Tuesday, 5 January 2016

Hivi karibuni, Balozi Seif Ali Iddi alitoa taarifa katika vyombo vya habari kuwa serikali imeshatenga bajeti maalum kwa madhumuni ya kugharamia uchaguzi wa marudio. Aliongeza kusema kuwa matayarisho kamili yameshafanywa na kinachosubiriwa ni Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kutangaza tarehe rasmi ya kufanyika uchaguzi.

Kusema kweli, kauli hii imenishangaza sana kwa sababu mbili zifuatazo:

Kwanza, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na Sheria za nchi kuhusiana na Matumizi na Mapato ya Serikali, Serikali haiwezi kukusanya Mapato au kufanya Matumizi yoyote yale bila ya kupata idhini ya Baraza la Wawakilishi.

Sasa, Balozi Seif Ali Iddi anapotuarifu kuwa fedha za kugharamia uchaguzi wa marudio zimeshatengwa na serikali, ni vyema vilevile akatuarifu fedha hizo zimepatikana kutokana na vianzio vipi na kwa idhini ya nani ikiwa hakuna Muswada wa Sheria uliotayarishwa na Serikali na kuwasilishwa Barazani kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa na wajumbe wa BLW.

Bila shaka, kwa kuzingatia ukweli kuwa Baraza la Wawakilishi lenyewe halipo baada ya kufutwa kwa uchaguzi, ni sahihi kabisa kuamini kuwa Serikali haitokuwa na fedha za kugharamia uchaguzi ikiwa chombo cha kutoa idhini hakipo; vyenginevyo mapato na Matumizi yoyote yatakayopatikana na kutumiwa kwa madhumuni ya kugharamia shughuli za uchaguzi yatakuwa si halali au batili kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.

La pili linalonishangaza linahusiana na hii kauli ya Balozi inayoashiria kuwa matayarisho yote ya uchaguzi wa marudio yameshakamilika isipokuwa kinachosubiriwa ni tangazo la Tume ya Uchaguzi litakalotoa tarehe ya kufanyika uchaguzi. Nimeshangazwa na hili pia kwa sababu kwa mujibu wa Katiba na sheria ya uchaguzi, Tume haina mamlaka ya kutangaza tarehe ya kufanyika uchaguzi. Serikali ndiyo yenye mamlaka ya  kutangaza tarehe ya uchaguzi baada ya kuamua kufanyika kwa uchaguzi wenyewe. Kazi ya Tume ya Uchaguzi ni kusimamia na kuendesha shughuli za uchaguzi na wala sio kutangaza tarehe ya uchaguzi.

Mfano mzuri ni pale Serikali zetu zote mbili zilipotangaza kuwa tarehe 25 Oktoba 2015 ndiyo itakayokuwa siku ya upigaji kura nchi nzima. Au pale Serikali ya Tanzania ilipotangaza kuwa kura ya maoni kwa ajili ya Katiba Inayopendekezwa itapigwa tarehe 30 Aprili 2015. Na kama tujuavyo, Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) ndiyo iliyotoa kauli ya kuakhirisha tarehe hiyo kutokana na sababu za kiufundi.

Sasa, Balozi Seif Iddi anapoitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kutangaza tarehe ya kufanyika uchaguzi wa marudio, Tume inapata wapi mamlaka hayo?

Namalizia kwa kusema tu kuwa nimejaribu kuichambua na kuifanya mapitio kauli ya Balozi Seif Iddi kuhusu uamuzi wake wa kutenga bajeti kwa ajili ya kugharamia shughuli za uchaguzi na kuitaka Tume ya Uchaguzi kutangaza tarehe ya uchaguzi. Nimefanya hivyo kwa kuzingatia masharti ya Katiba na sheria za nchi.

Lakini, pengine ni kazi bure tu kwa upande wangu kujaribu kujadili mambo kwa mtazamo wa Katiba na sheria wakati zingatio kubwa la Balozi Seif ni kupata fedha za kugharamia uchaguzi hata ikiwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na masharti ya Katiba na sheria za nchi.

No comments: