Monday 3 October 2016

Sababu tatu za CUF kupigwa vita na dola


Nimeichukuwa tena na kuisoma kwa makini zaidi taarifa ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) ya tarehe 15 Septemba 2016 iliyotolewa mbele ya waandishi wa habari katika ukumbi wa habari wa Bunge hilo mjini Dodoma na ambayo ilizungumzia kadhia nzima ya mgogoro wa mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba. Sehemu ya taarifa hiyo ilisomeka hivi: “Tumepata taarifa kutoka kwa vyanzo vinavyoaminika serikalini kuwa kuna njama zinazopangwa na washindani wetu wa kisiasa Chama Cha Mapinduzi (CCM), vyombo vya ulinzi na usalama na serikali ya CCM kutaka kuitumia ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kumtangaza Prof. Ibrahimu Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa CUF. Dhumuni la yote hayo ni kutaka kukiyumbisha chama chetu na kutupandikizia mgogoro usiopaswa kuwepo. Kama kitendo hicho kikifanyika kitakuwa kinyume kabisa na katiba, kanuni na taratibu za chama chetu, lakini kitakuwa kinyume na sheria ya Vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992 ambayo haitoi mamlaka yoyote kwa Msajili wa vyama vya siasa kukipangia chama cha siasa viongozi wake.”

Kwa ufupi, taarifa nzima ya siku hiyo ya wabunge hao ilikuwa ni kueleza wasiwasi wao huo kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kuitumia ofisi yake kinyume cha sheria na taratibu ili kukidhi matakwa ya kukiharibu chama chao. Lakini kama lengo lao lilikuwa ni kuzuwia hilo walilohofia lisitokee, basi hawakuweza, kwani siku tisa tu baadaye, Jaji Mutungi aliwasilisha barua yake kwa CUF, barua ambayo inamtambua Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa CUF, licha ya msajili huyo kutambuwa pia kwamba Lipumba aliwahi kukiandikia chama chake barua rasmi ya kujiuzulu uongozi wa chama hicho.


Kitendo hiki cha Jaji Mutungi kinaweza kumshawishi yeyote kwamba tuhuma za wabunge wa CUF walizozitoa tareh 15 Septemba 2016 dhidi yake sasa zinaanza kupata mashiko. Tuhuma hizi zikaongezewa nguvu pale jeshi la Polisi lilipoyasindikiza maandamano ya Lipumba kuingia Ofisi Kuu za CUF Buguruni kwa nguvu kwa kuvunja mageti na milango ya ofisi hizo na kufanya uharibifu wa mali na kuwajeruhi walinzi huku polisi wakibaki kimya bila kutoa kemeo lolote.

Kwa hivyo, ni wazi kuwa CUF kama chama inapambana kwa sasa na maadui wakubwa kuliko Lipumba na kundi lake tu. Mikono inayomshikilia Lipumba kwenye hili ina mafungamano ya moja kwa moja ya vyombo vya dola, ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, na hapana shaka makundi mengine yenye maslahi na kile anachokifanya yeye, Lipumba. Hilo liko wazi. Lisilokuwa wazi ni sababu ambazo zinaifanya CUF ipigwe vita hivi vikubwa wakati huu na wapigaji wenyewe wawe hawa tuliowataja.

Makala hii imeziona sababu tatu kuu, kati ya nyingi nyenginezo zinazoweza kuwepo, zote zikihusiana na mafanikio ya CUF: kwanza ni mafanikio yake ya kuthibitisha kuwa ni chama pekee cha siasa ambacho hasa cha kitaifa, pili ni mafanikio ya CUF kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2o15 ule wa Marudio wa Machi 2016 na, tatu, ni mafanikio yake katika jukwaa la kimataifa baada ya chaguzi hizo mbili.

CUF kuwa chama halisi cha kitaifa

Unaweza kujiuliza kwa nini iandamwe CUF na sio CHADEMA, ambacho ni chama chenye wabunge wengi zaidi na ndicho kilichojizolea ushindi mkubwa kwenye uchaguzi wa 2015 upande wa Tanzania Bara kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)? Ni CHADEMA iliyopata wabunge 70 kiujumla katika uchaguzi huo, huku CUF ikiwa na wabunge 48 tu kwa Bara na Zanzibar.

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad (kushoto) akitaniana na Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi na pia mbunge, James Mbatia, kwenye mkutano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) tarehe 1 Mei 2014, Gombani ya Kale, Pemba.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad (kushoto) akitaniana na Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi na pia mbunge, James Mbatia, kwenye mkutano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) tarehe 1 Mei 2014, Gombani ya Kale, Pemba.

Ukweli ni kuwa, licha ya Tanzania kuwa na jumla ya vyama 22 vyenye usajili wa kudumu, vingi vyao vinaitwa vya kitaifa kwa jina tu, vikionesha utaifa wake kwa kushiriki chaguzi zinazoandaliwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na ile ya Tanzania (NEC) na au kutoa matamko yanayohusu nchi, ni vyama viwili tu pekee ndivyo vilivyoweza kuthibitisha kwamba kweli ni vya kitaifa.

Kwa muktadha wa makala hii, utaifa wa chama ni kuwa kwake na wafuasi na wanachama wa kutosha pande zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wanakipa chama hicho uwezo wa kushinda angalau kiti kimoja cha ubunge wakati uchaguzi mkuu pindi unapoitishwa.

Tangu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania irudi katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi mwaka 1992, katika chaguzi zote zilizofanyika kuanzia ule wa mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na uliomalizika mwaka jana 2015, ni chama tawala (CCM) na CUF pekee ndivyo vinavyothubutu kushinda viti vya ubunge pande zote mbili za Jamhuri hii.

Hivyo katika upinzani wa Tanzania, CCM inaiangalia CUF kuwa ndiye adui wake wa karibu na hatarishi zaidi kuliko chama chengine chochote kile. Hata pale UKAWA ilipojaribu kutaka kutengeneza adui wa pili, kwa mfano, pale walipokubaliana kuachia jimbo la Kikwajuni, kisiwani Unguja, waachiwe CHADEMA ili chama hicho nacho kiweze kupenya kidogo kidogo upande wa Zanzibar, lakini hilo halikuwa. CCM ilihakikisha kuwa CHADEMA haiingii Zanzibar, na hivyo kuendelea kukifanya kuwa chama kikuu cha upinzani Tanzania Bara tu, licha ya CUF kuifungulia milango.

Lakini UKAWA iliyoshindwa kufungua milango kwa vyama vyengine kuingia Zanzibar, bado iliimarisha zaidi CUF kwenye nafasi yake ya kuwa chama cha kitaifa kuliko chama chengine chochote kwenye umoja huo kwa upande wa Bara pia. Kabla ya uchaguzi huo wa Oktoba 25, CUF ilikuwa imeshapoteza nguvu zake upande wa Bara, ikiwa na wabunge wawili tu – wa Kilwa na Lindi Mjini. Lakini kupitia UKAWA, CUF ikapata viti 10 upande wa Bara.

Mafanikio haya, hapana shaka yoyote, yameitisha sana CCM na, kwa mara nyengine, imejithibitishia kuwa adui yake mkubwa kitaifa ni CUF tu. Ndiyo maana si jambo la ajabu kuwa inatumia nguvu zake zote, ikisaidiwa na mawakala wake ndani na nje ya dola, kuhakikisha kuwa inaiangamiza CUF kabla ya 2020.

Mafanikio ya Oktoba 2015 na wa Marudio Machi 2016

Kila mfuatiliaji wa uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 2015 anakubali kuwa huo ulikuwa ni wa kwanza kuwa na unafuu kushinda chaguzi zote zilizofanyika Zanzibar tangu kurudishwa kwa siasa za vyama vingi mwaka 1992. Waangalizi wote wa kitaifa na kimataifa waliusifu uchaguzi huu wa tarehe 25 Oktoba 2015 kuwa ulikuwa uchaguzi huru, wa haki na uwazi.

Uchaguzi Zanzibar
Mpigakura akitumbukiza kipande chake cha kura kwenye uchaguzi wa Oktoba 25,2015 mjini Zanzibar.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyokuwepo kabla ya uchaguzi huo ilijitahidi pakubwa kuandaa mazingira ya uchaguzi unaokidhi viwango vya kilimwengu, licha ya matatizo ya hapa na pale.

Lakini siku tatu baada ya kura kupigwa, yaani Oktoba 28, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha, aliufuta uchaguzi wote, baada ya kusuasua katika zoezi la utoaji matokeo licha ya yeye mwenyewe kuusifu uchaguzi huo mbele ya waangalizi wa kimataifa.

Mpaka anaufuta uchaguzi huo, tayari nusu na robo ya majimbo ya uchaguzi yalishahakikiwa na kuwekwa sahihi na pande zote za vyama vilivyoshiriki uchaguzi, ambapo majimbo 40 yalihakikiwa na kukubalika, majimbo 31 yalishatangazwa matokeo yake, na majimbo yaliyobakia yalikuwa ni 13 pekee kutimiza majimbo 54.

Baada ya kufutwa kwa uchaguzi huo, chama cha CUF, ambacho kinaaminika na wengi kuwa mgombea wake wa urais, Maalim Seif Sharif Hamad, alikuwa amepata ushindi wa 53%, kkilizikataa hatua za maamuzi yote mawili, kuanzia lile la kufutwa kwa uchaguzi na pia hatua ya kurejewa kwa uchaguzi mwengine wa Machi 20. ‘Uchaguzi wa Machi 20’ ndio uliomuweka madarakani Dkt. Ali Mohammed Shein.

Maamuzi hayo yalikataliwa na taasisi mbalimbali za waangalizi wa uchaguzi wa kitaifa na kimataifa, miongoni mwao ni Jumuiya ya Madola (Common wealth), Jumuiya ya Ulaya (European Union), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC), ambayo kwa sasa mwenyekiti wake ni Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mafanikio haya ya CUF ya waziwazi kwenye uchaguzi ambao unatazamwa kama wa haki na huru zaidi kuwahi kufanyika Zanzibar, hapana shaka ni donda ndugu kwenye kiwiliwili cha CCM. Tangu kumalizika kwa uchaguzi wa Oktoba, CCM imejikuta haina uso wowote mbele ya yeyote, wa ndani na wa nje, kila mtu mwenye kujiheshimu, amekuwa upande wa CUF. CCM imekuwa peke yake. Ndiyo maana itafanya iwezalo kuhakikisha kuwa CUF, mshindi halali wa uchaguzi huo, anaporomoka iwe iwavyo!

Mafanikio kwenye jukwaa la kimataifa

Mara baada ya kushindikana kwa mazungumzo kati ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, na viongozi wakuu wa sasa na wa zamani wa Zanzibar kuhusiana na uchaguzi huo na uamuzi wa kibabe wa CCM kwenda kwenye uchaguzi wa Machi 20, CUF iliamua kuachana kabisa na kuwashika miguu CCM na badala yake ikageukia jumuiya ya kimataifa.

Washiriki kutoka taasisi mbali mbali ikiwa ni pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje (FCO) ya Uingereza, University of Oxford, University of Edinburgh, Britain-Tanzania Society (BTS), Jarida la Tanzania Affairs, na taasisi ya Africa Matters Limited wakimsikiliza Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza kwenye mkutano maalum ulioandaliwa na Taasisi ya Africa Research Institute (ARI) yenye makao makuu yake mjini London, nchini Uingereza leo Jumatano, tarehe 13 Julai kuhusu haja ya kuheshimiwa kwa maamuzi ya Wazanzibari na mwelekeo wa kisiasa na kikatiba wa Zanzibar katika siku zijazo. Hii ilikuwa tarehe 14 Julai 2016.
Washiriki kutoka taasisi mbali mbali ikiwa ni pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje (FCO) ya Uingereza, University of Oxford, University of Edinburgh, Britain-Tanzania Society (BTS), Jarida la Tanzania Affairs, na taasisi ya Africa Matters Limited wakimsikiliza Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza kwenye mkutano maalum ulioandaliwa na Taasisi ya Africa Research Institute (ARI) yenye makao makuu yake mjini London, nchini Uingereza leo Jumatano, tarehe 13 Julai kuhusu haja ya kuheshimiwa kwa maamuzi ya Wazanzibari na mwelekeo wa kisiasa na kikatiba wa Zanzibar katika siku zijazo. Hii ilikuwa tarehe 14 Julai 2016.

Hilo lilifanyika kimahisabu na hatua kwa hatua, kwanza kwa kuwafuata mabalozi wa mataifa ya kigeni na asasi za kimataifa ndani ya Tanzania, kisha ikawa kuyafuata mataifa makubwa duniani huko huko yaliko. Kila hatua moja iliyopiga, CUF ilikuwa inajijengea heshima na jina mbele ya uso wa dunia, hasa kwa kuthubutu kwake kuwatuliza wananchi waliokuwa na hasira na badala ya kuwajaza barabarani kuandamana, wakawafanya wabakie majumbani mwao kungojea suluhu ya amani.

Maalim Seif na ujumbe wake wakaranda kote – tangu Marekani kwenye Umoja wa Mataifa hadi Uingereza kwenye Jumuiya ya Madola hadi Ubelgiji kwenye Umoja wa Ulaya hadi Uholanzi kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC). Na mote humo walipokelewa na kufanya mazungumzo ya kina na wahusika. Wakasikilizwa, wakafahamika.

Miongoni mwa matokeo ya karibuni zaidi ya ziara hizo kwenye jumuiya ya kimataifa yakawa ni tamko rasmi la kimaandishi lililowasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon mnamo Septemba 2016 Muungano wa Vyama vya Kiliberali Duniani (LI) juu ya uvunjwaji wa haki za binaadamu na misingi ya kidemokrasia visiwani Zanzibar.

Tamko hilo lilikabidhiwa kisheria kwa kutumia ajenda Namba 3 ya Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja la Umoja wa Mataifa, likielezea kwa dhahiri na shihiri kila ambacho kilitokea Zanzibar kuanzia Uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 na ule wa marudio wa Machi 20 mwaka huu pamoja na mikanda ya video na picha za matukio yote ambayo Umoja huo wa Kiliberali ulijiridhisha kwamba ni kweli haki za binaadamu zilikiukwa Zanzibar.

Sasa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotawaliwa na CCM imekalia kuti kavu mbele ya jumuiya ya kimataifa na aliyeifanya iwe kwenye hali hiyo ni CUF. Ndio maana, CCM haitalala usingizi hadi hapo itakapohakikisha kuwa inaizika CUF. Hilo halina mjadala. Lakini lenye mjadala ni ikiwa je, CUF itakubali kubwaga chali na kuuliwa kifo cha mende na CCM, baada ya miaka yote hii ya kuhimili vishindo vya ndani na nje yake? Wakati utaamua.
Sauce Tanzania Daima

No comments: