UAMUZI WA WAZIRI KIGWANGALA UNAHITAJI MAJIBU YA ZIADA.
Na Awadh Ali Said,
Nimeusoma Waraka uliotolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania Bara, Dkt Hamisi Kigwangwalla, MB, uliolenga kutoa ufafanuzi juu ya hatua yake ya kuteua ile aliyoiita Kamati ya Kitaalam ya kuandaa Utambulisho Mpya wa Tanzania kwenye masoko ya Kimataifa ya Utalii.
Ikumbukwe kuwa Uteuzi wa Kamati hii hapo mwanzoni ulishirikisha wajumbe kutoka upande wa Tanzania Bara tu, jambo lililopelekea Wazanzibari kulalamika sana (katika mitandao ya kijamii, na hata baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi) juu ya hatua hiyo , na baada ya malalamiko hayo Mh Waziri haraka akaongeza Wajumbe watano wakitokea Zanzibar na hapo ukafuatia Waraka huo wa Ufafanuzi.
Kama ielewekavyo Utalii haumo katika ile orodha endelevu ya Mambo ya Muungano. Hivyo hoja kuu inayotaka majibu kwa hapa sio kuwa Kamati imeundwa bila kuingiza Wazanzibari, bali Jee pande mbili hizi za Muungano kwa maana ya Zanzibar na Tanzania Bara ziliwahi kukaa pamoja na KUKUBALIANA kuwa zifanye utambulisho wa utalii KWA PAMOJA katika masoko ya nje? Huu ndio uwamuzi wa msingi. Ndio uwamuzi wa kisera na wa kimwelekeo. Kama pande mbili hizi zilikaa na kukubaliana basi hilo ndio la kuelezwa na kujadiliwa. Tuarifiwe kuwa pande mbili hizi zilikubaliana hilo na kuwa baada ya Makubaliano hayo Waziri wa Utalii wa Tanzania Bara alipewa mamlaka na madaraka ya kuunda Tume. Vinginevyo ni sawa na kusema kuwa Mh. Waziri alijichukulia mamlaka asiyo kuwa nayo. Na ndio kusema kuwa maamuzi yake hayo yako nje ya mamlaka yake (ultra vires) na hivyo ni batili (null and void) Kama hili la Makubaliano halikufanyika, maamuzi yake ya kujiamulia kufanya Utambulisho wa Utalii na kuishirikisha Zanzibar ni batili kisheria na Tume yake ni batili kwa kiwango cha ushirikishwaji wa Wajumbe wanaosadikiwa kuiwakilisha Zanzibar. Jaribio lake la kuingiza Wajumbe Wazanzibari hakulipi uhalali jambo ambalo msingi wake na tokea mwanzoni kwake ni batili (void ab initio). Pia karaha inayoambatana na khatua hii ni kuwa Zanzibar imewekwa kama KIVUTIO kimoja tu cha Utalii wa Tanzania, vyengine ni Kilimanjaro na Serengeti. Waelewa wa Nini Tanzania katika muktadha wa mambo yasiyo ya Muungano wanajua kuwa kinacholengwa ni Tanzania Bara. Hivyo Zanzibar inatumika tu kuutangaza utalii wa Tanzania Bara. Inashangaza ni vipi Waziri wa upande mmoja wa Muungano anaehusika na jambo lisilo la Muungano anavyoweza kuingilia na kujiamulia kuchukua hatua mchana kweupe kwa jambo lisilokuwa chini ya dhamana yake kwa kujiamini kulikopitiliza.
Yawezekana hili ni jaribio jengine la "kuimarisha" Muungano ambao maisha yote tafsiri yake ni kupunguza mamlaka ya Zanzibar katika maeneo mbali mbali na kuyaingiza katika kapu la Muungano, ambalo kimsingi ni kapu la Tanzania Bara. Yanapofanyika haya inatukumbusha ile mizani mashuhuri iliyozoeleka hapa Zanzibar kuwa kila unapoongeza mambo ya Muungano basi upande wa mizani kwa upande wa Zanzibar huwa umepunguzikiwa na upande wa pili wa mizani ambao ni upande wa Jamhuri ya Muungano/Tanzania Bara huwa kumeongezeka uzito. Na hiyo imekuwa ndiyo tafsiri ya "kuimarisha" Muungano. Kama alivyojinasib mwenyewe Mh. Waziri kuwa yeye ni "muumin mahiri" wa Muungano. Pengine anauimarisha kwa umahiri kwa kuchanganya uendeshaji wa mambo yasiyo ya Muungano na kuyaendesha kwa kutokea Dodoma yaliko Makao Makuu ya Nchi.
Utalii kwa Zanzibar ni uti wa mgongo wa uchumi wake. Unachangia takriban asilimia 30 ya pato lake la Taifa baada ya zao la karafuu linalochangia asilimia 45 ya pato la Taifa. Utalii umesababisha uchangamfu wa kiwango kikubwa wa harakati mbalimbali za kiuchumi Zanzibar, zile za moja kwa moja na zile zinazofaidika ikiwa ni taathira/neema ya utalii (multiplier effects). Utalii unachangia kwa kiasi kikubwa sekta ya ajira kwa vijana na wajasiriliamali. Ni wazi kuwa umuhimu wa sekta ya utalii kwa Zanzibar, ambayo haina uchumi wa rasilimali za asili, na ambayo inategemea uchumi wa huduma (Service Economy) ni mkubwa mno tofauti na upande wa Tanzania Bara ambao uchumi wao una vyanzo lukuki.
Pamoja na lugha zote za ulaghai wa kisiasa ambazo mtu angejitumbuiza nazo lakini ukweli wa maumbile ya kibiashara unabaki pale pale kuwa Zanzibar, Kenya na Tanzania Bara kwa ukaribu wao wa kijiografia wanabaki kuwa ni washindani katika soko la utalii. Iweje leo mshindani wako ndie akufunge ujamu akuingize kwenye zizi lake akunadi sawia na mifugo yake halafu utegemee manufaa. Ni ajabu kuwa mshindani wako umkabidhi jukumu la kukutangazia biashara yako.
Utalii ni suala la kibiashara na kiuchumi. Hapa hakuna nafasi ya siasa chakavu za udugu na umoja. Kwenye maslahi ya kibiashara hata ndugu tena walio mapacha, udugu unaimarika pale tu maslahi ya pande zote yanapotimizwa, vinginevyo ghafla unaweza kuwakuta ndugu mapacha wamefikishana mahkamani!!! Seuze Nchi ambayo uhai wake ni vyanzo vyake vya mapato. Naamini hatujasahau wakati Tanzania Bara ilipozua sokomoko kubwa kupinga "branding" ya utalii wa Kenya walipoweka kaulimbiu ya kitalii isemayo "Visit Kenya, Visit Kilimanjaro" Wakenya waliweka kaulimbiu ile kwa kuzingatia ukaribu wa Nairobi na Mlima wa Kilimanjaro. Kwamba ukifika Kenya ni karibu mno kufika Mlima wa Kilimanjaro (Masafa kutoka Nairobi mpk Kilimanjaro ni Km 206 wakati masafa kutoka Dar mpaka Kilimanjaro ni Km 462 : Dar iko mbali kwa mara mbili na zaidi kuliko Nairobi) Wakati ule T/Bara iliiweka pembeni sera ya "Utangamano" tunaoaminishwa leo, ila Tanzania Bara ilimchachamalia Ndugu yake Kenya mpaka Kenya ikasalim amri.
Mimi ninadhani ingeingia akilini kulitumia jambo lililo la Muungano kwa kujitangaza kwa pamoja. Kwa mfano Shirika la Ndege la Tanzania ni la Muungano. Tungeweka kaulimbiu kuwa "Air Tanzania - The Wings of Kilimanjaro and Zanzibar" badala yake tunaona kaulimbiu maaruf ya "Air Tanzania - The Wings of Kilimanjaro" Shirika la wawili ila linamtangaza mmoja tu!!! Muumin wetu Mahiri wa Muungano kweli hajaliona hili???
No comments:
Post a Comment