Saturday 28 March 2015

Kuelekea Uchaguzi Mkuu na Julius Mtatiro

MKOA WA MBEYA (II): MAJIMBO YA ILEJE, LUPA NA SONGWA – CCM INA KARATA MKONONI.
Na. Julius Mtatiro,
Gazeti la Mwananchi, Jumapili- 08 Machi 2015. Safu ya leo ni sehemu ya pili ya uchambuzi wa majimbo ya Mkoa wa Mbeya ambapo leo tuna majimbo matatu mapya, Ileje, Lupa na Songwa.
WILAYA YA ILEJE
Wilaya ya Ileje ni moja kati ya wilaya 8 zinazounda mkoa wa Mbeya. Wilaya hii inapakana na jiji la Mbeya na wilaya ya Rungwe kwa upande wa Kaskazini, wilaya ya Kyela upande wa Mashariki, wilaya ya Mbozi upande wa Kaskazini Magharibi na nchi za Zambia na Malawi upande wa Kusini. Wilaya ina jumla ya kata 18, vijiji 71 na Vitongoji 317 – vyote vikiwa ndani ya eneo la kilomita za mraba 1,880.35.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 wilaya ya Ileje ina wakazi 124,451 kati yao wanaume wakiwa 58,453, wanawake 65,988 huku kukiwa na wastani wa wakazi 4 katika kila kaya.
JIMBO LA ILEJE
Jimbo la Ileje linaundwa na sehemu yote inayotajwa kuwa wilaya ya Ileje na ni moja kati ya majimbo ambayo yamekuwa ngome ya CCM tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa hadi hivi leo huku upigaji kura wake ukionekana kuwagawanya wapiga kura kuelekea kwa mgombea wanayemtaka zaidi kuliko chama cha siasa, japokuwa kimtandao CCM imekuwa na nguvu.
Katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 jumla ya vyama 7 viliweka wagombea kwenye uchaguzi ambao ulishuhudia kampeni za nguvu na ushindani uliopitiliza huku kila mgombea akionesha kuwa kitisho kwa mwingine. Hata vile vyama vilivyodhaniwa kuwa dhaifu vilipata “sapoti” kubwa hapa Ileje.
Mwisho wa siku ni mgombea wa CCM, Gideon Asimulike Cheyo ndiye aliyeongoza kwa kupata kura 13,122 (61.3%) akifuatiwa na mgombea wa NCCR, Mmanyi Masebo Malang’ombe aliyepata kura 5,630 (26.3%).
Wagombea wa CHADEMA na CUF walipata asilimia 3.8 na 3.5 ya kura zote huku wagombea wa vyama vya TADEA, UDP na NRA wakipata asilimia 1.7 kila mmoja. Jimbo hili lilionesha tofauti kubwa sana kiutafiti, vyama vilivyoonekana kuwa dhaifu walau vilikaribia kupata asilimia 2 ya kura zote jambo ambalo huwa siyo rahisi, mara nyingi vyama vinavyodhaniwa kuwa dhaifu huangukia asilimia chini ya 1.
Gideon Asimulike Cheyo aliwaongoza wana Ileje kipindi cha kwanza cha mwaka 1995 – 2000 na kukimaliza salama na CCM ikampa ridhaa ya kupeperusha bendera tena katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 ambapo hakupata ushindani wa maana na hivyo alichaguliwa tena na kuwa mbunge wa Ileje kwa miaka mitano ya pili (2000 – 2005).
Mwaka 2005 CCM haikuwa na hofu yoyote katika ngome yake, ilimleta tena Gideon Asimulike Cheyo ili apewe ridhaa ya kuongoza kwa mara ya tatu. Vyama vya NCCR na CUF vilijitutumua kwa nguvu za kutosha walau kuleta heshima ya upinzani jimboni humo, matokeo yalipotangazwa Lusekelo Edmara Mbembela wa CUF alipata kura 2,175 (6.5%), Akimu Mwalilino Kajuni wa NCCR alipata kura 8,160 (24.3%) na Gideon Cheyo wa CCM aliibuka mshindi kwa kura 23,277 (69.3%).
Gideon akafanikiwa kuwaongoza wana Ileje kwa mara ya tatu mfululizo akiwa mmoja wa watanzania wachache waliopata fursa ya kuongoza majimbo miaka 15 ndani ya siasa za vyama vingi.
Ungeweza kudhania kuwa kwa sababu upinzani ulipata jumla ya asilimia 30.8 ya kura zote mwaka 2005, kwamba kungekuwa na ongezeko kubwa na labda kufikia kupata asilimia 40 mwaka 2010, hali haikuwa hivyo. CCM ilimuweka mgombea mpya katika kipindi hiki, huyu ni Kibona Nikusuma Aliko, CHADEMA ilichukua nafasi ya NCCR na CUF na kumsimamisha Henry Raphael Kayuni.
Kazi ilikuwa rahisi kama ‘kumsukuma mlevi’, CCM ilishinda kwa kishindo kwa kura 24,126 (83.69%) huku CHADEMA ikipata kura 4,146 (14.38%). Ushindi huu wa CCM ulikuwa na maana kuwa upinzani ulianguka kwa zaidi ya asilimia 16 ukilinganisha na mwaka 2005.
Pamoja na uimara wa CCM jimboni Ileje huku upinzani ukionekana kuwa na sura mbili (udhaifu na uimara) kati ya mwaka 1995 – 2010, ukweli unabakia kuwa CHADEMA imeweza kufanya uhamasishaji mkubwa jimboni humu na ina wagombea vijana wanaopigana vikumbo kutafuta idhini ya wananchi. Matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa yanaonesha kuimarika zaidi kwa upinzani kwani kati ya vijiji 71 vya jimbo hili CHADEMA imepata vijiji 23 (32.3%) huku kati ya vitongoji 317 ikijipatia 59 (18%).
Ikumbukwe kuwa kabla ya hapo upinzani haukuwa na vijiji na vitongoji vya kuhesabu moja hadi tatu hapa Ileje.
Siwezi kuipa CHADEMA asilimia 50 ya kulipata jimbo hili, lakini naliona kama jimbo litakalotoa ushindani mkubwa uliopitiliza na labda ushindani wa sasa na harakati za 2015 – 2020 vitahalalisha jimbo hili kuondoka mikononi mwa CCM ifikapo mwaka 2020.

WILAYA YA CHUNYA
Chunya ni moja kati ya wilaya 8 za mkoa wa Mbeya, wilaya hii inapakana na Mkoa wa Tabora kwa upande wa Kaskazini, Mkoa wa Singida kwa upande wa Kaskazini Mashariki, Wilaya ya Mbarali kwa upande wa Mashariki, jiji la Mbeya na wilaya ya Mbozi kwa upande wa Kusini na Mkoa wa Rukwa kwa upande wa Magharibi.
Wilaya ya Chunya ina ukubwa wa kilometa za mraba 29,997.19 ikiwa wilaya inayobeba takribani asilimia 48.05 ya eneo lote la mkoa wa Mbeya. (Mkoa wote wa Mbeya una eneo la kilomita za mraba 62,420)
Wilaya inaundwa na mamlaka ya mji mdogo pamoja na kata za kawaida ambapo kuna jumla ya kata 30, vijiji 86 na vitongoji 399 (bila kujumuisha mamlaka ya mji mdogo). Mamlaka ya mji mdogo inaundwa na kata nne ambazo ni Makongolosi, Bwawani, Mkola na Matundasi: na kwa ujumla kata hizi zina vitongoji 35. Kwa ujumla maeneo yote haya ya utawala yanapatikana ndani ya majimbo mawili ya uchaguzi ambayo ni Songwe na Lupa.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, wilaya ya Chunya ina wakazi 290,478 ambapo wanaume ni 145,420 na wanawake ni 145,058 huku kukiwa na wastani wa watu 4.9 katika kila kaya moja.
Hivi karibuni (Mwezi Machi 2015) Mbunge wa jimbo mojawapo wilayani humu (Philipo Mulugo) alionekana akipiga magoti chini kumuomba waziri Mkuu (Mizengo Pinda) aigawe wilaya ya Chunya ili kupata wilaya mbili, katika chagizo hilo walionekana kina mama wakijigalagaza chini ili kumuhamasisha Waziri Mkuu atekeleze ombi lao. Waziri Mkuu katika kuwajibu alisisitiza kuwa serikali haina namna zaidi ya kuigawa wilaya ya Chunya ili kuwe na wilaya mbili ambazo zitasaidia ukimbizaji wa gurudumu la maendeleo na kufanya utawala na huduma kwa wananchi kupatikana kirahisi.
Wilaya ya Chunya ina hali mbaya sana kiuchumi, halmashauri yake inaweza kujiendesha kwa asilimia 15 tu jambo lenye maana kuwa ikiwa serikali kuu inakosa bajeti ya kusaidia maendeleo katika wilaya hii, wilaya inaweza kusimama. Umasikini uliopitiliza wa wilaya na wananchi wake haufanani hata kidogo na hali halisi ya fursa nyingi za kiuchumi zilizomo wilayani humu. Wilaya kwa kipindi kirefu imekosa viongozi wabunifu na wawakilishi wenye visheni pana ya kuweza kuwavusha wananchi wake kwenda hatua ya mbele kimaendeleo.
Majimbo mawili ya wilaya hii ya Chunya ni ngome za kujivunia za CCM mpaka unaweza kufikiri kuwa “CCM ndiye mzazi wao dam dam”.
JIMBO LA SONGWE
Jimbo la Songwe lilikuwa alama muhimu ya ushindani wa kimageuzi tangu kuanza kwa uchaguzi ulioshirikisha vyama vingi na wachambuzi wa mambo ya siasa wakati huo walidhani lingechukuliwa na NCCR na hata baada ya uchaguzi wakadhani kwamba litakwenda kwa vyama vya upinzani katika uchaguzi ambao ungefuata, mambo hayakuwa kama ilivyotabiriwa.
Mwaka 1995 kinyang’anyiro kilikuwa na mvutano wa ‘kufa mtu’, CCM “ilipapana” kwenye ulimbo wa wapinzani kiasi kwamba watu wote walijua itaanguka. Hata hivyo ikitegemea uwakilishi wa John Lingstone Mwakipesile, iling’ara kwa ushindi wa kukimbizwa na wapinzani uliotokana na kura 23,938 (59.5%). NCCR ililikosa jimbo hili kwa sababu tu ya ugeni katika mazingira ya siasa, ilijipatia kura 13,059 (32.4%) na vyama vya TADEA, PONA, TLP na UPDP vilipata asilimia 7.2 ya kura zote.
Mwaka 2000 CCM iliwakilishwa na Paul Edward Ntwina aliyepambana kirahisi na kuwashinda wapinzani wake na kuliongoza jimbo hili kwa kipindi cha mwaka mmoja (2000 – 2005) ikiwa na maana kuwa CCM imefanikiwa kuliongoza kwa kipindi cha pili bila kupata msukosuko mkubwa kutoka kwa wapinzani.
Kituko kilitokea mwaka 2005, ile nguvu ya upinzani iliyoonekana sana mwaka 1995 ilipotea. Safari hii (mwaka 2005) Dr. Guido Gorogolio Sigonda wa CCM akapita bila kupingwa, yaani wapinzani wakamwacha aende zake bungeni bila kumghasi (Hakuna raha kama hii katika siasa, yaani unapita bila kupingwa!).Tukumbuke hili ni jimbo ambalo almanusura lichukuliwe na upinzani mwaka 1995.
Ilipotimu mwaka 2010 vyama vilijipanga na CCM ikamtanguliza mwakilishi wake mpya, Philipo Augustino Mulugo. Kituko cha mwaka 2005 kikajitokeza tena mwaka 2010, wapinzani waliokuwa wamechukua fomu wakaingia mitini bila kufahamika nini kimewatokea, Philipo Mulugo akafunga safari kwenda kusaidia ushindi wa CCM kwenye majimbo mengine, jimboni kwake kazi amemaliza (amesaidiwa na wapinzani).
Nimeongea na Mzee mmoja wa miaka 75 aliyemo jimboni Songwe, anasema siku aliyotambua Mulugo anapita bila kupingwa alinyonga baiskeli yake usiku kucha hadi kwa mgombea mmoja wa upinzani ambaye wananchi walikuwa wanamtegemea sana, alipofika kwake akakuta makufuli. Siasa zina mambo yake!
Pamoja na utendaji usioeleweka wa Philipo Mulugo, serikali ya Rais Jakaya Kikwete ilimteua kuwa Naibu Waziri wa Elimu na baadaye kumwondoa. Moja kati ya mambo ya kukumbukwa mno alipokuwa waziri ni pale alipofanya uwasilishaji wa masuala ya kimataifa akiwakilisha nchi yetu huko Afrika ya Kusini na katika wasilisho lake akasikika akisema kuwa Tanganyika ilipata uhuru wake mwaka “mia moja sitini na moja” na kwamba Tanzania ni “muungano wa Bahari ya Hindi ya Zimbabwe na Pemba pamoja na nchi ya Bara iiyojulikana kama Tanganyika”.
Vituko hivyo havijamfanya Mulugo akose fursa ya kuwawakilisha wana Songwe na hata katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwezi Disemba mwaka jana (2014) chama chake (CCM) kimepata ushindi wa zaidi ya asilimia 90 ya vijiji na vitongoji, jambo lenye maana kuwa bado ana nguvu jimboni kwake na hajapata mpinzani wa kumtikisa.
Kati ya majimbo ambayo yatatangazwa mapema kwenda CCM mwezi Oktoba mwaka huu, hili la Songwe ni mojawapo. Upinzani haujafanya kazi kubwa hapa na muda uliobakia hauwezi kutosha kushinda katika jimbo hili.
JIMBO LA LUPA
Jimbo la Lupa limewahi kuzalisha wanasiasa wenye vipaji, ushawishi na uwezo mkubwa sana. Mmoja wa wanasiasa wa aina hiyo ni Njelu Kasaka. Sote tunaikumbuka hoja ya kudai serikali tatu iliyowahi kuwasilishwa na wabunge wa CCM wakiongozwa na Njelu Mulugala Kasaka mwaka ule wa 1993. Njelu alikuwa ni moto wa kuotea mbali na alikubalika mno kwa wana Lupa mkoani Mbeya.
Katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 CCM ilimtanguliza mkongwe na gwiji huyu wa siasa na kwa sababu ya umuhimu wake katika siasa za Mbeya na Tanzania kwa ujumla wakati huo, hakupata shidasana kuwashinda wapinzani.
Baada ya kushinda aliongoza jimbo hili chini ya mfumo wa vyama vingi kati ya mwaka 1995 – 2000. Katika kipindi hiki Njelu Kasaka ambaye ana stashahada ya Uchumi, Shahada ya Uchumi na Shahada ya Uzamili ya Sayansi ya Uchumi na Kilimo, aliteuliwa kuwa Naibu waziri wa Kilimo na Ushirika katika serikali ya rais Mkapa na baadaye Mkuu wa mikoa ya Iringa na Tabora.
Katika uchaguzi wa mwaka 2000, Njelu Mulugala Kasaka alihitaji kipindi kingine na aliomba ridhaa ndani ya CCM, akafanikiwa kupewa kibali kwa mara ya pili ambapo hakufanya “masihara”, aliwaangusha wapinzani na akaendelea kutamba katika siasa za mkoa wa Mbeya akiwakilisha jimbo la Lupa hadi mwaka 2005.
Uchaguzi wa 2005 ulipokaribia, Njelu alitaka tena CCM impe kibali cha uwakilishi kwa mara nyingine, safari hii aliishia kugonga mwamba kwa kuangushwa kwenye kura za maoni ndani ya chama chake. CCM ilimpitisha Victor Kilasile Mwambalawaswa.
Mwambalawaswa wakati anajiandaa kufanya mapambano na wapinzani, wagombea wa upinzani walitokomea kusikojulikana na akapita bila kupingwa (raha zile zile za kuchagua picha na kivuli au jembe na nyundo – zikawakuta wananchi wa Lupa). Zama hizo zimewahi kutokea sana katika ukanda huu wa Nyanda za juu Kusini.
Wakati Mwambalawaswa anajipanga kuongoza wana Lupa, mwenzake Njelu Kasaka hakuwa ameridhishwa na kitendo cha kuangushwa ndani ya chama hicho, aliamua kuhamia Chama Cha Wananchi CUF ambako huko nako hakudumu – akarejea tena CCM ambako yupo hadi sasa. Hata hivyo kususa kwa Njelu kulionekana kama hasira za mkizi na hakukumzuia Mwambalawaswa kupita bila kupingwa na kuliongoza jimbo la Lupa hadi mwaka 2010.
Kinyang’anyiro cha 2010 kilipopamba moto CCM ilitaharuki kuwa zile zama za wagombea wake kupita bila kupingwa zimeondoshwa ghafla. Vyama vitatu vilijitokeza kupambana na CCM na safari hii ile michezo ya ‘kutokomea kusikojulikana” ilikoma, CCM iliipata! Kampeni zilikuwa za hali ya juu sana huku mgombea wa TLP, Sanga Sande Samson akionekana kung’ara na kushawishi wachambuzi wengi wa siasa za Lupa kuwa angeliweza kuiangisha CCM.
Matokeo ya mwisho hayakuleta kile ambacho wengi walitajia kwani CCM ilishinda kwa shida. Mgombea wa CCM Mwambalaswa Victor Kilasile akipata kura 12,202 (55.05%) huku Sande Samson wa TLP akifuatia kwa karibu akiwa na kura 8,746 (39.46%). CHADEMA na CUF kwa pamoja viliambulia asilimia 3.2 ya kura zote na hivyo Mwambalawaswa ndiye mbunge wa Lupa hadi hii leo.
Matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwezi Disemba 2014 yanadadavua upoteaji wa TLP jimboni Lupa na kwamba CHADEMA ndiyo ina nafasi. Nafasi ya CHADEMA nayo inaonekana “kuchechemea” kwa sababu chama hicho kimepata vijiji 4 tu kati 52 hapa jimboni huku pia ikipata vitongoji 29 kati ya 176 vilivyomo jimboni humu.
Jimbo la Lupa bado litakuwa ngome ya CCM na upinzani wataishia kulionea gere tu labda hadi uchaguzi mwingine lakini siyo huu wa 2015. Hapa Lupa, vyama vingine ukiondoa CCM havijajipanga. Na kulikosa jimbo hili hakuwezi kuwa lawama yoyote dhidi ya hujuma ambazo hutuhumiwa na hata kuelekezwa kwa CCM.
(Julius Mtatiro ni kiongozi mzoefu katika siasa. Ana shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A), na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (L LB): +255787536759, kuelekeamajimboni@yahoo.com – Uchambuzi huu ni maoni binafsi ya mwandishi).

No comments: