Friday, 15 May 2015

Tuendelee na kona ya Julius Mtatiro.

Leo tunaanza uchambuzi wa majimbo ya Mkoa wa Morogoro, tukiukamilisha mkoa huu tutakuwa tumehesabu jumla ya mikoa 17 ambayo tumefanikiwa kuchambua majimbo yote yaliyomo kwenye mikoa hiyo.Morogoro ni moja ya mikoa mikubwa  inayopatikana Tanzania au Mashariki mwa nchi yetu. Mkoa huu una historia tele ambazo hazitoshi kuelezewa na safu hii. Mkoa huu una tarafa 30, kata 141 na vijiji 543.Morogoro inapakana na mikoa ya Tanga, Pwani, Lindi, Ruvuma, Iringa, Dodoma na Arusha, huku ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 73,939 na jumla ya wakazi 2,218,492. Hii ni kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.Pia mkoa huu unaundwa na wilaya saba ambazo ni Morogoro Manispaa, Morogoro Vijijini, Kilombero, Kilosa, Gairo, Mvomero na Ulanga.
Eneo la Mkoa wa Morogoro liko katikati ya mikoa ya pwani ya Bahari Hindi na Nyanda za Juu. Kuna tambarare za chini kama vile Ifakara, Kilombero, pia milima ya juu kama Uluguru penye mlima wa Kimhandu wenye mita 2646 juu ya usawa wa bahari.Pia kuna mito mikubwa kama vile Wami na Ruvu inayoanzia kwenye milima ya Uluguru. Ruvu ndiyo mto wa pekee unaosaidia usambazaji wa maji katika jiji la  Dar es Salaam.Karibu nusu ya eneo la Mkoa wa Morogoro ni hifadhi za wanyama za Mikumi na Milima ya Udzungwa, bila kusahau sehemu ya eneo la kuwinda wanyama la Selous.Kabila kubwa la asili hapa Morogoro ni Waluguru waliotoa jina kwa mji wa Morogoro pamoja na milima ya Uluguru. Makabila mengine makubwa zaidi ni Wangulu, Wakagulu, Wasagala, Wapogolo, Wandamba, Wabena, Wambungu, Wakutu na Wavidunda
.
Mkoa wa Morogoro ni muhimu hata katika eneo la miundombinu muhimu ya usafiri wa nchi. Barabara kuu za lami za Dar es  Salaam - Morogoro - Mbeya - Zambia/Malawi na Dar es Salaam - Morogoro - Dodoma, hupita eneo la mkoa huu. Hata reli ya kati hupita hapa kuelekea Mwanza au Kigoma. Reli ya Tazara nayo inapita mkoani hapa katika wilaya ya Kilombero.Kwa upande wa shughuli za kiuchumi, wakazi wa mkoa wa Morogoro kwa kiasi kikubwa wanategemea kilimo ambacho pia hutegemea uwepo wa mvua. Kutokana na hali nyepesi ya unyevunyevu, Morogoro hupokea mvua nyingi kwa mwaka na hivyo mazao ya biashara kama vile miwa, mahindi na mengineyo hulimwa kwa wingi. Ndiyo maana, viwanda vikubwa vya kuzalisha sukari vinapatikana mkoani hapa. Mkoa huu kisiasa una majimbo 10 ya uchaguzi; majimbo ya Ulanga Magharibi na Ulanga Mashariki yaliyoko wilaya ya Ulanga. Majimbo ya Gairo, Kilosa na Mikumi yaliyoko Wilaya ya Kilosa, Majimbo ya Morogoro Kusini na Morogoro Mashariki yaliyoko katika Wilaya ya Morogoro Vijijini, jmbo la Morogoro Mjini lililoko katika Manispaa ya mji wa Morogoro, jimbo la Mvomero wilayani Mvomero na lile la Kilombero katika Wilaya ya Kilombero.
Jimbo la Mvomero 
Jimbo la Mvomero ni eneo lote la mamlaka ya Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na linaundwa na jumla ya kata 28, vijiji 130 na vitongoji 691.Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Mvomero ina wakazi 312,109, wanaume ni 154,843, wanawake 157,266 na kuna wastani wa watu wanne katika kila kaya.Mvomero halikuwa jina maarufu miaka ya 1995 wakati mfumo wa vyama vingi unaanza. Wakati huo jimbo hili liliitwa Morogoro Kaskazini hadi baada ya mwaka 2000 ndipo Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikalipa jina jipya Mvomero.
Kivumbi cha hali ya juu kilitokea jimboni hapa  mwaka 1995, baada ya jumla ya vyama saba kujitokeza na kuweka wagombea. Vyama vilivyojitokeza ni UDP, NRA, TLP, CCM, CUF, NCCR na Chadema. Hata hivyo, vyama vilivyoonekana kuwa na nguvu ya kutosha ni Chadema, NCCR na kwa mbali  sana NRA.
Lakini kama ilivyokuwa kwa majimbo mengi, CCM ilitumia fursa ipasavyo ikiwakilishwa na Profesa Nicas Mahinda ambaye aliibuka mshindi wa jumla kwa kura 27,717 akifuatiwa na mgombea wa NCCR, Odillo s Msimbe aliyepata kura 11,068, huku yule wa NRA, Athumani Mdoe akipata kura 1,985. Huu ni uchaguzi ambao uliwaacha wagombea kutoka vyama vingine vinne vilivyobakia wakiwa na asilimia 8.4 ya kura zote.
Mwaka 2000 pia wana Kilombero walimchagua mbunge kutoka CCM na aliongoza hadi mwaka 2005.
Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 tayari jimbo hili lilianza kuitwa mvomero na si Morogoro Kaskazini. Kama ilivyokuwa mwaka 1995. Mara hii pia vyama saba vilijitokeza na wagombea wake mkononi. Kulikuwa na  na Jahazi Asilia, UPDP, UDP, CCM, TLP, Chadema na CUF. Nguvu ya CCM ilikuwa haina mfano, kwa hiyo upinzani haukutarajiwa kuvuna matunda makubwa. Ndiyo maana matokeo ya mwisho yalimtangaza mshindi kutoka CCM tena kwa kura zilizopitiliza.Mgombea huyo, Ahmed Saddiq Suleiman alipata kura 77,564. Waliomfuatia walikuwa wagombea kutoka Chadema, Owden Matokeo aliyepata kura 6,160  na CUF, Thabiti Idi  aliyepata kura 5.960. Ushindi huu ndiyo uliendelea kuifanya CCM iliongoze jimbo hili hadi mwaka 2010.
Mwaka 2010, kasi ya mchezo ilianzia ndani ya CCM ambako makada wawili wenye nguvu walipambana na kutoana jasho ipasavyo. Hawa ni Amos Makala aliyekuwa Katibu wa NEC wa fedha na uchumi na mbunge aliyekuwa anamaliza muda wake, Ahmed Saddiq Suleiman. Saddiq aliangushwa na Makala vibaya baada ya kuzidiwa kwa kura takribani ya 7000 kati ya kura takribani 20,000 zilizopigwa na wana CCM. Kwa hiyo, Makala alipewa dhamana ya kukutana na kushindana na wapinzani.
Katika kiini cha uchaguzi chenyewe, Makala alifanikiwa kuongoza kwa kupata kura 41,884 na aliyemfuata kwa kasi nzuri ya ushindani ni mgombea wa Chadema, Owden Matokeo ambaye aliyepata kura 17,796, huku wagombea wa CUF, NCCR na UDP wakipata asilimia mbili  ya kura zote.Amos Makala alianza uongozi wa jimbo hili tangu kipindi hicho hadi leo na amefanikiwa kufanya mambo mengi kwa kadri alivyoweza, lakini pia akishindwa mambo mengi kadhaa ya msingi.Jambo moja kubwa hadi leo ambalo limemshinda Makala hadi leo ni kushughulika na kero za wakulima wa miwa ambao wamefanya hivyo kwa kipindi kirefu bila mafanikio.
Jimbo la Kilombero
Jimbo la Kilombero ni eneo lote la Wilaya ya Kilombero. Jimbo hili linaundwa na jumla ya kata 35, vijiji 100 na vitongoji 495 na kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, kuna jumla ya watu 407,880, wanaume ni 202,789 na wanawake wakiwa 205,091. Pia, kuna wastani wa watu wanne katika kila kata.Katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, mwanamichezo maarufu, marehemu Abbas Gulamali ambaye amewahi kuongoza klabu Yanga, ndiye alikuwa mgombea wa CCM akipambana na wagombea wengine kutoka vyama vya UDP, TPP, Chadema, NCCR na CUF.
Kilombero ni jimbo lenye mwelekeo mkubwa wa mabadiliko, ndiyo maana “unguli” wa Gulamali na ukongwe wa CCM haukumpa asilimia za ushindi wa daraja la kwanza. Gulamali alipata kura 32,912 akafuatiwa na mgombea wa NCCR, Reginald Chimulimuli Magwaja aliyepata kura 9,659. Wagombea kutoka vyama vya CUF, Chadema, UDP na TPP walipata asilimia 5.5 ya kura zote kwa jumla. Kwa hivyo, Abas Gulamali wa CCM ndiye alikuwa mbunge wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi.
Kwenye uchaguzi wa mwaka 2000, alishinda pia Abas Gulamali wa CCM wakati ambapo upinzani haukuonyesha nguvu za kuthubutu. Hata hivyo, Gulamali alifariki dunia  mwaka 2003 na hivyo uchaguzi mdogo uliitishwa na Abu Kiwanga wa CCM akashinda lakini naye kabla ya kumaliza muda wake akafariki dunia. Kwa kuwa muda wa uchaguzi ulikaribia, Tume ya Uchaguzi haikutangaza uchaguzi mwingine wa marudio.
Mwaka 2005 ulipofika, vyama vinne vilijiandaa kuligombana jimbo hili, CCM, UPDP, CUF na Chadema. Kura zilipopigwa mapambano yalikuwa baina ya CUF na CCM huku Chadema ikiwa mpambanaji wa mbali. Mara hii CCM ilimleta Castor Ligallama ambaye alipata asilimia kura 90,245, wakati mshindani wake mkuu kutoka CUF, Kassim Mtalam akipata asilimia kura 20,814.Mgombea wa Chadema katika uchaguzi huo, Susan Kiwanga (sasa Mbunge wa viti maalumu Chadema), alipata kura 7,421, huku yule wa UPDP akiambulia asilimia 0.8. Ligallama   aliongoza jimbo hili na kulifikisha mwaka 2010.
Mwaka 2010, wagombea wanne wenye nguvu walishindana kutafuta tiketi ya kukiwakilisha chama hicho, miongoni mwao alikuwa ni mbunge anayemaliza muda wake Ligallama ambaye aliangushwa vibaya na Abdul Mteketa kwenye kura hizo.Kwa hiyo CCM ikawakilishwa na Abdul Mteketa katika uchaguzi wa jumla ulioshuhudia mabadiliko na kiu kubwa ya mabadiliko kwa wana Kilombero. Aliyevumisha mabadiliko makubwa ya kisiasa hapa Kilombero ni mwanadada Regia Mtema (sasa Marehemu) aliyekuwa kada kindakindaki wa Chadema.
Wananchi wa Kilombero niliobahatika kuongea nao, wanasema hawaelewi kwa nini Regia hakushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, kwani mgombea wa CCM hakuwa anakubalika na chama hicho kiliingia kwenye uchaguzi kikiwa kwenye mpasuko mkubwa.Katika uchaguzi huo, Mteketa wa CCM alipata kura 43,459 na Regia wa Chadema akiwa na kura 38,550, huku  Zainabu Ibrahim wa CUF akipata asilimia 5.02 ya kura zote. Hata hivyo, ikiwa vyama vya CUF na Chadema vingesaidiana kumuunga mkono mgombea mmoja, jimbo hili lingekwenda upinzani bila ubishi wowote.
Mbunge wa sasa wa Kilombero kwa tiketi ya CCM ana nafasi ndogo ya kurejea tena, kwa sababu haungwi mkono na wananchi wa jimbo hili na hata ndani ya CCM kwenyewe. Mipasuko ya ndani ya CCM ya mwaka 2010 imeibuka tena na hali hiyo inamnyima nafasi.
Vyama vya CUF na Chadema vimezidi kujiimarisha nadhani kuliko wakati wowote ule kihistoria. Ndiyo maana kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Disemba mwaka jana Chadema ilifanikiwa kuchukua vijiji 39, CUF ikipata vijiji 14 na CCM ikiachiwa vijiji 59 tu. Kabla ya uchaguzi huo, CCM ilikuwa inaongoza vijiji zaidi ya 80 na mabadiliko haya yana maana kubwa.
Makada wa Chadema zaidi ya 15 waliandika barua kuomba nafasi ya kugombea kwenye kura ya maoni kulisaka jimbo hili wakati CUF wakijitokeza zaidi ya makada watano. Wawili ambao nawafahamu ni Remija Mtema (Mdogo wa marehemu Regia Mtema) na Dismas Lyassa –ambaye ni mwandishi wa habari wa siku nyingi.
Nachokiona hapa Kilombero ni kwamba wananchi wako tayari kulikabidhi jimbo hili kwa upinzani, kitakachohitajika ni kutokuwepo kwa mpasuko ndani ya chama kitakachokabidhiwa jimbo hili na Ukawa. Hakika, jimbo hili la Kilombero halitabaki CCM kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Jumamosi ya wiki hii (Tarehe 16 Mei 2015) tutaendelea na uchambuzi wa majimbo ya Morogoro Mjini, Morogoro Kusini na Morogoro Mashariki, yote ya mkoani hapa na keshoye (Jumapili, 17 Mei) tutajikita kwenye majimbo ya Gairo, Kilosa na Mikumi.

No comments: