Wednesday, 19 July 2017
Kauli za Lodi Lofa inawasikitisha wengi
KAULI chafu za Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, kila mara anapofungua kinywa chake kuzungumza dhidi ya wale anaowahesabu kuwa wapinzani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinaudhi, lakini hazishangazi.
Kwa hivyo, haikushangaza aliporejelea kauli kama hizo hivi karibuni wakati akiwa Chato mbele ya mwanafunzi wake wa kauli kama hizo, Dk. John Magufuli.
Hakikuwa kitu kigeni pia kuwa aliwafurahisha waliokuwapo jukwaa kuu na wanachama wa kawaida wa CCM waliohudhuria shughuli ya kukabidhi nyumba 50 za watumishi wa umma katika sekta ya afya.
Hata hivyo, tukiacha ukweli kwamba miongoni mwa mambo mema aliyofanya Rais Mkapa ni kuondoka madarakani muda wake wa kikatiba ulipokwisha, tofauti na jirani zake wanaobadili katiba ili waendelee madarakani, ilitarajiwa kauli gani njema kwake?
Mkapa aliyeingia madarakani kwa mgongo wa Mwalimu Julius Nyerere kwa kudhani kwamba mwanafunzi wake huyo angeendeleza kile alichokiamini yeye, alianza awamu ya utawala wake kwa kuhubiri alichokiita “Ukweli na Uwazi.”
Wakati huo, alitaka nchi imwamini yeye ndiye “Bwana Msafi” aliyeaminiwa na Mwalimu Nyerere, kwamba angeweza kuwa mpigavita rushwa kwelikweli. Alinza fungate hiyo kwa kutaja mali alizokuwa nazo, akawashawishi mawaziri wake, kina Waziri Mkuu Frederick Sumaye, wafanye vivyo.
Hakuishia hapo. Akawataka wananchi wamuamini yeye ni mpambanaji kwelikweli dhidi ya ufisadi. Akaunda Tume ya kuchunguza mianya ya rushwa na kumteua Jaji Joseph Warioba kuiongoza. Lakini kutaka kujua alivyokuwa hakuwa akimaanisha akisemacho, angalia kilichotokea baada ya tume kukamilisha kazi yake.
Kwanza, baada ya kupelekewa majina ya “wala rushwa” katika serikali yake, aling’aka kwamba watu wana wivu wa kike na eti, “badala ya kuangalia maendeleo yao, wanaendekeza choyo cha kuona kila mwenye mali basi ameipata kwa rushwa.”
Akasema watu wasimpelekee majina tu, bali wampelekee ushahidi, hali anajua fika katika kutoa na kupokea rushwa, kila jitihada huchukuliwa kufuta ushahidi.
Pili, ripoti ya Tume ya Jaji Warioba iliishia kapuni. Ikachapwa, bila ya shaka, katika magazeti, lakini mambo yakaenda taratibu mno. Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKURU) aliyoiunda ikawa kama mbwa mkubwa anayetisha lakini kibogoyo asomeno ya kutosha kuwang’ata walarushwa.
Wengine tunaamini kuwa kihoro kilichomuingia Mwalimu Nyerere kwa kuangushwa na chaguo lake, kiliharakisha mauti yake Oktoba 14, 1999. Haikuwa kazi nyepesi, kwa mtu wa heshima kama yeye katika umri ule, kuzunguka nchi na kumnadi mtu wake, kisha mtu huyo akaja kumwangusha kwa kiwango kile.
Mwalimu Nyerere hakumuunga mkono tena Rais Mkapa tangu alipoanza kutekeleza madaraka yake kwa kusabilia mali za nchi kwa wawekezaji.
Kuna suala la ununuzi wa rada na ndege ya rais, ambayo baadaye uchunguzi wa polisi ya Uingereza uligundua kuwa ulitandwa na kashfa kubwa ya rushwa. Waziri wake wa Fedha, Basil Mramba, alitwambia ilikuwa heri wananchi wale nyasi lakini ndege ya rais inunuliwe.
Kuna mkasa kama ule wa kina Jenerali Twaha Ulimwengu ambaye, licha ya kuwa mpiga debe wake mkubwa katika siku za kampeni, alipoanza kumuona anakwenda mrama, naye akamsema kwa hilo, mara akatangazwa si raia.
Hatua hiyo ilichukuliwa huku uongozi ukisahau kuwa Ulimwengu aliwahi kuwa mkuu wa wilaya, mbunge wa taifa na Mtanzania aliyeongoza Umoja wa Vijana wa Afrika uliokuwa na makao makuu yake nchini Algeria.
Hata sakata la uraia wa mwandishi mwingine mkongwe wa habari, marehemu Ali Nabwa, lilianza katika siku za mwisho mwisho za utawala wa Mkapa na kwa hakika alilijua vyema, lakini akaondoka na kuliacha kama lilivyo.
Kuna mauaji ya Mwembechai ya mwaka 1997 ambayo pamoja na serikali yake kuwafanya ilivyowafanyia waumini wa Kiislamu ndani ya msikiti, bado alikataa kuunda tume ya uchunguzi. Hata alipotokea msomi Dk. Hamza Njozi, kuandika kile hasa kilichotokea katika kitabu chake cha The Mwembechai Killings (Mauaji ya Mwembechai), serikali yake ilikipiga marufuku kitabu hicho.Kuna kasheshe la Bulyanhulu lililotandwa na malalamiko ya mauaji, watu kufukuzwa makaazi yao na wengine kufukiwa migodini. Si tu kwamba serikali yake ililikanusha, bali pia ilizuia vyanzo vyovyote vya habari kutoa taarifa hizo popote na kukamata wanaharakati waliokuwa wakichunguza madhila hayo.
Likaja suala kubwa la mauaji ya Januari 2001, Zanzibar, ambalo mwenyewe aliwahi kusema eti liliwahi kumkosesha usingizi na karibuni na mwisho wa utawala wake, alipokuwa ziarani Marekani, akasema lilimsononesha hadi siku anamalizia muhula wake madarakani.
Lakini wakati anazungumza na Tim Sebastian wa BBC wakati huo, alimwaga kiburi chake kuwa hatua ya serikali yake kuua watu ilikuwa sahihi.
Alikuwa anaamini zaidi nguvu ya vyombo vya dola katika utawala. Sio nguvu ya wananchi. Mdomoni, alikuwa akisema watu ndio wenye nguvu, katika vitendo alikuwa akionesha yeye na vyombo vyake vya dola ndio mwanzo na mwisho.
Ndiyo maana niliwahi kupendekeza utawala wake uitwe Mkapakrasia. Ndio uliozaa mauaji yale ambayo yalithibitishwa na Tume ya Hashim Mbita aliyoiunda. Ndio uliowafanya dada zetu wabakwe, na ndugu zetu waikimbie nchi yao. Mkapa hakuwa aina ya rais anayekubali changamoto katika utawala wake.Alipenda na kuhusudu mataifa ya magharibi na waandishi wa huko. Akiwa kule, akitoa maneno ya kistaarabu na kidemokrasia. Lakini alipogeukia wananchi wake, akitoa kauli za ujuba na kebehi.
Sote tunakumbuka kauli zake za kuapa kutumia nguvu za dola kuzima nguvu ya umma iwapo baada ya uchaguzi, watu wangeandamana kupinga matokeo yaliyotangazwa na tume zake za uchaguzi.
Mifano ya kuendesha ovyo nchi haihesabiki. Na yote inamharamishia haki ya kuita wengine “wapumbavu,” maana mwenye akili hasa asingeitendea Tanzania alichokitenda, na nafsi yake ikabakia salama.
Leo Tanzania inachukua jitihada za kurekebisha majanga mengi ya kiuchumi, aliyoyaumba. Ni bahati mbaya kwamba wakati Rais Magufuli anasafisha uchafu ulioasisiwa na Mkapa kwenye uchumi, anautukuza ulimi wa mwanasiasa huyo anayeamini ndiye aliyemjenga kisiasa na kumbeba kumfikisha kileleni mwa ulwa.
Pamoja na ukweli kwamba Watanzania wengi wanaweza kuwa wajinga kielimu, wana akili ya kutambua haki na batili. Wao si wapumbavu.
TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la MwanaHalisi la tarehe 17 Julai 2017
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment