kusikiliza malalamiko ya mtu au watu wanaopinga uhalali wa vikao vya Chama au wasioridhika na maamuzi ya vikao vya Chama na pia hazikupi mamlaka ya kudai maelezo ya Chama kuhusiana na malalamiko hayo.

Tunaomba tuzinukuu Kanuni hizo hapa chini:

“13-(1) The Registrar may at any time require a party to submit to him a return or report relating to the constitution, objects, office-bearers or membership as well as the finances of the party.
(2) Every office-bearer and every person managing or assisting in the management of a party shall forthwith comply with any requirement made by the Registrar under paragraph (1) of this Regulation.

16. In the event of a breach by a party of the provisions of Regulation 6,7,8,11,12 or 13, every office-bearer of the party concerned shall be guilty of an offence and shall be liable on conviction to a fine not exceeding thirty thousand shillings or to imprisonment for a term not exceeding six months or to both such fine and imprisonment.”

(Msisitizo wa maneno yaliyopigiwa mstari ni wetu).

Ukiwa ni mwanasheria na Jaji wa Mahakama Kuu, tunaamini unafahamu maana ya maneno yaliyotumika kwenye Kanuni ya 13 kwamba, “The Registrar may at any time require a party to submit to him a return or report relating to the constitution, objects, office-bearers or membership as well as the finances of the party”.

Maelezo ambayo umekuwa ukitutaka tuwasilishe kwako hayahusiani na Katiba, malengo, viongozi, wanachama au fedha za Chama kama inavyotakiwa na Kanuni ya 13 tuliyoinukuu hapo juu. Badala yake umekuwa ukiitumia visivyo Kanuni hiyo na hata kututisha kwa kutumia Kanuni ya 16 kututaka tukupatie maelezo kuhusiana na malalamiko yanayohusu uhalali wa vikao vya Chama na maamuzi yanayofikiwa, na kisha kujipa mamlaka ya kutoa uamuzi kuhusiana na malalamiko hayo na hata kutuamulia nani wawe viongozi wetu. Tunarudia kusema kwamba hayo ni mamlaka ya Mahakama na siyo ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Kwa misingi tuliyoieleza hapo juu, tunaamini tutakuwa tunavunja sheria za nchi kwa kuendelea kukupa maelezo ambayo unayatumia vibaya kujipa mamlaka usiyokuwa nayo na ambayo Ofisi yako ilishaonywa na Mahakama Kuu katika shauri tulilolitaja hapo juu kwamba hunayo.

Tukuombe tu umshauri Profesa Ibrahim Lipumba au mtu mwengine yeyote mwenye malalamiko kuhusiana na uhalali wa vikao vya Chama au maamuzi yake aende Mahakamani ambako ndiko kwenye uwezo wa kuchunguza uhalali wa vikao na maamuzi yake.

Hata hivyo, tukuhakikishie kwamba CUF itaendelea kukupa mashirikiano kwa kukupatia taarifa na maelezo kuhusiana na mambo yote yaliyotajwa kwenye Sheria ya Vyama vya Siasa [Sura 258] pamoja Kanuni za Usajili wa Vyama vya Siasa [Tangazo la Serikali Namba 111 la mwaka 1992] kila pale utakapohitaji, kama ambavyo tumekuwa tukifanya tokea CUF ilipoasisiwa.

Tunatanguliza shukrani zetu za dhati kwako na kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

HAKI SAWA KWA WOTE


SEIF SHARIF HAMAD
KATIBU MKUU

No comments: