Friday 28 July 2017

MAAMUZI YA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA LA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF - CHAMA CHA WANANCHI) KUHUSIANA NA HUJUMA DHIDI YA CUF

Image may contain: 1 person
 YA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA LA
THE CIVIC UNITMAAZIMIOED FRONT (CUF - CHAMA CHA WANANCHI) KUHUSIANA NA HUJUMA ZA DLA DHIDI YA OCHAMA
UTANGULIZI:
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi) leo hii Ijumaa, tarehe 28 Julai, 2017 limefanya kikao cha dharura kilichoitishwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa kwa kufuata masharti ya Katiba ya Chama ya mwaka 1992 (Toleo la 2014), kifungu cha 80 (1). Wajumbe 45 kati ya wajumbe 52 halali wa Baraza Kuu wamehudhuria ambao ni sawa na asilimia 86 ya wajumbe wote.
Katika kikao hiki, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lilipokea, kujadili na kufanya maamuzi kuhusu ajenda moja tu iliyowasilishwa kwake na Kamati ya Utendaji ya Taifa ambayo ilikuwa ni:
• Taarifa kuhusu kile kinachoitwa kuwavua uanachama Wabunge wanane (8) na Madiwani wawili (2) wa Viti Maalum kupitia CUF kilichotangazwa kufanywa na Ibrahim Lipumba na kikundi chake ikiwa ni mwendelezo wa hujuma za Dola dhidi ya Chama cha CUF.
Baada ya mjadala wa kina, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linapenda kutoa maazimio yafuatayo kuhusiana na tukio hilo na mwendelezo wa vitendo na matukio mengi ya hujuma yanayofanywa na Dola dhidi ya CUF:-
1. KUHUSU UHALALI WA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA:
Kutokana na mkanganyiko unaosababishwa na upotoshaji wa makusudi unaofanywa na Ibrahim Lipumba na kikundi chake wa kuitisha watu wa kuokota barabarani na kuwakusanya Buguruni huku akiwaita kuwa ndiyo Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF, tumeona kuna haja ya kuweka kumbukumbu sahihi ili kuepusha upotoshaji huo usiendelee.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama huwa linaundwa kila baada ya miaka mitano kupitia Uchaguzi Mkuu wa Chama ndani ya Chama na hupata wajumbe wake kupitia uchaguzi unaofanywa na Mkutano Mkuu wa Taifa (wajumbe 25 kutoka Tanzania Bara na wajumbe 20 kutoka Zanzibar), wajumbe 14 wanaoteuliwa na Mwenyekiti kwa kushauriana na Makamu Mwenyekiti na kisha kuthibitishwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, wajumbe wanaoingia kwa nafasi zao wakiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chama, Wenyeviti na Makatibu wa Jumuiya za Chama na Viongozi wa Kambi za Wabunge na Wawakilishi wa Chama. Viongozi Wakuu wa kitaifa wa Chama pia ni wajumbe.
Wafuatao ndiyo Wajumbe halali waliochaguliwa na Mkutano Mkuu wa Taifa uliomalizika Juni 27, 2014 hapo Ubungo Plaza, Dar es Salaam kuwa wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT) watakaokaa madarakani kwa kipindi cha miaka mitano (2014 – 2019) hadi watakapochaguliwa wengine na Mkutano Mkuu wa Taifa kwa mujibu wa Katiba ya CUF ya mwaka 1992 (Toleo la 2014):-
VIONGOZI WAKUU:
1. Mwenyekiti (alijiuzulu tarehe 5 Agosti, 2015 na kujiuzulu kwake kuthibitishwa na Mkutano Mkuu wa Taifa wa dharura tarehe 21 Agosti, 2016).
2. Makamu Mwenyekiti (alitekeleza agizo la BKUT kuhama Chama kuwa mgombea mwenza wa Urais kupitia UKAWA).
3. Katibu Mkuu – Maalim Seif Sharif Hamad (ambaye bado yupo).
KUTOKA KUNDI LA WAJUMBE 25 WA TANZANIA BARA AMBAO BADO WAPO:
1. Mhe. Nuru Awadh Bafadhil
2. Mhe. Moza Abeid
3. Mhe. Athumani Henku
4. Mhe. Fatuma Omar Kalembo
5. Mhe. Sophia M. Khaify
6. Mhe. Katani A. Katani
7. Mhe. Salum Kh. Barwani
8. Mhe. Bonifasia Mapunda
9. Mhe. Fatuma A. Chitepete
10. Mhe. Juma S. Nkumbi
11. Mhe. Nassir A. China
12. Mhe. Kulthum Mchuchuli
13. Mhe. Karume J. Mgunda
14. Mhe. Twaha I. Taslima
15. Mhe. Julius N. Samamba
KUTOKA KUNDI HILI WALIOFARIKI:
16. Mhe. Ashura Mustapha
KUTOKA KUNDI HILI WALIOHAMA CHAMA:
17. Mhe. Lwebora P. Ndarpoi
18. Mhe. Mohamed A. Khalifa
19. Mhe. Mkiwa A. Kimwanga
KUTOKA KUNDI HILI WALIOFUKUZWA UANACHAMA:
20. Mhe. Chief L. Yemba
KUTOKA KUNDI HILI WALIOSIMAMISHWA UANACHAMA:
21. Mhe. Magdalena H. Sakaya
22. Mhe. Kapasha H. Kapasha
23. Mhe. Thomas D.C. Malima
24. Mhe. Abdul J. Kambaya
25. Mhe. Omar M. Masoud
KUTOKA KUNDI LA WAJUMBE 20 WA ZANZIBAR AMBAO BADO WAPO:
1. Mhe. Hamad Masoud Hamad
2. Mhe. Abubakar Khamis Bakari
3. Mhe. Said Ali Mbarouk
4. Mhe. Khalifa Mohamed Issa
5. Mhe. Omar Ali Shehe
6. Mhe. Riziki Omar Juma
7. Mhe. Masoud Abdalla Salim
8. Mhe. Hija Hassan Hija
9. Mhe. Najma Khalfan Juma
10. Mhe. Salim Bimani
11. Mhe. Nassor Ahmed Mazrui
12. Zahra Ali Hamad
13. Fatma Abdulhabib Ferej
14. Mhe. Shaaban Iddi Ame
15. Mhe. Pavu Juma Abdallah
16. Mhe. Abdilahi Jihad Hassan
17. Mhe. Hassan Jani Masoud
18. Mhe. Mohamed Kombo Ali
19. Mhe. Hemed Said Nassor
KUTOKA KUNDI HILI ALIYEFUKUZWA UANACHAMA NA TAWI LAKE NA KUTHIBITISHWA NA BKUT:
20. Mhe. Rukia Kassim Ahmed
WAJUMBE WALIOTEULIWA NA MWENYEKITI KWA KUSHAURIANA NA MAKAMU MWENYEKITI NA KISHA KUTHIBITISHWA NA BKUT:
1. Mhe. Zainab A. Msafiri
2. Mhe. Hashim B. Mzirai
3. Mhe. Shaweji M. Mketo
4. Mhe. Abdalla Mtolea
5. Mhe. Joran Bashange
6. Mhe. Elina Kimei
7. Mhe. Mustapha Wandwi
8. Mhe. Ahmed Marshed Khamis
9. Mhe. Ismail Jussa Ladhu
10. Mhe. Nunuu S. Rashid
11. Mhe. Shambuli A. Makame
12. Mhe. Abdalla Bakari Hassan
13. Mhe. Yussuf Salim Hussein
KUTOKA KUNDI HILI WALIOSIMAMISHWA UANACHAMA:
14. Mhe. Shaaban Kaswaka
VIONGOZI WAKUU WA JUMUIYA ZA CHAMA:
1. Mhe. Hamidu Bobali – Mwenyekiti Jumuiya ya Vijana
2. Mhe. Mahmoud A. Mahinda – Katibu Mtendaji Jumuiya ya Vijana
N.B.
- Viongozi wa Jumuiya ya Wanawake ambao ni Mhe. Fatma Abdulhabib Ferej (Mwenyekiti) na Mhe. Fatma Omar Kalembo (Katibu) walikuwa wameshaingia kwa nafasi za wajumbe wa kuchaguliwa.
- Jumuiya ya Wazee bado haijafanya uchaguzi na viongozi wake wa Sekretarieti ya Wazee hualikwa tu kuhudhuria vikao vya BKUT.
KIONGOZI WA WABUNGE WA CUF BUNGENI:
1. Mhe. Riziki Shahari Mngwali
MWENYEKITI WA BODI YA WADHAMINI YA CHAMA:
1. Mhe. Abdalla S. Khatau
JUMLA YA WAJUMBE HALALI WALIOPO SASA:
Kutokana na mchanganuo huu, idadi ya sasa ya Wajumbe halali tuliopo tunaounda Baraza Kuu la Uongozi halali la Chama ni 52 ambapo wajumbe 25 wanatoka Tanzania Bara na wajumbe 27 wanatoka Zanzibar.
Mkutano Mkuu wa Taifa haujalivunja wala haujachagua Baraza Kuu jengine. Kama lipo jengine la pili hilo litakuwa ni Baraza Kuu feki, na chombo chochote kitakachoundwa na Baraza Kuu lisilokuwa hili lililotokana na Mkutano Mkuu wa Taifa katika kipindi hiki cha miaka mitano (2014 – 2019), chombo hicho nacho kitakuwa ni feki kama ilivyo kwa Kamati feki inayojiita ya Nidhamu na Maadili.
Kwa msingi huo huo, maamuzi halali ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa ni yale yanayofanywa na Baraza Kuu linaloundwa na wajumbe walioorodheshwa hapo juu. Wajumbe wengine feki watakaojiita Baraza Kuu wakifanya maamuzi kuhusu jambo lolote lile, maamuzi yao hayo yatakuwa feki pia.
2. KUHUSU KINACHOITWA KUFUKUZWA UANACHAMA WABUNGE WANANE (8) NA MADIWANI (2) WA CUF:
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa halijakutana popote siku ya Jumapili, tarehe 23 Julai, 2017 kufanya maamuzi yoyote ya kuwafukuza uanachama Wabunge wanane (8) na Madiwani wawili (2) wa CUF kama ilivyodaiwa na mtu anayeitwa Ibrahim Lipumba na kikundi chake. Kwa msingi huo, Baraza Kuu linawataka Watanzania kufahamu kwamba:-
(a) Linaendelea kuwatambua Wabunge na Madiwani hao kuwa wanachama halali wa CUF tena ni wanachama wa kupigiwa mfano wenye nidhamu na maadili ya hali ya juu. Baraza Kuu linawapongeza kwa mapenzi yao kwa Chama chao na msimamo wao thabiti usioyumba katika kukitetea Chama waliouonesha pale walipokataa kuitikia wito wa Kamati feki ya Maadili na Nidhamu.
(b) Pamoja na matangazo ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutangaza kwamba Wabunge hao wanane wamepoteza sifa za Ubunge kwa hicho kinachoitwa “kufukuzwa uanachama” na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza majina ya wateule wengine wa kujaza nafasi hizo, Baraza Kuu ambalo ndilo lililowateua hapo awali bado linaendelea kuwatambua wafuatao kuwa Wabunge wake halali:
1. Mhe. Severina Silvanus Mwijage, (MB);
2. Mhe. Saumu Heri Sakala, (MB);
3. Mhe. Salma Mohamed Mwassa, (MB);
4. Mhe. Riziki Shahari Mngwali, (MB);
5. Mhe. Raisa Abdallah Mussa, (MB);
6. Mhe. Miza Bakari Haji, (MB);
7. Mhe. Khadija Salum Ally Al-Qassmy, (MB); na
8. Mhe. Halima Ali Mohamed, (MB).
(c) Baraza Kuu pia linaendelea kuwatambua Madiwani wa Viti Maalum, Mhe. Leila Hussein Madibi (Ubungo) na Mhe. Elisabeth Magwaja (Temeke) kuwa madiwani halali wa CUF katika Wilaya zao.
(d) Baraza Kuu limeridhika kwamba hicho kinachoitwa “kuwafukuza uanachama” na kuwatangaza kuwa wamepoteza sifa za Ubunge na papo hapo kutangaza majina mengine eti kujaza nafasi zao, ni mpango kabambe uliosukwa na Dola kwa kushirikiana na kibaraka Ibrahim Lipumba na kikundi chake na ndiyo maana Watanzania wameshuhudia KASI YA AJABU (supersonic speed) katika utekelezaji wake, kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa katika utekelezaji wa maamuzi kama hayo huko nyuma. Bunge hili hili liliendelea kuwatambua Wabunge kadhaa katika vipindi tofauti miaka iliopita ambao walishafukuzwa uanachama tena na vikao halali vya vyama husika.
(e) Baraza Kuu limeshangazwa na hatua ya Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai kujifedhehesha na kujiaibisha kwa kusema uongo kwa Watanzania kwamba eti alijiridhisha kuwa Wabunge wanane wa Chama Cha Wananchi (CUF) ‘wamefukuzwa Uanachama kulingana na taratibu za Chama hicho na hivyo wamekosa sifa za kuendelea na Ubunge”.
(f) Baraza Kuu limejiridhisha kwamba Katibu Mkuu wa Chama, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye kwa mujibu wa Katiba ya CUF ndiye Mtendaji Mkuu wa shughuli za Chama na pia kwa nafasi hiyo ndiye Katibu wa vikao vya Mkutano Mkuu wa Taifa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama alimuandikia Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai barua rasmi, Jumanne, tarehe 25 Julai, 2017 akimueleza kwamba hilo lililoitwa Baraza Kuu la Uongozi la CUF halikuundwa na wajumbe halali wa Baraza Kuu. Hiyo ni mbali na ukweli kwamba hakuna Mtanzania asiyejua kuwa uhalali wa kibaraka Lipumba na genge lake unapingwa na Chama cha CUF kwa kesi ambazo ziko Mahakamani. Kwa hakika Spika Ndugai amepoteza sifa na haiba ya kuongozo Bunge ambalo ni mhimili mmojawapo wa Dola na ambao ulipaswa kuwa alama ya uadilifu katika nchi na anapaswa kujiuzulu kwa kuidhalilisha na kuichafua heshima na haiba ya nafasi ya Spika.
(g) Baraza Kuu linapongeza na kuunga mkono hatua waliyoichukua Wabunge hao ya kufungua kesi Mahakama Kuu kupinga uhalali wa hatua iliyotangazwa ya kwamba ati wamefukuzwa uanachama na ambapo katika kesi hiyo wanaiomba Mahakama Kuu itamke kwamba wao bado ni wanachama halali wa CUF na hivyo bado ni Wabunge halali wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CUF katika nafasi za Viti Maalum na kutupilia mbali tangazo la Spika la kuwatangaza kuwa si Wabunge na lile la Tume ya Taifa ya Uchaguzi la kutangaza majina mengine ya kujaza nafasi hizo.
(h) Baraza Kuu linamuagiza Katibu Mkuu wa Chama, Maalim Seif Sharif Hamad, kuwaandikia Rais wa Bunge la Afrika (PAP), na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kuhusu fedheha na aibu hii iliyofanywa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuonesha jinsi demokrasia isivyoheshimiwa Tanzania.
(i) Baraza Kuu linawataka Watanzania hususan wanawake kuona ni jinsi gani CCM kupitia taasisi za kidola isivyowajali, isivyowaheshimu na isivyowathamini wanawake ambao ni zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania wote kwa kuwatendea kitendo cha kuwadhalilisha kwa kuwaondoshea uwakilishi wao halali kupitia Wabunge wazoefu waliokuwa watetezi madhubuti wa haki za wanawake katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.
(j) Baraza Kuu linawataka Wabunge na Madiwani wote wa CUF nchi nzima kukipuuza kikundi cha wahuni kinachojiita “Baraza Kuu” na kwamba Baraza Kuu halali la Chama linaendelea kuwatambua wote kama Wabunge na Madiwani halali wa CUF.
3. KUHUSU KUJIDHALILISHA KWA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI NA KUKIUKA KANUNI ZAO WENYEWE KATIKA UTEUZI WA WABUNGE WA VITI MAALUM:
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limesikitishwa na hatua ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kujidhalilisha na kujishushia hadhi kwa kushiriki katika hujuma hizi za Dola dhidi ya CUF. Mbali na yale yaliyoyaelezwa hapo juu, hata kama ingekuwa kufukuzwa Wabunge hao wa CUF kulikuwa na halali na kumefanywa na chombo halali cha Chama, basi Kanuni walizojiwekea wenyewe Tume katika uteuzi wa watu wa kujaza nafasi hizo huo unafuata mpangilio wa majina kama ulivyokuwa umewasilishwa na Chama husika wakati wa uteuzi wa wagombea wa ubunge wa viti maalum wakati wa uchaguzi mkuu uliopita. CUF ilipeleka orodha yake ambayo haihusishi majina yaliyotangazwa. Hivyo ndiyo kusema hata kama hicho kinachoitwa kufukuzwa uanachama Wabunge hao kingekuwa halali (jambo ambalo si halali kama ilivyokwisha elezwa hapo juu), basi kwa Kanuni za Tume yenyewe, watu wa kujaza nafasi hizo wasingekuwa hao waliotangazwa. Kwa maelezo haya, Baraza Kuu linaweka bayana yafuatayo:-
(a) Kitendo kilichofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kimezidi kuidhalilisha na kuishushia hadhi Tume hiyo na kwamba kwa kushiriki kwake katika hujuma hizi chafu ni ushahidi mwengine kwamba Tanzania hatuna Tume huru ya Uchaguzi; bali Tume iliopo inafuata maelekezo ya Dola tu kuhujumu vyama vya upinzani.
(b) Baraza Kuu linaitaka (linai-challenge) Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutoa hadharani barua ya Katibu Mkuu wa CUF iliyoandikwa kwao mwaka 2015 ikiwa na majina ya wanachama wake walioteuliwa kuwa wagombea wa viti maalum vya wanawake na kuonesha iwapo hao iliowatangaza walikuwa katika mpangilio wa majina yaliyoteuliwa na Chama. Iwapo haitofanya hivyo, iwaeleze Watanzania na jumuiya ya kimataifa kwa nini waendelee kuiamini Tume hiyo.
(c) Baraza Kuu linatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na hususan Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Shirika lake la Mpango wa Maendeleo (UNDP) ambalo limekuwa likifanya kazi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutafakari upya iwapo Tume hiyo bado ina hadhi na heshima ya kuendelea kuungwa mkono na Shirika hilo, Umoja wa Mataifa, na washirika wa maendeleo kwa ujumla wakati imejianika waziwazi kuwa inafanya kazi ya kuhujumu demokrasia Tanzania badala ya kuimarisha.
4. KUHUSU HUJUMA ZA DOLA DHIDI YA CUF, VYAMA VYENGINE VYA SIASA NA TAASISI NYENGINE ZA KIDEMOKRASIA NA HAKI ZA BINADAMU HAPA NCHINI:
Baada ya kujadili kwa kina mwendelezo wa mipango ya hujuma dhidi ya CUF iliyoanza mwaka jana na ambayo inaendelezwa kwa nguvu na kwa kasi, na kwa kutafakari matukio mengine ya hujuma dhidi ya vyama vyengine vya siasa na taasisi nyengine zinazosimamia demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria hapa nchini, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limeazimia yafuatayo:
(a) Limeridhika kwamba Wakuu wa Dola nchini Tanzania wana mpango mkubwa wa kuua demokrasia hapa nchini kwa kuviangamiza vyama makini vya siasa vilivyoonekana tishio kwa chama kinachotawala cha CCM katika uchaguzi mkuu uliopita na pia kupambana na taasisi zinazoheshimika na zinazojiamini katika kusimamia masuala ya demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria.
(b) Baraza Kuu liamini kuwepo mpango huo baada ya sasa kuonekana wazi kwamba mipango ya hujuma dhidi ya CUF hadi sasa imeshahusisha Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Polisi, baadhi ya Wakuu wa Wilaya, Ofisi ya Spika wa Bunge, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na bila shaka yoyote Idara ya Usalama wa Taifa (TISS). Vipi Idara ya Usalama wa Taifa iwe haioni hujuma hizi za wazi na athari zake kwa usalama wa Taifa?
(c) Baraza Kuu linaona kuwa hujuma dhidi ya CUF zinatokana na ushindi mkubwa wa chama hiki katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 25, 2015 ambapo kilimbwaga mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM kwa tofauti ya kura 25,836 pale mgombea wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alipopata jumla ya kura 207,847 dhidi ya mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, aliyeambulia kura 182,011. CUF pia ilifanikiwa kuongeza majimbo yake kisiwani Unguja kutoka manne (4) hadi tisa (9) mbali ya kuendelea kubakisha majimbo yake yote 18 kisiwani Pemba. Mafanikio haya na ushindi huu mkubwa umekuwa mwiba kwa watawala na ndiyo hujuma zote hizi zinatelekezwa ili kuisambaratisha CUF, jambo ambalo Baraza Kuu linawahakikishia Watanzania kuwa halitofanikiwa.
(d) Kwa upande mwengine, mafanikio ya UKAWA katika Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na uthubutu uliooneshwa na Watanzania wanaotaka mabadiliko ndiyo yanayopelekea pia kuandamwa kwa:
- CHADEMA;
- NCCR;
- Wabunge wa Upinzani wanaoongoza katika ukosoaji wa Watawala;
- Wanaharakati wanaotetea uhuru wa kujieleza kama Jamii Forums;
- Wasanii ambao wametumia vipaji vyao kuwakosoa Watawala;
- Watumiaji wa mitandao ya kijamii hasa vijana;
- Vyombo vya habari yakiwemo magazeti, vituo vya radio na TV;
- Taasisi za fani na stadi zinazohoji kama ilivyotokea kwa TLS; na
- Wana-CCM wenye mawazo yanayokinzana na yale ya Watawala.
(e) Baraza Kuu linasikitishwa na mtindo unaoonekana kutaka kujengwa wa kutojali Katiba na Sheria katika kuongoza na kuendesha nchi na badala yake kutegemea matamko ya Rais. Mengi ya matamko hayo na matendo yanayofuatana nayo hayaendani na Katiba na Sheria za nchi ambazo aliapa kuzilinda wakati anashika madaraka ya nchi.
(f) Baraza Kuu linaona mwenendo huu unaoelekea kukandamiza demokrasia na hatimaye kuiua kabisa hauleti taswira njema kwa mustakbali wa Taifa letu. Taifa ambalo halitoi nafasi kwa watu wake kutoa mawazo yao hadharani huwa linakaribisha manung’uniko ya chini kwa chini ambayo ni hatari kwani yanapelekea watawala kutojua hisia halisi za wananchi. Baraza Kuu linaitaka Serikali na vyombo na taasisi zake kujitathmini upya juu ya wapi wanalipeleka Taifa na nini zinaweza kuwa athari zake.
(g) Baraza Kuu linawatanabahisha Watawala kwamba kwa kuhujumu kwao demokrasia na taasisi zinazosimamia demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria watambue kwamba wanatengeneza mazingira ya hali hatarishi nchini. Mfumo wa vyama vingi vya siasa umeshakuwa ni sehemu ya utamaduni wa kisiasa wa Watanzania na kuuhujumu ni kuvuruga usalama wa nchi yetu na watu wake ambao wameshajenga imani kwamba wana uwezo wa kuchagua na kuwawajibisha viongozi wao kupitia mfumo huo na vyama vilivyo huru.
(h) Baraza Kuu linatoa wito kwa viongozi wa kidini na kijamii na watu wanaoheshimika hapa nchini kuingilia kati hali hii na kuishauri Serikali na vyombo na taasisi zake juu ya haja ya kuzingatia Katiba na Sheria za nchi, misingi ya demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria.
5. KUHUSU WANACHAMA WALIOSIMAMISHWA AMBAO WAMEENDELEA NA HUJUMA ZAO DHIDI YA CHAMA:
(a) Itakumbukwa kwamba Baraza Kuu la Uongozi la Taifa liliwasimamisha uanachama wanachama kadhaa kutokana na vitendo vyao vya kukihujumu Chama. Kwa kuwa Baraza Kuu limejiridhisha kwamba wanachama hao waliosimamishwa hawajajirudi au kujirekebisha na badala yake wanaendelea na hujuma zao dhidi ya Chama, hivyo basi limeamua kuchukua hatua ya kuwafukuza uanachama. Walifukuzwa kwa mujibu wa uwezo uliopewa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa chini ya vifungu 83(5)(c) na 83(6) vya Katiba ya Chama ya mwaka 1992, Toleo la 2014 kupitia kura za siri ambapo wajumbe 43 walipiga kura za NDIYO kuridhia kufukuzwa na wajumbe wawili hawakupiga kura. Waliofukuzwa ni hawa wafuatao:
(i) Magdalena H. Sakaya;
(ii) Maftaha Nachuma;
(iii) Kapasha H. Kapasha;
(iv) Thomas D.C. Malima;
(v) Abdul J. Kambaya;
(vi) Omar M. Masoud;
(vii) Shaaban Kaswaka.
(b) Mbali na hao waliokuwa wamesimamishwa awali, itakumbukwa kwamba kikao cha Baraza Kuu kilichofanyika tarehe 19 Machi, 2017 kilikwisha thibitisha hatua ya matawi husika kuwafukuza uanachama wafuatao pia kwa kushiriki kukihujumu Chama:
(i) Rukia Kassim Ahmed;
(ii) Mohamed Habib Mnyaa;
(iii) Mussa Haji Kombo;
(iv) Khalifa Suleiman Khalifa;
(v) Haroub Mohamed Shamis;
(vi) Thney Juma Mohamed;
(vii) Nassor Seif Amour.
(c) Miongoni mwa ushahidi wa vitendo vya hujuma vilivyofanywa na Magdalena Sakaya ni kitendo chake utovu wa nidhamu wa hali ya juu kwa kutenda kazi za Katibu Mkuu wa Chama wakati Katibu Mkuu mwenyewe yupo; na pia kushirikiana na Ibrahim Lipumba ambaye si mwanachama tena wa CUF baada ya kufukuzwa na Baraza Kuu, kujivika wadhifa usiokuwepo kwenye Katiba ya Chama wa kujiita Kaimu Katibu Mkuu wakati Katibu Mkuu yupo na anafanya shughuli zake ipasavyo. Amefanya yote hayo kwa lengo la kukivuruga na kukidhoofisha Chama.
(d) Ushahidi mwengine kwa Magdalena Sakaya na Maftaha Nachuma ambao ulizingatiwa na Baraza Kuu katika kuchukua hatua hizi ni ukweli uliothibitishwa hadharani na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Dk. John Pombe Magufuli, alipokuwa ziarani Kaliua hivi karibuni ambapo aliwathibitishia Watanzania kwamba Magdalena Sakaya ni mwana-CUF lakini anafanya kazi ya CCM na kwamba damu na roho yake ni vya CCM. Pia mapema mwaka huu akiwa ziarani Mtwara, aliwathibitishia Watanzania kwamba Maftaha Nachuma atahamia CCM. Kauli hizi zimedhihirisha kwamba watu hawa ni mapandikizi ya CCM ndani ya CUF wanaofanya kazi ya CCM. Kwa msingi huo, Baraza Kuu limeona ni bora kuwafukuza uanachama wa CUF ili waweze kupata uhuru mpana zaidi wa kuendelea kufanya kazi ya CCM.
6. WITO KWA JUMUIYA YA KIMATAIFA:
Kwa kuzingatia hali ya mambo inavyokwenda nchini Tanzania na hasa vitendo tulivyovitaja vya ukiukwaji wa Katiba na Sheria za nchi, ukandamizaji wa demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linaunga mkono wito uliotolewa na Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mhe. Tundu Lissu kwa Jumuiya ya Kimataifa kuibana Tanzania kwa kuiwekea vikwazo vya kiuchumi na kuitenga kisiasa na kidiplomasia hadi hapo Watawala watakapoamua kuheshimu Katiba, Sheria, misingi ya demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria.
7. WITO KWA WANACHAMA NA WATANZANIA:
(a) Baraza Kuu limetiwa moyo na ukweli unaozidi kujitokeza kila uchao kwamba kadiri matokeo haya ya hujuma dhidi ya demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria yanavyoendelezwa, ndivyo Watanzania nao wanavyozidi kuamka na kuelewa thamani ya tunu hizo na haja ya kuzilinda.
(b) Baraza Kuu linaitaka CCM ijifunze kutoka katika historia na uzoefu wa nchi nyengine kwamba matumizi ya nguvu na ukandamizaji wa haki haviwezi vikaifanya ipendeze kwa umma wa Watanzania bali vinaifedhehesha na kuwaonesha Watanzania kwamba ina woga na haijiamini katika ushindani ulio huru na ulio sawa.
(c) Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linatoa wito kwa wanachama wa CUF na Watanzania kwa ujumla kuungana kuikabili hatari iliopo na kwa njia za amani kabisa na zilizomo ndani ya mipaka ya sheria kutetea demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria kwani bila ya hayo hakutakuwa na maendeleo yatakayopatikana.
(d) Baraza Kuu linawataka Watanzania kutambua kwamba hujuma hizi hazilengi CUF tu bali zinalenga kuua demokrasia. Watawala wakifanikiwa kuisambaratisha CUF watahamia kwa vyama vyengine makini vya siasa, na hata taasisi nyengine makini na watu wanaotetea misingi ya demokrasia na haki. Tukiwaachia Watanzania kuhujumu demokrasia na taasisi za kidemokrasia, hakuna Mtanzania atakayesalimika.
(e) Baraza Kuu linawapongeza Watanzania pamoja kwa kuwa imara hadi sasa katika kutetea Katiba, Sheria, misingi ya demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria.
MWISHO:
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linaungana na wito alioutoa Katibu Mkuu wa Chama, Maalim Seif Sharif Hamad, wa kuwaomba na kuwasihi wanachama na wapenzi wote wa THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi) waendelee kuwa watulivu na kufuata maelekezo wanayopewa na Chama kupitia viongozi halali na vikao halali vya Chama. CUF kimepita katika dhoruba na misukosuko mingi katika historia yake tokea kilipoasisiwa mwaka 1992. Tulishinda dhoruba na misukosuko hiyo na tutaushinda huu uliopo na hatimaye kuibuka tukiwa IMARA ZAIDI.
Baraza Kuu kwa upande wake litaendelea kutoa miongozo mbali mbali mbali inayolenga kukilinda na kukinusuru Chama na pia kukiimarisha zaidi ili kiendelee kutekeleza wajibu wake katika uendeshaji wa siasa za kistaarabu, za ZANZIBAR, 28 JULAI, 2017
amani na zinazofuata Katiba na Sheria hapa nchini.
HAKI SAWA KWA WOTE
Maazimio haya yameidhinishwa na kutolewa na:
BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA

No comments: