Saturday, 19 September 2015
Balozi Seif Afungua Mkutano wa Siku Amani Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiufungua Mkutano wa Siku Mbili wa Marafiki wa Zanzibar unaofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. kushoto ya Balozi Seif waliokaa ni Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Fadhil Suleiman Soraga na Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji Khamis.
Muwakilishi wa Taasisi ya Kiislamu kutoka Nchini Uganda Ustaadhat Asma Kunagwa akitoa salamu za Taasisi yake katika Mkutano wa siku mbili wa Amani Zanzibar.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Siku Mbili wa Amani ulioandaliwa na Taasisi ya Marafiki wa Zanzibar unaofanyika Zanzibar Beacha Resort ukihudhuriwa na washiriki wa Nchi 9 za Afrika.
Balozi Seif Ali Iddi aliyepo kati kati ya waliokaa akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mkutano wa Amani unaofanyika katika Hoteli ya Zanzibar Beacha Resort Mzizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.Picha na – OMPR – ZNZ.
Na. Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema upo uhakika kwa Taifa kujiepusha na mauaji, chuki, mifarakano na maasi yote yanayokatazwa na Mwenyezi Muungu endapo kila Kiongozi wa Dini atatumia muda mchache kuwausia wafuasi wake kuishi kwa amani, kuvumiliana, kuheshimiana pamoja na kupendana.
Alisema kazi kubwa iliyo mbele kwa Viongozi hao wa Dini kwa kushirikiana na Wazazi ni kuwasaidia Vijana wao ambao ndio wengi katika Jamii ili waweze kufuata maadili mema ambapo watakuwa na uhakika wa kutoa mchango mkubwa katika kuliendeleza Taifa lao.
Akiufungua Mkutano wa Siku mbili wa Amani Zanzibar unaofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Taifa likipoteza Vijana katika itikadi zisizo sahihi jamii inapaswa kuelewa kwamba Amani ya Nchi inawekwa Rehani.
Balozi Seif alisema ukosefu wa kuwalinda vijana kwa kuwatayarisha kuelekea katika kuleta Maendeleo na Dini na Taifa lao, watafanywa kuwa silaha za maangamizo.
Alifahamisha kwamba inasikitisha kuona Vijana wa Kiislamu wanaingia na kujihusisha na vikundi vya tikadi zisizokuwa za ukweli katika Dini jambo ambalo baadaye huwaingiza katika majanga na matokeo yake kutengwa na jamii zao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliiomba Taasisi ya Marafiki wa Zanzibar ambayo ndio iliyoandaa Mkutano huo wakijumuika pamoja na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali kuliangalia kwa uana suala hilo la Amani kwa vijana.
“ Neno Amani limekuwa likitajwa na kurudiwa mara kwamba na watu wengi. Ukweli ni kwamba amani haina mbadala. Mbadala wa amani ni machafuko na ili kusiwepo machafuko lazima misingi ya amani ifuatwe “. Alisema Balozi Seif.
Alieleza kwamba njia pekee kwa jamii ambayo itasaidia kudumisha amani ya Taifa ni kutii sheria na taratibu zilizowekwa na Wananchi wenyewe jambo ambalo ni muhimu katika kuelekea kwenye safari ya kulinda amani na usalama wa Nchi.
Balozi Seif alitanabahisha Wazanzibari na Watanzania wote kuelewa kwamba Taifa hivi sasa linahityaji amani, kuvumiliana na kuheshimiana ili liweze kumaliza zoezi zima la uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba kwa salama.
Mapemba Mwenyekiti wa Taasisi ya marafiki wa Zanzibar Dr.Mustafa Yussuf Ali alisema kwamba utumiaji vibaya wa Dini ndio chanzo kikuu cha migogoro inayosababisha umwagaji wa Damu na hatimae kusababisha vifo.
Dr. Mustafa alisema Jamii imekuwa ikishuhudia kila mara baadhi ya Makundi yakiwemo yale ya harakati na ya Kidini yamekuwa yakichangia vurugu zinazoibuka kufuatia kauli na vitendo vyao.
Mwenyekiti huyo wa Taasisi ya Marafiki wa Zanzibar aliwakumbusha na kuwasa Viongozi wa Vyama cha CCM na CUF ambao ndio wenye wafuasi wengi hapa Zanzibar kuwa mfano mwema kwa Watoto wao katika kulinda Amani ya Nchi.
Alifahamisha kwamba Wazanzibari na Watanzania ndio wadau wakubwa wa kuhakikisha amani na utulivu wa Taifa unaendelea kubakia muda wote kabla na baada ya uchaguzi Mkuu ujao.
Wakiwakilisha salamu za urafiki na upendo kutoka Mataifa rafiki washiriki wa Mkutano huo kutoka Nchi tofauti za Afrika hasa zile zilizo katika jangwa la Sahara walisema waislamu wa Zanzibar wana dhima kubwa ya kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba unafanyika kwa amani.
Washiriki hao walisema suala la amani ndio hasa katiba ya Kiislamu iliyochambua sera na mfumo wa Dini ya Kiislamu ambalo linapaswa kusimamiwa kwa hatma ya vizazi vya sasa na vile vya baadaye.
“ Utovu wa Amani unaelezwa kwamba ni uovu ambao inasisitizwa katika uislamu ama uondoshwe, ukemewe au muhusika anayeuona kama anashindwa na hayo ana wajibu wa Kuchukia “. Alisema Mmoja wa washiriki wa Mkutano huo kutoka Nchi rafiki.
Walieleza kwamba hakuna Muislamu wa kweli asiyeelewa umuhimu wa amani ambayo ndiyo inayotoa nafasi kwa jamii kuendelea kufanya shughuli zao za Kimaisha za kila siku sambamba na kutekeleza ibada.
Mapema Naibu Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Thabit Nauman Jongo akitoa muhtasari wa Mikutano ya Taasisi ya Marafiki wa Zanzibar baada ya kukubaliwa kuendesha shughuli zao hapa Zanzibar alisema yapo mafan ikio makubwa yaliyojitokeza ya kuisimamia amani kufuatia mikutano ya Taasisi hiyo.
Sheikh Jongo alisema Taasisi ya Marafiki wa Zanzibar imeingia Zanzibar Mwaka 2014 na kuomba Kibali cha kufanya kazi zake hapa Zanzibar katika kuelezea umuhimu wa kudumishwa kwa amani ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.
Alisema hatua ya Taasisi hiyo imekuja kufuatia matukio mbali mbali yaliyowahi kutokea katika baadhi ya mataifa ya Afrika ya kuichezea amani na kusababisha majanga yatakayoendelea kukumbukwa milele na vizazi vya Mataifa hayo.
Washiriki wa Mkutano huo wa Marafiki wa Zanzibar wanatoka katika Mataifa ya
Mzumbiji, Malawi, Zambia, Namibia, Rwanda, Uganda Kenya, Tanzania Bara na wenyeji Zanzibar.
Ujumbe wa Mkutano huo wa Siku mbili wa Marafiki wa Zanzibar unaeleza kwamba Uchaguzi utapita Zanzibar itabaki. Piga kura kwa amani na Maendeleo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment