Tuesday 8 September 2015

Wazanzibari wanapoikana sheria ya Mitandao

Kifungu ulichokirejea ambacho ni 132 cha Katiba ya Zanzibar 1984 kinasema:


132(1) Hakuna sheria yoyote itakayopitishwa na Bunge la Muungano ambayo itatumika Zanzibar mpaka sheria hiyo iwe ni kwa ajili ya mambo ya Muungano na ipitishwe kulingana na maelekezo ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

(2) Sheria kama hiyo lazima ipelekwe mbele ya Baraza la Wawakilishi na Waziri anaehusika"


Utaona hapo masharti ya kikatiba ili sheria hii (au nyengineyo yoyote iliyopitishwa na Bunge la Muungano) itumike Zanzibar ni matatu:

1)Iwe ni kwa jambo la Muungano.

2)Ipitishwe kulingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

3)Iwasilishwe Baraza la Wawakilishi.


Swali la kujiuliza : Mambo ya Mtandao wa Mawasiliano ya Intaneti ni jambo la Muungano? Katiba ya JMT Nyongeza ya Kwanza imetaja orodha ya mambo 22 kuwa ni Mambo ya Muungano. Lakini Mawasiliano ya Intaneti halimo. Ingawaje kipengele cha orodha cha 11 yanatajwa mambo ya " Bandari, mambo yanayohusiana na usafiri wa anga , posta na simu"

Jee ukisema SIMU unamaanisha pia Mawasiliano ya intanet?

Katika Katiba Inayopendekezwa , nadhani kwa kuona kasoro hii , imewekwa wazi kuwa "Mawasiliano " ni jambo la Muungano.

Maoni yangu ni kuwa SIMU haijumuishi mawasiliano ya  INTANETI na kwa  vile Cybercrime Law inahusu intanet tu , na kwa vile hilo si jambo la Muungano sheria hio haiwezi kutumika Zanzibar kikatiba. Ama kimabavu uwanja uko wazi.

MAONI: Kuwepo kwa Sheria ya Mitandao katika nchi yoyote ile kwa madhumuni ya kulinda amani na utulivu wa nchi, ikiwa ni pamoja na kuhifadhi silka, mila na tamaduni za nchi, ni jambo zuri sana.

Lakini, tatizo linakuja pale ambapo Sheria hii imepelekwa bungeni kwa Hati ya Dharura, na kwa hivyo, wadau mbali mbali hawakupata fursa ya kuijadili kwa kina. Na hata kule bungeni wabunge wa vyama vya upinzani walikuwa wamesusia vikao; na wengi kati ya wabunge kutoka chama tawala hawakuwepo bungeni kwa vile walikuwa wanazuru majimbo yao. Yote haya yanaifanya kupitishwa kwa sheria hii na kusainiwa na rais haraka haraka kunaleta suitafahamu na mfadhaiko wa aina fulani.

Na kwa upande wa Zanzibar, kwa vile sheria hii haijafikishwa katika Baraza la Wawakilishi kwa mujibu wa Ibara ya 238 ya Katiba ya Zanzibar kwa madhumuni ya kuliridhisha Baraza kuwa sheria hiyo imefuata mashart ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuhusu upitishwaji wa sheria za Muungano zinazopaswa kutumika katika pande zote mbili za Muungano, nafikiri mapungufu haya yanaifanya sheria hiyo isiweze kutekelezwa Zanzibar kikatiba na kisheria; isipokuwa tu labda serikali itaamua kuitekeleza kimabavu tu. Inafaa ikumbukwe hapa kuwa Baraza la Wawakilishi lilikuwa limeshafungwa na Rais wa Zanzibar wakati sheria hiyo inapitishwa bungeni.



No comments: