Monday 19 July 2021

DR MWINYI AMEMSALITI MAALIM SEIF.

*DK. MWINYI AMEMSALITI MAALIM SEIF* Na Makame Ussi Nahoda Siku ya leo ya tarehe 17 Julai 2021, tunatimiza miezi mitano kamili tangu kufariki dunia kwa mwanasiasa mkongwe na mashuhuri wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad (Mwenyezi Mungu amughufirie dhambi zake na ajaaliye kaburi lake kuwa bustani katika bustani za peponi). Siku ya tare 17 Februari 2021 ilikuwa ya majonzi makubwa yasiyomithilika kwetu Wazanzibari kwa kuondokewa na Kipenzi chetu huyo. Nchi nzima ilijiimania. Si wapenzi tu wake tu, bali hata waliokuwa maadui zake wa kisiasa waliungana katika majonzi hayo. Ndio maana, maziko ya Maalim Seif yamebaki katika historia ya kusimuliwa na vizazi kwa vizazi vijavyo. Kwa kuondoka kwa Maalim Seif, kila mtu aliliona pengo lililo wazi aliloliwacha, kwani alikuwa kiongozi wa mfano aliyewaongoza Wazanzibari katika safari ndefu ya kupigania nchi yao ili iweze kurejea katika nafasi yake ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Dhamira yake ilikuwa ni kujenga jamii ya haki na usawa. Na kuielekea dhamira hiyo, alipaswa kupitia safari ngumu iliyojaa milima, mabonde na bahari yenye mawimbi ya dhoruba za kila aina. Lakini chini ya uongozi wake, tuliweza kuyavuuka yote hayo hatua kwa hatua; na kila siku moja ikipita, tukawa tunauona mwangaza wa matumaini ukichomoza. Ndiyo maana baada ya kifo chake, Wazanzibari tukajiona tupo njiapanda. Tulikuwa tunajiuliza nani kama yeye? Nani wa kutuongoza kwa ujasiri na uwezo wake? Lakini cha kushukuru ni kuwa Maalim Seif alituachia misingi madhubuti juu ya namna ya kuziendeleza harakati alizokuwa akizipiginia katika uhai wake wote. Siku ya tarehe 8 Disemba 2020, mara tu baada ya kula kiapo cha kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi, ambaye tunajuwa wazi kuwa kuingia kwake madarakani kulikuwa na walakini mkubwa, Maalim Seif alitowa hotuba nzito, ambayo ndani yake alituaminisha kuwa yeye binafsi na chama chake cha ACT Wazalendo wamekubali kujiunga katika Serikali ya hiyo ya Umoja wa Kitaifa kwa kuvutiwa na imani iliyojengeka kwa Dk. Mwinyi kama Dk. Mwinyi binafsi. Imani ya Maalim Seif kwa Dk. Mwinyi ilikuwa ni kwamba anaamiliana na mtu muungwana, mcha Mungu, mkweli na mpenda haki. Kwa sababu hii, Maalim Seif aliamini mambo mengi ambayo mtu angeliweza kuwa na wasiwasi nayo, yangeliweza kuwekwa sawa na Dk. Mwinyi katika utawala wake siku za usoni mara baada ya kuundwa kwa SUK, kwani kwa kauli na muonekano wake, Dk. Mwinyi alionekana kubeba ukweli na uungwana. Maalim Seif aliwaambia watu wake wa karibu na wanachama wa chama chake kauli hiyo. Na akaitumia kumsaidia Dk. Mwinyi aaminike na akubalike hata na wale waliokuwa wakimpinga waziwazi. Waliompinga walikuwa na hoja nzito na Maalim Seif alitambuwa hivyo. Kwamba kwa jinsi alivyoingia kupitia uchaguzi ambao haukuwa na sifa hata moja ya kuitwa uchaguzi, Dk. Mwinyi hakuwa mtu wa kuungwa mkono, bali kupingwa na kutengwa. Lakini kwa heshima waliyokuwa nayo kwa Maalim Seif, wakosoaji hao wakaamuwa kusamehe yote yaliyotendwa na watawala ili Dk. Mwinyi awe rais, wakitumaini kuwa imani ya Maalim Seif italipwa kwa ihsani. Hata hivyo, Mwenyezi Mungu akamukhitari Maalim Seif mapema sana, hata miezi mitatu bado tangu aingie serikalini. Kwa hivyo, Maalim Seif hakupata fursa ya kuishi na Dk. Mwinyi kwa muda mrefu akamuona na ukweli wake. Ingawa watu waliokuwa karibu naye wanasema katika siku za mwisho za uhai wake - muda mchache kabla hajauguwa maradhi yaliyopelekea kifo chake, Maalim Seif alikwishaanza kumtilia shaka mtu huyo aliyemuamini. Kuna matukio mawili muhimu ambayo yalitokea, mojawapo likiwa siku mbili kabla ya kulazwa hospitalini, na yote yalianza kumfanya Maalim Seif afikirie tafauti kuhusu dhamira ya Dk. Mwinyi. Alaakullihali. Halo yatakuja kuelezwa kwa undani siku moja na wahusika wenyewe, lakini kwa sasa itoshe kusema kuwa Maalim Seif alitangulia mbele ya haki na kutuacha sisi nyuma yake. Sisi ndio tunaoishi na Dk. Mwinyi. Tunamuona na tunauona ukweli wake halisi ukiibuka kila siku. Laiti tungelipata fursa ya kumpa salamu Maalim Seif huko aliko katika maisha ya barzakhi, basi tungemwambia waziwazi kuwa: “Ile shaka yako ya siku za mwisho mwisho za uhai wako juu ya Dk. Mwinyi imetimia. Huyu mtu si mkweli. Uchamungu wake ni wa mdomoni na sio wa moyoni. Kauli zake haziendani na matendo yake. Si mpenda haki na amejaa unafiki.” Kwa ufupi, tunamuambia Maalim Seif kuwa amesalitiwa na Dk. Mwinyi, tena mchana kweupe wakati bado kaburi lake pale Mtambwe Nyali lingali bichi. Dk. Mwinyi amekaa kama shetani aliyekunywa damu: ameingia madarakani kwa kunywa damu za watu, anaishi madarakani kwa kuendelea kunywa damu za watu na hatatoka hapo madarakani ila damu imwagike. Muhimu kwake yeye ni ulwa tu, na si chengine. Chaguzi za Pandani na Kinuni zilikuwa ni halindwa tu. Haya yaliyotokea Konde ndiyo yamethibitisha usaliti wa kiwango cha juu wa Dk. Mwinyi. Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, CCM hawajapatapo kuvuuka kura 700 kwenye jimbo la Konde. Kituko kilichofanyika kinaingia katika historia ya chaguzi chafu zinazoharibiwa kwa makusudi na watawala. Watawala hawa wasiotosheka, kwao wizi ndio umekuwa mfumo wao wa maisha. Hawajali chochote. Hawana haya wala junaha. CCM ilipora majimbo yote 50 ya Zanzibar, kwa hiyari yao wakabakisha majimbo manne tu na kuwapa ACT. Leo inatokea mbunge wa ACT anafariki dunia, basi jambo la mwanzo linalowajia kichwani ni kwa nini wameyaacha haya majimbo manne kwenda kwa ACT. Kwa hiyo, kila ikitokea fursa, wao wanachotamani ni kuyachukuwa na hayo majimbo manne kwa nguvu zile zile za Oktoba 2020. Ni bahati mbaya sana kwamba mwanasiasa mkongwe mwenye haiba kubwa, Maalim Seif Sharif Hamad, alijikusuru kumuamini mtu asiyeaminika. Lakini alifanya hivyo kwa dhamira yake njema kwa Zanzibar na kwa Jamhuri nzima ya Muungano wa Tanzania. Hakutanguliza chochote chengine isipokuwa hayo. Allah amlipe kwa jitihada yake hiyo. Lakini ukweli ni kuwa AMESALITIWA na Dk. Mwinyi. Jukumu la uongozi wa chama chake na wananchi wote waliomuamini kwenye uhai wake ni kutokutowa nafasi kwa usaliti aliotendewa kiongozi wao kuendelea. Wachukuwe maamuzi ya kulinda heshima ya kiongozi wao, nchi yao na dhamira yao.

No comments: