Tuesday 9 June 2015

Neno ni Mamlaka Kamili ya Wazanzibari

Video za uzinduzi wa Mgombea Urais kwa CUF kwa upande wa Zanzibar Shughuli  mbalimbali zilisimama kwa muda wakati wa Mkutano wa Chama cha Wananchi (CUF) uliohutubiwa na  Viongozi wa juu wa CUF pamoja na Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad.Maalimu Seif ambaye tayari amechukua fomu kugombea urais kupitia chama hicho, alihutubia maelfu ya wananchi na wakazi wa Zanzibar kwenye Uwanja wa Kibandamaiti.
Hali ilivyokuwa, wakazi wengi wanaoishi karibu na uwanja huo walisimamisha shughuli zao na kuungana na wananchi kutoka maeneo mbalimbali visiwani humo ili kuhudhuria mkutanmo huo.
Katika mkutano huo, Maalim Seif aliwaahidi Wazanzibar kubadilisha kisiwa hicho na kuwa kisiwa chenye matumaini na fursa mbalimbali za kiuchumi tofauti na ilivyo sasa chini ya utawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). “Nakusudia kuifanya Zanzibar kuwa visiwa vya fursa za biashara na ajira kwa wananchi.”


Maalim Seif ambaye tayari chama chake kimemteua rasmi kuwa mgombea wa nafasi ya urais visiwani humo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015. Amesema, Zanzibar inazo fursa nyingi za kuweza kunyanyua kipato cha wananchi, na kwamba ataweka kipaumbele katika kuziibua na kuziendeleza fursa hizo. Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema katika kujenga mazingira bora ya uwekezaji, ataisimamia ipasavyo Mamlaka ya vitega uchumi, ili kuondosha vizingiti vinavyokwamisha uwekezaji nchini.


Amefahamisha kuwa wapo wafanyabiashara wengi wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya kuwekeza miradi mikubwa ya kiuchumi, lakini wamekuwa wakipata usumbufu, jambo ambalo ameahidi kulishughulikia muda mfupi baada ya kuingia madarakani. Sambamba na hilo, Maalim Seif amesema iwapo atachaguliwa kuiongoza Zanzibar, atahakikisha kuwa Zanzibar inakuwa na shirika lake la ndege ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, ili kurahisisha shughuli za kibiashara ikiwemo Utalii.
Amesema hatua hiyo itakwenda sambamba na uboreshaji wa huduma za viwanja vya ndege, ambavyo vitaweza kutoa huduma bora kitaifa na kimataifa.

Aidha amesema chini ya uongozi wake iwapo atapata ridhaa ya kuongoza nchi baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015, ataitangaza Zanzibar kuwa bandari huru, sambamba na kujenga bandari mpya itakayotoa huduma bora kwa mwambao wa Afrika Mashariki. Katika hatua nyengine Maalim Seif amesema anakusudia kuongeza viwango vya mishahara kwa wafanyakazi wote, pamoja na kuzingatia maslahi ya wastaafu na wazee wasiojiweza.


Akizungumzia kuhusu mafuta, Maalim Seif amesema anakusudia kuanzisha Wizara ya Mafuta na Gesi ili kurahisisha uchimbaji wa nishati hiyo, itakayoondosha hali ya umasikini katika visiwa vya Zanzibar.Maalim Seif pia alizungumzia hali ya amani na utulivu nchini, na kueleza kuwa amani ya kweli itapatikana iwapo vyombo vinavyohusika vitatoa haki kwa wananchi wote.

Mapema akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CUF Taifa, Prof. Ibrahim Lipumba, amesema Baraza Kuu la Uongozi la CUF limeshawishika kumuidhinisha Maalim Seif kuwa mgombea Urais wa Zanzibar, kutokana na uwezo na nia ya dhati ya kuwatumikia wazanzibari.


Amesema, viongozi waliopo madarakani wana dhamana na wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu ujao unafanyika katika hali ya amani, sambamba na kuheshimu maamuzi ya wananchi katika uchaguzi huo.






Amwasisitiza kuwa Zanzibar mpya haitakua na ubaguzi kwa yoyote yule .

No comments: