Friday 25 March 2016

NAMBARI ZA JECHA KAMA BUSU, LA BINTI MFALME.

Hapa tusifanye uchambuzi wala tusifanye majumuisho, bali tusome tu hizi nambari kwa kuzingatia tafauti iliyopo. Katika ongezeko hilo, unaweza kuona kuwa kwenye baadhi ya majimbo, siku ya tarehe 20 Machi, Dk. Shein alipigiwa kura na “watu” 3,000+ wa ziada kutoka wale wa 25 Oktoba. Hiyo ndiyo hadithi ya Uzini, Tunguu, Mtopepo, Kikwajuni, Kwahani na hata jimbo la Malindi ambalo ni ngome ya CUF.
Majimbo yaliyotia fora katika haya ni la Mwanakwerekwe, ambako watu 5,594 wa ziada walijitokeza ‘kumpigia’ kura Dk. Shein siku ya tarehe 20 Machi, ikilinganishwa na wale wa Oktoba 25. Jimbo hilo linafuatiwa na la Chumbuni, ambalo lina ongezeko la kura 4,062.
Jimbo pekee ambalo linaweza kusemwa kuwa na ongezeko dogo kabisa kwa kura za Dk. Shein katika haya 31, ni la Donge ambalo liliongeza 53 tu likifuatiwa na Mkwajuni ambalo lina kura 66 za ziada.

Namshukuru sana ndugu yangu Yussuf Juma kwa msaada wake wa kunitumia matokeo ya majimbo kwa kura za urais ya ule unaoitwa "uchaguzi" wa tarehe 20 Machi, ambayo yamenisaidia kuyapiganisha na matokeo ya majimbo 31, ambayo binafsi niliyakusanya kutoka kinywani mwa Mwenyekiti wa ZEC na Makamu wake baina ya tarehe 25 na 26 Oktoba 2015 kabla ya Jecha hajatangaza "kuufuta" uchaguzi huo.


Sitaki kuingia kwenye ta'awili na uchambuzi wa chochote. Naweka tu hapa jadweli la mlinganisho wa zile kura ambazo Jecha Salum Jecha alizitangaza kwenda kwa Dk. Ali Mohamed Shein wa CCM katika uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015 na zile ambazo anadai zilikwenda tena kwa Dk. Shein siku ya tarehe 20 Machi.Picha nyengine ni ya kibuku cha kunakilia matokeo na kalamu nilotumia nikiwa Bwawani. Nilikuwa pia na kinasa sauti na kamera lakini sioni umuhimu wa kuweka picha zake hapa.Ukiacha hayo, sijaongeza chochote cha kukibuni mwenyewe, zaidi ya kuweka wino mwekundu kwenye jadweli la matokeo ili kuonesha tafauti ya ongezeko iliyopo.

Katika ongezeko hilo, unaweza kuona kuwa kwenye baadhi ya majimbo, siku ya tarehe 20 Machi Dk. Shein alipigiwa kura na "watu" 3,000 wa ziada kutoka wale wa 25 Oktoba. Hiyo ndiyo hadithi ya Uzini, Tunguu, Mtopepo, Kikwajuni, Kwahani na hata jimbo la Malindi ambalo ni ngome ya CUF.
Majimbo yaliyotia fora katika haya 31 ni la Mwanakwerekwe, ambako watu 5,594 wa ziada walijitokeza 'kumpigia' kura Dk. Shein siku ya tarehe 20 Machi, ikilinganishwa na wale wa Oktoba 25. Jimbo hilo linafuatiwa na la Chumbuni, ambalo lina ongezeko la kura 4,062 .Jimbo pekee ambalo linaweza kusemwa kuwa na ongezeko dogo kabisa kwa kura za Dk. Shein katika haya 31, ni la Mkwajuni, ambako ni kura 66 tu zilizoongezeka.

Watafiti katika siku zijazo wataweza kutupa maana ya ongezeko hili kwa namna tafiti zao zitakavyowaelekeza.Binafsi, kama mwandishi wa habari na juu ya yote kama Mzanzibari, nawasilisha andiko hili fupi ambalo sio uchambuzi wala tafsiri hasa, bali wasilisho tu la namna ambavyo nambari na Jecha zilivyokuwa busu la Bint Mfalme la kuweza kumgeuza chura kuwa Mwana Mfalme.Matokeo hayo yalinisaidia ‘kuyapiganisha’ na matokeo ya majimbo 31, ambayo binafsi nilikuwa nimeyakusanya kutoka kinywani mwa Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, na Makamu wake, Jaji Abdulhakim Ameir Issa, baina ya tarehe 25 na 26 Oktoba 2015 kabla ya Jecha hajatangaza “kuufuta” uchaguzi huo tarehe 28 Oktoba.
Hii ni kwa sababu mimi mwenyewe nilikuwepo kwenye ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwanani mjini Unguja, kushuhudia utangazwaji wa matokeo hayo.
Sitaki kuingia kwenye ta’awili wala uchambuzi wa chochote ule, isipokuwa hapa naweka tu majadweli ya kulinganisha, kwanza, zile kura ambazo Jecha na Issa walizitangaza kwenda kwa mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk. Ali Mohamed Shein, katika uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba na zile ambazo ZEC inadai zilikwenda tena kwa Dk. Shein siku ya tarehe 20 Machi kwa majimbo 31 (namba 1 hadi 31). Kisha kuanzia namba 32 hadi 36, ni majimbo matano pia ya kisiwani Unguja (Donge, Tumbatu, Amani, Kijitoupele na Shaurimoyo) ambayo licha ya kuwa yalikuwa hayajakuja kutangazwa hadharani, majumuisho yake yalishakamilika na kukubalika ndani ya chumba cha majumuisho, ikawa tunasubiri kutangaziwa tu. Na mwisho kuna jadweli la tafauti ya kura kisiwani Pemba.
Tafauti ya kura kwa kila jimbo imeandikwa kwa wino mwekundu na kuwekewa alama ya + kumaanisha kuwa ni ongezeko lililozidi kwenye kura ya 20 Machi.
Ongezeko la kura za Dk. Shein kisiwani Unguja
Na.JIMBOOKT. 2015MACHI 2016TAFAUTI
1.CHWAKA6,0678,294+2,227
2.UZINI9,94112,995+3,054
3.DIMANI4,8187,122+2,304
4.PANGAWE3,0095,168+2,159
5.MTONI5,3367,977+2,641
6.TUNGUU7,58910,589+3,000
7.CHUMBUNI4,8928,954+4,062
8.KIWENGWA2,9953,539+544
9.MAHONDA4,3525,665+1,313
10.NUNGWI3,5564,064+508
11.MPENDAE3,9746,642+2,668
12.MFENESINI4,1925,790+1,598
13.KIJINI2,3962,787+391
14.MAGOMENI5,4458,173+2,728
15.MTOPEPO3,6716,788+3,117
16.M/KWEREKWE4,0039,597+5,594
17.MWERA2,5543,449+895
18.BUBUBU4,3566,593+2,237
19.CHAANI4,1205,208+1,088
20.PAJE5,5857,099+1,514
21.WELEZO2,5284,033+1,505
22.BUMBWINI2,3513,490+1,139
23.JANG’OMBE6,2168,810+2,594
24.KIKWAJUNI5,9989,942+3,944
25.CHUKWANI3,5715,922+2,351
26.MKWAJUNI4,2854,351+66
27.MAKUNDUCHI8,1619,800+1,639
28.FUONI8891,386+497
29.K/SAMAKI4,4136,976+2,563
30.MALINDI2,3345,873+3,539
31.KWAHANI5,9609,360+3,400
32.DONGE5,2555,308+53
33.TUMBATU5,4246,081+657
34.AMANI4,1076,026+1,919
35.KIJITOUPELE4,3736,911+2,538
36SHAURIMOYO5,5939,006+3,413


Ongezeko la kura za Dk. Shein kisiwani Unguja
Hiyo ni kesi ya kisiwani Unguja, ambako kisiasa kunasemekana CCM ina ufuasi mkubwa zaidi. Hata hivyo, hata hadithi ya kisiwani Pemba, ambako kunaambiwa ni ngome ya Chama cha Wananchi (CUF), nayo si tafauti hata kidogo, panapohusika ongezeko la kura ambazo ZEC inasema alipata Dk. Shein tarehe 20 Machi.
Ingawa Jecha hakuwahi kuyatangaza matokeo ya majimbo ya Pemba kabla ya hatua yake ya tarehe 28 Oktoba 2015 ya ‘kuufuta’ uchaguzi wa Oktoba 25, siku ya tarehe 26 Oktoba, CUF ilikuwa imetuita waandishi wa habari saa 3:00 asubuhi kwenye ofisi zake za Mtendeni na kutupa matokeo ya majimbo yote 54 kwa nafasi ya urais.
Unapoyalinganisha matokeo hayo waliyotoa CUF na yale ya majimbo 31 yaliyotangazwa na ZEC kati ya tarehe 25 na 26 Oktoba, huwezi kukuta tafauti yoyote ya kimsingi. Hiyo ni kusema kuwa – ingawa matokeo ya majimbo mengine hayakuwahi kutangazwa na ZEC kabla ya Jecha ‘kuufuta’ uchaguzi, kwa kuwa hesabu ya CUF na ZEC ilikuwa sawa sawa kwenye hayo ya awali, basi kuna uwezekano wa kuwa sawa kwenye haya yaliyobakia.
Kwa msingi huo, matokeo yaliyopo hapa yanalinganisha kura alizoambiwa amepata Dk. Shein katika uchaguzi wa Oktoba 25 na zile ambazo ZEC inasema alizipata tarehe 20 Machi kisiwani Pemba.
Na.JIMBOOKT. 2015MACHI 2016TAFAUTI
1.CHAMBANI7253,129+2,404
2.MTAMBILE7983,093+2,295
3.KIWANI1,4993,892+2,393
4.MKOANI3,1106,407+3,297
5.CHAKECHAKE1,1134,551+3,438
6.CHONGA1,5153,598+2,083
7.OLE6173,818+3,201
8.WAWI1,2434,147+2,904
9.ZIWANI5712,890+2,319
10.GANDO7953,298+2,503
11.MTAMBWE3201,789+1,469
12.MGOGONI6373,395+2,758
13.KOJANI1,0033,994+2,991
14.WETE8633,737+2,874
15.KONDE6911,606+915
16.MICHEWENI1,4363,273+1,837
17.TUMBE3721,520+1,148
18.WINGWI3942,062+1,668

Hapa napo unaona ongezeko kubwa lililopo kama ilivyokuwa kwa Unguja. Majimbo yaliyotia fora kwa ongezeko ni Chake Chake (3,438), Mkoani (3,297) na Ole (3,201), huku ziada ndogo kabisa ikiwa jimbo la Konde, ambapo Dk. Shein ameongeza kura 915, ikifuatiwa na jimbo jirani la Tumbe, ambako kuna ziada ya kura 1,148.
Matokeo haya ‘yamepatikana’ hata baada ya ripoti za waandishi wa habari na mashahidi waliokuwepo siku ya tarehe 20 Machi kote visiwani Unguja na Pemba kuelezea idadi ndogo kabisa ya wapiga kura vituoni, kufuatia CUF na vyama vyengine tisa kutangaza kuususia uchaguzi huo.
Matokeo haya ‘yamepatikana’ pia hata baada ya picha za mnato na za vidio kusambaa mitandaoni zikionesha namna baadhi ya wale waliojitokeza kupiga kura walivyozifanya kura hizo ndani ya vituo – kuchorachora kwa nia ya kuziharibu.
Lakini kama nilivyotangulia kusema, huu si uchambuzi wala tafsiri ya chochote kilichotokea, bali ni wasilisho tu la namna busu la kimiujiza la Bint Mfalme lilivyofanikiwa kumgeuza chura akawa Mwana Mfalme.
Watakaokuja kukitafiti kipindi cha miezi mitano, kuanzia 25 Oktoba 2015 hadi 22 Machi 2016, bila ya shaka watakuja kutupa majibu zaidi kwa masuala tunayojiuliza. Hata hivyo, kitu kimoja nina hakika nacho – Zanzibar yangu itaendelea kuongoza kwenye kuanzisha mambo na wengine kufuata.
Ni Zanzibar, kwa mfano, ambao Ukristo uliingia kwa mara ya kwanza kabla ya kusambaa kwenye maeneo yote ya ndani ya Afrika Mashariki na Kati. Hiyo ilikuwa mwaka 1448.
Ni Zanzibar ambayo ilijenga Jumba la Maajabu (jengo la Baitul-Ajab) la pale Forodhani, ambalo lilikuwa ajabu ya kweli wakati huo kwenye eneo lote la Afrika ya Mashariki na Kati. Hiyo ilikuwa mwaka 1833, ambapo hapakuwahi kuwepo na jengo kubwa la namna ile, likiwa na umeme na lifti zaidi ya jengo hili.
Ni Zanzibar ambayo ilikuwa ya kwanza kuwa na treni yake yenyewe. Hiyo ilikuwa mwaka 1879.
Ni Zanzibar ambako magazeti yalianza kuandikwa na kusambazwa kwa mara ya kwanza ndani ya eneo zima la Afrika Mashariki na Kati, ambapo gazeti la Samachar lilichapishwa mwaka 1903.
Kwenye siasa pia, ni Zanzibar iliyokuwa ya mwanzo katika Afrika ya Mashariki kufanya uchaguzi kamili mwaka 1957, ambapo chama cha Afro-Shiraz (ASP) kilishinda viti vitano kati ya sita vilivyowaniwa.
Hiyo ndiyo Zanzibar yangu. Sio Zanzibar ya kwenye riwaya wanaoijuwa wengi hapa Ulaya.
Zanzibardaima.

No comments: