Monday 12 May 2014

MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI OFISI YA MAKAMO WA RAIS


MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO), MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.) KUHUSU MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO) KWA MWAKA 2014/2015

(Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2013)
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Mwaka huu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefikisha umri wa nusu karne tangu ilipozaliwa tarehe 26 Aprili, 1964. Kama anavyosema Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda katika hotuba yake ya tarehe 7 Mei, 2014 ‘Kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2014/2015’: “Miaka 50 kwa lugha yoyote ile siyo kipindi kifupi.” Waziri Mkuu ametumia takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 zinazoonyesha
kwamba asilimia 90.6 ya Watanzania wote “wamezaliwa ndani ya Muungano na nchi wanayoifahamu ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Kwa maneno ya Waziri Mkuu, “sote tunawajibika kuwatendea haki watu hawa kwa kuulinda, kuuimarisha na kuudumisha Muungano wetu.”
Mheshimiwa Spika,
Kama ilivyo kwa Watanzania wengine wengi, na mimi pia nimezaliwa ndani ya Muungano. Ninaamini kwamba ukweli huu unawahusu pia waheshimiwa wabunge wengi waliomo ndani ya Bunge hili tukufu. Na sisi pia tunaomba kutendewa haki kuhusu Muungano huu. Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, haki tunayoomba Page 2 of 27 kutendewa ni moja tu: kuambiwa ukweli juu ya Muungano huu na historia yake, hali yake ya sasa na mwelekeo wake wa baadaye. Haki tunayoomba kutendewa ni kwa watawala kuacha propaganda na uongo juu ya Muungano na kutuambia ukweli wote juu ya Muungano huu. Bob Marley, aliyekuwa mwanamuziki mpigania uhuru wa watu weusi maarufu kutoka Jamaica, aliwahi kusema katika wimbo wake ‘Get Up, Stand UP, Stand Up For Your Rights’ (‘Amkeni, Simameni, Simameni kwa Haki Zenu’) kwamba: “You can fool some people some time, but you cannot fool all the people all the time”, yaani, unaweza kuwadanganya baadhi ya watu kwa muda fulani, lakini huwezi kuwadanganya watu wote kwa muda wote! Baada ya nusu karne ya uongo na propaganda kuhusu Muungano huu, Watanzania wa kizazi hiki cha Muungano wanataka ukweli. Na Watanzania hawa hawataulinda, wala kuuimarisha au kuudumisha Muungano huu endapo wataendelea kudanganywa au kufichwa ukweli juu ya mambo mengi yanayouhusu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Spika, sisi kizazi cha Muungano tunahitaji kutendewa haki: acheni propaganda na uongo kuhusu Muungano huu ndipo muweze kutuambia tuulinde, tuuimarishe na tuudumishe!



SHEREHE ZA MUUNGANO NA ‘WAASISI’ WA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Sherehe za Miaka 50 ya Muungano ni mahali pazuri pa kuanzia kudai ukweli juu ya Muungano huu. Mtu yeyote anayetembea sasa katika Barabara ya Nyerere kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere hadi katikati ya jiji la Dar es Salaam; au Barabara ya Ali Hassan Mwinyi kuanzia Morocco hadi katikati ya jiji, ataona kila mlingoti wa taa za barabarani umepambwa kwa picha za Waasisi rasmi wa Muungano, yaani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, wakiwa
katika matukio mbali mbali ya siku za mwanzo za Muungano. Page 3 of 27

Picha hizo za Waasisi hao pia zimepambwa karibu kila mahali katika barabara za katikati ya Eneo Kuu la Kibiashara (CBD) la Jiji la Dar es Salaam. Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Zanzibar,
barabara zote kuu za Mji wa Zanzibar, ikiwamo ile inayotoka Mji Mkongwe kupitia Ikulu ya Zanzibar hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, hakuna picha hata moja ya Waasisi wa Muungano katika matukio yanayoonyeshwa kwenye picha zilizoko Dar es Salaam. Badala yake, barabara hizo zimepambwa kwa picha za Marais wa Zanzibar toka Mapinduzi ya mwaka 1964 hadi wa sasa. Ni ndani ya eneo la wageni maarufu (VIP) pekee ndio kuna picha moja ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume. Hii ni katika wiki ambayo Muungano huu umeadhimisha miaka hamsini tangu kuzaliwa kwake!
Kwa jinsi ambavyo tangu mwaka huu uanze Watanzania tumepigwa propaganda za kila aina juu ya Muungano na TBC na vyombo vingine vya habari vya serikali na vya binafsi, kukosekana kwa dalili yoyote ya sherehe za Muungano kwa upande wa Zanzibar wakati wa kilele cha sherehe hizo kunatilia shaka juu ya
uimara wa misingi ya Muungano wenyewe. Hii ndio kusema kwamba pengine kuna ukweli katika hitimisho la Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwamba Tanganyika ndiyo imevaa koti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na pengine ndio maana Muungano huu haujawahi kuungwa mkono Zanzibar kwa kiasi
ambacho wanaopenda kutuaminisha vinginevyo wamekuwa wakidai. Aidha, pengine ndio maana hata picha za kuchanganya udongo zinazoonyeshwa na TBC kila kukicha zinamwonyesha Mwalimu Nyerere akichanganya udongo peke yake, wakati Sheikh Karume haonekani kabisa!
Mheshimiwa Spika,
Kuna jambo lingine linalofikirisha sana kuhusu picha hizi za
Sherehe za Miaka Hamsini ya Muungano zilizopamba mitaa ya Page 4 of 27

Dar es Salaam. Baadhi ya picha hizo zinawaonyesha watu wengine ambao wamefutwa kabisa katika historia rasmi wanayofundishwa watoto wetu mashuleni na vyuoni. Hivyo, kwa mfano, katika picha maarufu ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume wakisaini Hati za Makubaliano ya Muungano wapo pia, kwa upande wa Tanganyika, Oscar Kambona, Bhoke Munanka na Job Lusinde, wakati kwa upande wa Zanzibar wanaoonekana kwenye picha hiyo ni Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Ali Mwinyigogo. Aidha, kuna picha inayowaonyesha Mwalimu Nyerere, Sheikh Karume na Kassim Hanga wakitabasamu kwa
furaha kubwa.
Katika kitabu chake Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru! Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia kilichochapishwa mwaka 2010, Harith Ghassany ameonyesha jinsi ambavyo Oscar Kambona, Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Saleh Saadalla Akida walitoa mchango mkubwa katika kufanikisha Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964, na baadaye kufanikisha Muungano na Tanganyika wa Aprili 26 ya mwaka huo. Katika kitabu chake The Partner-ship: Muungano wa Tanganyika na Zanzibar: Miaka 30 ya
Dhoruba, Rais wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Alhaj Aboud Jumbe ameeleza kwamba ni Kambona, Bhoke Munanka na Job Lusinde ndio waliompelekea Sheikh Karume nakala za Hati
ya Makubaliano ya Muungano kabla ya Hati hizo kusainiwa tarehe 22 Aprili, 1964.
Mheshimiwa Spika,
Swali kuu ambalo sisi tuliozaliwa ndani ya Muungano tunataka lijibiwe kwa ukweli kabisa ni ‘waasisi’ hawa wengine wa Muungano, akina Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Saleh Saadalla Akida kwa upande wa Zanzibar; na Oscar Kambona, Bhoke Munanka na Job Lusinde kwa upande wa Tanganyika walipotelea wapi na kwanini hawatajwi katika historia rasmi ya Muungano na waasisi wake? Kassim Hanga alikuwa Waziri Mkuu na baadaye Makamu wa Rais wa Serikali ya Page 5 of 27

Mapinduzi ya Zanzibar; wakati Twala alikuwa Waziri wa Fedha wa Serikali hiyo na Saleh Saadalla alikuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi. Kwa upande wa Tanganyika, Oscar Kambona alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wakati wa Mapinduzi ya Zanzibar na baadaye wakati wa kuzaliwa kwa Muungano; Bhoke Munanka alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais mwenye dhamana ya masuala ya usalama, na Job Lusinde alikuwa Waziri wa Serikali za Mitaa. Katika Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!, Ghassany ameonyesha jinsi ambavyo akina Hanga, Twala na Saadalla pamoja na viongozi wengine waandamizi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kama vile Othman Shariff, Mdungi Ussi na Jaha Ubwa waliuawa na kuzikwa katika handaki moja katika sehemu inayoitwa Kama, nje kidogo ya mji wa Zanzibar. Sisi wa kizazi cha
Muungano tunataka kujua ukweli juu ya makosa waliyoyafanya hawa waasisi wa Muungano hadi wakauawa na kuzikwa katika kaburi au handaki moja. Tunataka kujua ukweli kama walifanya makosa walishtakiwa katika mahakama gani iliyowahukumu adhabu ya kifo. Aidha, tunataka kuambiwa ukweli kwanini
mchango wao katika kuzaliwa kwa Muungano umefichwa kwa muda wote wa nusu karne ya Muungano huu. Kuhusu Oscar Kambona, inafahamika kwamba katika miaka ya mwisho ya ukoloni na miaka ya mwanzo ya uhuru, ‘mwasisi’ huyu wa Muungano alikuwa mtu wa karibu sana wa Mwalimu Nyerere.
Mwalimu Nyerere ndiye alikuwa ‘Best Man’ wa Kambona wakati wa harusi yake iliyofanyika London, Uingereza mwaka 1960. Inafahamika, hata hivyo, kwamba mwaka 1967 Oscar Kambona alikosana na Mwalimu Nyerere na akalazimika kukimbilia uhamishoni nchini Uingereza alikoishi hadi aliporudi nyumbani
wakati wa kurudishwa tena kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992. Tuliosoma miaka ya sabini na ya themanini tulifundishwa mashuleni na kuimbishwa nyimbo zilizotuaminisha kwamba Oscar Page 6 of 27
Kambona alikuwa msaliti aliyetaka kuipindua Serikali yetu tukufu. Hata hivyo, hatukuwahi kuambiwa kama alishtakiwa katika mahakama yoyote ya hapa nchini na, kama ni hivyo, kama alipatikana na hatia yoyote na kuadhibiwa na mahakama. Tunachojua ni kwamba aliporudi nyumbani mwaka 1992, Mzee Kambona hakukamatwa wala kushtakiwa kwa kosa lolote lile. Sisi tuliozaliwa ndani ya Muungano huu tunataka tutendewe haki kwa kuambiwa ukweli juu ya tuhuma za usaliti dhidi ya Mzee Oscar Kambona ambaye sasa anaandikiwa vitabu kuwa ni mmoja wa watu waliotoa mchango mkubwa katika kuzaliwa kwa Muungano huu.
KUTOLEWA KWA NYARAKA ZA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Katika maoni yake wakati wa Bunge la Bajeti la mwaka wa fedha 2012/2013, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza kwamba Serikali iweke wazi “nyaraka mbali mbali zinazohusu historia ya Muungano wetu na ‘mapito’ yake ili Watanzania waelewe masuala yote yaliyotokea yanayouhusu. Hii ni muhimu
zaidi kwa kuzingatia ukweli kwamba mataifa ya magharibi kama vile Marekani na Uingereza yalikwishatoa hadharani nyaraka za mashirika yao ya kijasusi pamoja na balozi zao za Tanzania zinazoonyesha jinsi ambavyo serikali za mataifa hayo zilihusika katika kuzaliwa kwa Muungano.” Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilifafanua kwamba “kuanikwa kwa nyaraka zilizoko katika mamlaka mbali mbali za Serikali
kutasaidia kuthibitisha au kukanusha taarifa ambazo chanzo chake ni nyaraka za kidiplomasia na kijasusi za nchi hizo kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulitokana na njama za kibeberu za kudhibiti ushawishi wa siasa za kimapinduzi za Chama cha Umma na viongozi wake ndani ya Baraza la Mapinduzi
Zanzibar la wakati huo. Aidha, nyaraka hizo zitatoa mwanga juu ya kilichowasibu viongozi waandamizi wa chama hicho ambao Page 7 of 27 bila uwepo wao kutambuliwa rasmi, historia ya Mapinduzi ya
Zanzibar na ya Muungano inabaki pungufu.” Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilisisitiza juu ya haja ya taifa letu kuambiwa ukweli juu ya Muungano huu: “... Miaka karibu hamsini ya Muungano ni umri wa kutosha kwa taifa la Tanzania kuambiwa ukweli wote juu ya kuzaliwa kwake na mapito ambayo limepitia katika kipindi hicho.” Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilirudia wito wake huo wakati wa kuwasilisha maoni yake juu ya Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais mwaka jana.
Mheshimiwa Spika,
Mjadala juu ya nyaraka za Muungano huu ulichukua picha mpya wakati wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba walipohoji uwepo wa Hati ya Makubaliano ya Muungano na uhalali wa Muungano wenyewe wakati wa mjadala juu ya Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba. Baada ya wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne kuonyesha ushahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haijawahi kuwa na nakala ya Hati hiyo, na kwamba haijawahi kupelekwa na kusajiliwa katika Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa, Serikali hii ya CCM ililazimika kutoa kile ilichokiita nakala ya Hati ya Makubaliano ya Muungano.
Hatuhitaji kuzungumzia tofauti kubwa ya sahihi ya Sheikh Karume iliyoko kwenye Hati hiyo na sahihi ya Sheikh Karume iliyoko katika Sheria mbali mbali alizosaini kama Rais wa Zanzibar na wakati mwingine kama kaimu Rais wa Jamhuri ya Muungano. Cha muhimu ni kwamba mgogoro juu ya Hati ya Makubaliano ya Muungano unathibitisha ukweli kwamba matokeo ya utamaduni huu wa kufichaficha nyaraka muhimu za nchi ni kwa wananchi kukosa imani na serikali iliyoko madarakani, kwa kuwa wananchi wanajenga hisia kwamba nyaraka hizo zinafichwa kwa sababu zina ushahidi wa maovu yaliyofanywa na serikali hiyo.
Kwa sababu hizi zote, kwa mara nyingine tena, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM kutoa nyaraka za Page 8 of 27
Muungano huu hadharani ili Watanzania waweze kuelewa historia halisi ya Muungano badala kuendelea kulishwa propaganda na TBC na kwenye majukwaa ya kisiasa ya CCM na Serikali yake! Vinginevyo, chochote kitakachosemwa na TBC na watawala katika majukwa yao ya kisiasa kuhusu Muungano huu
hakitaaminika tena na wananchi wa Tanzania.

KIELELEZO CHA UMOJA NA MSHIKAMANO AU UNYONYAJI WA
KIKOLONI?
Mheshimiwa Spika,
Katika hotuba ya Waziri Mkuu Bunge lako tukufu limeambiwa kwamba “Muungano huu ni wa kipekee na wa kupigiwa mfano duniani kote. Aidha, ni kielelezo kamili cha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi....” Ni kweli kwamba Muungano huu ni wa kipekee kwa sababu haujawahi kuigwa na
nchi nyingine zozote katika Afrika. Na kama Muungano huu ungekuwa wa ‘kupigiwa mfano duniani kote’, kama inavyodaiwa na Waziri Mkuu, basi kungekuwa na angalau nchi moja iliyoomba kujiunga katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Angalau kungekuwa na nchi zilizoiga mfano wa Muungano huu
kwingineko Afrika na duniani kote.
Kwa kuwa hakuna nchi hata moja iliyowahi kuomba kujiunga nasi, na kwa kuwa hakuna nchi nyingine zilizoiga mfano wa Muungano huu, pengine huu ni muda muafaka wa kuhoji ukweli wa kauli kwamba Muungano huu ‘ni kielelezo cha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi’ wa Tanganyika na Zanzibar.
Mzee Pius Msekwa, Mwenyekiti Mstaafu wa CCM na Spika Emeritus wa Bunge hili tukufu, aliwahi kusema katika mada yake Hali ya Muungano kwa semina iliyofanyika Tanga miaka 20 iliyopita kwamba, muundo wa sasa wa Muungano huu umepelekea wengi kuamini kwamba Muungano huu ni kiini macho tu. Page 9 of 27

Hii ni kwa sababu, chini ya Muungano huu, Zanzibar ilikabidhi sehemu muhimu ya mamlaka yake (mahusiano ya nchi za nje, ulinzi na usalama, uraia, kodi na ushuru, sarafu, nguvu kuu za kuendeshea uchumi na mengineyo) kwa Tanganyika; na kisha Tanganyika ikajigeuza jina na kujiita Jamhuri ya Muungano. Spika
Emeritus Msekwa aliongeza kwamba kwa jinsi mambo yalivyo sasa, Zanzibar inaonekana kama vile ni ‘invited guest’ (mgeni mwalikwa) katika Muungano huu. Naye msomi mashuhuri wa Kiafrika, Profesa Ali A. Mazrui katika makala yake ‘Imperialism after the Empire: Lessons from Uganda and Tanzania’, yaani ‘Ubeberu Baada ya Himaya: Funzo Kutoka Uganda na Tanzania’, iliyochapishwa katika gazeti la Kenya, The
Sunday Nation, la Mei 22, 1994, alisema kwa sababu ya Muungano, Zanzibar imepoteza kila kitu chake muhimu, wakati
Tanganyika imebadilika jina tu na kuwa Tanzania, huku ikiwa na
mamlaka zaidi lakini ikibaki na Rais wake, nembo yake ya Taifa,
wimbo wake wa Taifa na hata kiti chake katika Umoja wa
Mataifa. Kama tunavyoonyesha katika Maoni haya, gharama ya
kuyapuuza maneno haya ya watu hawa wazito imekuwa kubwa
kweli kweli, hasa kwa Zanzibar.

MISAADA NA MIKOPO YA KIBAJETI
Mheshimiwa Spika,
Ushahidi wa nyaraka ambazo zimewasilishwa kwenye Bunge lako
tukufu na Serikali hii ya CCM unaonyesha kwamba Muungano
huu ni kielelezo cha unyonyaji na ukandamizaji mkubwa ambao
nchi ndogo ya Zanzibar imefanyiwa na nchi kubwa ya
Tanganyika. Ni mfano wa jinsi ambavyo nchi moja kubwa ya
Kiafrika inaweza kuigeuza nchi nyingine ndogo ya Kiafrika kuwa
koloni lake. Kwa sababu maneno haya yanaweza kupotoshwa na
wale ambao wamefaidika na uhusiano huu wa kikoloni kati ya
Tanganyika na Zanzibar naomba kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo. Page 10 of 27

Kwa miaka mingi Zanzibar imelalamika kwamba inapunjwa katika
mgawanyo wa mapato yanayotokana na fedha zinazotolewa na
nchi wafadhili na taasisi za kimataifa kwa Jamhuri ya Muungano.
Kwa sababu ya malalamiko hayo, mwaka jana Kamati ya
Kudumu ya Bunge lako tukufu ya Katiba, Sheria na Utawala
iliiagiza Ofisi ya Makamu wa Rais kwamba: “Utaratibu wa
mgawanyo wa mapato yanayotokana na fedha zinazotoka kwa
wafadhili ni vyema ukaangaliwa upya kwa Serikali zote mbili yaani
SMZ na SMT.” Aidha, Kamati ilishauri kwamba “Serikali itolee
uamuzi mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha
yaliyowasilishwa Serikalini tangu mwaka 2006 na kuwasilishwa
tena mwaka 2010 kuhusu utaratibu wa mgao wa fedha za Serikali
zote mbili.”
Serikali hii ya CCM imejibu maagizo haya ya Kamati kama
ifuatavyo: “Serikali zetu mbili bado zinaendelea kushughulikia
mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Pamoja ya Fedha. Aidha,
kuhusu mgawanyo wa fedha zinazotoka kwa wafadhili, upo
utaratibu wa mgawanyo wake ambapo, kwa upande wa
misaada na mikopo ya kibajeti isiyokuwa na masharti maalum,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ... hupata gawio la asilimia 4.5.”
Mheshimiwa Spika,
Kauli hii ya Serikali ni ya uongo. Katika maelezo yake mbele ya
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais, Muungano, aliitaarifu Kamati kwamba “Kwa
mwaka wa fedha 2013/14, hadi kufikia mwezi Machi, 2014 SMZ
imepata Gawio la Misaada ya Kibajeti (General Budget Support –
GBS) shilingi 27,190,502,190.97/= kati ya shilingi 32,627,535,000/=
zilizoidhinishwa na Bunge.” Hii ndio kusema kwamba kati ya fedha
zilizoidhinishwa na Bunge lako tukufu kama gawio la misaada na
mikopo ya kibajeti kwa Zanzibar, ni asilimia 83 ndizo zilizolipwa
hadi kufikia robo ya tatu ya mwaka huu wa fedha. Page 11 of 27

Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, hili sio tatizo, kwani kwa mwelekeo
wa takwimu hizi, hadi kufikia mwisho wa mwaka huu wa fedha,
gawio lililoidhinishwa na Bunge lako tukufu linaweza kuwa
limelipwa lote. Tatizo kubwa na la msingi ni kwamba gawio
lililoidhinishwa na Bunge hili tukufu sio gawio halali kwa Zanzibar.
Hii kwa sababu, kwa mujibu wa Maelezo ya Waziri wa Fedha
Mheshimiwa Saada Mkuya Salum (MB.) Akiwasilisha
Mapendekezo ya Mfumo wa Mapato na Matumizi ya Serikali kwa
Mwaka 2014/15 kwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, ya tarehe 30 Aprili, 2014, mapato halisi
ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano yanayotokana na misaada
na mikopo nafuu ya nje ilikuwa shilingi bilioni 1,163 au trilioni 1.163.
Kama Zanzibar ingepatiwa asilimia 4.5 ya mapato hayo, kama
inavyotakiwa kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na Serikali hii ya
CCM, basi kwa mwaka jana peke yake, gawio halali la Zanzibar la
misaada na mikopo ya kibajeti lingekuwa shilingi bilioni 52.335.
Badala ya kupatiwa shilingi bilioni 52.335 ambazo ni fedha zake
halali, Zanzibar iliidhinishiwa shilingi bilioni 32.627 au asilimia 52 ya
fedha zake halali. Fedha hizo ni sawa na asilimia 2.8 ya fedha zote
za misaada na mikopo ya kibajeti kwa Jamhuri ya Muungano.
Fedha zilizobaki, yaani shilingi trilioni 1.130 au asilimia 97.2 ya fedha
zote za misaada ya kibajeti zimetumika na zitatumika Tanganyika.
Kwa ushahidi huu wa nyaraka za Serikali hii ya CCM, kwa sababu
ya Muungano huu, kwa mwaka jana peke yake Zanzibar iliibiwa
shilingi bilioni 25.145 au asilimia 48 ya fedha zake halali za gawio la
misaada na mikopo ya kibajeti.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mapendekezo yaliyoletwa kwenye Bunge lako tukufu na
Serikali hii ya CCM, Zanzibar itaibiwa fedha nyingi zaidi kwa
mwaka huu wa fedha 2014/15. Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa
maelezo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano,
kwa mwaka huu wa fedha, “fedha zitakazokwenda SMZ
zinajumuisha shilingi 21,639,608,000.00 mgao wa misaada ya Page 12 of 27 kibajeti....” Kwa upande mwingine, kwa mujibu wa Maelezo ya Waziri wa Fedha, ‘misaada na mikopo ya kibajeti’ kwa mwaka
huu wa fedha itakuwa shilingi bilioni 992.170. Hii ina maana
kwamba kwa mwaka huu wa fedha, Zanzibar itapata asilimia 2.18
tu ya fedha za misaada na mikopo ya kibajeti. Hii inaonyesha pia
kwamba, kwa mwaka huu, fedha za misaada na mikopo ya
kibajeti ambazo zitabaki na kutumika Tanganyika ni shilingi bilioni 970.531 au asilimia 97.82 ya fedha hizo.Kama Serikali hii ya CCM ingeheshimu utaratibu wake wa asilimia 4.5 ya fedha hizo kwa Zanzibar, gawio halali la Zanzibar kutokana na fedha za misaada na mikopo ya kibajeti kwa mwaka ujao wa fedha lingekuwa shilingi bilioni 44.647! Kwa maana hiyo, Serikali hii ya CCM inapendekeza kuilipa Zanzibar asilimia 48.47 ya fedha zake alali. Endapo Bunge lako tukufu litapitisha mapendekezo haya kama inavyoombwa na Serikali hii ya CCM, Zanzibar itaibiwa shilingi bilioni 23 au asilimia 51.53 ya fedha zake halali kwa
mwaka ujao wa fedha.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM ilieleze Bunge lako tukufu na iwaeleze Watanzania, na hasa
Wazanzibari, kwa nini fedha halali za Zanzibar kutokana na
misaada na mikopo ya kibajeti inayokuja kwa jina la Jamhuri ya
Muungano hazijalipwa kwa mwaka jana wa fedha. Aidha, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM ilieleze
Bunge lako tukufu na iwaeleze Watanzania, na hasa Wazanzibari,
kwa nini inapendekeza kuipatia Zanzibar pungufu ya fedha zake
halali kama gawio la misaada na mikopo ya kibajeti kwa mwaka
huu wa fedha.Vile vile, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM ilete mbele ya Bunge lako tukufu takwimu za fedha zote zilizopokelewa na Serikali kama misaada na mikopo ya kibajeti kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita na sehemu ya fedha hizo Page 13 of 27

zilizolipwa kwa Zanzibar kama gawio lake katika kipindi hicho.
Takwimu hizo ni muhimu ili Watanzania, na hasa Wazanzibari,
waweze kufahamu kama Zanzibar imekuwa ikipata sehemu yake
halali ya mapato ya Jamhuri ya Muungano yanayotokana na
misaada na mikopo ya kibajeti. Mwisho, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inalitaka Bunge lako tukufu kuunda Kamati Teule ya
Bunge hili itakayochunguza mgawanyo wa mapato
yanayotokana na misaada na mikopo ya kibajeti kati ya
Tanganyika na Zanzibar ili kupata ukweli juu ya uhalali wa malipo
ya mapato hayo kwa Zanzibar.
MISAADA NA MIKOPO ISIYOKUWA YA KIBAJETI
Mheshimiwa Spika,
Misaada na mikopo ya kibajeti sio eneo pekee ambapo Zanzibar
inanyonywa na Tanganyika kwa sababu ya Muungano huu.
Ukweli ni kwamba hali ni mbaya zaidi kuhusiana na fedha za
misaada na mikopo isiyokuwa ya kibajeti. Hapa pia takwimu za
Serikali hii ya CCM zinatisha na kusikitisha. Hivyo, kwa mfano, kwa
mujibu wa Maelezo ya Waziri wa Fedha, kwa mwaka wa fedha
2013/14 fedha za nje kwa ajili ya miradi ya maendeleo
zikijumuisha misaada na mikopo ya Basket Fund na misaada na
mikopo ya miradi zilikuwa shilingi trilioni 2.692 au bilioni 2,692.
Fedha hizi zote zilitumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya
Tanganyika. Hapa Zanzibar haikupata kitu chochote!
Maelezo ya Waziri wa Fedha yanaonyesha kwamba kwa mwaka
wa fedha 2014/15, misaada na mikopo isiyokuwa ya kibajeti
kutoka nje inatazamiwa kuwa shilingi bilioni 2,019.43 au trilioni
2.019. Hizi zote ni fedha zitakazotumika kwa ajili ya miradi ya
maendeleo ya Tanganyika. Hapa pia Zanzibar haitapata kitu
chochote. Ni muhimu kwa Bunge lako tukufu kukumbuka
kwamba, kwa sababu ya Muungano huu, Zanzibar
imenyang’anywa mamlaka ya kuomba mikopo au misaada
kutoka nje bila kwanza kupata kibali cha Wizara ya Fedha ya Page 14 of 27

Jamhuri ya Muungano, aka Wizara ya Fedha ya Tanganyika. Sisi
tuliozaliwa ndani ya Muungano tunataka kujua unyonyaji na wizi
huu wa fedha za Wazanzibari utakomeshwa lini. Aidha, sisi tulio
kizazi cha Muungano huu tunataka kuambiwa kama mgawanyo
wa aina hii wa mapato yanayokuja kwa jina la Jamhuri ya
Muungano ndio kielelezo cha umoja, mshikamano na upendo
miongoni mwa wananchi wa Tanganyika na Zanzibar ulioletwa na
Muungano huu.
Mheshimiwa Spika,
Sio tu kwamba Zanzibar haipati stahili yake ya mapato
yanayopatikana kwa jina la Jamhuri ya Muungano kutoka vyanzo
vya nje, bali pia fedha zinazopatikana kutokana na mambo ya
Muungano zinatumika kwa mambo yasiyo ya Muungano ya
Tanganyika. Moja ya matokeo ya mjadala wa katiba wa mwaka
1983/84 uliopelekea ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa
Zanzibar’ na kung’olewa madarakani kwa Alhaj Aboud Jumbe ni
kuingizwa kwa Sura ya Saba inayohusu ‘Masharti Kuhusu Fedha za
Jamhuri ya Muungano’ katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, 1977.
Kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Tano ya Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1984, ibara
mpya ya 133 ya Katiba iliweka masharti kwamba “Serikali ya
Jamhuri ya Muungano itatunza ‘Akaunti ya Pamoja ya Fedha ...
ambamo kutawekwa fedha yote itakayochangwa na Serikali
mbili kwa kiasi kitakachoamuliwa na Tume ya Pamoja ya Fedha ...
kwa madhumuni ya shughuli za Jamhuri ya Muungano kwa
Mambo ya Muungano.”
Aidha, ibara ya 134 iliweka masharti ya kuwa na Tume ya Pamoja
ya Fedha yenye majukumu ya “kuchambua mapato na matumizi
yanayotokana na, au yanayohusu utekelezaji wa Mambo ya
Muungano na kutoa mapendekezo kwa Serikali mbili kuhusu
mchango na mgawo wa kila mojawapo ya Serikali hizo.” Page 15 of 27

Majukumu mengine ya Tume hiyo ni “kuchunguza ... mfumo wa
shughuli za fedha kwa Jamhuri ya Muungano na pia uhusiano
katika mambo ya kifedha kati ya Serikali mbili.”
Mheshimiwa Spika,
Kwa miaka thelathini tangu kupitishwa kwa Mabadiliko ya Tano
ya Katiba, masuala ya Tume ya Pamoja ya Fedha na Akaunti ya
Pamoja ya Fedha yamekuwa mojawapo ya kile kinachoitwa
‘Kero za Muungano’ ambayo ufumbuzi wake umeshindikana.
Kwa mfano, licha ya Katiba kuelekeza kuundwa kwa Tume ya
Pamoja ya Fedha, sheria ya kuunda Tume hiyo, yaani Sheria ya
Tume ya Pamoja ya Fedha, ilipitishwa miaka kumi na mbili
baadaye, yaani mwaka 1996.
Baada ya hapo Tume yenyewe iliundwa rasmi mwaka 2003, yaani
miaka saba baada ya kutungwa kwa sheria na miaka 19 tokea
Katiba iweke masharti ya kuundwa kwa Tume hiyo. Kwa upande
wa Akaunti ya Pamoja ya Fedha, leo ni mwaka wa thelathini
tangu Katiba kuelekeza Akaunti hiyo kufunguliwa na bado
haijafunguliwa. Kutokana na kushindikana kufunguliwa huko, kwa
miaka yote hii, bajeti ya Muungano imekuwa ndio bajeti ya
Tanganyika, kinyume na maelekezo ya Katiba.
Mwaka 2006 Tume ya Pamoja ya Fedha iliajiri wataalamu
waelekezi kutoka kampuni kimataifa ya uhasibu ya
PriceWaterhouseCoopers kuangalia suala la gharama na
mgawanyo wa fedha za Muungano. Wataalamu hao walifanya
uchambuzi halisi wa mambo yapi ni ya Muungano na yapi ni ya
Tanganyika na yapi ni ya Zanzibar na gharama za uendeshaji wa
kila moja. Baada ya orodha kupatikana, watafiti hao walitafuta
matumizi halisi ya bajeti ya vifungu hivyo kwa muda wa kiasi cha
miaka 10 iliyopita.
Watafiti wa PriceWaterhouseCoopers walikwenda mbali zaidi ya
hapo na kukusanya mapato yote kwa kila kifungu cha mambo ya Page 16 of 27

Muungano halisi. Mwishowe, wakalinganisha iwapo mapato hayo
yanakidhi matumizi ya Muungano au yana upungufu. Taarifa ya
uchambuzi wa PriceWaterhouseCoopers ilitolewa kama
Mapendekezo ya Tume Kuhusu Vigezo vya Kugawana Mapato
na Kuchangia Gharama za Muungano ya mwezi Agosti 2006.
Taarifa ya Tume ya Pamoja ya Fedha inaonyesha hali ya
kusikitisha kuhusu mapato na matumizi ya fedha za Muungano,
hasa kwa upande wa Tanganyika. Ili kupata picha kamili ya hali
halisi ilivyo, tunaomba kunukuu sehemu ya Taarifa hiyo in extenso,
kwenye ukurasa wake wa 18: “Uchambuzi unaonyesha kuwa
mapato yanayotokana na vyanzo vya Muungano yanakidhi
matumizi ya Muungano na kuwa na ziada ya kutosha. Takwimu
zinaonyesha kuwa kiasi kidogo cha mapato hayo kimekuwa
kinagharimia matumizi ya Muungano. Kwa mfano, uwiano huu
ulikuwa ni (shilingi bilioni 360.679 kati ya (shilingi bilioni 1,030.513)
sawa na asilimia 35 mwaka 1999/2000, (shilingi bilioni 468.450) kati
ya (shilingi bilioni 1,801.733) sawa na asilimia 26 mwaka 2002/03,
na (shilingi bilioni 636.078) kati ya (shilingi bilioni 2,271.710) sawa na
asilimia 28 mwaka 2003/04.
“Uchambuzi unaonyesha kuwa kiasi kikubwa cha ziada ya
mapato ya Muungano kimekuwa kinatumika kugharimia mambo
yasiyo ya Muungano. Viwango hivi kwa mwaka 1999/2000
vilikuwa ni (shilingi bilioni 39.822) sawa na asilimia 5.9 kwa (Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar) na (bilioni 631.714) sawa na asilimia 94.1
kwa Tanzania Bara. Viwango hivi vilibadilika kwa kiasi kikubwa
kwa mwaka wa fedha 2003/04 ambapo kwa (Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar) kilishuka hadi (shilingi bilioni 37.053) sawa na
asilimia 2.3, na (shilingi bilioni 1,588.494) sawa na asilimia 97.7 kwa
(Serikali ya Muungano wa Tanzania).”
Takwimu za utafiti wa PriceWaterhouseCoopers zinaonyesha
kwamba kwa mwaka wa fedha 2003/2004 pekee, matumizi halisi
kwa vifungu vya Muungano yalikuwa shilingi bilioni 537.258
ambayo ni asilimia 20 tu ya bajeti yote ya Serikali ya Muungano
kwa mwaka huo. Mapato halisi ya vyanzo vya mapato Page 17 of 27

vinavyotokana na mambo ya Muungano kwa mwaka huo
yalikuwa ni shilingi bilioni 1,030.826, au takriban shilingi trilioni 1.030.
Kwa maana nyingine, mapato na matumizi ya fedha
zinazotokana na vyanzo vya mambo ya Muungano yaliacha
ziada ya shilingi bilioni 493.567 kwa mwaka huo mmoja. Ziada hii ni
nje ya mapato yaliyotokana na misaada na mikopo kutoka nje,
na ilitumika kwa shughuli za maendeleo za Tanganyika zisizo za
Muungano.
Kwa sababu Tanganyika imekuwa inafaidika sana na utaratibu
huu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano - ambayo kiuhalisia ni
Serikali ya Tanganyika iliyovaa joho la Muungano – imekataa
kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha kwamba
uwekwe utaratibu utakaowezesha kutenganisha mapato na
matumizi ya Muungano na yasiyo ya Muungano. Miaka nane
tangu mapendekezo hayo yatolewe mwaka 2006, “Serikali zetu
mbili”, kwa maneno ya Mh. Samia Suluhu Hassan, “bado
zinaendelea kushughulikia mapendekezo yaliyotolewa na Tume
ya Pamoja ya Fedha.”
Mheshimiwa Spika,
Kero nyingine kubwa ya Muungano huu na ambayo ina umri
karibu sawa na Muungano wenyewe inahusu hisa za Zanzibar
zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki kabla ya Bodi
hiyo kuvunjwa mwaka 1965 na Benki Kuu ya Tanzania kuanzishwa.
Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri Suluhu Hassan, hisa za Zanzibar
katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki ni mojawapo ya “kero
zilizobaki katika orodha ya mambo ya kutafutiwa ufumbuzi....”
Kufuatana na maelezo hayo, “masuala ya Bodi ya Sarafu ya
Afrika Mashariki na mgawanyo wa faida ya Benki Kuu yapo katika
ngazi ya Mawaziri wa Fedha wa (Serikali ya Jamhuri ya
Muungano) na (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) kwa hatua za
majadiliano.” Page 18 of 27

Alipohojiwa juu ya hisa za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika
Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki mwezi Januari 2013, Waziri huyo
huyo aliiambia Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala kwamba:
“Katika Kikao cha Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ ya
Kushughulikia Masuala ya Muungano kilichofanyika tarehe 14
Januari 2013 imeelezwa kwamba Mawaziri wa Fedha wa SMT na
SMZ wamepatiwa nyaraka maalum zenye taarifa za siri na
wamekubaliana kujadili suala hili mwezi Februari, 2013 baada ya
kuzipitia nyaraka hizo.” Kwa vile bado mawaziri wanajadiliana,
kama tulivyosema mwaka jana, “sio tu kwamba Wazanzibari
hawajui ni kiasi gani cha fedha zao zilichukuliwa na Serikali ya
Jamhuri ya Muungano kufuatia kuvunjwa kwa Bodi ya Sarafu ya
Afrika Mashariki, bali pia hawana uhakika watazirudishiwa lini!”
Mheshimiwa Spika,
Kwa vile fedha za Zanzibar katika Bodi ya Sarafu zilichukuliwa na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano baada ya masuala ya fedha,
sarafu na Benki Kuu kufanywa kuwa mambo ya Muungano
mwaka 1965, sisi tuliozaliwa ndani ya Muungano tuna haki ya
kuambiwa ukweli kwanini Serikali hii ya CCM imeshindwa
kurudisha fedha hizo kwa Wazanzibari kwa takriban miaka hamsini
tangu fedha hizo zinyakuliwe na Serikali ya Jamhuri ya Muungano
aka Serikali ya Tanganyika? Tunahitaji kuelezwa Serikali hii ya CCM
inahitaji muda wa miaka mingapi mingine ili iweze kurudisha
fedha za watu na kuwaepusha Watanganyika na laana ya wizi
wa fedha za Wazanzibari?
Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar au Wazanzibari wenyewe katika umoja wao,
wana haki ya kutumia njia yoyote ile watakayoona inafaa,
ikiwamo kufungua kesi za madai katika mahakama za ndani au
mahakama za kimataifa, kudai fedha zake zote halali ambazo
zimeibiwa na Tanganyika kwa kutumia kivuli cha Muungano
katika kipindi chote cha miaka hamsini ya Muungano huu. Page 19 of 27

Mheshimiwa Spika,
Kwa vyovyote vile, takwimu hizi zinaonyesha kwamba, kwa
sababu ya Muungano huu, uhusiano kati ya Tanganyika na
Zanzibar ni uhusiano wa kinyonyaji. Kwa sababu hiyo, huu ni
uhusiano wa kikoloni. Ni uhusiano kati ya ‘himaya’ ya Tanganyika
na ‘koloni’ lake la Zanzibar. Himaya za kikoloni huwa zinadhibiti
masuala yote ya ulinzi na usalama, mambo ya nje na uhusiano
wa kimataifa, uraia, kodi, fedha, sarafu na benki kuu ya makoloni
yao. Na himaya za kikoloni huwa zinatumia nguvu na udhibiti wao
wa masuala haya kuyanyonya makoloni yao kiuchumi,
kuyadidimiza kijamii na kuyatawala kisiasa. Hivi ndivyo ambavyo
imekuwa kwa mahuasiano kati ya Tanganyika na Zanzibar tangu
kuzaliwa kwa Muungano huu tarehe 26 Aprili, 1964.
Mheshimiwa Spika,
Tarehe 20 Aprili, 1968, Mwalimu Nyerere alisema yafuatayo wakati
akihojiwa na gazeti la The Observer la London, Uingereza: “If the
mass of the people of Zanzibar should, without external
manipulation, and for some reason of their own, decide that the
Union was prejudicial to their existence, I could not bomb them
into submission.... The Union would have ceased to exist when the
consent of its constituent members was withdrawn.” Yaani,
“endapo umma wa wananchi wa Zanzibar wataamua, bila
kurubuniwa kutoka nje na kwa sababu zao wenyewe, kwamba
Muungano unaathiri kuendelea kuwepo kwao, sitaweza
kuwalazimisha kwa kuwapiga mabomu.... Muungano
hautaendelea kuwepo pale ridhaa ya washirika wake
itakapoondelewa.”
Miaka 45 baada ya kauli hiyo ya Mwalimu Nyerere, Maalim Seif
Shariff Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema
yafuatayo katika Maoni aliyoyatoa kwa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba tarehe 13 Januari, 2013: “Mfumo (wa Muungano) uliopo
sasa hauinufaishi Zanzibar na hivyo haukubaliki kwa Wazanzibari. Page 20 of 27

Koti la Muungano kama lilivyo sasa linabana sana. Wakati
umefika tushone koti jipya kwa mujibu wa mahitaji ya zama hizi.”
Nalo Baraza la Wawakilishi Zanzibar, katika maoni yake kwa Tume
ya tarehe 5 Februari, 2013, limetaka ‘kuwa na Muungano wa
dhati’, yaani “... Muungano wa kweli, hata kama ni kwa maeneo
machache, kwa dhati ya wanasiasa na Watanzania kwa ujumla.”
Kwa mujibu wa Baraza hilo, Muungano ‘wa dhati’ na ‘wa kweli’ ni
ule ambao kuna “... Mamlaka ya Zanzibar huru na Mamlaka ya
Tanganyika huru ndani ya Muungano, (na) Mamlaka ya
Muungano iwekwe wazi – maeneo yake, uwezo au nguvu zake,
na utendaji wake. Mambo yote hayo yawekwe wazi na mipaka
yake.”
Aidha, Baraza la Wawakilishi limependekeza kwamba “rasilmali za
Muungano ziwe ni milki ya pande mbili za Muungano; na rasilmali
hizo ndio zitumike katika uendeshaji wa Mamlaka za Muungano.
Ugawaji wa rasilmali ufanywe kwa uwiyano maalum
utakaokubaliwa kwa pamoja na pande mbili za Muungano.”
Hata kama baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
Zanzibar baadaye waliyakana maneno yao haya walipofika
mbele ya wakubwa wao wa Tanganyika wakati wa vikao vya
Bunge Maalum hapa Dodoma, haya sio maneno ya kupuuza
hata kidogo kwa sababu yanathibitisha kwamba hata wale
Watanzania wachache, kama wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
Zanzibar, ambao wamefaidika kwa kupata nafasi za uongozi kwa
sababu ya Muungano, hawauoni Muungano huu kama kielelezo
cha umoja, mshikamano na upendo wao. Kuyapuuza maneno
haya ni kujenga misingi imara na hakika ya Muungano huu
kuvunjika.
NCHI MOJA AU NCHI MBILI?
Mheshimiwa Spika, Page 21 of 27

Kuna propaganda na uongo mwingine juu ya Muungano huu
ambayo imeenezwa sana katika kipindi hiki cha nusu karne ya
uhai wake. Propaganda hii inahusu kile kilichozaliwa na Hati ya
Makubaliano ya Muungano, yaani Jamhuri ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar. Baada ya jina la Jamhuri hiyo
kubadilishwa kuwa Tanzania tarehe 28 Oktoba, 1964, ilizaliwa
dhana kwamba Makubaliano ya Muungano yaliua nchi za
Tanganyika na Zanzibar na kuanzisha ‘nchi moja’ ya Tanzania.
Dhana hii imetumika, katika miaka hamsini ya Muungano huu,
kuhalalisha ukiukwaji wa matakwa ya Makubaliano ya Muungano
kwa kutumia dhana nyingine ya ‘kuimarisha Muungano.’ Dhana
hizi mbili ndio msingi wa nyongeza zote za mambo ya Muungano,
na ndio sababu kubwa ya kuporomoka kwa uhuru na mamlaka
ya Zanzibar katika kipindi hicho.
Mheshimiwa Spika,
Dhana kwamba Hati ya Makubaliano ya Muungano iliua nchi
mbili na kuzaa nchi moja ya Tanzania ni dhana potofu na
isiyokuwa na msingi wowote katika Hati yenyewe. Kwanza, Hati ya
Makubaliano ya Muungano ilitamka wazi kwamba sheria
zilizokuwepo Tanganyika na Zanzibar kabla ya Muungano
zitaendelea kutumika ‘katika nchi zao’ hadi hapo
zitakaporekebishwa ili kutilia nguvu Muungano na Hati za
Muungano; au sheria mpya zitakapotungwa na mamlaka husika
au kutolewa kwa amri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa ajili
ya utekelezaji wa Mambo ya Muungano kwa upande wa
Zanzibar.
Pili, vifungu mbali mbali vya Katiba zilizofuatia Makubaliano ya
Muungano ziliweka wazi kwamba Tanganyika na Zanzibar
hazikuuawa na Makubaliano ya Muungano. Hivyo basi, hata
baada ya mabadiliko ya jina kwenda Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Katiba na sheria mbali mbali ziliendelea kutumia jina la
Tanganyika na Zanzibar. Kwa mfano, Sheria ya Kuongeza Muda
wa Kuitisha Bunge la Katiba, 1965, iliyosainiwa na Rais Nyerere Page 22 of 27

tarehe 24 Machi, 1965, inataja, katika vifungu vyote vitatu, ‘Sheria
za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.’
Aidha, Sheria ya Kutangaza Katiba ya Muda ya Tanzania ya
tarehe 11 Julai, 1965, ilitangaza kwamba ‘Tanzania ni Jamhuri
Huru ya Muungano’; kwamba eneo lake ni “... eneo lote la
Tanganyika na Zanzibar ...” na kwamba chama kimoja cha siasa
“... kwa Tanganyika kitakuwa Tanganyika African National Union
(TANU)....” Kwa wakati wote wa uhai wake, Katiba ya Muda
haikuwahi kutamka kuwa Tanzania ni nchi moja. Badala yake,
ibara ya 27(1) ya Katiba hiyo iliyokuwa inahusu sifa za
kuchaguliwa kuwa mbunge ilitamka wazi kwamba: “Raia yeyote
wa Tanganyika ambaye amefikisha umri wa miaka ishirini na moja
na ni mwanachama (wa TANU) atakuwa na sifa ya kuchaguliwa
kuwa mbunge wa jimbo....”
Kwa upande wake, licha ya kuanza kutumia jina la Tanzania Bara
na Tanzania Visiwani kwa mara ya kwanza, Toleo la Kwanza la
Katiba ya sasa ya Muungano lilitamka kwamba Tanzania ni
‘Jamhuri ya Muungano.’ Hapa pia hapakuwa na tamko la ‘nchi
moja.’
Mheshimiwa Spika,
Maneno ya ibara ya 1 ya Katiba ya sasa ya Muungano kwamba
“Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano” yaliingia
katika kamusi ya kikatiba na kisiasa ya nchi hii kufuatia ‘kuchafuka
kwa hali ya kisiasa ya Zanzibar’ na kung’olewa madarakani kwa
Rais Aboud Jumbe. Kufuatia hali hiyo, Katiba ya Jamhuri ya
Muungano ilifanyiwa marekebisho makubwa ambayo, pamoja
na mengine, yalitangaza kuwa “Tanzania ni nchi moja na ni
Jamhuri ya Muungano.” Kwa sababu ya upinzani mkubwa wa
Wazanzibari, Marekebisho hayo ya Katiba yaliondoa pia maneno
‘Tanzania Visiwani’ na kuweka ‘Tanzania Zanzibar’ badala yake.
Maneno ‘Tanzania Bara’ yalibaki kama yalivyowekwa mwaka
1977. Page 23 of 27

Kwa maana hiyo, dhana ya Tanzania kama nchi moja
haijatokana na Makubaliano ya Muungano bali ilitokana na siasa
za Muungano, yaani mvutano kati ya viongozi wa Tanganyika
wakiwa wamevalia joho la Jamhuri ya Muungano na viongozi wa
Zanzibar waliotaka uhuru zaidi kwa nchi yao. Pili, dhana hiyo
haina umri mkubwa sana kuliko inavyodhaniwa, kwani iliingia
kwenye Katiba mwaka 1984, miaka thelathini iliyopita, na miaka
ishirini baada ya Muungano.
MUUNGANO USIO WA USAWA
Mheshimiwa Spika,
Tangu mwanzo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar haukuwa
Muungano wa usawa. Huu ni Muungano ulioipa Tanganyika –
ikiwa imevalia koti la Jamhuri ya Muungano - mamlaka ya
kuingilia uhuru na mamlaka ya Zanzibar. Hii inathibitishwa na Hati
ya Makubaliano ya Muungano yenyewe. Kwanza, kwa kutamka
kwamba katika kipindi cha mpito “Katiba ya Jamhuri ya
Muungano itakuwa ni Katiba ya Tanganyika...”, ni wazi kwamba
Mshirika wa Muungano aliyekuwa na nguvu katika Muungano
huu ni Tanganyika.
Pili, kwa kuweka orodha ya mambo 11 ya Muungano, ni wazi
kwamba Zanzibar ilinyang’anywa mamlaka juu ya masuala hayo
na mamlaka hayo yalihamishiwa kwa Tanganyika ikiwa imevaa
koti la Jamhuri ya Muungano. Kwa maana hiyo, Zanzibar
ilinyang’anywa mamlaka yake juu ya masuala ya nchi za nje,
ulinzi, polisi, mamlaka ya hali ya hatari, uraia, uhamiaji, biashara
ya nje na mikopo na masuala mbali mbali ya kodi. Hati ya
Makubaliano ya Muungano yenyewe inasema wazi kwamba
“Bunge na Serikali (ya Jamhuri ya Muungano) litakuwa na
mamlaka kamili kwenye mambo hayo kwa Jamhuri ya Muungano
na, kwa nyongeza, mamlaka kamili kwa ajili ya mambo mengine
yote ya na kwa ajili ya Tanganyika.” Page 24 of 27

Tatu, kwa kutangaza kwamba rais wa kwanza wa Jamhuri ya
Muungano atakuwa Mwalimu Nyerere na Makamu wa kwanza
wa Rais atakuwa Sheikh Abeid Karume; na kwa kutangaza
kwamba Makamu wa Kwanza wa Rais atakuwa ndiye msaidizi
mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika utekelezaji wa
majukumu yake ya kiutendaji kuhusu Zanzibar, ni wazi kwamba
Hati ya Makubaliano ya Muungano ilithibitisha nafasi ya chini
(subordinate position) ya Zanzibar katika Muungano.
Nne, kwa kuzifanya alama za utaifa (national emblems) za
Tanganyika kuwa ndio alama za taifa za Jamhuri ya Muungano,
kuna-emphasize superior position ya Tanganyika ndani ya
Muungano na subaltern position ya Zanzibar katika Muungano
huu. Ukweli huo huo unahusu masuala ya kuzifanya taasisi na
watumishi wa Serikali ya Tanganyika kuwa ndio taasisi na
watumishi wa Jamhuri ya Muungano.
Tano, hata kwa kuangalia watu ambao wamewahi kupata fursa
ya kuongoza Jamhuri ya Muungano, ni wazi kwamba
Watanganyika ndio wamekuwa mabwana na Wazanzibari
wamefanywa watwana katika masuala ya haki za kiutawala.
Hivyo, kwa mfano, katika kipindi cha miaka hamsini ya Muungano
huu, ni Mzanzibari mmoja tu ndiye aliyepata fursa ya kuwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano, kwa miaka kumi kati ya miaka hamsini
hiyo.
Kwa utaratibu huo huo, tokea mwaka 1964, Zanzibar haijawahi
kutoa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Mkuu wa Jeshi la Polisi au
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania. Zote hizi ni taasisi za
Muungano. Aidha, Zanzibar imewahi kutoa Waziri Mkuu mmoja tu,
tena kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu, na Jaji Mkuu mmoja
tu katika kipindi hicho cha nusu karne ya Muungano huu. Vile vile,
katika Diplomatic Corps, kwa sasa kuna Wazanzibari wawili tu
ambao ni mabalozi wa Tanzania nchi za nje kati ya mabalozi 32
wanaoiwakilisha Tanzania nchi za nje. Page 25 of 27

Mheshimiwa Spika,
Hata Bunge lako tukufu lina rekodi mbaya katika masuala haya.
Hivyo, kwa mfano, katika miaka yote ya Muungano, hakuna
Mzanzibari ambaye amewahi kushikilia nafasi ya Spika au Naibu
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano. Aidha, licha ya Kanuni
za Bunge lako tukufu kuruhusu kufanyika kwa vikao vya Kamati
zake za Kudumu nje ya Dodoma, yaani Dar es Salaam na/au
Zanzibar; na licha ya Kanuni kuruhusu Mikutano ya Bunge
kufanyika nje ya Dodoma ikiwa ‘itaelekezwa vinginevyo’, hakuna
Kamati hata moja ya Bunge hili tukufu ambayo imewahi kufanya
vikao vyake Zanzibar na haijawahi kutokea Bunge hili likaelekezwa
kufanya Mikutano yake nje ya Tanganyika!
KURA YA MAONI JUU YA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Baada ya nusu karne ya Muungano wa aina hii, wananchi wa
Tanganyika na, hasa wa, Zanzibar hawako tayari kuendelea na
utaratibu huu wa kinyonyaji na kikandamizaji. Wananchi
wanataka mabadiliko ya msingi ya muundo wa Muungano na
uendeshaji wake. Wananchi wanataka kusikilizwa juu ya
Muungano. Wananchi wanataka kufanya maamuzi kuhusu kama
wanataka kuendelea na Muungano na, kama jibu ni ndiyo,
muundo wa Muungano huo.
Wakati wa mjadala wa Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya
Katiba katika Bunge Maalum, Kamati nyingi zilishindwa kufanya
maamuzi kwa sababu ya kukosa uungwaji mkono wa theluthi
mbili ya wajumbe wote wa Kamati kutoka Tanganyika na idadi
hiyo hiyo ya wajumbe kutoka Zanzibar. Kama hali ni hiyo katika
Bunge Maalum licha ya Bunge hilo kujazwa wajumbe wengi wa
CCM kutoka kundi la 201, hali ni mbaya zaidi nje ya Bunge
Maalum na nje ya Bunge lako tukufu. Nje ya mabunge haya,watu wengi, hasa Wazanzibari ambao ndio wamekuwa waathirika wakubwa wa Muungano huu katika nusu karne ya Page 26 of 27 maisha yake, wananchi wengi hawataki tayari kuendelea na Muungano huu.
Mheshimiwa Spika,
Katika mazingira haya, namna muafaka ya kutoka katika
constitutional impasse inayokuja mbele yetu, ni kuwauliza
wananchi wa Tanganyika na Zanzibar – kwa kutumia kura ya
maoni - kama bado wanataka kuendelea na Muungano huu. Na
kama jibu lao litakuwa ni ndiyo, basi wananchi waamue, katika
kura hiyo, ni muundo gani wa Muungano wanautaka. Miaka
hamsini ya watawala kuamua masuala haya muhimu peke yao
inatosha. Huu ni wakati muafaka kwa wananchi kufanya
maamuzi haya makubwa kwa maisha yao na kwa nchi zao mbili.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawataka wabunge wa Bunge
lako tukufu wawe kwenye upande sahihi wa historia, yaani
upande wa wananchi katika jambo hili.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
Katika kuhitimisha maoni haya, napenda kuchukua fursa hii
kuwashukuru na kuwapongeza viongozi wakuu wa vyama vyetu
vitatu vinavyounda Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa
kufanya maamuzi ya kuendeleza ushirikiano ulioanzia ndani ya
Bunge Maalum, kwenye Bunge lako tukufu. Wananchi wetu
wanataka mabadiliko ya msingi ya utawala wa nchi zetu mbili na
usimamizi wa rasilmali zake. Kama ilivyokuwa kwa Umoja wa
Katiba ya Wananchi (UKAWA) ndani ya Bunge Maalum, ndivyo
wananchi wanavyotutazamia kuendesha shughuli zetu ndani ya
Bunge hili tukufu. Historia itatuhukumu vikali endapo tutashindwa
kukamata fursa hii ya kihistoria katika nchi zetu mbili.
Baada ya maelezo haya marefu, naomba kukushukuru na wewe
binafsi na naomba kuwasilisha.
 Page 27 of 27

---------------------------------------------------------------
Tundu Antiphas Mughwai Lissu
MSEMAJI & WAZIRI KIVULI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS
(MUUNGANO)
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI

No comments: