Saturday 16 January 2016

Maalim Seif awahakikishia Wazanzibari kuwa atipigania maamuzi ya Wazanzibari kwa nguvu zetu zote.

Ni bahati mbaya sana kwamba wengine wanauchukulia uungwana na ustaarabu wetu kwamba labda ni dalili ya udhaifu na wanadhani labda wanaweza kutuburuza. Kwa hilo, nawaambia wazi kwamba WASAHAU. Nataka niwahakikishie kwamba sisi si dhaifu ila tunaongozwa na uzalendo na mapenzi kwa nchi yetu na wananchi wenzetu. Lakini uzalendo huo huo na mapenzi hayo hayo kwa nchi yetu na wananchi wenzetu yanatutaka tusimame kuitetea na kuilinda Katiba na Sheria za nchi yetu, haki za raia na maamuzi yao ya kidemokrasia.
 
MAELEZO YA MGOMBEA URAIS WA ‪ZANZIBAR KUPITIA CUF, MAALIM SEIF SHARIF HAMAD, KWENYE MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI – SERENA HOTEL, DAR ES SALAAM, TAREHE 11 JANUARI, 2016
KIINI CHA MZOZO WA KIKATIBA NA KISHERIA #ZANZIBAR ULIOTOKANA NA KUFUTWA ISIVYO HALALI KWA UCHAGUZI MKUU, CHANGAMOTO ZAKE NA NAMNA YA KUUTATUA
Ndugu zangu Waandishi wa Habari,
Awali ya yote, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uhai na uzima wa afya na tukaweza kukutana hapa asubuhi hii ya leo. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu pia kwa kuijaalia nchi yetu kuendelea kubaki katika hali ya amani na utulivu licha ya changamoto nyingi zinazotukabili. Tunapoona watu wa nchi nyengine, zikiwemo nchi jirani, wanateseka kwa kukosa amani ndipo tunapozidi kutambua umuhimu wa neema hii ya amani katika nchi yetu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuibariki nchi yetu na watu wake na atujaalie hekima na busara katika kuendesha mambo yetu ili tuendelee kuitunza neema hii aliyotupa.

Pili, nichukue fursa hii kukushukuruni nyinyi wahariri na waandishi wa habari kwa kuitikia wito wetu na kuja kutusikiliza. Naamini mtatusikiliza kwa makini, hususan kutokana na uzito wa suala tulilowaitia, na kisha mtawafikishia Watanzania yale ambayo tumekuja kuwaeleza.
Tumewaita leo hii ili kuzungumzia kwa kina suala la Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na matukio yaliyofuata, ikiwemo hatua isiyo halali kikatiba na kisheria ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, kudai kwamba amefuta uchaguzi huo na matokeo yake, mgogoro uliosababishwa na kitendo hicho haramu, mazungumzo yanayoendelea kutafuta ufumbuzi wa suala hilo, pamoja na njama za kuhujumu jitihada zinazoendelea za kutafuta ufumbuzi kwa njia ya amani.
Naomba mnivumilie wakati nasoma maelezo haya niliyoyaandaa kwani kwa faida yenu na kwa faida ya Watanzania nimeona kuna haja ya kutoa maelezo ya kina kidogo ili suala hili liweze kufahamika kwa ukamilifu wake.
  1. UTANGULIZI
    Kitendo cha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salum Jecha kutoa tamko lisilo halali kikatiba na kisheria la kuufuta Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar pamoja na matokeo yake kumeitumbukiza Zanzibar katika mzozo mkubwa wa kikatiba na kisheria. Aidha, kitendo hicho kimeifedhehesha sana Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mbele ya Jumuiya za kikanda na kimataifa. Mzozo huo pia umeiweka Zanzibar katika njia panda sio tu kwa hali ya sasa lakini kwa mustakbala wake wa baadaye na kuirejesha nyuma sana katika jitihada za kujenga umoja wa kitaifa unaozingatia misingi ya utawala wa sheria, demokrasia na mfumo wa utawala bora.
Kubwa zaidi, mzozo huo umeleta fadhaa kubwa sana kwa wananchi wa mirengu yote ya kisiasa. Uchumi na ustawi wa Zanzibar nao umeathirika sana. Wananchi wako taaban huku hali ya maisha ikizidi kuwa ngumu na bidhaa zikipanda bei kwa kasi wakati mzunguko wa fedha ukiwa umepotea.
Katika hali hii, hapana budi juhudi za kuutatua mzozo huu zikamilishwe kwa haraka kwa kuzingatia misingi ya kikatiba, kisheria na pia mustakbala utaowafanya wananchi wa Zanzibar waamini kwamba mfumo uliopo wa kikatiba, kiutawala na kisheria ambao umechukua muda kuujenga unaweza kufanya kazi na pale penye kasoro unaweza kuimarishwa hatua kwa hatua kama ambavyo tumekuwa tukifanya kwa miaka kadhaa sasa.
  1. YALIYOJITOKEZA KATIKA UCHAGUZI
1) Hali ya Uchaguzi
Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015 kama zilivyo chaguzi nyengine unakwenda sambamba na Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Chaguzi hizo mbili zinafanyika katika vituo sawa kwa kutumia utaratibu, ulinzi na usimamizi ulio sawa. Kwa hivyo, siku ya uchaguzi mkuu mwananchi wa Zanzibar ndani ya kituo kimoja anapiga kura tano (5) badala ya tatu (3) anazopiga mwananchi aliyepo Tanzania Bara. Kura ambayo mwananchi wa Zanzibar anapiga ni:
a) Kura ya Rais wa Zanzibar;
b) Kura ya Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi;
c) Kura ya Diwani;
d) Kura ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na
e) Kura ya Mbunge
Kwa jumla uchaguzi ulifanyika katia njia ya amani, utulivu na bila ya kutokea vurugu. Waangalizi wa uchaguzi wa ndani na wa nje ya nchi katika taarifa zao za awali walisifu na kupongeza jinsi uchaguzi ulivyofanyika.
2) Kutangazwa Matokeo ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani
Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Namba 11 ya 1984, kama ilivyo kwa Sheria ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, matokeo ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani unatangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo husika (Returning Officer). Kifungu cha 88 cha Sheria ya Uchaguzi kinaeleza kama ifuatavyo:
“baada ya matokeo ya uchaguzi kuthibitishwa Msimamizi wa Uchaguzi:
(a) Atamtangaza mgombea aliyepata kura nyingi mshindi hapo hapo;
(b) Atampatia aliyechaguliwa taarifa ya kuchaguliwa kwa maandishi;
(c) Atatuma taarifa ya uchaguzi kwa Tume ya Uchaguzi kwa ajili ya kuchapishwa katika Gazeti rasmi la Serikali.”
Kifungu cha 123 cha Sheria ya Uchaguzi kinaeleza wazi kuwa uchaguzi wa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi hautahojiwa isipokuwa kwa njia ya Kesi ya Uchaguzi mbele ya Mahkama Kuu. Kifungu cha 116 cha Sheria ya Uchaguzi kinaeleza watu ambao wana haki ya kufungua Kesi ya Uchaguzi. Mwenyekiti wa Tume wala Tume yenyewe haimo katika orodha ya wanaoruhusiwa kufungua kesi ya uchaguzi kuhoji matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi.
3) Kukamilika kwa Uchaguzi wa Wawakilishi na Madiwani
Hadi kufikia asubuhi ya tarehe 26 Oktoba, matokeo ya majimbo yote 53 ambayo yalifanya uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi yalitangazwa na Wasimamizi wa Uchaguzi na kuwapatia shahada za kuchaguliwa wale wote walioshinda. Aidha, uchaguzi wa madiwani ulikamilika na kupatiwa shahada katika Wadi zote zilizofanya uchaguzi.
Kwa maana hiyo, kufikia tarehe 26 Oktoba, uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani ulishakamilika. Aidha, uchaguzi wa Wabunge nao ulishakamilika na washindi kukabidhiwa vyeti vyao vya kuwa wamechaguliwa.
Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, kifungu cha 123 kimeeleza wazi kwamba baada ya uchaguzi kukamilika, unaweza kuhojiwa tu kwa njia ya Kesi ya Uchaguzi sio vyenginevyo.
4) Matokeo ya Uchaguzi wa Rais wa Zanzibar
Hadi kufikia tarehe 26 Oktoba, asubuhi kazi ya kuhesabu kura za urais na kukusanya matokeo katika Majimbo yote ya Zanzibar ilishakamilika. Sheria ya Uchaguzi kifungu cha 42 kinaelekeza ifuatavyo:
“Baada ya kukamilika kuhesabu kura katika vituo vyote vya uchaguzi katika jimbo (na ikihitajika kazi ya kuhesabu tena kura) Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo atawasilisha kwa Tume ya Uchaguzi na kwa mgombea urais au wakala wake:
a) Idadi ya kura za urais zilizopigwa katika Jimbo;
b) Idadi ya kura alizopata kila mgombea;
c) Kama mgombea urais ni mmoja tu idadi ya kura zilizomchagua
Baada ya hapo Tume itajumlisha kura zote za Urais kutoka kila Jimbo.”
Sheria ya Uchaguzi, kifungu cha 42(2) inaeleza kwamba Tume inaweza, ikiwa itakuwa na sababu za msingi, kabla ya kutangaza matokeo kuagiza kura katika majimbo au jimbo fulani kuhesabiwa upya.
Baada ya kujumuisha matokeo ya urais kutoka katika Majimbo, Sheria ya Uchaguzi kifungu cha 42(3) kinaelekeza kwamba Tume itamtangaza mshindi.
Tume ilifanya kazi ya kujumlisha matokeo ya Urais kutoka katika Majimbo kama inavyoagizwa na Sheria. Baada ya majumuisho hayo, hakuna pahala ambapo Tume iliagiza kura zihesabiwe upya kama Sheria inavyoagiza ikiwa kutakuwa na sababu ya kufanya hivyo. Bila ya shaka kwa vile hakukuwa na kasoro iliyopelekea haja ya kuhesabiwa upya Tume haikuchukua hatua hiyo.
Hadi kufikia tarehe 28 Oktoba, Tume ilishatangaza matokeo ya kura za Urais kutoka katika majimbo 31; na ilishakamilisha kujumlisha matokeo ya majimbo mengine 9 (ambayo ilikuwa bado haijayatangaza). Kwa maana hiyo, kazi ya kujumlisha na kuhakiki matokeo ya majimbo 40 kati ya majimbo 54 ilikuwa imeshakamilika. Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi kifungu cha 42(6) Tume inatakiwa itangaze matokeo ndani ya siku 3 tokea siku ya kupiga kura. Hivyo, tarehe 28 Oktoba ilikuwa ndiyo siku ya mwisho ambayo Tume ilitakiwa itangaze matokeo ya Urais.
Hata hivyo, majumuisho ya matokeo ya Urais kupitia taarifa ambayo Tume iliwapatia mawakala wa wagombea au wagombea wenyewe chini ya kifungu cha 42(1) cha Sheria ya Uchaguzi baada ya kujumuishwa yalikuwa yanaonyesha kwa ufupi kama ifuatavyo:
MGOMBEA KURA ZA MGOMBEA ASILIMIA
DR. ALI MOHAMED SHEIN 182,011 46.28%
MAALIM SEIF SHARIF HAMAD 207,847 52.84%
IDADI YA KURA HALALI 393, 323
Hapa hatukuorodhesha matokeo ya wagombea wengine kwani hakuna hata mmoja aliyefikisha angalau asilimia 1 ya kura zilizopigwa.
  1. KUFUTWA KWA UCHAGUZI NA MWENYEKITI WA TUME
1) Mwenendo wa Mwenyekiti wa Tume na Yaliyojitokeza kabla ya Kufuta Uchaguzi
Kabla ya Mwenyekiti wa Tume kutoa tamko lake peke yake la kufuta uchaguzi alionesha dhahiri kuwa alikuwa na ajenda ya siri. Kwanza, alichelewesha kwa makusudi zoezi la kujumuisha matokeo kwa visingizio mbali mbali ikiwemo kuchelewa kufika kwenye kituo cha majumuisho kilichokuwepo Hoteli ya Bwawani, kuondoka mapema na kusingizia anaumwa. Kwa mfano siku ya tarehe 27 Oktoba aliahirisha zoezi hilo kwa madai ya kuwa na tatizo la sindikizo la damu. Siku ya tarehe 28 Oktoba ambayo kwa mujibu wa Sheria ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ya kutangaza matokeo, Mwenyekiti hakuonekana kabisa katika kituo cha kutangaza matokeo katika Hoteli ya Bwawani. Baada ya Wajumbe waliobaki wa Tume kuona wanachelewa na siku hiyo ilikuwa ya mwisho, waliamua kwamba Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji Abdulhakim Ameir Isssa aendelee kuongoza Tume kukamilisha kazi ya kutangaza matokeo ya Urais kwa vile kifungu cha 119(10) cha Katiba ya Zanzibar kinaruhusu kufanya hivyo. Wakati zoezi hilo likiendelea mambo matatu makubwa yalijitokeza:
a) Kituo cha Bwawani kilizingirwa na Jeshi la Ulinzi la Tanzania (JWTZ) wakitoa amri ya kuzuia kila aliyekuwemo ndani asitoke na aliyekuwa nje asiingie katika eneo hilo;
  1. b) Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Abdulhakim Ameir Issa alipewa taarifa ya wito muhimu na mmoja wa watumishi wa Tume na alipotoka nje ya ukumbi wa kikao cha Tume alichukuliwa na askari Polisi na kupelekwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Kilimani;
  2. c) Televisheni ya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na redio ya Shirika hilo yalitoa matangazo ya tangazo la Mwenyekiti wa Tume kufuta uchaguzi na matokeo yake;
Baada ya hapo Tume haikuitishwa tena hadi tarehe 1 Novemba, 2015 ambapo Mwenyekiti aliwaarifu Wajumbe wa Tume yafuatayo:
i. Kwanza alitangulia kuomba radhi Wajumbe kwa vile baada ya kukutana na vyombo (bila ya kutaja vyombo gani) alilazimika kusema baadhi ya mambo ya uongo katika taarifa yake na kufuta uchaguzi ili kuokoa hali;
ii. Alitaka Wajumbe wamuunge mkono kwa kitendo alichofanya;
Tarehe 12 Novemba, Mwenyekiti wa Tume alitoa Tangazo rasmi Namba 130 la kufuta uchaguzi (matokeo) kupitia Gazeti Rasmi la Serikali lililochapishwa tarehe 6 Novemba. Hata hivyo, Tangazo hilo lilikuwa na kasoro za wazi za kisheria ambazo nitazieleza hapo mbele.
2) Uhalali wa Mwenyekiti wa Tume kufuta Uchaguzi
Mbali ya kwamba kitendo cha Mwenyekiti wa Tume kimedhihirika kuwa ni njama za wazi za kisiasa ambazo zilipangwa na kutekelezwa na Mwenyekiti wa Tume, vyombo vya ulinzi na viongozi wa kisiasa ambao sasa wanamtetea, uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume kufuta uchaguzi hauna uhalali wowote kwa sababu zifuatazo:
  1. a) Uchaguzi Kukamilika: Uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ulishakamilika. Kwa upande wa uchaguzi wa Rais nao ulishakamilika isipokuwa hatua ya kutangaza matokeo ambayo nayo kwa mujibu wa sheria ilitakiwa iwe imeshakamilika. Kama ilichelewa ilicheleweshwa makusudi na Mwenyekiti katika juhudi zake za kutafuta visingizio vya kuharibu uchaguzi ili mshindi halali asitangazwe. Tume haina mamlaka ya kuahirisha, kutengua matokeo au kufuta uchaguzi uliokwisha kamilika. SHERIA YA UCHAGUZI imeeleza wazi mamlaka ya Tume baada ya kazi ya kuhesabu kura kukamilika. Mamlaka pekee ni ya kurudia kuhesabu kura kwa majimbo yote au kwa Jimbo moja iwapo itaridhika kwamba ipo sababu ya msingi ya kufanya hivyo. Kifungu cha 42(2) cha Sheria ya Uchaguzi imeeleza wazi juu ya uwezo huo wa Tume. Kuipa mamlaka Tume kutengua uchaguzi uliokwisha kamilika ni sawa na kuingilia kazi za mhimili wa Mahkama. Hata Mahkama yenyewe inafungwa na Sheria ya Uchaguzi. Kifungu cha 123 kimeeleza watu ambao wanaweza kuhoji matokeo ya uchaguzi baada ya kutangazwa na Returning Officer. Mwenyekiti wa Tume au Tume hawamo katika orodha ya wanaoweza kuhoji uchaguzi baada ya kutangazwa matokeo. Aidha, chini ya Sheria ya Ukomo, Mahkama haiwezi kusikiliza tu shauri lolote lazima izingatie muda unaokubalika kusikiliza shauri;
  2. b) Mamlaka ya Mwenyekiti: Ni wazi kuwa Mwenyekiti alivunja Katiba. Alikwenda kinyume na kifungu cha 119(1) cha Katiba na alikiuka kifungu cha 119(10) cha Katiba juu ya utaratibu wa Tume kufanya maamuzi kwa kuamua kufuata uchaguzi bila ya kuitisha kikao cha Tume wala kushauriana na Tume. Kifungu cha 119(1) cha Katiba ya Zanzibar kinaeleza muundo wa Tume ambayo imeshirikisha wadau wakuu wa uchaguzi na watu wengineo huru. Kifungu cha 119(10) kinaweka utaratibu wa Tume kufanya maamuzi na kimeeleza kwa maelezo ya wazi kama ifuatavyo:
    “kiwango cha mikutano ya Tume ya Uchaguzi ni Mwenyekiti au Makamo Mwenyekiti na Wajumbe wanne na kila uamuzi wa Tume ni lazima uungwe mkono na Wajumbe walio wengi.”
Ni dhahiri kuwa Katiba imesisitiza suala la maamuzi ya Tume kufanywa kwa kupitia vikao na uamuzi kufanywa baada ya kuungwa mkono na Wajumbe walio wengi. Katiba imetumia daraja mbili za msisitizo kwa kutumia neno “kila” (maamuzi ya Tume) na neno “lazima”.
Kwa kufanya maamuzi peke yake, Mwenyekiti alipaswa achukuliwe hatua na Rais ya kusimamishwa, kuchunguzwa na akipatikana na kosa kufukuzwa chini ya vifungu vya 119(6), (7) na (8) vya Katiba;
  1. c) Mamlaka ya Tume: Ingawa Mwenyekiti aliitisha kikao tarehe 1 Novemba na kuitaka Tume ihalalishe kitendo chake cha kufuta matokeo, lakini Tume haina mamlaka ya kuhalalisha kitendo chochote kinachokiuka Katiba au Sheria. Tume ingeweza kuhalalisha jambo ambalo kwanza Mwenyekiti mwenyewe ana mamlaka nalo na Tume ina mamlaka nalo kulifanya lakini pengine taratibu tu hazikukamilika. Kwa vile Tume haina mamlaka ya kuhalalisha jambo ambalo ni kinyume na Katiba na Sheria, kitendo cha Tume kutaka kuhalalisha kitendo cha Mwenyekiti cha kufuta uchaguzi uliokwisha kamilika ni batili;
  2. d) Udanganyifu na Ubatili wa Tangazo Rasmi la Kufuta Uchaguzi: Kama nilivyotangulia kueleza kwamba tarehe 6 Novemba, Mwenyekiti wa Tume alitoa Tangazo Namba 130 katika Gazeti rasmi la Serikali kufuta uchaguzi. Tangazo hilo lina udanganyifu wa wazi na kasoro nyengine kadhaa za kisheria kama ifuatavyo:
  • Udanganyifu: Tangazo linaeleza kwamba ni uamuzi wa Tume ya Uchaguzi uliofanywa tarehe 28 Oktoba. Kuna ushahidi usio na shaka kwamba tarehe 28 Oktoba, Tume ya Uchaguzi haikukutana kabisa hata kwa njia isiyo rasmi kwa vile Mwenyekiti hakwenda katika kituo cha kutoa matokeo ya uchaguzi seuze kukutana rasmi kwa mujibu wa Katiba na kutoa maamuzi kama Katiba inavyoelekeza;
  • Migongano: Tamko la Mwenyekiti alilolitoa tarehe 28 Oktoba kupitia vyombo vya habari vya ZBC lilieleza wazi kuwa anafuta uchaguzi na matokeo yake yote. Hata hivyo, Tangazo katika Gazeti Rasmi linaeleza kuwa amefuta matokeo ya uchaguzi. Huu ni mgongano mkubwa ambao una maswali mengi bila majibu;
  • Uhalali wa kisheria: Katika Tangazo la Kisheria namba 130, Mwenyekiti amenukuu vifungu vya Katiba na Sheria anavyodai vinampa uwezo kufuta Uchaguzi. Vifungu vyote alivyonukuu sio tu kwamba havizungumzii mamlaka ya kufuta uchaguzi lakini pia havitoi uwezo kwa Tume kufanya hivyo. Amenukuu kifungu cha 119(10) cha Katiba ambacho kinaeleza tu akidi ya vikao vya Tume na kwamba lazima maamuzi yote ya Tume yaungwe mkono na Wajumbe walio wengi. Amenukuu kifungu cha 3 cha Sheria ya Uchaguzi ambacho kinazungumzia utaratibu wa kutoa matangazo ambayo Tume kisheria ina mamlaka kuyatoa na amenukuu kifungu cha 5 cha Sheria ya Uchaguzi ambacho kinazungumzia kazi za Tume na sio mamlaka ya Tume. Ni dhahiri vifungu hivyo vimenukuliwa kwa ubabaishaji kwa nia ya kupotosha kwamba Tume inao uwezo wa kufuta uchaguzi.
  1. e) Hoja ya Kasoro katika Uchaguzi: Hoja inayotumika kuwa uchaguzi ulikuwa na kasoro nyingi lazima izingatiwe kwa makini. Kwanza, Sheria yenyewe ya Uchaguzi imetoa utaratibu wa kufuatwa endapo kuna malalamiko ya ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi. Kwa mfano, kifungu cha 74 kinaweka utaratibu wa kufunga kituo iwapo itajitokeza fujo katika kituo cha uchaguzi. Vifungu vya 71, 76, 80B na 85 vinaelekeza kwa ufasaha namna ya kushughulikia kasoro mbali mbali zitazojitokeza katika uchaguzi. Sheria imetoa fursa za wazi kwa mwenye malalamiko kuyawasilisha kwa kupitia fomu maalum. Kujaza fomu hizo ni sharti la msingi katika kuyafanya malalamiko kuwa halali.
Ingawa hazikufuata taratibu, malalamiko yaliyowasilishwa na CCM kwa barua yalijadiliwa na Tume na kutupiliwa mbali kwa kauli moja. Hivyo, kwa mujibu wa Sheria hapakuwa na malalamiko yaliyowasilishwa mbele ya Tume. Mwenyekiti wa Tume alibuni mwenyewe kasoro na kuzitolea uamuzi yeye mwenyewe na peke yake. Aidha, tokea chaguzi za vyama vingi zianze zimekua na kasoro. Kasoro kubwa kuliko zote ilitokea katika uchaguzi wa mwaka 2000 ambapo majimbo 16 ya Mkoa wa Mjini Magharibi ilibidi yarudie uchaguzi. Pamoja na kasoro hizo chaguzi zilikamilishwa na Serikali kuundwa. Kasoro kwa kawaida zilishughulikiwa baadaye kwa kurekebisha Sheria na hata Katiba ili chaguzi zinazofuata ziwe bora zaidi. Suala la kujiuliza kuwa kasoro za mara hii ambazo hazikuwasilishwa kwa taratibu zinazofaa zilikuwa kubwa kiasi gani (were the irregularities so fatal to the election process?). Hivi kweli Uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa na kasoro nyingi kuliko hata ule wa mwaka 2000? Uchaguzi hauwezi tu kurejewa bila kufanyika uchunguzi huru na wa kitaalamu usiokuwa na maslahi ya kisiasa au kuficha ukweli;
  1. f) Tume Kuingiliwa Katika Kazi zake: Kwa mujibu wa kifungu cha 119(12), Tume haipaswi kupokea maagizo au kufuata maagizo ya chombo au chama chochote cha siasa. Ni dhahiri kwamba uamuzi wa Mwenyekiti, kama yeye mwenyewe alivyowaeleza Makamishna wenziwe tarehe 1 Novemba, umetokana na kufuata maagizo ya vyombo, maagizo ya Chama na amri ya Serikali. Aidha, kitendo cha Makamu Mwenyekiti wa Tume kukamatwa na kupelekwa Polisi wakati anatekeleza majukumu yake ni ukiukwaji uliochupa mpaka wa Katiba na pia ni kuingilia kazi za Tume kwa uwazi kabisa;
Athari ya mambo yote haya ni ukiukwaji mkubwa na wa wazi wa Katiba ambao hauwezi kutetewa au kuhalalishwa kwa kutambua ufutwaji usio halali wa uchaguzi unaodaiwa kufanywa na Mwenyekiti wa Tume.
  1. ATHARI NA CHANGAMOTO ZINAZOTOKANA NA KUFUTWA KWA UCHAGUZI
    Kufutwa kusiko halali kwa uchaguzi kumepelekea kuwepo athari kadhaa za kikatiba, kisiasa na kijamii. Miongoni mwa athari kubwa ni kama zifuatazo:
    1) Mgogoro Mkubwa wa Kikatiba na Kisheria
  2. a) Kutokuwepo Rais Halali wa Zanzibar
    Mgogoro wa kikatiba ulioikumba Zanzibar kutokana na kufutwa kusiko halali kwa uchaguzi una nyanja nyingi. Ya kwanza ni suala la Rais kumaliza muda wake kikatiba. Katiba ya Zanzibar chini ya kifungu cha 28(2) kimeeleza wazi kwamba muda wa Rais kushikilia wadhifa huo ni miaka mitano. Kifungu cha 29 kinaeleza masharti ya kuongeza muda huo wa miaka mitano ambayo ni magumu na yenye ukomo maalum. Hata hivyo, washauri wa Rais kwa kutumia tafsiri isiyo sahihi ya Katiba wamemshauri kwamba kwa kutumia kifungu cha 28(1)(a) anaweza kuendelea kuwa Rais hadi Rais mpya atapoapishwa. Kwa ufupi tunaangalia athari ya tafsiri hiyo:
    Mipaka ya Kifungu cha 28(1)(a)
Kifungu cha 28(1)(a) kinachoruhusu Rais aendelee mpaka Rais anayefuata ale kiapo kina mipaka ya wazi katika Katiba. Mpaka wa kwanza unahusu muda wa Urais. Katiba chini ya kifungu cha 28(2) kimeweka bayana kuwa muda wa Urais ni miaka mitano. Hili ni sharti mahsusi na ndio maana Katiba haijaruhusu suala la kuongezwa muda wa miaka 5 lifanywe kiholela au kwa mlango wa nyuma. Kifungu cha 29 cha Katiba kimeweka bayana sababu na utaratibu wa kuongeza miaka mitano. Sababu hizo ni nzito na muda kuongezwa ni mahsusi. Kifungu cha 29 kinaeleza: “ikiwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imo katika vita na ikiwa Rais anaona kuwa ni muhimu kuzuia uchaguzi, Baraza la Wawakilishi linaweza kwa kupitisha azimio, kuzidisha muda wa miaka mitano uliotajwa kwenye kijifungu cha (2) cha kifungu cha 28 katika kipindi hadi kipindi lakini hakuna kipindi kitachozidi miezi sita mfululizo.”
Mpaka wa pili unaoonesha ni kwa kiasi gani Katiba haitoi mwanya wa kujiongezea miaka mitano, ni ile ya ukomo wa vipindi viwili vya miaka mitano chini ya kifungu cha 30(1)(b). Katika kuonesha jinsi Katiba ilivyo strict katika ukomo wa miaka mitano, tafsiri ya miaka mitano chini ya kifungu cha 34(iv) imefanywa kwa namna ambayo Katiba inaruhusu miaka mitano ipungue kuliko kuzidi. Kifungu hicho kinaeleza: “bila kujali masharti ya vifungu vya 28(3) na 30(1) (b) vya Katiba, endapo mtu anayemfuata Rais kwa madaraka atashika kiti cha Rais kwa kipindi kinachopungua miaka minne ataruhusiwa kugombea nafasi ya Rais mara mbili lakini kama atashika kiti cha Rais kwa muda wa miaka minne au zaidi ataruhusiwa kugombea nafasi ya Rais mara moja tu.”
Kama Katiba ingekuwa imelichukulia kipindi cha miaka mitano kwa wepesi kama alivyotaka kutuaminisha aliyetoa ushauri basi isingechukua shida ya kutafsiri maana ya miaka mitano kwa namna iliyofanywa na kifungu cha 34(iv).
Hivyo tafsiri yoyote ya Katiba inayotoa mwanya wa kuongeza kipindi cha Urais cha miaka mitano kwa njia nyepesi, ya kiholela na ya kiujanja, tafsiri hiyo haiwezi kuwa sahihi. Katika kutafsiri Katiba Profesa Crabe ametoa angalizo muhimu kwa kusema kuwa: “its [the constitution] provisions are not mere rules of conduct for the guidance of society, but also commands to be obeyed. It is not an equation in mathematics to be interpreted by reference to numbers, it is, in a sense, organic….all the duties, obligations, powers, privileges and rights must be exercised in accordance with the letter of the constitution. More than that, they should be exercised and enforced in accordance with the spirit of the constitution”
Mgongano wa Tafsiri na Kifungu cha 28(2) na 29
Ushahidi mwengine wa wazi kuwa tafsiri inayotolewa ya kifungu cha 28(1) (a) kuwa sio sahihi ipo katika Kanuni za tafsiri ya sheria. Moja ya Kanuni za msingi ni kuwa tafsiri yoyote ya sheria au kifungu cha sheria inayopelekea kufanya kifungu chengine cha sheria kisiwe na maana (irrelevant) au kisiwe na haja ya kuwepo (redundant) basi tafsiri hiyo ni ya kituko (absurd). Na tafsiri yoyote ya kituko basi sio sahihi. Tafsiri inayotolewa kumruhusu Rais aendelee inakifanya kifungu cha 28(2) kinachoweka muda wa Urais kuwa miaka mitano kisiwe na maana. Aidha, inakifanya kifungu cha 29 cha Katiba kinachoeleza sababu na utaratibu wa kuongeza huo muda wa miaka mitano kisiwe na haja ya kuwepo. Lakini pia inafanya mfumo mzima wa kuvunjwa Baraza la Wawakilishi na kuitishwa uchaguzi mkuu ndani ya muda maalum na muda wa ukomo wa vipindi vya Urais vyote visiwe na maana. Kifungu cha 28(1) (a) hakizungumzii muda wa Urais bali kinazungumzia wakati tu mahsusi ndani ya hiyo miaka mitano ambapo kiti cha Rais atakabidhiwa mtu mwengine.
Kifungu hicho kinaweza tu kutumika kuongezeka kwa miaka mitano iwapo itatokea dharura halali kwa mujibu wa sheria (exigency by operation of the law) kama vile Uchaguzi katika jimbo au majimbo fulani unapotokea kuharibika kwa sababu inayokubalika na ambayo sheria imeiruhusu Tume kuakhirisha uchaguzi na kuitisha siku nyengine. Hii ni dharura ambayo sheria imeshaiwekea misingi yake. Au dharura isiyotazamiwa na inayokubalika (unforeseeable legitimate exigency). Mfano mzuri hapa ni pale mgombea anapofariki kabla tu ya uchaguzi au kabla ya kuapishwa. Hizi ni dharura ambazo mifumo yote ya kisheria inazitambua na hata Mahkama imezitambua.
  • Athari za Tafsiri isiyokuwa sahihi
    Tafsiri isiyo sahihi iliyotolewa ina athari kubwa zifuatazo:
    • Kwanza, Katiba haikuweka muda maalumu wa kufanya uchaguzi uliofutwa katika mazingira yasiyokuwa halali. Kisheria uchaguzi uliofutwa katika mazingira hayo hauitwi kwamba ni uchaguzi uliofutwa bali ni uchaguzi unaodaiwa umefutwa (purported nullification of election). Katiba imeweka muda kwa chaguzi zinazoitishwa kihalali tu ama kwa kuvunjwa Baraza, kufariki mwenye wadhifa au matokeo kulingana. Kwa tafsiri iliyotolewa ina maana kuwa Rais aliyepo anaweza kushika wadhifa huo hadi Tume ya Uchaguzi itapoamua kuitisha uchaguzi. Kwa vile hakuna ukomo wala muda maalum uliowekwa ndani ya Katiba wala Sheria uchaguzi unaweza kuitishwa hata baada ya mwaka mmoja au miwili kwa vile hakuna ukomo wa kikatiba wala wa kisheria. Athari ya jambo hili ni sawa na kuisimamisha sehemu ya Katiba;
  • Pili, tafsiri hiyo ya Katiba inatoa mwanya kwa Rais kutosimamia Katiba kwa kutomchukulia hatua Mjumbe wa Tume aliyekwenda kinyume na Katiba au sheria iwapo tu Mjumbe huyo amefanya hivyo kwa manufaa ya Rais. Kifungu cha 119(6) (7) na (8) vinaeleza wajibu wa Rais kusimamia nidhamu na uadilifu wa Tume. Kama Rais atafumbia macho wajibu huo kwa vile amefaidika na uhalifu huo dhidi ya Katiba ni sawa na kusema kuwa Tume ya Uchaguzi ipo juu ya Katiba na Sheria za nchi kwa vile Rais ana hiari ya kusimamia vifungu vya Katiba vinavyosimamia nidhamu yao. Kubwa zaidi kuliko yote ni kujiuliza iwapo mwendo huo wa Rais hauendani kinyume na masharti ya kifungu cha 37(2) cha Katiba kinachokataza Rais kufanya kitendo kinachokwenda kinyume na Katiba na kwamba akifanya hivyo anaweza kushitakiwa mbele ya Baraza la Wawakilishi.
    Tafsiri sahihi ni kwamba Rais lazima ashike madaraka ya Urais na aachie nafasi hiyo ndani ya muda huo wa miaka mitano isipokuwa kwa dharura halali za kisheria ambazo zinakubalika. Ikiwa ukomo huo hautazingatiwa basi Katiba yenyewe haitakuwa na maana na masharti yaliyowekwa bayana tena kwa maandishi yatakuwa pia hayana maana. Aliyewahi kuwa Jaji Mkuu wa Marekani, Justice John Marshall aliwahi kueleza haja ya wanaotakiwa kulinda Katiba kutii masharti ya Katiba kwa kueleza yafuatayo: “ to what purpose are powers limited, and to what purpose is that limitation committed to writing, if these limits may, at any time, be passed by those intended to be restrained?” [Marbury v. Madison, pg 137]
    Hivyo, mgogoro wa kwanza ni kutokuwepo Rais halali wa Zanzibar tokea tarehe 3 Novemba, 2015. Pamoja na hali hiyo, anayedai kuendelea na Urais amekuwa akifanya maamuzi makubwa yakiwemo ya uteuzi ambayo yana athari kubwa hapo baadaye.
  1. b) Kutokuwepo Mawaziri
Baraza la Wawakilishi tokea tarehe 12 Novemba, limemaliza muda wa uhai wake kwa mujibu kifungu cha 92(1) cha Katiba. Hali hii ni tofauti sana na kipindi ambacho Baraza limevunjwa chini ya vifungu vya 90(1) na 91(1) vya Katiba. Katika Katiba ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano na takriban katika nchi zote zenye asili ya mfumo wa Westminster na hata mfumo wa Jamhuri (republican form of government) zipo dhana mbili kuu kuhusiana na uhai wa Baraza la Wawakilishi (Bunge). Dhana ya kwanza ni ya Baraza kuvunjwa (dissolution of parliament) na dhana ya pili ni ile ya Baraza kumaliza muda wake (lapse of tenure of Parliament). Dhana hizi mbili ni tofauti na zina athari tofauti katika uhai wa Bunge na wa Serikali. Hata katika Katiba ya Zanzibar ya 1984, tokea awali ilipotungwa mwaka 1984 dhana hizi mbili zilitenganishwa na ziliwekewa masharti tofauti juu ya uhai wa Baraza.
Dhana ya Baraza kuvunjwa na athari zake iliwekwa chini ya kifungu cha 90(1) na ile ya Baraza kumaliza muda iliwekwa chini ya kifungu cha 92 sawa na Katiba ilivyo sasa hivi. Tofauti yao ni neno tu ambalo limetumika; chini ya Toleo la mwanzo la Katiba neno lililotumika ni “Baraza litapovunjika” na Toleo la 2010 neno linalotumika ni “Baraza litapovunjwa”. Tofauti hii ya maneno ilifanywa na kifungu cha 25 cha Sheria ya Marekebisho ya Kumi ya Katiba, Namba 2 ya 2002. Hata hivyo mabadiliko haya ya maneno hayakubadili dhana hizi mbili kwa namna yoyote ile.
Katiba ya Zanzibar imeweka dhana mbili katika uhai wa Baraza. Kwanza Baraza linavunjwa. Madhumuni ya kuvunjwa ni kutoa fursa ya kuandaa uchaguzi mkuu. Katiba imetoa siku 90 kufanyika maandalizi ya uchaguzi hadi Baraza na Rais mpya kuapishwa. Katika kipindi hicho ndipo ambapo Mawaziri wanaendelea kuwa Mawaziri. Kifungu cha 48(b) kimetumia maneno ya wazi kwamba nafasi ya Waziri itakuwa wazi: “iwapo mjumbe ameacha kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa sababu nyengine zaidi ya kuvunjika kwa Baraza hilo”. Hivyo, Baraza kumalizika muda (lapse or expiration of tenure) ni wazi haingii katika dhana ya Baraza kuvunjika (dissolution). Baraza likimalizika muda linakuwa halipo na ndio maana hata Katiba, kifungu cha 92(1) kimetumia maneno “Maisha ya Baraza la Wawakilishi yataendelea kwa muda wa miaka mitano”. Kwa hivyo baada ya miaka mitano uhai wa Baraza husika unaisha na kwa hivyo Waziri anakosa sifa ya kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi. Tafsiri ya Waziri iliyopo katika kifungu cha 134 inaliweka hili bayana zaidi kama ifuatavyo: “Waziri maana yake ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi aliyekabidhiwa wadhifa wa kazi ya Waziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar”. Aidha kifungu cha 42(2) na 43(2) vinavyohusu uteuzi wa Mawaziri na Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi vimeeleza wazi kuwa Mawaziri na Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi watateuliwa kutoka miongoni mwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Kwa kuelewa kwamba dhana ya kuvunjwa Bunge (dissolution) na kumalizika muda au uhai wa Bunge (lapse or expiration of tenure) ni vitu viwili tofauti, ndio maana Katiba ya baadhi ya nchi wameweka bayana dhana hizi mbili katika suala la kuendelea nafasi ya uwaziri baada ya Bunge kuvunjwa au kumaliza muda. Katiba ya Fiji kwa mfano, katika kifungu cha 105(2) inaeleza: “subject to subsection (2), appointment of a Minister terminates if;
(a)…
(d) the Minister ceases to be a Member of Parliament
(2) if a Minister ceases to be a Member of Parliament because of the expiry or dissolution of the House of Representatives, he or she continues in office as Minister until the next appointment of a Prime Minister.
Katiba ya Zanzibar imeruhusu kwa maneno ya wazi kuwa Waziri aendelee na uwaziri katika kipindi ambacho Baraza limevunjwa tu na sio wakati ambao Baraza limemaliza muda. Kwa hivyo tokea Baraza kumaliza muda wake tarehe 12 Novemba, Zanzibar haina mawaziri. Hata hivyo baadhi ya waliokuwa mawaziri wamefanywa kama bado ni mawaziri na wanaendelea kufanya maamuzi makubwa jambo ambalo ni la hatari.
  1. c) Kutokuwepo Baraza la Wawakilishi
    Baraza la Wawakilishi limemaliza muda tokea tarehe 12 Novemba. Hoja kuhusu suala hili yameelezwa kwa kina katika aya (b) hapo juu inayohusu kutokuwepo mawaziri. Aidha, Spika wa Baraza hilo amethibitisha kwamba Baraza halipo ingawa jambo la kushangaza naye amedai yeye na Naibu wake wanaendelea kushika madaraka yao mpaka Spika mpya atapoapishwa. Katiba ya Zanzibar imeeleza wazi chini ya kifungu cha 5A mgawanyo wa kazi baina ya mihimili mikuu ya Serikali. Miongoni mwa mihimili hiyo ni Baraza la Wawakilishi. Kazi muhimu ya Baraza ni kuisimamia Serikali. Kutokuwepo chombo hicho huku Serikali ikiendelea na kazi zake ni jambo la kuvunja katiba kwa kiasi kikubwa.
2) Hoja ya Kurudiwa Uchaguzi
Hoja ya kurudiwa uchaguzi ambayo imeshikiwa bango na Chama cha Mapinduzi, Zanzibar ni ya kutafuta manufaa ya kisiasa baada ya Chama cha Mapinduzi kushindwa katika uchaguzi. Mbali ya matokeo ya uchaguzi ya Urais wa Zanzibar ambayo yanaonyesha wazi kuwa CCM imeshindwa kwa kura nyingi sana kwa kiwango na uzoefu wa Zanzibar, hata kura za Urais wa Jamhuri ya Muungano kwa upande wa Zanzibar zinaonyesha hivyo hivyo na kwa hiyo kuthibitisha kuwa CCM ilipoteza uchaguzi huo. Kwa muhtasari matokeo ya Urais wa Muungano kwa upande wa Zanzibar ni kama yafuatavyo:
MGOMBEA KURA HALALI ASILIMIA
DR. JOHN POMBE MAGUFULI 194,317 46.5%
EDWARD NGOYAYE LOWASSA 211,033 50.50%
IDADI YA KURA HALALI 417,882
Matokeo ya kura za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani yote yanaonyesha CCM imeshindwa kwa idadi ya kura za walio wengi (popular votes). CCM imeweza kupata viti sawa na CUF katika uwakilishi na ubunge kwa sababu ya mbinu zilizotumika katika ukataji wa majimbo.
Hivyo, kimsingi Hoja ya kurudia uchaguzi haina msingi na haiwezekani kutekelezwa kwa sababu kadhaa. Miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na zifuatazo:
a) Kukosekana Uhalali wa Msingi wa Kurejea Uchaguzi
Kama ilivyoelezwa awali kwamba hatua ya Mwenyekiti wa Tume kufuta uchaguzi haikuwa halali na ina kasoro nyingi za kikatiba na kisheria. Kurejea uchaguzi ni sawa na kuhalalisha kitendo batili alichofanya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi. Aidha ni kuweka “precedent” mbaya kwamba uchaguzi unaweza kufutwa kwa sababu zozote zile japo kama sio halali.
b) Kujenga Msingi Batili Kisheria Katika Mustakbala wa Uchaguzi
Kiini cha mzozo uliozushwa katika uchaguzi ni uamuzi batili wa Mwenyekiti wa Tume. Kurejea uchaguzi bila kupatia ufumbuzi juu ya uhalali wa uamuzi wa Mwenyekiti ni sawa na kuhalalisha kitendo cha Mwenyekiti na kutoa ruhusa kuwa huko mbele anaweza kufanya tena kitendo kama hicho au Tume inaweza kufanya kitendo kama hicho. Hii ni kujenga msingi wa kuwa na chaguzi zisizokwisha na mizozo isiyo na mwisho. Lazima mipaka ya Mwenyekiti na Tume iwekwe bayana ili hapo baadaye ijulikane nini ukomo wa mamlaka yao.
  1. c) Kujenga Imani ya Wapiga Kura
    Uchaguzi ni wa wapiga kura na sio wa vyama au wagombea. Lazima wapiga kura waridhishwe kuwa uchaguzi ulikuwa na tatizo la kiasi cha kuufanya matokeo yake yasionyeshe dhamira na uamuzi wa wapiga kura. Hadi sasa hakuna mwelekeo unaonyesha kuna ukweli katika tuhuma za kasoro za uchaguzi. Moja ya madai ya CCM ni kwamba eti Pemba watu waliopiga kura walikuwa ni zaidi ya walioandikishwa lakini ukweli ni kwamba takriban watu 29,000 walioandikishwa hawakupiga kura kisiwani humo. Katika mazungumzo yanayoendelea Ikulu, Zanzibar baina ya viongozi, CCM imetakiwa mara kadhaa kuleta ushahidi wa tuhuma zake kwamba kulikuwa na hujuma lakini imeshindwa kufanya hivyo. Matamko ya Waangalizi wa Uchaguzi na namna tuhuma za kasoro za uchaguzi zilivyoibuliwa na Mwenyekiti wa Tume haziwezi kuwashawishi wapiga kura kwamba kulikuwa na kasoro katika uchaguzi. Hoja ya kurudiwa uchaguzi inaonekana wazi kuwa ni ajenda ya kisiasa ya chama kilichoshindwa. Hali hii ni sababu tosha ya kuleta fujo iwapo hatua yoyote ya kurudia uchaguzi itachukuliwa.
  2. d) Changamoto za Kuunda Tume Mpya ya Uchaguzi
    Ni dhahiri kuwa uchaguzi wa Zanzibar umehujumiwa na Mwenyekiti wa Tume kwa sababu ya sindikizo la kisiasa. Kwa vyovyote vile yeye hafai tena kuendelea kuiongoza Tume hiyo katika kazi yoyote ya Tume iliyobaki. Ni lazima akae pembeni.
    Kurejea uchaguzi ni sawa na kuihukumu Tume nzima kuwa ina makosa wakati makosa hayo yalifanywa na mtu mmoja tu. Hivyo, kwa vyovyote vile, kama uchaguzi utarudiwa, haitawezekana kwa Tume iliyopo na Sekretarieti kusimamia uchaguzi wa marudio. Kufanya hivyo ni mgongano mkubwa wa maamuzi kwamba Tume iliyokiri kuharibu uchaguzi isimamie tena uchaguzi wa marudio. Hivyo, kama Tume na Sekretarieti itabidi iondoke na kuunda Tume na Sekretarieti mpya, bado kutakuwa na changamoto kubwa zaidi ya kuunda Tume mpya ya uchaguzi. Miongoni mwa changamoto kubwa ni kama zifuatazo:
  3. Kuondolewa Wajumbe waliopo: kwa mujibu wa kifungu cha 119(6),(7) na (8) cha Katiba, Wajumbe wa Tume wana kinga ya kutoondolewa katika nafasi yao isipokuwa kwa kufuata utaratibu maalum sawa na ule wa kumuondoa Jaji wa Mahkama Kuu (security of tenure). Njia nyengine nyepesi ni kwa Mjumbe kujiuzulu kwa hiari yake. Hii ni changamoto kubwa hasa kwa kuzingatia kwamba Wajumbe wanaamini kwamba hawakufanya makosa yoyote na aliyefanya makosa tena kwa makusudi anajulikana lakini analindwa kwa maslahi ya kisiasa;
  4. Utaratibu wa Kuunda Tume ya Uchaguzi; kwa mujibu wa kifungu cha 119(1)(b) cha Katiba, Wajumbe wawili wa Tume ya Uchaguzi wanateuliwa na Rais kutokana na mapendekezo ya Kiongozi wa Shughuli za Serikali katika Baraza la Wawakilishi. Ni ukweli ulio wazi kwamba sasa hivi Baraza la Wawakilishi limemaliza muda tokea tarehe 12 Novemba. Kwa sababu hiyo, hakuna Kiongozi wa Shughuli za Serikali katika Baraza ambalo halipo. Kiongozi wa Shughuli za Serikali katika Baraza lililopita, tukiweka siasa upande, kisheria, ni dhahiri kuwa amesita kuwa na wadhifa huo kwa vile Baraza limemaliza muda chini ya masharti ya kifungu cha 92(1) cha Katiba. Kabla ya Baraza kumaliza muda wake, ni wazi kuwa alikuwa akilindwa na kifungu cha 48(b). Baada ya Baraza kumaliza muda wa uhai wake, kifungu hicho hakiwezi kutumika. Aidha kifungu cha 48(d) ambacho baadhi ya watu wanadhani kinaweza kutumika hakiwezi kutumika kwa vile masharti ya aya za (a) mpaka (d) ya kifungu cha 48 ni ya kujitosheleza kila moja ndio mana ikatumika neno au baina ya kila aya. Hivyo kwa vile Kiongozi wa shughuli za Serikali katika Baraza lililomaliza muda wake amesita kuwa Mjumbe wa Baraza kwa sababu ya Baraza kumaliza uhai wake, hawezi kutumia masharti ya kifungu cha 48(d) kwa vile tayari ameshaondokewa na sifa chini ya kifungu cha 48(b) ambayo ni sifa ya lazima chini ya kifungu cha 39(6) ya kuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali ndani ya Baraza. Hivyo haitowezekana kuwapata Wajumbe 2 wa Tume kutokana na kutokuwepo msingi halali wa kikatiba wa kuwapata;
iii. Muda wa kujenga uwezo wa kiutendaji na wa kitaasisi:Hata kama changamoto zilizotajwa hapo juu zitapatiwa ufumbuzi, changamoto kubwa ni ile ya muda utaohitajika kujenga uwezo wa kiutendaji kwa Sekretarieti na wasaidizi wao katika ngazi ya Mikoa na Wilaya na Wajumbe wa Tume ili waweze kusimamia uchaguzi kwa ufanisi wa viwango vinavyokubalika. Changamoto nyengine ni ya muda utaohitajika wa Tume kuhakiki na kujiridhisha na daftari la wapiga kura ambayo ndio nyenzo kuu ya uchaguzi. Kwa vyovyote vile muda utaohitajika kwa Tume mpya kujiandaa hadi kufanya uchaguzi mwengine kwa kiwango cha chini kabisa ni angalau mwaka mmoja. Suala muhimu ni kwamba nchi itawezaje kwenda wakati hakuna Baraza la Wawakilishi wala hakuna Baraza la Mapinduzi. Kutokuwepo kwa Baraza la Mapinduzi kwa maana ya mawaziri kutaathiri sana utendaji kwa vile mawaziri wana mamlaka makubwa ya kisheria chini ya Sheria mbali mbali kama vile za fedha hivyo kutokuwepo kwao au uwepo wao usiokuwa halali kisheria kuna athari kubwa katika utendaji wa Serikali. Changamoto kubwa zaidi ni suala la bajeti ya Serikali ambayo ni lazima iandaliwe na ipitishwe ndani ya muda maalum.
Kwa kuzingatia sababu zote hizo, ni wazi kuwa Hoja ya kurudiwa uchaguzi haina uhalali, haina msingi na ni chachu ya kuiweka nchi katika utawala usiokuwa halali na kusababisha fadhaa kubwa kwa wananchi. Ni hoja ambayo inaweza kuzaa fujo na vurugu katika nchi na kupelekea mzozo mkubwa zaidi wa kikatiba na kisheria. Sidhani kama tunataka tuifikishe huko nchi na tuwafikishe huko wananchi tulioapa kuwatumikia na kuwalinda.
  1. MAZUNGUMZO YANAYOWAHUSISHA WAGOMBEA URAIS WA CUF NA CCM PAMOJA NA MARAIS WASTAAFU WA ZANZIBAR
    Kufuatia jitihada kubwa nilizozifanya kwa njia ya simu na hatimaye kufikisha maombi yangu kwa maandishi kumtaka Dk. Ali Mohamed Shein akutane na mimi, hatimaye alikubali na kupendekeza tuwashirikishe viongozi wengine wastaafu wa Zanzibar.
    Hadi sasa tumeshafanya vikao vinane, cha kwanza kikiwa ni kile cha tarehe 9 Novemba, 2015.
Wengi wenu mmehoji kwa nini nikakubali kushiriki vikao ambavyo niko peke yangu kutoka CUF wakati CCM wako watano. Nilikubali hivyo kwa kutumia msingi wa kuwashirikisha Marais wastaafu wa Zanzibar lakini pia nikiamini kwamba tungeongozwa na busara na kuheshimu Katiba na Sheria badala ya utashi wa vyama vyetu.
Tokea mazungumzo hayo yaanze, wananchi wengi wamekuwa wakitaka tuwaeleze kinachoendelea. Mimi binfasi niliamua kubaki kimya kwa kuheshimu msingi tuliojiwekea kwamba taarifa ya mazungumzo hayo itolewe kwa pamoja baada ya mazungumzo kukamilika. Hata hivyo, inasikitisha kuona wakati mimi nikiheshimu hilo na kuwa kimya kipindi chote hicho, viongozi wenzangu kutoka upande mwengine wamekuwa wakiliuka hilo na kutoa taarifa ambazo zimekuwa zikiwachanganya wananchi.
Kutokana na mwenendo huo, nimeona kuna haja na mimi kuwaeleza wananchi ukweli wa kile kinachoendelea.
Rais John Pombe Magufuli amefanya kazi kubwa ya kututia moyo ili tukamilishe mazungumzo hayo kwa ufanisi na kwa kuzingatia matakwa ya Katiba na Sheria. Alikutana na mimi na baadaye akakutana na Dk. Ali Mohamed Shein. Hata hivyo, inasikitisha kwamba hata yeye Rais Magufuli hakuachwa kufitinishwa na wananchi wa Zanzibar pale Balozi Seif Ali Iddi alipodai hadharani kwamba eti Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katutaka turudi Zanzibar tukakamilishe taratibu za kurudia uchaguzi, jambo ambalo si kweli.
Ukweli ni kwamba katika vikao hivyo vinane bado Dk. Ali Mohamed Shein na Balozi Seif Ali Iddi wanan’gan’gania kurudia uchaguzi huku wakimtetea kwa nguvu zote Jecha Salum Jecha, na mimi nimesisitiza haja ya kuheshimu matakwa ya kikatiba na kisheria na maamuzi ya wananchi wa Zanzibar waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015 katika uchaguzi ambao waangalizi wote wa ndani na nje na hata Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar walisema kwamba ulikuwa huru, wa haki na uliofanyika katika hali ya amani.
Kwa hakika hadi jana, ukiangalia tovuti ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar utaona taarifa zinazosema kwamba uchaguzi hadi hatua ya kuhesabu kura ulifanyika kwa utulivu nchi nzima.
Kutokana na kutofikia muafaka pamoja, tulikubaliana kuandaa taarifa ya pamoja ambayo ilielezwa kwamba ingeandaliwa na Katibu wa vikao hivyo lakini sasa ni zaidi ya wiki mbili, hakuna kikao kilichoitishwa. Nimeandika barua kuhimiza kikao cha kupokea taarifa hiyo na kuipitisha lakini bado Dk. Shein anasema wanahitaji muda.
Ni wazi kwamba Dk. Ali Mohamed Shein hakuwa na nia njema katika mazungumzo haya na amepoteza sifa ya kuongoza vikao hivyo.
  1. NJAMA ZA CHINI KWA CHINI ZA KUHUJUMU UTAFUTAJI WA UFUMBUZI WA HAKI
    Wakati Dk. Ali Mohamed Shein akikwepa kwa makusudi kuitisha kikao cha kupokea taarifa ya mazungumzo hayo, tumegundua kwamba lengo halisi ni kuisindikiza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kutangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio ili baadaye itolewe hoja kwamba suala hilo limeshaamuliwa.
    Tunazo taarifa za uhakika kwamba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imetakiwa kukutana tarehe 14 Januari, 2016 kwa lengo la kutangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio ambao unatajwa kuwa umepangwa ufanyike tarehe 28 Februari, 2016.
    Taarifa hizo zinaeleza kwamba lengo la hatua hiyo ni kukwamisha juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli, za kutaka kuona ufumbuzi wa haki na unaozingatia matakwa ya kikatiba na kisheria unapatikana.
    Tukiruhusu hatua hiyo maana yake ni kuwaruhusu kikundi cha watu wachache wanaotumia nafasi zao kujifaidisha kibinafsi na bila ya kujali maslahi mapana ya nchi na watu wake na wasiojali amani na utulivu wan chi kututumbukiza katika balaa kubwa sana.
Hivi tunavyozungumza wananchi wa Zanzibar wako taaban na wamekumbwa na fadhaa baada ya kushuhudia maamuzi yao waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015 kupitia uchaguzi huru, wa haki na wa wazi yakiwa yanakanyagwa. Wamesubiri kiasi cha kutosha kwa sababu sisi viongozi wao tunaojali amani ya nchi tumewataka wasubiri. Sasa umefika wakati uvumilivu na subira zao zinafikia kikomo. Wanahitaji kuona SUBIRA zao zinazaa HAKI.
Ni vyema tukaweka wazi wazi hapa kwamba kurudiwa uchaguzi sio suluhisho na HAKUKUBALIKI. Kwani kama nilivyoonesha, hakuna hoja wala msingi wa kikatiba na kisheria wa uchaguzi kurudiwa.
  1. NAMNA BORA YA KUTATUA MZOZO ULIOPO
    Kutokana na maelezo ya hapo juu, ni dhahiri kwamba mzozo huu wa kikatiba na kisiasa ambao umetokana na hujuma zilizofanywa katika uchaguzi wa Zanzibar haukuwa wa lazima na unaweza kutatuliwa kwa haraka kama utakuwepo utashi na utayari wa dhati wa kisiasa na wa kiuongozi ambao unazingatia maslahi mapana na endelevu ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ili kufikia utatuzi huo wa haraka na unaozingatia na kuheshimu Katiba na sheria ziliopo na misingi ya utawala bora njia zifuatazo ndizo zitakazotukwamua hapa tulipokwama:
    1) Ili kulinda misingi ya Katiba ya Zanzibar inayoelekeza utaratibu wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kufanya maamuzi kama inavyoelezwa na kifungu cha 119(1) na (10) na ili kujenga uhalali na heshima ya Tume katika kutekeleza kazi zake, ni lazima Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar atakiwe kukaa pembeni kwa kujiuzulu au kusimamishwa kazi hiyo kwa vile amefanya makosa makubwa yafuatayo:
  2. Yeye kama Mwenyekiti wa Tume hakuwa na mamlaka ya kufanya uamuzi kwa jambo lolote linalohusu Tume bila ya kupitia vikao halali vya Tume kinyume na maelekezo ya wazi ya kifungu cha 119(10) cha Katiba ya Zanzibar;
  3. Akiwa Mwenyekiti wa Tume ametoa Tangazo Namba 130 katika Gazeti Rasmi la Serikali linalodaiwa kuwa ni uamuzi wa Tume la kufuta matokeo ya uchaguzi huku akijua kwamba Tume ya Uchaguzi haikufanya kikao tarehe 28 Oktoba kupitisha uamuzi huo;
  4. Akiwa Mwenyekiti wa Tume ametoa tangazo la kufuta uchaguzi huku akijua kwamba hana mamlaka ya kufanya hivyo na akijua pia kwamba hata Tume ya Uchaguzi haina mamlaka ya kufanya hivyo;
  5. Akiwa Mwenyekiti wa Tume amesema uongo hadharani ili kuhalalisha kitendo chake cha kutoa tamko la kufuta uchaguzi kama alivyokiri yeye mwenyewe katika kikao cha Tume cha tarehe 1 Novemba, 2015;
    Mambo yote haya ni ukiukaji wa Katiba, Sheria na Maadili ya dhamana aliyokabidhiwa;
    2) Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar chini ya Makamu Mwenyekiti na Makamishna waliobaki wamalizie kutangaza matokeo ya Urais kwa majimbo 9 ambayo yalishahakikiwa na kumalizia kuhakiki matokeo ya Urais kwa majimbo 14 yaliyobaki na kutangaza matokeo. Hatimaye wamtangaze mshindi wa Urais wa Zanzibar. Hatua hii ni halali na sahihi chini ya kifungu cha 119(10) cha Katiba ya Zanzibar. Aidha, chini ya kifungu cha 42(6) cha Sheria ya Uchaguzi, hatua hiyo ni halali kwa vile kifungu hicho kinataka matokeo ya Urais yatangazwe ndani ya siku 3 ama ikiwa kutakuwa na matatizo basi ndani ya siku 3 baada ya matatizo haya kutatuliwa;
3) Kwa kuwa suala hili ni kubwa na limeathiri taswira ya nchi yetu mbele ya jumuiya ya kimataifa kwa kiasi kikubwa, na hasa kwa vile Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli, wakati alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kukutana na mimi Ikulu Dar es Salaam alisisitiza haja ya kukamilisha mazungumzo na kulipatia ufumbuzi wa haraka, tunaona wakati umefika yeye mwenyewe aongoze juhudi zenye lengo la kufanikisha hatua zilizopendekezwa hapo juu;
4) Uongozi wa juu wa Vyama vya CUF na CCM ufanye mazungumzo ya haraka ya kukamilisha taratibu za kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar chini ya mshindi wa uchaguzi wa Urais wa Zanzibar aliyepewa ridhaa na Wazanzibari kupitia uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015. Kupitia vikao hivyo, kama kuna mambo yoyote yanayohitaji kujadiliwa na kupata muafaka juu ya uundwaji wa Serikali hiyo yajadiliwe na kupata muafaka;
5) Mambo yoyote yanayohitaji kurekebishwa katika mfumo wa uchaguzi wa Zanzibar ili kuondoa kasoro ziliopo kwa nia ya kuimarisha mfumo huo kwa ajili ya chaguzi zozote za baadaye ni vyema yakawekewa muda maalum wa kujadiliwa na kupata muafaka.
HITIMISHO
Zanzibar imepita katika siasa za dhoruba na machafuko kwa zaidi ya miaka 50. Dhoruba na machafuko hayo yalifikia hadi kugharimu maisha ya watu. Ni kwa sababu ya kuchoshwa na siasa za aina hiyo na migogoro isiyokwisha ndiyo maana mwaka 2009, mimi na Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Karume, tulichukua maamuzi ya kijasiri ya kuleta MARIDHIANO ambayo yaliituliza Zanzibar.
Kila mmoja wetu ni shahidi kwamba kwa miaka sita iliyopita Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipumua kujibu hoja zisizokwisha kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar na badala yake tukawa tunapongezwa kwa kuleta maridhiano na kuanzisha muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Hatukutegemea kwamba baada ya kazi ile kubwa, sasa kutazuka kikundi cha viongozi waliopewa dhamana ya kuwaunganisha watu wafanye kazi ya kuyabomoa Maridhiano yetu na kuturudisha kwa nguvu kule tulikotoka. Watu hawa hawapaswi kupewa nafasi kufanikisha dhamira yao hiyo ovu. Na Wazanzibari hawatowapa nafasi hiyo. Ni kwa sababu hiyo tumeamua kuzungumza na Watanzania na kuwajuvya haya ili kuzuia nchi yetu isivurugwe na kurudishwa tulikotoka.
Tunaamini kwamba ufumbuzi wa mgogoro uliopo lazima uzingatie Katiba, Sheria na misingi ya utawala bora. Mapendekezo yaliyotolewa hapo juu ndio njia pekee ya kuutatua mzozo huo kwa kuzingatia misingi iliyotajwa. Utatuzi wowote nje ya hapo utakuwa ni wa nguvu na wa utashi wa kisiasa ambao hautaleta ufumbuzi endelevu na badala yake unaweza kuwa sababu ya mzozo mkubwa ambao hautaweza kutatuliwa kwa miaka mingi ijayo. Tumuombe Mwenyezi Mungu tusifike huko.
Mimi na wenzangu tumefanya kazi ya ziada kuwatuliza wananchi wa Zanzibar na kuwataka watoe nafasi kwa mazungumzo yanayoendelea huku kuwahakikishia kwamba suluhisho lolote litakalofikiwa litaheshimu maamuzi yao ya kidemokrasia waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015. Tumefanya hivyo kwa kutambua wajibu wetu kama viongozi kuhakikisha kwamba Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inabaki kuwa salama.
Ni bahati mbaya sana kwamba wengine wanauchukulia uungwana na ustaarabu wetu kwamba labda ni dalili ya udhaifu na wanadhani labda wanaweza kutuburuza. Kwa hilo, nawaambia wazi kwamba WASAHAU. Nataka niwahakikishie kwamba sisi si dhaifu ila tunaongozwa na uzalendo na mapenzi kwa nchi yetu na wananchi wenzetu. Lakini uzalendo huo huo na mapenzi hayo hayo kwa nchi yetu na wananchi wenzetu yanatutaka tusimame kuitetea na kuilinda Katiba na Sheria za nchi yetu, haki za raia na maamuzi yao ya kidemokrasia.
Zanzibar kuna tatizo kubwa ambalo halipaswi kuendelea kupuuzwa. Wakati umefika kwa mamlaka zinazohusika kutokwepa wajibu wao kwa wananchi wa Zanzibar.
Mimi na wenzangu, kama viongozi wenye dhamana kwa wananchi wa Zanzibar ambao walitupa ridhaa yao, tunawahakikishia kwamba tutakuwa tayari kushirikiana nao kuitetea haki yao na maamuzi yao ya kidemokrasia kwa nguvu zetu zote.
Nawashukuru kwa uvumilivu wenu na kwa kunisikiliza.

No comments: