Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika amesema mchanganyiko wa viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika ngazi ya Serikali za Mitaa ni dalili tosha ya kuking’oa madarakani Chama cha Mapinduzi.Mnyika alisema hayo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mabibo, Dar es Salaam uliokuwa na lengo la kuwashukuru wakazi wa kata hiyo kuwachagua viongozi wa Ukawa.Alisema CCM isitarajie mteremko katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu kwa kuwa Ukawa wana kila sababu ya kuibuka washindi.“Waswahili wanasema dalili njema huonekana asubuhi na umoja ni nguvu, utengano ni dhaifu, hivyo CCM ijiandae kuachia madaraka kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais.
“Huu mseto wenzetu unawapa shida kweli kweli na hautovunjika hadi tunahakikisha tunaingia Ikulu Oktoba mwaka huu,” alisema Mnyika, huku akishangilia na wananchi hao.Mnyika ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, aliwataka wenyeviti hao kufanya kazi kwa uadilifu, ikiwamo kuitisha mikutano ya mara kwa mara na wananchi ili kusikiliza kero zao na kuzitatua kwa wakati. Mwenyekiti wa Mtaa wa Mabibo, Francis Mayunga alikuwa mwenyeji wa mkutano huo, aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa safu hiyo mpya ya uongozi wa mtaa huo ili waletewe maendeleo waliyoyakusudia.“Narudia kusema tena mbele ya mbunge, huduma katika ofisi yetu zitakuwa ni bure tofauti na utawala mwingine uliopita uliokuwa ukiwalipisha Sh2,000 za kugongewa muhuri,” alisema Mayunga.
No comments:
Post a Comment