Friday, 16 October 2009
MZIMU WA NYERERE UNAWATESA WAZANZIBARI
Zanzibar yataka Nyerere mwengine
Na Ally Saleh
Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere hakuwahi kuwa kipenzi kikubwa sana cha wananchi wa Zanzibar. Na hilo ni kwa sababu nyingi ambazo kwa ukweli au dhana walizihusisha nae. Kama ningeruhusiwa kuwasemea Wazanzibari nigethubutu kusema kuwa Nyerere hakuliliwa sana wakati alipofariki kama vile ambavyo watu hawakutaka kumfurahia wakati wa uhai wake.
Lakini hii haina maana kabisa kuwa Nyerere hakuwa na heshima mbele ya Wazanzibari. Ukweli ni kuwa heshima yake ilikuwa ni ya hali ya juu kwa sababu wengi walimuona kuwa ni mtu mwenye uwezo sana wa kujenga hoja na ambaye daima hakuogopa kusema fikra zake wakati akiwa kwenye siasa na nje ya siasa.
Wanajua pia mchango wake katika suala zima la kuunganisha watu wa Zanzibar kupigania uhuru wao. Yeye ni chanzo kikuu kilichopelekea kuundwa au tuseme kuunganisha nguvu za Shirazi Association na African Association na kuzaliwa Afro Shirazi.
Binafsi wakati mmoja nilishangaa mwaka 1985 nilipopata maagizo kuwa Mwalimu ametaka kupata maelezo kutoka kwangu kuhusiana na taarifa niliokuwa nimeitoa kwenye Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC. Taarifa hiyo ni kuwa Wazanzibari walikuwa wanapendelea Rais wa Zanzibar Ali Hassan Mwinyi abakie kuwa Rais wa Zanzibar na asiende kushika wadhifa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Wakati huo ilikuwa tayari minon’gono ilikuwepo kuwa Mwinyi anaandaliwa kuwa Rais wa Muungano na ilhali alikuwa kipenzi cha Wazanzibari kwa hatua zake ambazo zilikuwa zimeanza kuifungua Zanzibar kibiashara na kiuwekezaji, lakini muhimu zaidi kwa Wazanzibari ilikuwa ni kurudishiwa uhuru wa maoni na haki za binaadamu.
Hivi kwa Wazanzibari ndivyo alivyokuwa Mwalimu kuwa hakuweza kuacha kitu chochote kile bila ya kukiulizia na kama si kukiulizia basi kukisema na zaidi ya hapo hata kukikemea. Na mifano ya hiyo iko mingi sana ingawa mara mbili tatu aliwaangusha Wazanzibari kwa baadhi ya mambo kuyaachia na kutishia hata uhai na usalama wa Zanzibar.
Nyerere hakuwa mkali au tuseme alikuwa mzito wa kumgomba au kumkosoa Rais Abeid Karume na wengine tunaamini ni kwa sababu kwa wakati ule alikuwa anataka Zanzibar ibakie katika Muungano wa Tanzania kwa gharama yoyote ile.
Maana Nyerere hakutoa sauti yake wakati wananchi walipokuwa wakichukuliwa usiku usiku na kupotea, wala Karume alipokuwa akiwamaliza viongozi wenzake na wala Karume aliposimamia zoezi la ndoa za lazima hasa dhidi ya Waasia wa Kizanzibari.
Lakini pia Nyerere alikuwa kimya kwa sera nzuri za Zanzibar kama elimu bila malipo, afya kwa wote, maji kwa wote na hata suala la kupewa ardhi wananchi, pamoja na makosa yake, hakuwa akiziunga mkono na kuzipa nguvu stahiki. Nyerere hakuonekana kusaidia kuhimiza mafanikio hayo na tuseme mpaka anaondoka la Zanzibar lilikuwa la Zanzibar na la Tanganyika la Tanganyika.
Tulimuona Nyerere aliyebadilika baada ya kuundwa kwa CCM na pengine ndio maana hakuwa na sauti wakati Afro Shirazi Party ilipokuwa hewani, ila baada ya kuja kwa CCM Nyerere alisogea karibu zaidi kukemea matukio ya Zanzibar na kwa hilo ndilo ambalo Wazanzibari watamkumbuka Nyerere.
Wengi tunakumbuka Nyerere alipokuwa mtu wa mwanzo kabisa kusema kuwa njia bora kabisa ya Zanzibar kukabili uwili wake wa siasa, maana siasa za Zanzibar ni uwili wa CUF/CCM ni kuundwa kwa Serikali ya pamoja, lakini wakati huo Dk. Salmin Amour alikataa kabisa wazo hilo.
Pengine kwa wakati ule sauti ya Nyerere haikuwa kubwa kwa sababu mabaki ya Afro Shirazi Party yalikuwa bado yana nguvu na kwa hakika wengine kati yao walikuwa na uchungu wa Nyerere kuingilia kuizuia Zanzibar isiwe na uhuru wa kuwa na ushirikiano wa kimataifa kupitia Jumuia ya Kiislamu (OIC).
Na hatujasahau mbele ya Nyerere mabaki ya Afro Shirazi yaliposimama kidete kumkataa Salim Ahmed kuwa Rais wa Zanzibar na mawazo kama hayo ya kuwa Mpemba na Muarabu hatawali Zanzibar kwa hakika mpaka leo yapo na yanapepea.
Kwa kupinga wito wa Mwalimu kufanya serikali ya pamoja Zanzibar ilikosa fursa muhimu sana ya kutandika msingi mzuri wa siasa za ushindani kwa kuendekeza mawazo kuwa kwa mujibu wa siasa za Zanzibar hasa kwa jicho la kihistoria basi vyama vya CUF na CCM haviwezi kuwa na serikali ya pamoja – ilhali vyama kinzani zaidi duniani tumeona vimeweza kufanya hivyo na mfano wa karibu ni huko Zimbabwe.
Naamini kama Nyerere angekuwapo basi asingekubali kabisa kuundwa kwa makundi ya vijana yaliyopewa jina la Janjaweed ambayo kila kipindi cha uchaguzi hupewa satwa kubwa kufanya kila watakalo katika kuviza demokrasia na kujenga mazingira ya nguvu ya kukipa ushindi Chama cha Mapinduzi Zanzibar. Na pia asingeridhi kabisa kwa vyombo vya dola kuonekana wazi wazi kulalia kwa upande wa chama tawala.
Nyerere katu asingekubali kabisa kuwa CCM Zanzibar iko tayari kufanya lolote lile lakini lazima ushindi wa uchaguzi ubakie na zaidi CCM Tanzania Bara ikinyamaza kimya na kubariki matendo hayo, yawe ni ya kupandikiza wapiga kura na kufanya ghilba mbali mbali.
Angekuwepo Mwalimu asingefurahi kabisa kuona Wapinzani wanafikia mpaka kufanya matumizi ya nguvu kama vile uripuaji wa baruti, ususiaji wa vikao vya Baraza la Wawakilishi na kukataa kushirikiana na Serikali.
Mwalimu angekuwepo angekasirika sana kuona nchi hii sasa inagawanyika kwa ugomvi wa rasilmali kama vile suala la mafuta, mgawano wa michango ya wafadhili na hata namna ambavyo uchumi wa Zanzibar unavyokabwa koo kwa taasisi kama Mamlaka ya Kodi (TRA) isivyokuwa na huruma kabisa kwa visiwa hivyo.
Naamini kuwa Mwalimu angekuja Zanzibar mara nyingi kadri ambavyo ingewezekana lakini asingekubali suala la Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi liwe kidonda kwa chama chake na hata Serikali za Zanzibar na Tanzania na kuhakikisha kuwa misingi ya demokrasia iliyowekwa ya kuwa kila raia anaweza kupiga kura apate fursa hiyo na sio kuvizwa kwa visingizio vya kukosa cheti cha kuzaliwa au ruhusa ya Sheha
Kwa fikra zangu naamini kuwa Zanzibar ina vitu kidogo sana vya kumuonyesha Mwalimu na yeye kuweza kuridhika kuwa visiwa alivyoviwacha vimesonga mbele kidemokrasia na kuhakikisha haki, usawa na umoja. Katika sheria hilo limefanikiwa lakini katika uhalisia au ukweli wa mambo hilo liko mbali sana.
Mwalimu hangesita kuikemea Halmashauri Kuu ya CCM, moyo na injini ya chama hicho kwa kubariki ya dhulumati ya kisiasa na kiraia inayoendela Zanzibar. Naamini angekuwa zamani ameshakutana na Rais Kikwete na Rais Karume kuwauliza mbona hawachukui uongozi?
Kama nilivyokuwa nimesema mwanzo kuwa Nyerere hakuwa kipenzi kikubwa cha Wazanzibari. Lakini sasa hivi wanamuhitajia sana maana wanaona wametupwa na Watanzania wenzao kuanzia taasisi za haki za binaadamu na hata wasomi wakubwa wakubwa.
Wanamkumbuka Nyerere kwa sababu jumuia ya kimataifa inaburura miguu kwa sababu wapiga kura hawaandikishwi kwa kisingizio au maelezo ni kwa ajili ya sheria. Si Watanzania wenzao – wasomi na taasisi za haki za binaadamu na wala si jumuia ya kimataifa inayohoji – hivi kweli sheria ambayo inatenga idadi kubwa ya watu kutoweza kupiga kura ina uhalali gani na uchaguzi unaofanywa chini ya msingi huo unaweza kuwa na uhalali gani?
Nyerere asinge nyamza. Angesema, akateta, akahoji mpaka akajua mwisho. Kama wangeweza kumpelekea salamu hizo hii leo kaburini kwake wangempelekea ujumbe wa wazi kabisa: Anaweza kumleta Nyerere mwengine aje awasemee? Asaa pengine atasikilizwa kwa kuwa amemleta yeye.
Lakini sote tunajua haliwezekani. Na ndio maana kumbukumbu ya miaka kumi tokea kufa kwa Mwalimu Nyerere haina maana yoyote ile kwa wengi wa Wazanzibari – hasa wanaoona hivi hivi kuwa nchini mwao wenyewe haki ya kupiga kura haiwezi kupatikana na kwa hivyo kuchagua na kuchaguliwa ni dhana tu kwao lakini haina mashiko.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment