Thursday, 26 June 2014

Agenda ya CUF mchakato wa Katiba Mpya

Wakati viongozi wa CCM wakizunguka jimbo kwa jimbo kutetea Mfumo wa Muungano wa Serikali mbili, Chama Cha Wananchi (CUF), kimesema hakiungi mkono hata pendekezo lililotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba la kutaka Muungano wa Serikali tatu.Migongano hiyo ya kimtazamo inazidi kuliweka taifa katika umbile la mshazari, huku matumaini ya kupatikana kwa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano yakionekana kupotea kutokana na kundi la wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kukataa kuendelea kushiriki Bunge la Katiba kwa madai kuwa CCM imekuja na rasimu yake.
Hata hivyo misimamo hiyo si kwamba inaonekana kuwachanganya wananchi tu bali pia inazidisha taharuki ya wananchi kutoelewa hatima ya upatikanaji wa Katiba na mfumo upi ambao ni sahihi katika kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofikisha umri wa miaka 50.Kundi la Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd limeeleza neema, fanaka na matunda ya Muungano wa Serikali mbili kiuchumi, kisiasa, kiulinzi na kiusalama. Wakati huohuo kundi la viongozi wa CUF chini ya Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, linasisitiza kuwa lazima Zanzibar ipate mamlaka kamili ya dola. Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF Ismail Jussa Ladhu, akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Vuga, amesema CUF iliunga mkono pendekezo la Serikali tatu kama ngazi ambayo ingekisaidia chama hicho kufikia malengo ya kupatikana mamlaka kamili ya Zanzibar.Jussa anasema bila Zanzibar kupata uraia wake, hati ya kusafiria, mambo ya nje, kiti Umoja wa Mataifa, Sarafu na benki kuu, Serikali tatu hazina tija wala faida yeyote kwa Wazanzibar.
Anasema madai ya msingi ya Wazanzibari ni kupatikana kwa mamlaka huru za Tanganyika na Zanzibar.Anasema yatakapopatika masuala hayo na kubaki katika mikono ya Zanzibar kama dola kamili, Zanzibar itakapoweza kujikwamua na kupiga hatua nyingi za kiuchumi, kinyume na hali ilivyo sasa ya kuwa kama mgeni mualikwa katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.Amesisitiza kuwa lengo kuu la kukutana kwa Rais mstaafu wa Zanzibar Dk Amani Karume na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Novemba 5 mwaka 2009, licha ya kusaka maridhiano ya kisiasa na kuzika uhasama, ilikuwa ni mpango wa kuweka nguvu ya pamoja ili kuipatia Zanzibar mamlaka kamili.
Bila ya kupepesa maneno Jussa amesema kwamba kwa bahati mbaya warithi wa Dk Karume wamekuwa wakiyumba, huku wakishndwa kuungana na kudai masuala ya msingi Bila ya Wazanzibari kuungana na kusimama pamoja, madai yao hayataweza kufikiwa.assira amjibu Jussa
Akijibu mapigo ya Jussa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Jimbo la Mtoni , Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Stephen Wasira anasema kimsingi wanachokitaka CUF na viongozi wake si Muungano bali wana nia na dhamaira ya kuligawa taifa na kuvunja Muungano.Wassira anasema Muundo wa Muungano wa Serikali mbili si kioja au kituko kwani hata mataifa ya Uingereza na Marekani yana mfumo wa aina hiyo, huku wakiwa na kiti kimoja Umoja wa Mataifa .Anasema kudai kiti Umoja wa Mataifa, sarafu, uraia au Benk Kuu ni mwelekeo wa kuvunja Muungano. Akamtuhumu Jussa na wenzake kuwa ni mawakala wa mabeberu na wakoloni wanaopigania Zanzibar irejee katika mikono ya watawala waliopinduliwa mwaka 1964.
Wassira anasema mwanasiasa huyo amekuwa akikerwa na kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi kwani hata wakiwa kwenye Kamati za Bunge maalumu la Katiba ametaka siku ya Januari 12,1964 iondolewe katika orodha ya sikuu za kitaifa.
Balozi Seif anasema ikiwa wajumbe wa Ukawa wataendelea kushikilia msimamo wao wa kukataa kurudi bungeni ili kujenga nguvu ya hoja na kupatikana katiba bora, watakaopoteza turufu na kupata hasara ni Wazanzibari
Anasema kwa kiasi kikubwa madai ya Zanzibar ili iweze kujikwamua kiuchumi na kushamirisha maendeleo yake, yamezingatiwa katika Rasimu ya Katiba Mpya, hivyo ni jukumu la Wazanzibari kutambua jambo hilo na kupigania kupatikana Katiba Mpya.
Seif naye anena
Maalim Seif anasema hakuna mbunge atakayerejea bungeni kupitisha rasimu ya katiba ambayo haikuzingatia matakwa na madai ya msingi ya wananchi.
Kwa kuwa CCM wanataka kubaki na serikali mbili, basi moja iwe ya Tanganyika na ya pili ya Zanzibar; zote zikiwa na mamlaka kamili .kama ilivyokuwa kabla ya kuungana mwaka April 26, 1964 Ni wazi kinachoonekana sasa kadri unavyofuatilia madai ya CCM na CUF ni kama mchezo wa paka na panya ambao unafanyika huku taifa likihitaji ipatikane katiba mpya ambayo itazingatia mahitaji mapya kulingana na wakati, usalama wa nchi, utulivu na mapatano ya kijamii.Matamshi ya Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP) Hellen Clark yanayowataka wabunge wa kundi la Ukawa kurudi bungeni, yanadhirisha madai kuwa nje ya bunge ni vigumu kupatikana Katiba mpya na wanachokifanya Ukawa ni kupoteza wakati.
Msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano uko wazi kufuatia kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwamba endapo rasimu mpya ya katiba haitapitishwa kwa kukosekana theluthi mbili ya maamuzi ya Wajumbe wa Bunge maalum la Katiba, taifa litaongozwa na Katiba ya mwaka 1977.

No comments: