Friday, 21 October 2016

UMILIKI NA MAMLAKA YA ZANZIBAR JUU YA KISIWA CHA LATHAM (FUNGU MBARAKA)

Image result for othman masoud pictures

Imetayarishwa na OTHMAN MASOUD OTHMAN (Former Attorney General of Zanzibar)

Nimefarajika sana kuona kwamba Wazanzibari wengi wamepata muamko mkubwa kuhusiana na maslahi ya Zanzibar katika suala la kisiwa cha Latham (Fungu Mbaraka).  Hii ni faraja kwa vile Tanganyika wameonyesha nia ya wazi, ya dhahiri na ovu katika kukichukua kwa nguvu kisiwa hichi kutoka katika milki ya Zanzibar.  Baada ya mwishoni mwa mwaka 2013 kuona kwamba Tanganyika wamefika kutumia hata nguvu ya vyombo vya ulinzi kudai kuwa kisiwa hichi ni cha Tanganyika na baada ya kuona baadhi ya wataalamu wao wanajenga hoja dhaifu kuwa kisiwa hichi ni cha Tanganyika, mimi binafsi nilifanya utafiti wa kina juu ya umiliki wa Zanzibar kwa kisiwa hichi na kuuwasilisha utafiti huo Serikalini.  Baada ya Serikali kuridhika nao ndipo Makamu wa Pili wa Rais alipomuandikia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda juu ya msimamo wa Zanzibar katika umiliki wa kisiwa hicho.  Hatimaye, Waziri Mkuu naye akajibu kuwa kwa kumbukumbu zao, ambazo hakuziwasilisha hata moja, kisiwa hicho ni cha Tanganyika.

Nimeona ni vyema niwasambazie MUHTASARI wa taarifa ya utafiti niliofanya na ambao ndio uliowasilishwa kwa Mizengo Pinda.  Naamini taarifa hii itasaidia kuanika uovu wa Tanganyika kwa Zanzibar katika umiliki wa kisiwa hicho.  Aidha, utaweka bayana udhaifu wa baadhi ya viongozi wa Zanzibar katika kusimamia maslahi ya Zanzibar.


1. UTANGULIZI

Kisiwa cha Latham au kwa jina jengine Fungu Mbaraka (au Fungu Kizimkazi) kipo usawa wa kijiografia wa 6’ 54’ 5 S na 39’ 55’ 45’ E (Angalia ramani katika ukurasa wa 2).  Masafa kutoka Rasi ya Kizimkazi hadi katika Kisiwa hichi ni maili 36 (kilomita 57.9) na masafa kutoka kusini mwa Dar es salaam ni maili 37 (kilomita 59.5).  Aidha, masafa ya karibu kabisa baina ya kisiwa hicho na Tanzania Bara (sehemu za Kimbiji) ni maili 23 na nusu.  Kisiwa hichi kina urefu wa yadi 350 sawa na mita 320 na upana wa yadi 180 sawa na mita 164.5(kwa vipimo vya mwaka 1898).  Inaaminika kwamba kisiwa cha Latham kiliitwa jina hilo kutokana na meli ya kiingereza iliyokuwa ikiitwa Latham ambayo ilitia nanga katika kisiwa hicho mwaka 1758.  Aidha, kinajulikana kwa jina la Fungu Mbaraka kutokana na Bwana Ahmed Mbaraka ambaye alipewa ruhusa na Sultani kuzamia katika mabaki ya meli iliyozama jirani na kisiwa hicho na akapata fedha nyingi zilizomuwezesha kupata utajiri na kununua ardhi kubwa sehemu ya Nyamanzi.  Kisiwa hichi kina mnyanyuko wa futi 10 kutoka usawa wa bahari na kinakaliwa na ndege tu hali iliyopelekea kuwa maarufu kwa samadi ya ndege (guano) ambayo watu na makampuni kadhaa wamewahi kuomba kukitumia au hata kwenda kukichukua bila ya ruhusa.  Rasilimali hiyo ya samadi nyingi ya ndege ni miongoni mwa mambo yaliyokipa umaarufu sana kisiwa hichi hapo siku za nyuma.

2. HISTORIA YA UMILIKI

Kabla ya mikataba baina ya Waingereza na Wajerumani; ule wa 1886, 1888 na ule wa Heligoland wa mwaka 1890, kisiwa hicho kilikuwa chini ya mamlaka ya Zanzibar bila ya ubishi wala utatanishi wowote.  Mikataba hiyo miwili ndiyo iliyozusha utatanishi kuhusu umiliki wa Zanzibar juu ya kisiwa hicho.  Sababu za utatanishi huo ni kama zifuatazo:
Ibara ya 1 ya Mkataba wa mwaka 1886, iliyatambua mamlaka ya Sultani wa Zanzibar juu ya visiwa vya Zanzibar na Pemba na visiwa vidogo vidogo ndani ya mzunguko wa meli 12.  Kwa vile kisiwa cha Latham kipo umbali wa maili 36, inafsirika kuwa hakikuwezi kuingia katika makubaliano ya ibara hiyo ya 1 ya mkataba wa 1886;

b) Sababu ya pili ni kuwa kwa mujibu wa ibara ya XI ya Mkataba wa Heligoland wa 1890, Ujerumani ilikubali kuyatambua mamlaka ya Sultani juu ya visiwa vya Zanzibar na Pemba na mamlaka nyenginezo zilizobaki.  Ibara hiyo haikuweka wazi kama kisiwa cha Latham kilikuwa miongoni mwa mamlaka hizo nyenginezo au la;

c) Sababu ya tatu ambayo iliongeza utatanishi ni kuwa mikataba yote haikutoa mamlaka bayana kwa Wajerumani wala Waingereza juu ya kisiwa cha Latham.

Hata hivyo, pamoja na utatanishi huo wa kimikataba, hakukuwahi kutokea ubishani wowote au hoja yoyote juu uhalali wa umiliki wa Zanzibar kwa kisiwa cha Latham kati ya mwaka 1886 hadi 1898.

3. UBISHANI JUU YA UMILIKI WA KISIWA CHA LATHAM

Hoja ya nani mmiliki halali wa kisiwa cha Latham ilizuka mwaka 1898 baada ya kampuni moja iitwayo Messr Dawson & Company ya 9 & 10 Pancras Lane, Queen Victoria Street, London ilipoiandikia Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza kuulizia nani mmiliki halali wa kisiwa cha Latham kati ya Ujerumani na Zanzibar.  Baada ya kupata suala hilo, tarehe 19 August, 1898, Wizara ya Mambo ya Nje ilimuandikia Waziri Kiongozi wa Sultani (First Minister) kutaka ufafanuzi wa jambo hilo.  Balozi Mdogo na Wakala wa Uingereza aliyekuwepo Zanzibar Sir Arthur H. Hardinge alijibu barua hiyo tarehe 4 Oktoba, 1898.  Katika barua yake alitoa ufafanuzi juu ya kisiwa hicho na msimamo wa kisheria unaotokana na mikataba ya 1886 na ule wa 1890.  Hatimaye alihitimisha kwa kusema kuwa kwa vyovyote vile kisiwa hicho hakiwezi kuwa cha Ujerumani.  Hata hivyo, alieleza pia utatanishi wa kisheria uliopo juu ya umiliki wa Zanzibar pia.
Baada ya kujibu barua hiyo, Sir Arthur Hardinge mnamo tarehe 15 Oktoba, 1898 alimuandikia barua Sir Lloyd Mathews ambaye alikuwa Waziri Kiongozi wa Sultani kutoa ufafanuzi zaidi na ushauri wake juu ya kisiwa cha Latham.  Katika barua yake alieleza kuwa chini ya mikataba yote miwili kisiwa hicho hakiko chini ya mamlaka ya Ujerumani wala Uingereza.  Aidha, mikataba hiyo haikuweka bayana kuwa kiko chini ya mamlaka ya Sultani.  Hivyo, alishauri kuwa kisheria kisiwa hicho si ardhi ya mtu (no man’s land).  Kwa sababu hiyo na kwa sababu Zanzibar ndiyo yenye uhusiano wa karibu zaidi na kisiwa hicho, alimshauri Sir Lloyd Mathews aende katika kisiwa hicho haraka iwezekanavyo na akaweke bendera ya Zanzibar ili kukichukua na kukitangaza rasmi kuwa ni kisiwa cha Zanzibar.

4. KISIWA CHA LATHAM KUTANGAZWA RASMI KUWA CHA ZANZIBAR

Mbali ya ushauri huo wa Sir Arthur Hardinge, ambao unaonyesha ulipelekwa pia kwa Sultani, tarehe 17 Oktoba, 1898, Sir Lloyd Mathews alipokea maelekezo kutoka kwa Sultani kuwa aende katika kisiwa cha Latham ili akapachike bendera ya Zanzibar na kukitangaza rasmi kisiwa hicho kuwa kiko chini ya mamlaka ya Zanzibar.

Kufuatia maelekezo hayo, Lloyd Mathews aliondoka Zanzibar tarehe 18 Oktoba, 1898 kwa kutumia boti ya SS Barawa.  Alifuatana na Captain Arthur Agnew, Port Officer wa Zanzibar na Dr. Alfred Andrew Spurrier, Medical Officer, wafanyakazi wa boti hiyo na vibarua wengine kadhaa.  Saa 12 asubuhi ya tarehe 19 Oktoba, 1898 bendera ya Zanzibar ilipandishwa ikifuatiwa na saluti ya mizinga 21.  Aidha, nyumba ya chuma ilijengwa na bao kubwa la Tangazo lililosomeka “LATHAM ISLAND, FUNGU KIZIMKAZI UNDER ZANZIBAR SOVEREIGNTY” na pembeni ya ubao huo wa Tangazo maneno ya kiarabu yaliandikwa ambayo yakisomeka kama ifuatavyo “ Seyyid Hamoud byn Mohamed byn Said wa Zanzibar”.  Ofisa mmoja aitwaye Captain Baw na wasaidizi wawili waliteuliwa kuwa wasimamizi wa kisiwa hicho.
Sir Lloyd Mathews alirejea Zanzibar na akaandika taarifa rasmi kumpelekea Sultani, Waziri Kiongozi na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza.

5. MADAI YA UJERUMANI JUU YA KISIWA CHA LATHAM

Kwa mara ya mwanzo kabisa Ujerumani ilizusha madai ya umiliki wa kisiwa cha Latham mnamo mwaka 1910.  Madai hayo hata hivyo yalianzia mwaka 1909.  Mnamo tarehe 23 Juni, 1909 Sir Edward Clarke alimuandikia Gavana wa Ujerumani wa Tanganyika akimueleza kuwa kuna taarifa kuwa wapo raia wa Uingereza wanaoishi kusini mwa Tanganyika ambao wanakwenda kuchukua samadi ya ndege (guano) bila ya ruhusa ya Serikali ya Zanzibar.  Alimtaka Gavana asitishe vitendo hivyo mara moja.  Tarehe 6 Disemba, 1910, Gavana wa Tanganyika aliandika Waraka kwa Serikali ya Zanzibar akidai kuwa Ujerumani ndiyo yenye mamlaka juu ya kisiwa cha Latham.  Katika kujenga hoja hiyo, Waraka huo ulinukuu zaidi vifungu vya mikataba baina ya Wajerumani na Waingereza ambayo ilitambua mamlaka ya Zanzibar.  Kwa tafsiri ya mikataba hiyo alidai kuwa Zanzibar haina mamlaka juu ya kisiwa hicho.

Mnamo tarehe 13 April, 1911 Sir Edward Grey alijibu Waraka huo kwa kuandika Waraka wa majibu kumpelekea Herr Von Kuhlmann wa Ofisi ya Gavana wa Tanganyika.  Katika majibu yake Sir Edward Grey alieleza hoja zifuatazo:

a) Kwamba kisiwa cha Latham kiliwekwa rasmi kuwa sehemu ya Zanzibar kuanzia tarehe 19 Oktoba, 1898 na akafafanua kwa urefu juu ya kazi ya uwekaji wa bendera ya Zanzibar kulikofanywa na Sir Lloyd Mathews;

b) Alikumbusha kwa urefu mawasiliano yaliyofanywa katika mwaka 1900 baina ya Serikali ya Uingereza na nchi kadhaa ikiwemo Ujerumani juu ya pendekezo ya kujenga minara ya kuongozea meli katika eneo la Zanzibar kikiwemo kisiwa cha Latham, Pemba Kaskazini na Chumbe.  Alieleza kuwa Ujerumani ilikuwa moja ya nchi zilizotoa maoni kuhusu pendekezo hilo lakini haikuwahi kudai
wala kuonyesha dalili ya kuwa Latham ni sehemu ya mamlaka ya Ujerumani wala kupinga mamlaka ya Zanzibar juu ya kisiwa cha Latham;

c) Alifanya uchambuzi wa mikataba hiyo na kuhitimisha kwa kueleza kuwa hakuna mkataba wowote kati ya hiyo ambayo imetoa mamlaka ya wazi kwa Ujerumani au Uingereza juu ya kisiwa cha Latham.  Alimalizia kwa kuishauri Ujerumani kama ina hamu ya kukimiliki kisiwa cha Latham iwasiliane na Serikali ya Zanzibar ambayo inaweza kuzungumza juu ya suala hilo.

Serikali ya Ujerumani haikuwahi hata mara moja kujibu Waraka huo wa Sir Edward Grey na wala haikuwahi kuwasiliana na Serikali ya Zanzibar juu ya kisiwa hicho.  Hatimaye iliwekewa kumbukumbu rasmi kuwa suala la hoja ya Ujerumani juu ya umiliki wa kisiwa cha Latham limefungwa rasmi.

6. SUALA LA UMILIKI WA KISIWA CHA LATHAM BAADA YA UJERUMANI KUONDOKA TANGANYIKA

Wakati wa utawala wa Uingereza katika Tanganyika suala la umiliki wa kisiwa cha Latham halikuwahi kujitokeza.  Badala yake, utawala wa Uingereza uliendelea kusisitiza kuwa kisiwa hicho ni mali ya Zanzibar.  Mtu mmoja aitwaye Mc Elderry aliiandikia barua Serikali ya Tanganyika akiomba ruhusa ya kuchukua samadi ya ndege kutoka katika kisiwa cha Latham.  Mnamo tarehe 16 Novemba, 1934 Sekretariat ya Serikali ya Tanganyika ilimuandikia barua Bw. Mc Elderry kujibu maombi yake.  Katika barua hiyo ya majibu Sekretariat ilieleza kuwa kisiwa cha Latham hakikuwahi kuwa chini ya mamlaka ya Ujerumani.  Aidha, katika kuthibitisha hilo, ilielezwa kuwa hata katika ramani ya Reich’s Kolonialamt iliyochapishwa Berlin mwaka 1908 haikuonyesha kuwa Latham ni sehemu ya mamlaka ya Ujerumani.

HATUA ZA KIUTAWALA NA KISHERIA ZA SERIKALI YA ZANZIBAR JUU YA UMILIKI WA KISIWA CHA LATHAM

Kumbukumbu zinaonyesha  kuwa Serikali ya Zanzibar iliendelea kukitumia na kukiendesha kisiwa cha Latham kwa shughuli mbali mbali.  Miongoni mwa shughuli hizo ni utafiti wa ndege, kupanda miti, utafiti juu ya kima cha samadi ya ndege (guano) kama inatosheleza kibiashara au la.

Mbali ya shughuli hizo, viongozi kadhaa, akiwemo Sultani na British Resident walitembelea kisiwa cha Latham na taarifa za safari zao zimewekewa kumbukumbu.  Mfano mzuri ni ziara ya British Resident ya tarehe 9 March, 1951.

Mnamo mwaka 1959, Serikali ya Zanzibar ilikitangaza kisiwa cha Latham kuwa ni hifadhi ya ndege (bird sanctuary) kupitia Tangazo Namba 56 la 1959 kama linavyoonekana hapa chini.  Kwa mujibu wa kumbukumbu tulizoweza kuzitafiti, Tangazo hili bado halijafutwa au kurekebishwa na hivyo, kisheria, kisiwa hicho bado ni hifadhi ya ndege ya Zanzibar.

8. HITIMISHO

Ni dhahiri kwamba kwa kumbukumbu za kisheria na za kiutawala ziliopo na ushahidi juu namna kisiwa cha Latham kimekuwa kikitumika, kusimamiwa na kuendeshwa, kisiwa hicho cha Latham kipo chini ya mamlaka ya Zanzibar tokea tarehe 19 Oktoba, 1898.

Aidha, Zanzibar imekuwa inakitumia na kukisimamia kisiwa hicho kiutawala kwa miaka yote hiyo mfululizo bila ya kuwepo madai wala haki ya mamlaka nyengine. Hivyo, kisheria kisiwa hicho ni sehemu ya Zanzibar na kwamba Zanzibar ina mamlaka halali juu ya kisiwa hicho tokea tarehe 19 October 1898.

OTHMAN MASOUD OTHMAN

ADVOCATE & NOTARY PUBLIC
Źanzibar

No comments: