Friday 8 May 2015

Mzee Ruksa atimiza miaka tisini.(90 yrs old bado anadai.

Wana Diaspora Tunamtakia Mzee Ruksa Maisha Marefu.
Rais mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi maarufu kwa jina la ‘Mzee Ruksa’ leo anatimiza miaka 90. Bado ana nguvu, mchangamfu, mcheshi na anapopata fursa, anawafundisha Watanzania matumizi ya Kiswahili Sanifu na kutoa ushauri juu ya umuhimu wa elimu na kuishi kwa amani na ushirikiano bila ubaguzi kwa misingi ya dini na ukabila.Alhaj Mwinyi aliyeingia madarakani kuiongoza Tanzania  Novemba 5, 1985, alizaliwa Mei 8, 1925 huko Kivule wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani. Hata hivyo, tarehe ya kuzaliwa kwake ina utata kutokana na baadhi ya kumbukumbu kuonyesha kuwa alizaliwa Mei 8, huku tovuti rasmi ya Ikulu ikionyesha kwamba alizaliwa Mei.

 5.Elimu
Alhaj Mwinyi alianza safari yake kielimu huko visiwani Zanzibar ambako alisoma katika Shule ya Msingi Mangapwani mwaka 1933 hadi 1936. Baadaye  alijiunga na Sekondari ya Dole mwaka 1937 hadi 1942, kisha alijiunga na Chuo Cha Ualimu Zanzibar mwaka 1943 hadi 1944.Baada ya kuhitimu ualimu kati ya mwaka 1945 hadi 1950 alirudi  Mangapwani safari hii siyo kusoma, bali kufundisha. Mwaka 1950 alipandishwa cheo akawa Mwalimu Mkuu katika shule hiyo hadi mwaka 1954.Mwinyi hakuwa mtu wa kuridhika na elimu aliyonayo hivyo, akiwa kazini, alikuwa akijiongezea elimu kwa njia ya posta na kuhitimu ‘General Certificate in Education’ (GCE). Pia, alisoma kwa njia ya posta na kuhitimu Stashahada ya Ualimu katika Taasisi ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Durban, Uingereza.
Mwaka 1956 Mwinyi aliajiriwa kuwa mkufunzi katika Chuo Cha Ualimu Zanzibar kazi aliyoifanya hadi mwaka 1961. Baadaye alijiunga tena na Taasisi ya Regent ya London, Uingereza ambako alisoma kwa njia ya posta na kuhitimu  cheti cha ufundishaji Lugha ya Kiingereza.Mwaka huohuo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Hall, Uingereza na kusomea kozi ya ufundishaji (Tutors’ Attachment Course) hadi mwaka  1962. Mwinyi pia ana cheti ya Lugha ya Kiarabu alichokipata kwa kusoma Cairo, Misri kati ya mwaka 1972 na 1974.Kwa hiyo, Mwinyi ni mwalimu aliyekamilika. Alipojitosa katika siasa na kupewa nafasi mbalimbali za uongozi, ni kama alikuwa amebadilisha darasa kutoka lile lenye kuta ambalo huwa na wanafunzi kati ya 24 na 45, wakati ule, hadi nchi nzima kuwa darasa na wananchi kugeuka kuwa wanafunzi.
Kazi na siasa
Mwaka 1964, akiwa na umri wa miaka 39, Mwinyi alianza rasmi harakati za kisiasa; alijiunga na Chama cha Afro Shiraz (ASP) huko Zanzibar. Umahiri wake katika kujenga hoja, ushawishi wake na mvuto kisiasa vilimwezesha kukitumikia chama katika ngazi na nafasi mbalimbali katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).


Kati ya mwaka 1964 na 1965 alishika wadhifa wa katibu mkuu wa muda katika Wizara ya Elimu kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Biashara Zanzibar – Zanzibar State Trading Corporation (ZSTC), mwaka 1965 hadi 1970.Ndani ya chama, kati ya 1966 na 1970 alikuwa mweka hazina msaidizi katika Tawi la ASP la Makadara, Zanzibar. Vilevile, amewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita) kati mwaka 1964 na 1977.
Majukumu mengine aliyowahi kushika Alhaj Mwinyi ni ujumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza la Chakula na Lishe na Mwenyekiti wa Zanzibar Censorship Board (1964-1965).
Aidha, Alhaji Mwinyi amewahi kuwa Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1972 – 1975), Waziri wa Mambo ya Ndani (1975 – 1976). Mwaka 1977 aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri hadi mwaka 1982 aliporejea nyumbani mwaka huo aliteuliwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii na mwaka 1983 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais.
Kuingia Ikulu
Mwaka 1984, hali ya hewa ya kisiasa ilipochafuka Zanzibar kutokana na hatua ya Alhaj Aboud Jumbe kubanwa kuhusu hoja aliyoibeba binafsi kutaka mfumo wa Muungano wa Serikali mbili ubadilishwe, Mwinyi alichaguliwa kurithi nafasi hiyo akiwa pia Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Agosti 1984, alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Lakini uongozi wake thabiti, upeo mkubwa na maono aliyokuwa nayo, mwaka 1985 alipendekezwa na CCM kuwa mgombea urais na kwa vile enzi zile zilikuwa za mfumo wa chama kimoja, hakuwa na mpinzani, akachaguliwa kuwa Rais wa Pili wa Tanzania akichukua mikoba ya Rais wa Kwanza wa Tanzania ,Mwalimu Julius Nyerere aliyeamua kung’atuka.Katika maisha ya kawaida, Mwinyi ni mpenda michezo na mara nyingi hushiriki ‘jogging,’ matembezi ya kuchangisha fedha na kufanya mazoezi mepesi ili kujiweka vyema kiafya.
Mzee Ruksa ana wake wawili; Sitti na Khadija na ana watoto na wajukuu kadhaa. Mmoja wa watoto wake ni Dk Hussein Mwinyi ambaye ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Mambo aliyofanya
Alhaj Mwinyi alirithi nchi yenye uchumi ulioharibika kutokana na kutokana na ugumu uliokuwapo, aliamua kufanya mazungumzo na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Benki ya Dunia (WB) na nchi wahisani ili kufufu uchumi.Halafu aliandaa Azimio la Zanzibar lililolegeza masharti na miiko ya uongozi iliyokuwamo katika Azimio la Arusha. Kwa hatua hiyo, akafungua madirisha ya soko huria na wananchi wakaanza kuagiza na kupata bidhaa mbalimbali kutoka nje ya nchi.Kwa kuzingatia Azimio la Zanzibar, ikawa ruksa kwa viongozi kuwa wakurugenzi katika mashirika binafsi, kuwa na hisa, kumiliki mali. Hii ilikuwa na maana kwamba sera ya Ujamaa ya CCM ilitupwa kapuni – mashirika ya umma na viwanda vya umma vikaanza kuuzwa kwa kisingizio cha ubinafsishaji Baada ya kibano kutoka mashirika ya fedha na nchi wahisani, Serikali ya Mwinyi aliamua rasmi kurejesha mfumo wa vyama vingi, lakini ilitumia mfumo wa kisheria ikaandaa Waraka wa Serikali Namba Moja (White Paper) ambao wananchi waliulizwa kama wanataka mfumo wa chama kimoja au vyama vingi. Asilimia 80 ya watu ilisema inataka chama kimoja, lakini kwa ushawishi wa Mwalimu Nyerere, Serikali iliridhia hoja za waliosema wanataka mfumo wa vyama vingi ili kufungua milango ya wengi kushiriki siasa.
Vyombo vya habari binafsi viliruhusiwa; magazeti, majarida, redio na televisheni viliruhusiwa ili kuwapa wananchi uhuru wa kupata habari. Kwa hiyo, uwazi ulianza kushamiri.Kadhalika, Mwinyi alianzisha utaratibu wa wizara kueleza zimefanya nini katika kipindi cha mwaka mmoja japokuwa utaratibu huo haukuendelea. Ili kuhakikisha unakuwapo uwajibikaji wa hali ya juu kwa wafanyakazi, katika mwaka wake wa kwanza wa uongozi, alikabidhiwa fagio la chuma ili kuwaondoa wafanyakazi wote wasiowajibika serikalini.Mwinyi ndiye aliyetuliza pepo mbaya alipotaka kulivamia Taifa baada ya waumini wa Kiislamu kuvamia na kuvunja mabucha ya nguruwe eneo la Manzese, Dar es Salaam.Aliwaambia waumini hao Tanzania ni nchi inayoamini katika uhuru wa kuabudu hivyo anayetaka kula nguruwe ruksa.
Vilevile, Mwinyi ndiye aliyetuliza pepo mwingine mbaya pale waumini wa dini ya Kiislamu Zanzibar walipoandamana kupinga kauli ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Kawawa (marehemu) aliyedai ndoa za wake wengi zinachangia maambukizi ya Ukimwi. Mwinyi aliwaambia yale yalikuwa maoni yake na si msimamo wa Serikali.Mwinyi atakumbukwa na wafanyabiashara ndogondogo kwa vile ndiye aliyeruhusu kila mtu kufanya kazi halali ya kumwingizia kipato. Mazingira hayo kwamba ni ruksa kufanya kazi yote halali ndiyo yalisababisha Watanzania kumbatiza jina la ‘Mzee Ruksa’.Mbali ya kuhimiza umuhimu wa elimu, alielimisha matumizi ya kondomu ili kujiepusha na maambukizi ya ukimwi. Hata hivyo, mwaka 2009 alipohutubia Baraza la Maulid na kuwataka Waislamu wajikinge na maradhi hayo, kijana mmoja alimpiga kibao.Hadi leo akipata fursa au akialikwa kwenye vipindi mbalimbali hufafanua matumizi sahihi ya maneno au mnyambuliko sahihi. Mfano ni maneno “onya” na “ona”. Anafundisha kitendo cha kutaka mtu aone kitu fulani unasema “onesha” na siyo “onyesha” kama ilivyozoeleka kwani onyesha linatokana na onya.Anapozungumza, hadi leo, hotuba yake hujaa methali na nahau au tamathali nyingine za semi na lafudhi inayoburudisha wasikilizaji. Huyo ndiye Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Mzee Ruksa ambaye kwa sasa anaishi Msasani, Dar es Salaam.

No comments: