Tuesday 3 November 2015

By Ibrahim Haruna Lipumba
Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) imetumia matokeo ya kura za Rais katika majimbo ya Zanzibar kujumlisha na matokeo ya majimbo ya Bara na hatimaye kumtangaza Dk John Magufuli kuwa mshindi wa kiti cha Rais katika Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano. Kwa uamuzi huo wa kuchukua matokeo ya majimbo ya Zanzibar yaliyotumia Daftari la Wapigakura la ZEC na kupiga kura kwenye vituo vilivyoandaliwa na ZEC, Tume ya Uchaguzi ya Taifa inatambua kuwa uchaguzi uliofanyika Zanzibar chini ya usimamizi wa ZEC ni halali na matokeo yake ni halali. ya Muungano wa Tanzania ikiwamo Zanzibar ilifanya Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, 2015. Kwa upande wa Visiwani, Wazanzibari walipiga kura kumchagua diwani, mwakilishi, Rais wa Zanzibar, mbunge wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kutumia Daftari la Wapigakura la ZEC.
Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) imetumia matokeo ya kura za Rais katika majimbo ya Zanzibar kujumlisha na matokeo ya majimbo ya Bara na hatimaye kumtangaza Dk John Magufuli kuwa mshindi wa kiti cha Rais katika Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano. Kwa uamuzi huo wa kuchukua matokeo ya majimbo ya Zanzibar yaliyotumia Daftari la Wapigakura la ZEC na kupiga kura kwenye vituo vilivyoandaliwa na ZEC, Tume ya Uchaguzi ya Taifa inatambua kuwa uchaguzi uliofanyika Zanzibar chini ya usimamizi wa ZEC ni halali na matokeo yake ni halali.
Oktoba 28, siku tatu baada ya uchaguzi, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha alitangaza kuwa uchaguzi wa Zanzibar umefutwa. Alipokuwa anatangaza alikuwa peke yake. Makamu Mwenyekiti hakuwepo. Mkurugenzi wa ZEC hakuwepo. Wajumbe wengine wa Tume hawakuwepo. Wajumbe wa ZEC walikuwa Bwawani wakimsubiri Mwenyekiti wao. Walijaribu kuendelea na kazi ya kuhakiki matokeo chini ya uongozi wa Makamu Mwenyekiti. Hawakuweza kuendelea na kazi hiyo baada ya Makamu Mwenyekiti kuondolewa na vyombo vya dola.
Sababu ambazo Mwenyekiti ametoa za kufuta uchaguzi ni pamoja na eti makamishna wa uchaguzi katika Tume hiyo walidundana kutokana na tofauti zao. Makamishna walikuwa wanapendelea vyama vyao. Katika vituo vingine, hasa Pemba, kura zilizopigwa zilikuwa zaidi ya zilizosajiliwa. Masanduku ya kupigia kura hayakupewa ulinzi wa kutosha na mawakala pamoja na maofisa wa uchaguzi. Mawakala wa vyama walifukuzwa katika vituo kadhaa. Vijana walivamia vituo vya kupigia kura wakiwa na lengo la kuzua ghasia na kadhalika.
Sababu za Mwenyekiti hazina mashiko. Malalamiko haya yalipaswa kutolewa na mawakala wa vyama mapema. Vituo vya kupigia kura vilikuwa na ulinzi wa kutosha wa vyombo vya dola. Watazamaji wa ndani na nje walisifia namna upigaji wa kura Zanzibar ulivyokuwa wa amani na utulivu.
Jecha alieleza kwamba, “Kwa kuzingatia hayo na mengine mengi ambayo sijayaeleza, Mimi Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, nimeridhika kwamba uchaguzi huu haukuwa wa haki na kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi. Hivyo kwa uwezo nilionao natangaza rasmi uchaguzi huu na matokeo yake yote yamefutwa na kwamba kuna haja ya kurudia uchaguzi huu.” Mwenyekiti Jecha hakuvitaja vifungu vya Katiba na sheria vinavyompa mamlaka ya kufuta uchaguzi.
Sura ya tisa ya Katiba ya Zanzibar inaelezea pamoja na mambo mengine uundwaji, mamlaka na taratibu za uamuzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Hakuna kifungu chochote cha Katiba kinachoipa tume au mwenyekiti wake maamlaka ya kufuta uchaguzi. Katiba inaeleza bayana kuwa uamuzi wa masuala yote unafanywa na tume kwa pamoja. Kifungu cha 119(10) kinaeleza kuwa “Kiwango cha mikutano ya Tume ya Uchaguzi ni Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti na wajumbe wanne na kila uamuzi wa tume ni lazima uungwe mkono na wajumbe walio wengi.” Mwenyekiti Jecha hakueleza kikao gani cha Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kilichokaa na kufikia uamuzi aliotangaza. Ukweli ni kwamba Jecha amevunja Katiba ya Zanzibar kwa kutoa uamuzi mzito bila kufuata taratibu zilizowekwa na Katiba ya Zanzibar. Uamuzi wake ni batili na hauna nguvu ya kisheria. Katiba na sheria ya Zanzibar hazijampa mamlaka mwenyekiti na hata tume yote kufuta uchaguzi. Kufanya hivyo ni kuvunja Katiba ya Zanzibar.
Inaelekea mwenyekiti amepewa shinikizo na ndiyo maana hakuwashirikisha wajumbe wengine wa ZEC. Bila shaka waliomshinikiza Mwenyekiti wa ZEC kuvunja Katiba watawashinikiza wajumbe wengine wa ZEC kuunga mkono uvunjaji wa Katiba uliofanywa na mwenyekiti wao.
Athari za kufuta uchaguzi ni kuleta vurugu za kisiasa na maafa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Kwa kuwa matokeo ya kura za Zanzibar kwa uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano hayaathiri ushindi wa mgombea wa CCM, matokeo hayo yamekubaliwa. Matokeo ya kura za uchaguzi wa Rais wa Zanzibar uliofanyika katika mazingira yaleyale na kutumia Daftari la Wapigakura la ZEC yanakataliwa kwa sababu mgombea wa CCM ameshindwa. Mwenyekiti wa ZEC ameshinikizwa kufuta uchaguzi wote wa Zanzibar.
Ni wazi wananchi wengi wa Zanzibar hawawezi kukubali kurudia uchaguzi kwa sababu wenye vyombo vya dola wameamua lazima CCM ishinde ndiyo matokeo ya uchaguzi yakubaliwe. CCM inawaeleza Wazanzibari mabadiliko ya Serikali hayawezi kuletwa na vikaratasi vya kura. Mapinduzi daima maana yake lazima CCM itawale Wazanzibari wakitaka au wasitake. CCM inawaeleza Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla kama wanataka mabadiliko aslani hawatayapata kupitia visanduku vya kura. Watafute njia nyingine. Hili ni jambo la hatari.
Nilidhani CCM imejifunza tangu matukio ya 2001 baada ya uchaguzi wa 2000, uchaguzi wa majimbo 16 ulifutwa na kurudiwa.
CUF ilipotoa taarifa ya kufanya maandamano ya amani nchi nzima kudai tume huru ya uchaguzi, Katiba Mpya yenye misingi ya demokrasia, utawala bora na kurudiwa kwa uchaguzi wote wa Zanzibar kama ilivyopendekezwa na watazamaji wa uchaguzi wa ndani na wa nje, mimi binafsi nilikamatwa nikapigwa na kuvunjwa mkono na kutupwa jela. Dhahama hiyo iliwakuta wanachama na viongozi wengine wa CUF. Wananchi wa Zanzibar walipojaribu kuandamana Januari 27, zaidi ya watu 60 waliuawa na kwa mara ya kwanza Watanzania zaidi ya 2000 walikimbia nchi yao kwenda Kenya kunusuru maisha yao. Watanzania tusikubali wanaoishinikiza ZEC kuturudisha huko.
Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano, Dk John Magufuli ataapishwa Novemba 5, 2015 na ndiye atakayekuwa Amiri Jeshi Mkuu. Rais Jakaya Kikwete hatamtendea haki Rais Magufuli kumwachia mgogoro wa Zanzibar ambao anaweza kuutatua.
Uchaguzi umefanyika Zanzibar na kwa kuzingatia matokeo kwenye vituo vyote vya wapigakura yaliyotiwa saini na wasimamizi wa vituo na mawakala wa vyama, mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ameshinda uchaguzi huo. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ikamilishe uhakiki wa matokeo na kumtangaza mshindi.
Tangu mwaka 1995 sera ya CUF ni kuunda serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar. Katiba ya Zanzibar ya 2010 imeingiza serikali ya umoja wa kitaifa kuwa sharti la kikatiba. CCM watakuwa sehemu ya serikali ya umoja wa kitaifa. Nina uhakika kwa uzalendo wa Kizanzibari wa Maalim Seif, ataunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayowaunganisha Wazanzibari.
Propaganda kubwa dhidi ya CUF ni kwamba ikipewa fursa ya kuongoza Zanzibar, itavunja Muungano. Msimamo rasmi wa CUF ni mfumo wa muungano wa shirikisho lenye serikali tatu ya Zanzibar, Tanganyika na Muungano kama uliopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba. Huu ndiyo msimamo wa CUF tangu mwaka 1995 wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi. Msimamo huu ulifanana na mapendekezo ya Tume ya Jaji Nyalali. CUF inaheshimu sheria mama ya Jamhuri ya Muungano ambayo ni Makubaliano ya Muungano.
Tume ya Jaji Warioba ilitoa uhuru kwa Watanzania kutoa maoni kuhusu Katiba wanayoitaka. Mjadala huu ulitoa mapendekezo mengi likiwamo la Muungano wa mkataba. Baada ya kuchambua mapendekezo yote, Tume ya Jaji Warioba iliandaa Rasimu ya Katiba yenye mfumo wa Muungano wa serikali tatu. Chama cha CUF na Katibu Mkuu wake waliunga mkono mapendekezo ya Tume ya Jaji Warioba na ndiyo sababu ya kuanzisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika Bunge Maalumu la Katiba. Wazanzibari wengi wanaoishi Tanzania Bara wanaunga mkono CUF, lakini pia wanaelewa umuhimu na faida za Muungano. CUF haitavunja muungano bali itauimarisha kwa kutumia njia za demokrasia na sheria kutatua kero za Muungano.
Kufuta uchaguzi wa Zanzibar ni kuwanyima Wazanzibari haki ya kuchagua viongozi wanaowataka. Nikuwaeleza hawawezi kupata mabadiliko kupitia visanduku vya kura. Watafute njia nyingine. Wanaowanyima Wazanzibari haki ya kuchagua viongozi wao kwa utaratibu wa kupiga kura ndiyo wanaoandaa mazingira ya kuvunja Muungano. Rais Kikwete na Rais Ali Mohammed Shein malizeni tatizo msiliingize taifa kwenye balaa na kumuachia Rais mteule mgogoro utakaomzuiwa kusimamia ajenda ya maendeleo ya nchi yetu.
Mwandishi wa makala haya, Profesa Ibrahim Lipumba alikuwa Mwenyekiti wa CUF.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: