Tuesday 5 May 2015

Serikali isipojiheshimu na ikachokwa, alaumiwe nani?

Joseph Butiku
Joseph Butiku
KUNA barua ya Josephat Butiku, ambaye wengi tunafahamu kama mwana CCM halisi na ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mwalimu Nyerere Foundation (MNF), aliyomwandikia Rais mstaafu Benjamin Mkapa, ambayo Fred Mpendazoe ameinukuu katika gazeti la Raia Mwema, toleo la 401.
Uzoefu wangu unaonyesha kuwa hili magazeti hayasomwi kwa wingi na wananchi hasa vijijini, ambao kwa kiasi kikubwa barua hii imejikita kuwasilisha kilio chao kwa Rais mstaafu Mkapa.              
Kadiri ya hali halisi ya mambo ilivyo sasa hivi hapa nchini, ni wazi barua hii haikufanyiwa kazi. Kwa mtazamo wangu, hii barua haipaswi kupuuzwa na mwanachama halisi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kisha akaendelea kutamba kuwa yeye ni muumini na anajivunia kuwa mwanachama wa CCM iliyokuwa mkombozi wa wanyonge. Haiwezekani!
Na kutokana na mimi kuamini hivyo, nina sababu mbili kubwa, tukiacha masuala mengi madogo madogo, kuandika andiko hili. Sababu ya kwanza, ni juu ya unyeti na ukweli ulioelezwa na Joseph Butiku, ambao sina nafasi ya kuunukuu hapa.Niseme tu kuwa CCM kimewasahau wanyonge kulingana na misingi yake asilia kuliyopaswa kurithi kutoka TANU na ASP enzi za Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hayati Mzee Abeid Amani Karume.Sababu ya pili ni kuona iwapo hata wazee wetu waasisi na wadhamini wa CCM tuliojaliwa na Mwenyezi Mungu kuwa nao hadi sasa, kwa mfano Mzee Peter Kisumo (kwa upande wa Bara) na Mzee Hassani Nassoro Moyo (Kwa upande wa Zanzibar), nikitaja wachache, kama nao walijua na kupuuza ile barua au la.

Kujua hili kuna umuhimu wake maalumu, maana penye wazee hapaharibiki kitu. Haifai na si busara kupuuza wazee hawa. Niseme wazi kuwa Fred Mpendazoe alitupatia fursa ya kutujulisha juu ya barua ile kwa dhumuni lake la kutushauri kuhusu mtu anayefaa kupeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi ujao.Mimi siko huko. Siamini kuwa maadiliko ya kiuongozi wa Taifa hili yanayoitajika sasa hivi yanaweza kupatikana chini ya hatamu za CCM. Huyo mtu ataanza wapi, pamoja na nani, tukichukua katiba inayopendekezwa kama nyenzo yake? Haitawezekana. Matatizo yanayolikabili Taifa hivi sasa hayatokani na ubavu wa katiba iliyopo, ingawa hilo nalo sio la kupuuzwa. Kutojiheshimu na kutowajibika kwa viongozi kwa wananchi kunaleta kutoheshimika kwa viongozi mbele ya jumuiya ya kimataifa na ni fedheha kwa wananchi wanaowaongoza.
Mwalimu Nyerere aliheshimika sio tu kwa kuwa alikuwa mkali bali na kwa kuwa aliheshimu wadhifa aliopewa kama dhamana na wananchi.Katika kipindi chote cha uongozi wake sio tu hakupata kutuhumiwa na rushwa bali pia hakuwa na chembe ya harufu ya rushwa au ufisadi. Kwa sababu ile, Tanzania iliheshimika mbele ya jumuiya ya kimataifa, na watanzania waliheshimika pia. Je, hali ikoje hii leo?
Mwalimu alisema kuwa Ikulu sio pango la walanguzi, na ilikuwa kweli enzi zake. Andiko hili halitakuwa kamili bila ya mapungufu ya katiba inayopendekezwa kugusiwa, angalau kwa kifupi. Uzuri wa katiba yoyote unatokana na kukidhi matakwa ya wananchi pamoja na katiba husika kuwawezesha wananchi kusimamia utekelezwaji wake.Kilichowafanya wananchi wadai kupata katiba mpya sio tu kwa kuwa katiba iliyopo ina mapungufu mengi bali pia haiwapi wananchi mamlaka ya kusimamia serikali yao ili iwajibike ipasavyo.
Upungufu huu umeendelezwa katika katiba inayopendekezwa, ikiwa ni pamoja na kuwavika wananchi kilemba cha ukoka kwa kutamka tu kuwa “wananchi ndio msingi wa mamlaka yote ya serikali na vyombo vyake…” na kwamba serikali itapata madaraka na mamlaka yake kutoka kwa wananchi” na hapo hapo inafanya rais asilazimike kufuata ushauri wa mtu yeyote, ikimaanisha si Bunge wala mahakama. Zaidi ya hayo, katiba inayopendekezwa imepuuza maoni ya wananchi, hasa kuhusu kupunguzwa kwa mamlaka ya rais na pendekezo kuwa wananchi wawe na uwezo wa kuwajibisha wabunge wao, na kwa vile kumteua mbunge kuwa waziri sio tu kunadhoofisha uwakilishi wake kwa wananchi bali pia anakuwa mwakilishi na mteule wa rais.
Hoja kuwa katiba inayopendekezwa imesheheni mambo mapya kama maslahi ya wakulima, wafugaji na wavuvi haina mashiko kwa kuwa utendaji wa rais chini ya katiba hii unategemea utashi wake na wananchi hawana uwezo wa kikatiba wa kumtaka atekeleze hiyo katiba kama hasipo timiza wajibu wake.
Rais ni sehemu ya Bunge, kiongozi wa muhimili serikali, Mkuu wa nchi na Amiri Jeshi mwenye uwezo wa kuvunja Bunge akitaka. Hii ndiyo sababu wabunge wa CCM wanaogopa kuikosoa serikali kwani bunge likivunjwa nao hupoteza ubunge, hivyo wanaikosoa serikali na hapo hapo kuiunga mkono asilimia mia moja. Hapa ndipo tatizo la bunge kudhibitiwa na serikali, lilipo.
Viongozi sasa hawajiheshimu. Wakituhumiwa kuhusiana na rushwa na ufisadi wanamezea badala ya kujisafisha kwa kukimbilia mahakamani. Na kiongozi kunuka rushwa au ufisadi sio kosa chini ya katiba iliyopo na inayopendekezwa. Kutokana na upungufu huu katika sheria zetu, serikali imeandamwa na kashfa za mara kwa mara na zote zinafichuliwa ama na upinzani au na vyomo huru vya habari.
Kwa nini kashfa hizi hazifichuliwi na vyombo vya usalama wa Taifa na vya ulinzi; ni kutokana na wakubwa wengi kuhusika na hizi kashfa.Hatima ya uchumi na maendeleo ya nchi sasa haitabiriki maana mali ya umma imegeuzwa shamba la bibi. Kwa mfano, kashfa ya Tegeta Escrow ilikoishia hapako wazi. Swali ni je zile hela zilikuwa mali ya umma au za IPTL? Ajuaye ni Mungu!
Formula ya ukokotaji wa Capacity Charges ya kudhihirisha uhalali kama zile hela zilikuwa za IPTL au za umma haijawekwa wazi lakini wakubwa wamepata mgawo kwa hiyo wanasema heri yaishe tu.
Uongozi wa sasa uko makini katika kutembeza bakuli huko ughaibuni kupata misaada lakini kutumika kwa hiyo misaaada kwa manufaa ya mwananchi wa kawaida ni kidogo sana, na sasa deni la Taifa linatisha.
Barabara nyingi zimejegwa kwa gharama kubwa lakini chini ya kiwango. Sera ya uwekezaji, hasa kwenye madini na hifadhi za wanyamapori zimeleta vilio kwa wananchi vijijini badala ya faraja.Mapigano kati ya wafugaji na wakulima yamekuwa tatizo sugu lisiloisha na ukichunguza sana harufu ya rushwa na ufisadi ni chimbuko la haya mapigano.
Tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana wasomi na walioishia darasa la saba linazidi kutishia amani na utulivu mijini na hakuna dalili kuwa litapatiwa ufumbuzi hivi karibuni.Swali ninalowatupia wazee wetu niliowataja na wengineo wa hadhi hiyo ni je bado CCM itarajiwe na mwananchi wa kawaida kuwa ni mkombozi wao katika hali hii?Je, wakati haujafika wa kubadili sheria zetu ili iwe ni kosa kwa kiongozi kumezea kashfa ya rushwa au ufisadi kama wafanyavyo sasa hivi kwa lengo la kuepuka makubwa kufichuka wakikimbilia mahakamani kujisafisha mbele ya sheria?
Je, wazee hamuoni kuwa ni fedheha Taifa kuongozwa na mtu mwenye harufu ya wazi ya rushwa na ufisadi?Je, wananchi wakichoshwa na ugumu wa maisha kutokana na viongozi kutojiheshimu kutokana na kutowajibika kwao, alaumiwe nani? Na ninyi wazee mtapona? Je, inafaa tungoje hilo litokee?
Mungu mbariki Joseph Butiku na Fred Mpendazoe, Mungu wabariki wazee wetu watumie busara zao ili kuliepusha Taifa na janga ambalo linaweza kuepukwa.
Mungu ibariki Tanzania
Mwandishi wa makala hii ni Robert K. Mnyone

No comments: