Wednesday, 6 May 2015

MIZENGO KAYANZA PINDA: NANI NI NANI URAIS CCM? HISTORIA YAKE

Mizengo Pinda alizaliwa Agosti 12, 1948 mkoani Rukwa (atafikisha miaka 67 Agosti mwaka huu). Pinda ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu mwaka 2008.Wazazi wa Mizengo Pinda wote walikuwa wakulima kwa hiyo kijana pia alifuata nyayo hizo huku akifanya jitihada kubwa kwenye masomo yake na kufanikiwa kuhitimu shule ya msingi na sekondari, akifaulu vizuri kila alikopita.
Baada ya masomo yake ya sekondari, Pinda alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea Shahada ya Sheria (LLB) mwaka 1971 hadi 1974. Baada ya kuhitimu, alijiunga katika utumishi kwenye Wizara ya Sheria akiwa Mwanasheria wa Serikali na alikaa katika utumishi huo tangu mwaka 1974 hadi 1978.Mwaka 1978, alifanya kazi akiwa “Ofisa Usalama wa Taifa” akiwa Ikulu hadi mwaka 1982, Rais wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere alipomteua kuwa katibu wake binafsi (Katibu wa Rais) nafasi aliyoishikilia hadi mwaka 1985.
Baada ya Mwalimu Nyerere kung’atuka na kuikabidhi nchi kwa Ali Hassan Mwinyi, Pinda alitakiwa kubaki kuendelea kumsaidia Mzee Mwinyi na alikubali wito huo. Akaendelea kuitumikia Ikulu chini ya utawala wa Mwinyi hadi mwaka 1992.
Mnamo mwaka 1995, Pinda alijaribu kugombea ubunge katika Jimbo la Mpanda Mashariki lakini alishindwa katika hatua ya kura za maoni na ikampasa kurejea kwenye kazi yake ya awali Ikulu.
Baada ya Mkapa kuteuliwa kurithi Ikulu mwaka 1995, alimteua Pinda kuwa karani wa Baraza la Mawaziri. Wadhifa alioushikilia kuanzia mwaka 1996 hadi 2000. Pinda amemuoa Tunu na wamepata watoto wanne; Janet, Jenifer, Hardwick na Narusi.
MBIO ZA UBUNGE
Mwaka 2000, Pinda aliachana na utumishi ndani ya Serikali na Ikulu akajitupa jimboni Katavi kusaka ubunge kwa mara nyingine, safari hii alipita ndani ya kura za maoni za CCM akafanikiwa kuwashinda wapinzani na kuwa mbunge. Nyota ya Pinda ilizidi kung’ara mwaka 2001, pale Rais Mkapa alipomteua kuwa Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) akifanya kazi chini ya waziri wake, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi, hadi mwaka 2005. Mwaka 2005, Pinda aliwashinda Sebastian Bedastus wa TLP na Albert Damian wa CUF na kuchaguliwa kwa mara ya pili kuwa Mbunge wa Katavi na aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa waziri kamili wa Tamisemi. Bahati ya Pinda kisiasa iliruka angani wakati wa “ajali ya kisiasa” ya Edward Lowassa iliyoacha nafasi ya uwaziri mkuu wazi kutokana na kashfa ya Richmond, Rais Kikwete alimteua Pinda kuwa Waziri Mkuu. Jimboni Katavi mwaka 2010, Mizengo Pinda alishinda uchaguzi kwa “kupita bila kupingwa” na aliteuliwa tena na Rais Kikwete kushika wadhifa wa Waziri Mkuu hadi sasa.
MBIO ZA URAIS
Pinda ni mwanasiasa aliyeamua kwa dhati kuachana na mambo ya ubunge na kujitosa miguu miwili kwenye kinyang’anyiro cha urais. Wanasiasa wengi hujaribu kugombea urais huku wakiwa wanautaka ubunge, hutupa ndoano kwenye urais lakini wanapiga hesabu za ubunge ikiwa watakosa ridhaa ya uteuzi, hawa ni aina ya watu ambao huamini kuwa wanapaswa kusalia madarakani kwa njia yoyote ile, Pinda si mmoja wao.
Hivi ninapoandika, Pinda amekwishawaaga wana Katavi tangu mwaka jana na amekuwa akijiweka hadharani na kuendelea na mikakati ya chini kwa chini ya kuingia Ikulu.
Hata hivyo, kutangaza nia kwake kumekuwa na maoni tofauti kutoka kwa wananchi hasa ikizingatiwa kuwa wengi wanamfahamu vizuri kwa uimara na udhaifu wake na kila mmoja ana sababu yake.
Oktoba, 2014 akiwa nchini Uingereza alieleza kuwa amejitokeza kugombea urais ili pamoja na wenzake walioanza harakati, Watanzania wapate muda wa kuwapima.
Mwandishi wa BBC alipomhoji kama na yeye ni miongoni mwa watu wanaotaka kuvaa viatu vya Kikwete alisema, “… umesikia kama nimo? … basi tukubali hilo na yeye Waziri Mkuu yumo. Hao wote waliojitokeza pamoja na Waziri Mkuu aliyejitokeza ni katika jitihada za kusema hebu Watanzania nitazameni je, mnaona nafaa au hapana?” 

NGUVU YAKE
Pinda ana nguvu ya asili, ni kiongozi mtulivu na msikivu. Mawaziri wakuu wengi waliopita hapa nchini si watu wa ‘chapchap’, Pinda yuko tofauti, ukimpigia simu muda wowote ambao yuko karibu nayo atapokea na atakusikiliza nini unasema, atakushauri hatua zipi zichukuliwe au atakuomba muda afuatilie suala husika kwa mawaziri wake. Mara nyingi husikiliza zaidi kuliko kuongea, hii ni sifa muhimu mno kwa kiongozi yeyote yule anayehitaji madaraka makubwa.
Jambo la pili linalompa nguvu ni kutojikweza. Pinda si mtu wa makuu wala mbwembwe, ni mtu asiyejikweza na kila mara anaishi maisha ya kawaida tofauti na mawaziri wakuu wengi duniani na hata baadhi ya waliopita hapa Tanzania. Yeye mwenyewe hujiita “mtoto wa mkulima” na aina ya maisha anayoishi yanafanana na “ukulima”.
Jambo la tatu ni “usafi wa kisiasa”. Ukiondoa kashfa ya Escrow ambayo almanusura imuondoe katika wadhifa alionao hivi sasa, Pinda hakuwahi kutuhumiwa kuhusika na ubadhirifu wowote ule serikalini. Hata Escrow kwa kiasi kikubwa tuhuma zilimwendea kwa sababu tu ya nafasi yake ya Waziri Mkuu lakini si kwa sababu alishiriki kukwapua fedha hizo.
Pinda ana nguvu ya asili ndani ya CCM, kwa sababu ni waziri mkuu anayemaliza muda wake, siyo jambo la ajabu kuwa ana watu wengi wanaomuunga mkono ndani ya chama hicho.
UDHAIFU WAKE
Udhaifu mkubwa wa Pinda ni kufanya uamuzi. Kiongozi yeyote huhitaji kuwa na uwezo mzuri wa kufanya uamuzi thabiti na kwa wakati, Pinda si miongoni mwao. Pamoja na kujua aina ya Rais anayefanya naye kazi, bado hakuchukua jukumu la kuwa thabiti nyakati zote na kufanya uamuzi mgumu kila inapowezekana.
Mwanya huo umeifanya Serikali ya Awamu ya Nne ionekane ina ombwe kubwa, ikizingatia kuwa mkuu wa nchi pia ana upungufu ambao ungeweza kuzibwa na waziri mkuu wake ambaye naye hatendi inavyopaswa. Uongozi mara zote ni kufanya uamuzi, siyo kutafakari mwaka mzima. Pinda amefeli katika eneo hili.
Si hivyo tu, Pinda pia ana udhaifu mkubwa mambo yakimzidia, anakata tamaa na kuona hakuna suluhisho. Mwaka 2013, alipoulizwa bungeni kuhusu tabia ya vyombo vya dola kuzuia maandamano ya wananchi na kuwapiga wanaoandamana bila sababu, aliishia kusisitiza kuwa “watu hao lazima waendelee kupigwa”, Pinda alisisitiza kuwa amechoshwa na maandamano na migomo na kwamba wanaofanya hivyo kilichobakia ni “kuendelea kupigwa tu”. Kwa mtu anayejua uongozi, hii ni kauli ya kukata tamaa kutolewa na kiongozi mkubwa wa nchi wakati ambao alipaswa kuonyesha uongozi wake unapanua demokrasia katika masuala ya msingi.
Hasira na pupa katika uamuzi na kukata tamaa kwake vilionekana pia wakati alipokuwa akitoa kauli ya Serikali juu ya mauaji ya albino. Pinda alijikuta ametamka kuwa wanaofanya hivyo nao “wauawe tu”. Hii ni kauli ya hatari. Kiongozi ni mtu wa kusaka utatuzi wa kudumu wa matatizo siyo kushadidia matatizo yatatuliwe kwa kuvunja sheria, kuongeza matatizo mengine na kuchukua uhai wa watu wengine. Hizi ni dalili za kiongozi anayekata tamaa.
Upole kupita kiasi ni udhaifu mwingine wa Waziri Mkuu anayemaliza muda wake. Pinda ni mpole mno kiasi kwamba duru za ndani ya Serikali zinasema kuna baadhi ya mawaziri wanatumia upole huo kumruka na kujifanyia mambo yao bila kibali chake na hata mara nyingine kumshauri ndivyo sivyo kwa kutumia udhaifu wake huo. Upole uliopitiliza wa Pinda ni kati ya mambo ambayo yameiumiza Serikali ya CCM katika awamu inayokwisha.
NINI KINAWEZA KUMFANYA APITISHWE?
Kama Pinda atapitishwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM, basi uzoefu wa uongozi wa Serikali ngazi za chini hadi juu ni jambo litakalombeba. Pinda ameitumikia Serikali hii kama mtumishi wa ngazi ya chini na amepanda ngazi moja baada ya nyingine hadi amekuwa waziri mkuu. Hakuna shaka kuwa amekuwa mtumishi wa Watanzania tangu mwaka 1974 – 2015 (miaka 41).
Kukaa serikalini muda mrefu kumemfanya aijue nchi hii na matatizo yake. Ikiwa chama chake kitakuja na ilani inayotekelezeka na yenye majibu ya matatizo ya wananchi, mtu aliyekaa serikalini miaka 41 si wa kumchukulia “poa”, huyu ni hazina kubwa na huenda CCM ikaliona jambo hilo.
Sababu nyingine inayoweza kumpa Pinda nafasi ni uadilifu. Kama nilivyosisitiza awali, Pinda hana kashfa yoyote kubwa inayomgusa moja kwa moja na CCM inajua kuwa inahitaji watu kama yeye iwapo itawekeza nguvu kumtafuta rais asiye na madoa lukuki. Ni mara chache kukuta mtu amekaa serikalini miaka 40 halafu hana “rundo la kashfa” lililomzunguka. Hii ni bahati kubwa.
Sifa nyingine itakayombeba Pinda ni kutokuwa na makundi ya muda mrefu. Kama kuna jambo lililomsaidia kuukwaa uwaziri mkuu mwaka 2008 ni hili na huenda likamsaidia tena katika kusaka tiketi ya urais kupitia CCM.
Tofauti na wanasiasa wengi ndani ya CCM, Pinda hakuwahi kuwa na makundi ya kudumu na hata hii majuzi alipoonyesha kuwa ataingia kwenye kinyang’anyiro cha urais watu wengi wanamchukulia kama mtu mtulivu na asiye na papara, lakini anaaminika kwa kuendelea na kasi kubwa ya mipango ya chini kwa chini kwa maandalizi. Ikiwa CCM itahitaji mtu “neutral” wa kuivusha katika uchaguzi mgumu kama huu, basi Pinda atakuwa moja ya karata za chama hicho.
NINI KINAWEZA KUMWANGUSHA?
Kama kuna jambo moja kubwa litakalokwamisha safari ya Pinda kwenye mchujo wa CCM ni makosa mengi yaliyofanywa na Serikali inayomaliza muda wake ambayo yeye alikuwa kiongozi wa juu kabisa.
Inawezekana CCM ikamuona Pinda kama sehemu ya udhaifu wa Serikali ya Kikwete na ikaona si mtu wa msaada tena kwa wakati huu hasa ikiwa kazi aliyoifanya kwa miaka saba (uwaziri mkuu) itatafsiriwa kuwa haikuwa ya mafanikio. Jambo hili linaweza kumtupa nje.
Kitu kingine kinachoweza kumwangusha ni kasumba ya “waziri mkuu anayemaliza muda wake hawezi kuwa Rais katika Serikali inayofuata hapa Tanzania”. Kasumba hii imekuwapo tangu enzi za uhuru hadi leo. Mawaziri wakuu wote tangu uhuru walipojaribu kuomba ridhaa ya urais ndani ya CCM katika Serikali iliyofuatia waliangushwa na jambo hili limezoeleka ndani ya CCM. Ikiwa kasumba hii itaendelea, ina maana yale yaliyowakuta mawaziri wakuu wengine wote yatamkuta pia mtoto wa mkulima.
Jingine linaloweza kumuondoa Pinda kwenye kinyang’anyiro ni kuchokwa na wana mabadiliko ndani ya CCM. Ikumbukwe kwamba kuna viongozi wengi ndani ya CCM wanahitaji mabadiliko makubwa ya kimfumo ndani ya chama chao na ili kuyafanya, kunahitajika watu wenye historia za kusimamia mabadiliko makubwa kitu ambacho Pinda hakiwezi. Ndani ya CCM, Pinda anaendelea kuonekana kama kiongozi asiye na mbinu mpya za kufanya uongozi wa kisasa na hivyo hatoweza kubeba matarajio ya wana mabadiliko waliomo ndani ya chama hicho kikongwe.
Pinda anaweza kuwa tishio kwa wasaka urais ndani ya CCM lakini katika jamii pana anatazamwa kama mtu wa kawaida sana ambaye hana uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko makubwa serikalini. Pinda amekuwa serikalini akiwa waziri mkuu kwa miaka sana na hakujawa na “maajabu” makubwa yaliyotendeka humo serikalini.
ASIPOPITISHWA (MPANGO B)
Kwa maoni yangu, ikiwa Pinda hatachaguliwa na chama chake kugombea urais, ataungana na msururu wa mawaziri wakuu wastaafu wengine kurudi ‘mtaani’ kulijenga taifa hili akiwa mshauri na mtu muhimu. Mwenyewe mara kadhaa amesikika akisema kuwa akistaafu siasa atajikita katika “ukulima” kazi ambayo ameizoea tangu akiwa kijana mdogo. Pinda atakuwa mmoja wa mawaziri wakuu ambaye hataumizwa kukosa nafasi ya chama chake kugombea urais, hali hii inasaidiwa na tabia yake ya kutokuwa na tamaa na kupapatikia mambo makubwa ambayo hayawezekani.
HITIMISHO
Serikali ya awamu ya nne inamaliza muda wake huku ikiwa na upungufu mwingi na yeye amekuwa sehemu ya historia hiyo. Nadhani CCM itapaswa kupiga hesabu za kutosha kabla ya kumfikiria Pinda, itaipasa ipige hesabu za aina ya mgombea ambaye atasimamishwa na vyama vya Ukawa na kupima kuona kama Pinda anauzika kiasi cha kumshinda mgombea bora wa upinzani ikiwa uchaguzi unakuwa huru na wa haki au la.
Namuona Pinda kama mshauri mzuri wa CCM siku za mbele lakini si kama mgombea urais bora sana, japokuwa kama nilivyosema awali, nguvu yake na mtandao wake ndani ya CCM vinawatisha wagombea wengine na huenda vikambeba. Mzee huyu “mtoto wa mkulima” tunamtakia kila la heri katika kuvuka vizingiti vinavyomkabili.
Like · Comment · 
KUHUSU MCHAMBUZI:
Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, ana uzoefu mkubwa wa uongozi wa kisiasa hapa Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi na Lugha, Shahada ya Sanaa “B.A” katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (L LB) – Anapatikana kupitia +255787536759,(juliusmtatiro@yahoo.com) Uchambuzi na huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi). (Uchambuzi huu umechapishwa na Gazeti la Mwananchi la Jumatatu, 04 Mei 2015).

No comments: