Nachukua fursa hii, kwa niaba ya sauti za watu wa Kibaha Vijijini, kukosoa na kutoa kushauri dhidi ya "uwakilishi dhaifu" uliooneshwa na Mbunge wa Kibaha Vijijini, Ndugu Michael Mwakamo, kwenye Bunge la Bajeti, akiwa ni sehemu ya uchochoro wa mapungufu ya Bunge zima.
*Kimsingi, malalamiko ya wananchi kuhusu tozo kubwa za miamala ya simu na hatimaye hatua ya serikali kutangaza kuyafanyia kazi malalamiko hayo; ni ushahidi wa dhahiri kwamba Ndugu Mwakamo alishindwa kuwawakilisha wananchi ipasavyo bungeni katika kujadili na kupitisha Bajeti na Sheria ya Fedha 2021/22, kwani hakujaribu kutimiza wajibu wake wa kibunge wa kuhoji, kukosoa, kushauri au kushawishi Bunge na Serikali kutopitisha tozo hizo!*
*Matokeo ya kushindwa huko, ni wananchi wa Kibaha Vijijini na Tanzania zima kwa ujumla kuamua kujiwakilisha wenyewe katika suala hili kwa kukosoa, kupinga na kutoa malalamiko mitandaoni na vijiweni dhidi ya tozo hizo mpaka serikali ilipolazimika kutoa ahadi hivi majuzi kwamba imeguswa na itayafanyia kazi malalamiko hayo!*
*Hakika, ni jambo la kusikitisha kuwa wananchi walilazimika kufanya kazi iliyomshinda mbunge ndani ya Bunge, licha ya kulipwa mishahara, mafuta, posho na marupurupu mengine mengi kwaajili ya kuwakilisha wananchi!*.
Kwa vyovyote vile, si busara wala ustaarabu kunyamaza kimya. Ni muhimu makosa na mapungufu ya mbunge yaanikwe na ushauri utolewe ili ajaribu kujirekebisha na kuyatendea haki majukumu mazito ya kibunge (kama ataweza).
*II. MAKOSA 10 YA MBUNGE*
Bila kuwashirikisha wananchi wala kutumwa na mwananchi hata mmoja wa Kibaha Vijijini; Mbunge alishiriki kikamilifu kufanya makosa makubwa yafuatayo katika kupitisha Bajeti na Sheria ya Fedha ya 2021/22:
1. *Kuongeza Mzigo wa Gharama za Miamala ya Simu*
Aliunga mkono wananchi waongezewe gharama za miamala ya kutuma na kupokea fedha bila kuzingatia hali mbaya ya umaskini wa kipato. Alifanya kosa hili kwa kukubali kurekebishwa kwa Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kielekroniki, Sura Na 306 na kuweka Tozo ya Tshs 10 hadi 10,000 katika kila muamala. Uamuzi huu umefanya makato kuwa makubwa sana kulingana na ukubwa wa fedha inayotumwa.
Ni ajabu kuwa Mbunge alikubali hili bila kuzingatia kuwa Kibaha Vijijini ina wananchi wengi wasio na akaunti benki na wanategemea zaidi simu kufanya miamala.
Aidha, kwa kuwa gharama kubwa za miamala ya simu zinaweza kusababisha wananchi kutafuta njia mbadala za kutumiana pesa, ni dhahiri kuwa Mbunge alishiriki kuhatarisha ajira za vijana wengi wanaofanya kazi za uwakala wa mitandao ya simu Kibaha Vijijini, wakiwemo mawakala wa
kata 7 za Mji wa Mlandizi na kata 7 za vijijini: Dutumi, Gwata, Magindu, Kwala,Soga, Boko Mnemela na Ruvu (achilia mbali wa maeneo mengine nchini).
2. *Kuongeza Gharama za Mawasiliano ya Simu*
Aliunga mkono wananchi watozwe Tshs 10 hadi Tshs 200 kila siku katika laini zao, kwa kadri watakavyoweka vocha kwenye simu. Alifanya kosa hili kwa kukubali kurekebishwa tena kwa Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kielektroniki, Sura Na. 306, na kubariki ushuru huo wa muda wa maongezi!
3. *Kuongeza Bei ya Mafuta ya Taa*
Aliunga mkono wananchi waongezewe gharama za kununua mafuta ya taa bila kuzingatia kuwa Kibaha Vijijini ina wananchi wengi wanaotegemea sana mafuta ya taa. Alifanya kosa hili kwa kupitisha marekebisho ya Sheria ya Petroli Sura Na 392 na kuongeza tozo ya mafuta ya taa kutoka Tshs 150 hadi Tshs 250. Serikali ilieleza bungeni kuwa lengo la tozo hiyo ni kuepusha uchakachuaji wa mafuta ya petroli. Alipaswa kuishauri serikali kuimarisha ukaguzi, usimamizi na ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kudhibiti uchakachuaji wa mafuta badala ya kukubali mwananchi abebeshwe mzigo wa bei kubwa ya mafuta ya taa.Alipaswa kujielimisha kuwa mafuta huwa yanawekwa vinasaba; kwa hiyo angeishauri serikali kudhibiti uchakachuaji wa mafuta kwa kutumia vinasaba. Hakufanya hivyo!
4.
*Kuongeza Bei ya Mafuta ya Petroli na Dizeli*
Aliunga mkono wananchi kupandishiwa bei ya petroli na dizeli. Alifanya kosa hili kwa kukubali kurekebishwa kwa Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta, Sura 220 kwa kuweka kifungu kinachoongeza makato ya Tshs 100 katika kila lita moja ya petroli na dizeli hadi kufikia makato ya Tshs 363 kwa lita. Uamuzi huu unaweza kuongeza gharama na ugumu wa maisha.
5. *Kupitisha Makato ya 2% katika Mauzo ya Mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi*
Bila kuzingatia kuwa anatokea kwenye jimbo la wakulima na kwamba wakulima wanaingia gharama kubwa za uzalishaji na hawana masoko ya uhakika, Ndugu Mwakamo alibariki makato ya 2% ya Kodi ya Zuio (Withholding Tax) kwa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi yanayouzwa kwa makampuni ya usambazaji mazao.
6. *Uwakilishi Dhaifu Sekta ya Afya*
Changamoto kubwa za sekta ya afya hapa Kibaha Vijijini ni uhaba wa zahanati na vituo vya afya. Mathalan, wakati Sera ya Afya imeelekeza kila kata kuwa na kituo kimoja cha afya, Kibaha Vijijini yenye kata 14, ina vituo viwili tu vya afya vya serikali (kata ya Magindu na Mlandizi). Wananchi wanaingia gharama kubwa na hata kuhatarisha uhai wao kwa kusafiri umbali mrefu kufuata kituo cha afya.
Wengi wao wanatokea kwenye maeneo ambayo hayana hata zahanati wala magari ya kubebea wagonjwa mahututi (ambulances). Mbaya zaidi, zahanati chache zilizopo na vituo hivyo viwili vya afya kwa pamoja, vinakabiliwa na uhaba mkubwa wa madawa! Kwa hali hii, mbunge alipaswa kuibana serikali itenge fedha za kutosha za kuongeza zahanati na vituo vya afya na kuipa Kibaha Vijijini kipaumbele! Kinyume chake, serikali ilikiri kuwapo kwa uhaba mkubwa wa zahanati na vituo vya afya, lakini iliishia kutoa ahadi tu kwamba, ikisema: *Serikali itaendelea na jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maboma ya zahanati ..."* Mbunge akaridhika na ahadi badala ya kudai fedha mahsusi zitengwe sasa.
Aidha, ni vema ikaeleweka kuwa maboma yaliyozungumziwa ni majengo 8,004 yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi maeneo mbalimbali nchini. Kwa Kibaha Vijijini maeneo mengi hakuna hata maboma hayo. Kwa uwakilishi huu dhaifu, bado hali ya huduma za afya itaendelea kuwa mbaya Kibaha Vijijini, achilia mbali nchi nzima. Bado itakuwa ni miujiza kwa Tanzania kufikia shabaha ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya kupunguza uwiano wa vifo vya akina mama na watoto ifikapo mwaka 2030.
7. *Uwakilishi Dhaifu Sekta ya Elimu*
Sera ya elimu bila malipo imeleta ongezeko kubwa la wanafunzi.
Mathalan, kwa mujibu wa Utafiti wa BEST 2020, idadi ya wanafunzi kwa elimu ya msingi imeongezeka kutoka wanafunzi milioni 8.2 mwaka 2016 hadi kufikia milioni 10 mwaka jana (2020).Ongezeko hili pia linatarajiwa kuongeza uandikishaji katika ngazi ya elimu ya sekondari hadi kufikia wanafunzi milioni 4.5 mwaka 2024. Kwa hiyo, ili kunusuru ubora wa elimu, mambo manne ya msingi sana yalipaswa kujengewa hoja nzito na mbunge ili yatengewe fedha za kutosha:
Mosi, Ndugu Mwakamo alipaswa kupigania Ruzuku ya Mwanafunzi (Capitation Grant) iongezwe kutoka Tshs 10,000 hadi kufikia angalau Tshs 30,000 kwa kila mwanafunzi wa elimu ya msingi kwa mwaka; na kutoka Tshs 25,000 hadi Tshs 50,000 kwa kila mwanafunzi wa sekondari kwa mwaka. Viwango vya sasa havitoshi na vimetumika tangu mwaka 2002 wakati gharama za mahitaji ya elimu zimeshapanda sana!
Pia kwasababu ya Miongozo ya hivi karibuni ya serikali, utoaji wa ruzuku hiyo umepungua sana kiasi kwamba shule za msingi hupokea Tshs elfu 6 tu (badala ya Tshs elfu 10), kwa kila mwanafunzi. Hapa Miongozo inasema kuwa Tshs 4,000 itabaki Wizarani kwaajili ya kuzinunulia shule vitabu vingi kwa pamoja. Mbunge alipaswa kuhoji ni vitabu vingapi vilifika kwenye shule za Kibaha Vijijini, lakini hakufanya hivyo.
Utafiti binafsi nilioufanya (Kinabo 2020) unaonesha bado kuna uhitaji mkubwa wa vitabu katika shule za Kibaha Vijijini.
Aidha, shule za sekondari hupokea Tshs elfu 12 tu (badala ya elfu 25) kwa kila mwanafunzi. Kwasababu hii, wananchi wanachangishwa michango mingi mashuleni na kuifanya *sera ya elimu bila ada* kugeuka kuwa *sera ya elimu kwa michango*. Michango mashuleni ni moja ya kero kubwa sana kwa wakazi wa Kibaha Vijijini. Ajabu, ndugu yetu hakuweza kujenga hoja nzito za kupigania kuongezwa kwa ruzuku ya maendeleo ya elimu kwa mwanafunzi!
Pili, ongezeko la wanafunzi limesababisha upungufu mkubwa wa madarasa. Kwa mujibu wa Utafiti wa BEST 2020, kuna upungufu wa madarasa 82,200 kwa shule za msingi na 4,647 kwa shule za sekondari kwasasa.Ndani ya miaka 4 ijayo kutakuwa na upungufu wa madarasa 41,833 kwa sekondari kwasababu ya kuongezeka kwa wanafunzi wa shule za msingi kutoka mwaka 2016 ambao watamaliza darasa la saba mwaka 2021/2022. Madarasa yamekuwa yakijengwa kwa kusuasua kwa kutegemea zaidi wananchi wachangie raslimali fedha, vifaa na nguvu kazi, wakati wananchi hawahawa hukatwa kodi nyingi kwaajili ya maendeleo! Inasikitisha kuwa Ndugu Mwakamo hakuweza kujenga hoja nzito katika eneo hili muhimu.
*Mbunge anapaswa kutambua kuwa jukumu lake la msingi si kuhamasisha wananchi wachangie tu fedha za ujenzi wa madarasa.
Hilo ni jambo jema, lakini si kazi ya msingi ya mbunge, maana hata mtu asiye mbunge bado anaweza kuhamasisha michango.Jukumu la msingi la mbunge ni kupigania bajeti ya kutosha ili kumpunguzia mwananchi mzigo wa michango*
Tatu, ongezeko la wanafunzi pia limesababisha uhaba mkubwa wa walimu. Kwasasa uwiano wa walimu kwa wanafunzi ni 1:169 kwa madarasa ya awali na 1:61 kwa madarasa ya shule za msingi badala ya uwiano wa 1:45 inayotakiwa kisera. Kwa miaka 4 ijayo watahitajika walimu 41,833 kwasababu ya ongezeko la wanafunzi 1,882,500. Ajabu, mbunge wa Kibaha Vijijini hakuweza kujenga hoja za kuibana serikali iajiri walimu wa kutosha. Katika eneo hili, bajeti aliyoshiriki kuipitisha hairidhishi.
Nne, Ndugu Mwakamo hakuweza kujenga hoja makini juu ya umuhimu wa kuongeza raslimali watu katika Idara ya Uhakiki wa Ubora wa Elimu. Mathalan, katika mwaka wa fedha uliomalizika, Idara ya Uhakiki ilipanga kufanya uhakiki wa ubora wa elimu kwenye shule za msingi 4,700 tu badala ya shule 18,152, na Sekondari 1,200 tu badala ya 5,072.
Hili nalo lilipita hivi hivi, licha ya Ndugu Mwakamo kutamba kuwa alipata nafasi ya kuchangia mara nyingi bungeni!
*Ni vema ndugu Mbunge akatambua kuwa ubora wa mbunge haupimwi kwa wingi wa maneno bungeni au kwa kutajataja tu matatizo, bali kwa kuyajengea hoja nzito zenye ushahidi wa kutosha wa maelezo na takwimu na hatimaye hoja hizo kuzingatiwa vizuri kwenye mafungu ya bajeti na kutekelezwa*
8. *Uwakilishi Dhaifu Sekta ya Maji*
Jimbo la Kibaha Vijijini lina shida kubwa ya maji safi na salama hasa vijijini, licha ya kuwa mto Ruvu unapita katika sehemu kubwa ya jimbo hili. Mathalan, katika kata za Dutumi, Magindu, Gwata, Soga, Boko Mnemela n.k bado kuna maeneo mengi yenye shida kubwa ya maji safi na salama. Kwa vyovyote vile, gharama za usambazaji wa maji ya uhakika ni ndogo sana kwa Kibaha Vijijini iliyo na mto Ruvu kuliko Dar es Salaam na maeneo mengine. Mbunge alipaswa kujenga hoja nzito na mahsusi kabisa za kuitaka serikali imalize kabisa tatizo la maji. Mchango wake katika eneo hili haukuwa wa kuridhisha.
9. *Uwakilishi Dhaifu Sekta ya Kilimo*
Ndugu Mwakamo ameshiriki kikamilifu kupitisha Tozo nyingine ya 5% kwaajili ya huduma za umwagiliaji kwa thamani ya mavuno yatakayovunwa na wakulima chini ya vyama vyao vya umwagiliaji maji kwenye maeneo ya "schemes" za umwagiliaji .Maana yake ni kwamba wananchi wa Mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji kule Mongomole Kibaha Vijijini sasa wamebebeshwa malipo haya, bila kujali uduni wa miundombinu yenyewe, gharama kubwa za uzalishaji na changamoto ya masoko kwaajili ya mazao yao. Ni vigumu kujua mbunge alifikiria nini wakati anapitisha Bajeti yenye mambo mengi magumu dhidi ya wananchi wa Kibaha Vijijini na Tanzania kwa ujumla!
Aidha, alishindwa kujenga hoja nzito za ujenzi wa malambo, majosho na miundombinu mingine ya ufugaji ili kupunguza tatizo kubwa la migogoro ya wakulima na wafugaji, mapigano na mauaji ya mara kwa mara ambalo limedumu kwa miaka mingi ndani ya Jimbo la Kibaha Vijijini.
Hapa mbunge aliishia kuyataja tu matatizo bila kuyajengea hoja zenye mantiki na ushawishi wa kutosha.Mchango wake kwenye eneo hili pia haukuwa wa kuridhisha.
10. *Kupitisha Bajeti Finyu ya Maendeleo*
Ni vema ikaeleweka kuwa bajeti ya serikali iliyopitishwa imetenga Tshs Trilioni 10.3 kwaajili ya miradi ya maendeleo nchini, kutoka kwenye vyanzo vya mapato ya ndani. Katika fedha hizo, matumizi ya maendeleo kwa halmashauri zote yametengewa Tshs Bilioni 331,090, sawa na asilimia 3 tu ya fedha zote za maendeleo!Fedha hizi kiduchu bado zitagawanywa kwa halmashauri zote. Kwa miaka mingi miradi ya maendeleo Kibaha Vijijini imekwama na kusuasua kwasababu ya ufinyu wa bajeti au kukosa fedha kabisa.Ni ajabu, Ndugu yetu alikubali asilimia 3 ya fedha za maendeleo, badala ya kupigania mgawo wa fedha za halmashauri uongezwe ili jimbo letu pia lipate fedha za kutosha. Kulikuwa na fursa nyingi za kufanya hivyo.
Mathalan, Bunge limepitisha nyongeza ya kodi ya majengo kutoka Tshs 10,000 hadi Tshs 12,000 kwa nyumba na majengo ya kawaida. Kodi hii itakuwa inakusanywa kwa kuchanganywa katika malipo ya umeme kwa njia ya Luku. Cha kusikitisha ni kwamba, Bunge limeamua kuwa ni 15% tu ya fedha zote zitakazopatikana kwenye kodi hii, ndiyo zitengwe kwaajili ya halmashauri, huku 85% yote ikienda serikali kuu! Ndugu Yetu alikuwa na fursa ya kujenga hoja kutaka mgawo wa kodi hiyo uongezwe kufikia angalau 50% kwa halmashauri, ili fedha nyingi za maendeleo zirudi moja kwa moja halmashauri kwa maendeleo ya wananchi. Ajabu, hili nalo lilimpita hivi hivi! Kwa hali hii bado miradi mingi ya maendeleo katika Jimbo la Kibaha Vijijini itakwama.Mbunge kurudi jimboni na asilimia 3 tu ya fedha za maendeleo si jambo la kujivunia hata kidogo!
*III. MADHAIFU YALIYOSABABISHA MAKOSA YA MBUNGE!*
Makosa hayo ya kiuwakilishi yanatoa tafsiri ya madhaifu yafuatayo ya mbunge:
a) Ndugu Mwakamo alienda kwenye Bunge la Bajeti ya 2021/22 akiwa na uelewa mdogo wa matatizo na kero za wananchi. Hakujua chanzo wala ufumbuzi wa msingi wa shida nyingi zinazowasibu wananchi.
Matokeo yake, aliongea ongea tu, lakini hakuweza kabisa kuwakilisha wananchi ipasavyo kwenye maeneo nyeti. Ajielimishe.Ajiongeze.
b) Ni dhahiri kuwa alikwenda bungeni akiwa hana ujuzi wala maarifa ya kutosha ya kuchambua bajeti wala sheria ya fedha. Hakika, aliachwa kapa kabisa kwenye mjadala wote wa masuala ya kodi, tozo, ushuru na ada mbalimbali. Matokeo yake, alishiriki kuitikia "ndiyooo" kwa kila kitu na kumbebesha mwananchi mzigo mkubwa wa gharama za maisha.
*Ubunge ni zaidi ya kuvaa suti na kusemasema bungeni. Ubunge ni kuwawakilisha wananchi kwa kuishauri na kuibana serikali kwenye maeneo nyeti*
C) Alifanya kosa kubwa kutowashirikisha wananchi ili kupata maoni mazuri na ya kitaalam juu ya hoja za msingi za kupeleka bungeni.Badala yake
alikurupuka tu ndani ya siku chache kuelekea mjadala wa bajeti kuu, na kuanza kuomba maoni ya haraka-haraka (zimamoto), ili apate chochote cha kusema bungeni! Hata baadhi ya maoni mazuri aliyopatiwa, bado hakuweza kuyachambua vizuri ili kupata hoja nzito na muhimu za kiuwakilishi. Alifeli.
d) Baada ya Bunge kumalizika, mbunge amefanya ziara jimboni, kwaajili ya kujisifia eti: *"aliwawakilisha wananchi ipasavyo na amewaletea zawadi"*. Ni dhahiri kuwa mbunge bado hayajui makosa na mapungufu yake. Tumsaidie.Tumuombee
e) Ni dhahiri kuwa mbunge amefanya kazi ya kuiwakilisha zaidi serikali bungeni kuliko wananchi, kwani alishiriki zaidi kuikubalia serikali kila kitu kuliko alivyowatetea wananchi!
*IV. MAMBO MUHIMU ALIYOSHINDWA KUSHAURI ILI KUEPUSHA MZIGO MKUBWA WA KODI, TOZO NA USHURU*
a) Alipaswa kushauri kuwa badala ya kuongeza kodi, ushuru na tozo, serikali ifanye tathmini ya kupunguza matumizi ya pesa yasiyo ya lazima.Nchi yetu ni maskini sana, lakini bado viongozi wengi wa kiserikali wanagharamiwa kwa hadhi inayokaribia, inayolingana au kuzidi hadhi ya viongozi wa nchi tajiri! Mathalan, ni muhimu kuondoa kabisa matumizi ya gari za gharama (mashangingi) n.k na kununua gari nafuu na imara za kikazi kama landrovers, Ford rangers n.k
b) Alipaswa kuishauri serikali kuziba mianya ya upotevu wa pesa unaotokea kwa njia mbalimbali ikiwemo ukwepaji wa kodi na wizi.
Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za kila mwaka zimeainisha mianya mingi ya fedha zinazopotea katika Mamlaka ya serikali za mitaa, kwenye Wizara, Idara, Mashirika ya Umma, Mamlaka na Wakala wa Serikali. Aidha, CAG ametoa ushauri mwingi kwa serikali wa jinsi ya kuongeza ufanisi katika kudhibiti upotevu wa mapato.
C) Alipaswa kuishauri serikali ifanyie kazi kwa 100% vyanzo vingine vya mapato vilivyopo na kubuni vingine vipya.
Mathalan, miaka 13 iliyopita, utafiti wa Mchumi mashuhuri wa Peru, Hernando De Soto, ulibaini kuwa 90% ya Watanzania wanajikimu kimaisha kwa kutegemea zaidi shughuli zisizo rasmi (infomal sector);kwamba 98% ya biashara haziko rasmi kwa kuwa hazijasajiliwa, hazitambuliki kisheria na hazijafungamanishwa na mfumo rasmi wa uchumi wa nchi; na kwamba 89% ya ardhi, nyumba na majengo mengine havijapimwa.
De Soto alisema kuwa wote huu ni mtaji mfu (dead capital) na aliuthaminisha mtaji wote huo na kuona kuwa una thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni 29. Alisema fedha hizo ni nyingi sana kuzidi hata misaada mingi ambayo nchi yetu ilipokea kutoka nchi wahisani tangu Uhuru (1961).Kwa hiyo, pamoja na mambo mengine, alishauri ardhi yote nchini ipangwe, ipimwe na kumilikishwa kwa hati ili wananchi wafaidike na ardhi yao na serikali nayo ipate kodi ya ardhi kila mwaka. Mapendekezo hayo ya De Soto na mengine mengi (Unlocking Dead Capital), ndiyo yaliyozaa mpango wa kurasimisha raslimali na biashara zisizo rasmi nchini (MKURABITA).
Hata hivyo, miaka zaidi ya 13 tangu De Soto aondoke nchini, bado serikali haijafanya uwekezaji wa kutosha kwenye maeneo mengi yaliyoshauriwa. Kwa mfano, ardhi iliyopimwa na kumilikishwa kwa hati nchi nzima mpaka sasa ni takribani 20% tu ya ardhi yote ya jumla (general land). Zaidi ya 80% ya ardhi yote haijapimwa na haina hatimiliki. Maana yake ni kwamba serikali imekuwa ikipoteza zaidi ya 80% ya mapato ya kodi ya ardhi kila mwaka. Haya ni mabilioni ya fedha. Mamlaka ya Mji Mdogo Mlandizi yenye kata 7 kwa mfano, bado ina eneo kubwa sana halijapimwa! Imebaki kuwa ni ardhi na makazi holela. Pakipimwa, wananchi watafaidika na serikali itapata kodi. Ajabu, mbunge hakuwa na jambo mbadala la kushauri ili kuwanusuru wananchi dhidi ya makato makubwa.
*V. USHAURI WANGU KWA MANUFAA YA WANANCHI*
*Kwa Ndugu Mbunge:*
1. Aache mara moja kudanganya na kujisifu kuwa eti amewawakilisha wananchi ipasavyo bungeni na badala yake awe muungwana, ajitokeze hadharani na kuwaomba radhi wananchi wa Kibaha Vijijini kwa kushindwa kuwawakilisha vema bungeni. Matokeo ya uwakilishi dhaifu ni wananchi wa Kibaha Vijijini kuwa sehemu ya Watanzania waliochukizwa na tozo kubwa za miamala ya simu na makato mengineyo. Mambo machache aliyoyaongea bungeni afahamu kuwa hayawezi kuwa muhimu kuzidi bajeti inayolalamikiwa aliyoshiriki kuipitisha.
Hana la kujitetea, isipokuwa kuomba radhi.
2. Wakati serikali ikiwa imeahidi kulifanyia kazi suala la tozo za miamala ya simu, Ndugu Mwakamo ajipange kuandaa hoja binafsi za kulitaka Bunge kupitia upya baadhi ya maamuzi mengine yasiyoridhisha yaliyopitishwa kwenye Bunge lililopita, ndani ya uwezekano wa kanuni za Bunge, ili kuleta nafuu kwa wananchi. Nipo tayari kusaidia hili kwa manufaa ya wananchi bila masharti yoyote yale.
3. Achague kusimama na wananchi na kuacha kuwa muwakilishi wa serikali bungeni.
4. Atambue kuwa ubunge ni kazi kubwa na nzito sana inayohitaji uelewa mkubwa wa mambo na maarifa ya kutosha. Ajitahidi kujifunza na asione haya kuomba msaada, kwani hakuna binadamu anayejuwa kila kitu.
*Kwa Wananchi:*
5. Kimsingi, ni muhimu wote tukatambua kuwa maamuzi yote hayo ya Bunge la Bajeti ni matokeo ya nchi kutokuwa na katiba nzuri, kukosa tume huru ya uchaguzi na wananchi kutoshiriki kikamilifu kupiga kura nyakati za uchaguzi. Matokeo yake yamekuwa ni kupata wawakilishi wasio bora na wanao ogopa zaidi chama na serikali yao, kuliko wananchi.
Hakika, ni matokeo ya kuwa na Bunge linalotawaliwa zaidi na chama kimoja!
Tunahitaji katiba mpya hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote ule. Katiba yetu ya sasa ni kikwazo kikubwa dhidi ya maendeleo ya wananchi. Kwa mfano: Ibara ya 99(1) ya Katiba yetu ya sasa inasema kwamba Bunge halitashughulikia Muswada wa Sheria kwaajili ya kutoza kodi au kubadilisha kodi kwa namna nyingine yoyote isipokuwa kupunguza....isipokuwa kama Rais amependekeza kwamba jambo hilo lishughulikiwe na Bunge na pendekezo hilo la Rais liwe limewasilishwa kwenye Bunge na Rais
.Ni dhahiri kuwa wananchi wote bila kujali tofauti zetu za kisiasa, tunahitaji Katiba Mpya ili, pamoja na mambo mengine, tuweze kupunguza madaraka na mamlaka makubwa yaliyolimbikizwa sehemu moja (kwenye nafasi ya urais wa nchi); badala yake, tulipe Bunge uhuru na mamlaka ya kutosha ya kuisimamia na kuiwajibisha serikali. Kupitia Katiba Mpya tutaweza kujiepusha na kupitishwa kwa bajeti zisizojali maslahi ya wananchi.
6. Mbali na ukweli kuwa tunahitaji kushiriki kwenye mchakato wa Katiba Mpya naTume Huru ya Uchaguzi; ni muhimu pia wananchi wote kujenga utamaduni wa kushiriki mikutano ya kisiasa na kupiga kura ili kupata viongozi wenye ubora wa kutosha.
*Huko nyuma tulikuwa na mwakilishi asiyeweza hata kusema chochote bungeni.
Baadhi yenu mlimwita "bubu". Hata hivyo, ni muhimu tukatambua kuwa mwakilishi wa kutufaa zaidi si yule wa kuongea ongea tu kama "Kasuku", bali anayeweza kujenga hoja kwa umakini na umahiri wa kutosha na kuibana serikali kwenye maeneo nyeti kwa faida ya wananchi. Mkutano wa Bunge la Bajeti lililopita, umethibitisha kuwa bado mwakilishi huyo hajapatikana! Kibaha Vijijini inastahili kilicho bora zaidi*
Kwa wananchi wanaopenda kusema *hayo ni mambo ya wanasiasa"*, bajeti hii ngumu ni ushahidi kuwa wanasiasa ndio wanaopanga tuishi maisha nafuu, mazuri na magumu kiasi gani. Tusidharau siasa. Ni wajibu wetu sote kuhakikisha wanasiasa wanaopewa dhamana ya kuongoza, wawe ni wale wenye maarifa na uthubutu wa kutosha wa kuwatetea wananchi. Siasa ndiyo maisha yetu.
Kwa ushauri huo, nawasihi kila mmoja atimize wajibu wake na kwa pamoja tutafika.
*Kijua ndio hichi, tusipouanika tutautwanga mbichi*
Mungu ibariki Afrika
Mungu ibariki Tanzania
Mungu ibariki Kibaha Vijijini;
Ahsanteni kwa kunisikiliza:
*Kinabo*
*Sauti ya Kibaha Vijijini*
No comments:
Post a Comment