Wednesday, 12 August 2015

Lipumba kajivua Uenyekiti au kavuliwa?WENGI yanasemwa siku hizi kumhusu Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, aliyekuwa mwenyekiti wa taifa wa Chama cha Wananchi (CUF) kabla ya kujiuzulu wadhifa huo Agosti sita mwaka huu. Hatua hiyo ya kujiuzulu uenyekiti, au kwa lugha ya kileo “kujivua” uenyekiti, ni hatua ambayo imekuwa ikijadiliwa usiku na mchana kwenye mitandao ya kijamii, vyombo vya habari, barazani na vijiweni kote nchini. Kwa hakika, ilianza kujadiliwa hata kabla ya Lipumba kutangaza rasmi kwamba anauachia uongozi wa chama chake. Mjadala huo ni wenye kustahiki kwasababu Lipumba ana uzito fulani katika siasa za taifa hili. Kwa kiwango kikubwa uzito wake wa kisiasa unatokana na chama alichokuwa akikiongoza. Hiki ni chama ambacho katika muda wa miaka michache kiliweza kujijenga, kikaimarika na kuwa chama kikuu cha upinzani Tanzania. Nafasi hiyo, kwa sasa, inashikiliwa na chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

 
Juu ya mikwaruzano tuliyoishuhudia miongoni mwa viongozi wake, Chadema kimeweza kukipiku chama cha CUF kwa kuwa na wabunge wengi waliochaguliwa Bara katika uchaguzi mkuu wa 2010. Mtu hataki kuambiwa kwa nini ikawa hivyo. Sababu za kuanguka kwa CUF Bara ni uongozi dhaifu wa chama hicho huko Bara. Udhaifu huo, kwa upande wake, umesababishwa na msimamo wa kiongozi wake mkuu ambao baadhi ya nyakati ulikuwa haueleweki na ukiwakanganya wenzake. Si siri kwamba kwa muda kumekuwako na mgongano wa fikra kati yake na wenzake kuhusu baadhi ya masuala ya kimsingi ya sera za chama hicho. Mgongano ulioibuka karibuni unahusu kukubaliwa waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa kuwa mgombea urais kwa niaba ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umoja unaovijumuisha vyama vikuu vya upinzani dhidi ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Mgongano huo ndio uliomfanya auache uenyekiti wa CUF.

Amechukua hatua hiyo katika wakati nyeti kabisa, wakati ambapo kwa mara ya mwanzo katika historia ya Tanzania chama kinachotawala kinakabiliwa na kitisho kikubwa kisichowahi kutokea kutoka vyama vya upinzani. Kitisho hicho kimezidi kukua kwa Lowassa kupeperusha bendera ya Ukawa katika uchaguzi wa urais wa Oktoba 2015. Kama Lowassa ni fursa ya upinzani kujipatia ushindi basi mwanasiasa wa upinzani aliye mahiri huinyakua fursa hiyo bila ya kusita. Ndipo Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe alipoonesha tena umahiri wake wa kisiasa kwa kumpisha Lowassa awe mgombea wa urais wa chama chao cha Chadema. Katika uchaguzi wa 2010, Mbowe alimpisha Dk. Wilbrod Slaa awe mgombea wa urais kwa niaba ya Chadema. Si kwamba yeye Mbowe hakuhisi kwamba ana uwezo lakini baada ya kuipima hali ya mambo ilivyokuwa wakati huo, aliamini kwamba mtu ambaye angalifaa kuwa mgombea wa urais wa Chadema alikuwa Slaa. Kwa kufanya hivyo, Mbowe aliyaweka nyuma maslahi yake binafsi. Safari hii Mbowe alitambua wazi kwamba Lowassa ana uwezo kushinda yeye wa kuunyakua urais. Lipumba hakuliona hilo; au labda ameliona lakini hataki kuamini; au labda kuna waliomshinda akili wenye kumuona kwamba yeye ndiye mwenye uwezo wa kumhakikishia ushindi mgombea urais wa CCM.

Si dhamira yangu kumsulubu Lipumba.Lakini kuna maswali ambayo hatuna budi kujiuliza. Kwa mfano, tunajuwa kwamba alipoamua kwa mara ya mwanzo kuwania urais kwa niaba ya CUF huo haukuwa uamuzi wake yeye mwenyewe binafsi. Ulikuwa uamuzi alioukata baada ya kushawishiwa na kushinikizwa na maswahiba wake fulani ambao ni miongoni mwa mihimili ya CCM. Swali linalozuka hapa ni: jee, Lipumba amehiari mwenyewe 2015 kujivua uenyekiti wa CUF au alishawishiwa na maswahiba wake walewale waliomzidi fikra na walio ndani ya CCM? Waliomuingiza CUF ndio haohao wanaotaka sasa kumtoa na kutimiza lengo la kuigawa CUF? Kweli, ndio wao waliomshikilia ajivue uenyekiti wa CUF katika jaribio la kuusambaratanisha Ukawa?Lengo lao la kuusambaratisha Ukawa ni wazi:kumzuia Lowassa asiunyakue urais Oktoba ijayo.

Hata hivyo, tukio hili la Lipumba si la ajabu hivyo. Tulikwishaandika kabla tukionya kwamba CCM na washabiki wake watatumia hila za aina kwa aina ili kuleta mtafaruku ndani ya kambi ya upinzani. Tutakuwa tunajidanganya tukidhani kwamba hapawezi kutokea pigo jengine katika kambi hiyo ya upinzani. Panaweza pakazuka mengine yaliyo makubwa zaidi. Lililo muhimu kwao wapinzani ni kuendelea kuwa imara na kuendeleza moyo wa ushirikiano bila ya kusahau kwamba lengo lao kuu ni moja: kuleta mfumo wa utawala ulio mbadala wa huu wa sasa ambao wenyewe umechoka na ambao wananchi wamechoka nao. Hatua ya Lipumba ya kujiuzulu uenyekiti wa CUF ni hatua isiyoeleweka unapozingatia dhamira kuu ya upinzani ya kuiondoa CCM madarakani. Kwa kuichukua hatua hiyo Lipumba ameonesha kwamba hakuwa na nia ya dhati ya kuung’oa utawala wa CCM.

Lipumba mwenyewe amesema kwamba alilazimika kuchukua hatua hiyo kwasababu za kimaadili. Amesema kwamba amekerwa na hatua ya Ukawa ya kumkubali Lowassa na kumsimamisha awe mgombea wake wa urais katika uchaguzi ujao. Aliongeza kwamba Lowassa ni mmoja wa waliokuwa wakiipinga Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba. Kwahivyo, alisema kumkubali Lowassa kunaifanya nafsi yake iwe inamsuta. Hayo ni matamshi ya ajabu kwani kwa mujibu wa waliokuwa karibu naye, Lipumba alishiriki katika mashauriano ya Ukawa ya kumkubali Lowassa.Iweje leo adai kwamba nafsi yake inamsuta? Ikiwa ni hivyo, kwamba anaacha hatamu za uongozi wa CUF kwa sababu ya Lowassa basi ameshindwa kung’amua kwamba katika mbinu za uchaguzi kuna kushinda na kushindwa. Ikiwa Lipumba amechukua hatua hiyo kwa ajili ya maadili basi hana uweledi wa kisiasa, hazijui namna siasa zinavyoweza kuwa chafu na namna anavyopaswa kuzicheza siasa zinapogeuka na kuwa chafu. Tuseme anakuwa hatambui kwamba kuna nyakati ambapo mtu hulazimika kufanya maamuzi magumu, kuyameza aliyoyatapika, kuyakubali yale aliyokuwa akiyakanya akitambua kwamba kwa kufanya hivyo atalifikia lengo lake.

Aghalabu hilo lengo huwa ni kubwa zaidi kushinda pengine hata huo anaoamini kuwa ni msimamo wake wa kimaadili. Katika muktadha wa mgombea wa urais , kwa mfano, mwanasiasa aliye mahiri huangalia nani anayefaa kuwa mgombea huo kwa wakati huu. Huangalia nani anayefaa, sio nani anayestahiki. Huo ndio ukweli wa kisiasa, utambuzi wa hali halisi zilivyo katika wakati fulani. Ukifanya uchunguzi wa kina kwa hivi sasa hutakosa kutambua kwamba miongoni mwa viongozi wa Ukawa, kwa wakati huu tulionao, si Lipumba, wala si Slaa, wala si mwengine yeyote miongoni mwao anayefaa kuchuana na Dk. John Magufuli, mgombea urais wa CCM. Hiyo ndiyo hali halisi ilivyo.Tukitaka tusitake, ndio ukweli ulivyo. Ikiwa lengo ni kuing’oa CCM madarakani basi katika wakati huu tulio nao anayefaa ni Lowassa. Utambuzi huo unaweza ukawa na uchungu wa shubiri lakini mwanasiasaa aliyeazimia kutekeleza lengo fulani hana budi ila kuinywa shubiri hiyo naiwe chungu namna gani. Kwanza huhakikisha kwamba lengo linapatikana na halafu mingine yatafuata. Ikiwa kwa kumpokea Lowassa kutawafungulia njia wengine wakihame chama cha CCM na hatimaye kuking’oa madarakani basi viongozi wa Chadema na Ukawa watakuwa wanaitumia kete hiyo ipasavyo. Huenda Lowassa akawa siye anayestahiki.Lakini hamna shaka kwamba yeye ndiye anayefaa.Na anafaa kwa sababu anaonekana kuwa mwanasiasa mwenye uwezo ambao Lipumba na Slaa hawaoneshi kuwa nao kwa wakati wa sasa. Sio kwamba hao wawili ni wajinga. Ukawa ishinde isishinde suala la ufisadi halitoondoka mara moja. Na huko si kuashiria kushindwa kwa jitihada za kuupiga vita ufisadi, lakini ni kutambua kwamba haitoshi kuupigia kelele na kuukemea. Itabidi ung’olewe, usiote tena mizizi. Mwisho wamambo. Katika hali ambapo siasa hugeuka na kuwa chafu, mwanasiasa mwenye uweledi huziba pua yake akaendelea kuutekeleza mkakati wake. Lipumba, kama kweli ni kiongozi mwenye nia ya kusafisha mambo, alishindwa kulitekeleza. Kwa hali ilivyo sasa Tanzania hamna shaka yoyote kwamba tumo katika kipindi muhimu cha kihistoria cha kuelekea mageuzi ya mfumo wa utawala. Wapinzani wanaamini hivyo, wananchi wanaamini hivyo, na hata kuna baadhi ya viongozi wa CCM yenyewe wenye kuamini hivyo.

 Wanatambua kwamba safari hii wapinzani wameungana na kuwa kitu kimoja, kinyume na ilivyokuwa katika uchaguzi za huko nyuma. Leo wameonyesha kuwa wanaweza kuwa na nguvu moja, ile Lowassa anayoiita “People’s Power” (Nguvu ya Umma). Miongoni mwa wafuasi wake Lowassa mna vigogo wa CCM ambao bado wangaliko ndani ya chama hicho. Hawajatoka kumfuata Lowassa. Pengine unajiuliza: kulikoni? Hawa wasikushangaze. Wanabakia ndani ya CCM kuzidi kuichimba ndani kwa ndani kama mchwa. Matokeo yake ni kwamba CCM haijijui tena; haijui nani wa kumuamini na nani wa kutomuamini. Kwa chama kilichozoea kushika madaraka kwa zaidi ya nusu karne hii ni hali nyeti na yenye hatari kwake. Aghalabu katika hali kama hiyo chama cha kisiasa huanza kutapatapa na kutumia nguvu Kinachotakikana ni uongozi ulio imara na wenye muono mpya utaolingana na mageuzi yanayotarajiwa kutokea karibuni. Kwa ufupi, ningesema kwamba ingawa Lipumba ni mtaalamu aliyebobea katika fani ya iktisadi na masuala ya uchumi,kwa jumla, lakini tukija katika medani ya siasa inaonesha wazi kwamba ana kasoro fulani. Hesabu zake za kisiasa hazikukamilika. Ndio maana waliomzidi maarifa hawakuwa na kazi ngumu ya kumsaidia ajivue uenyekiti wa CUF.

No comments: