Thursday 27 December 2012

Siasa za Jirani zetu lini Donda la ukabila litapona

Vitimbi na sarakasi tunavyoendelea kuvishuhudia kila uchao baina vigogo wa chama hiki na vyama vile, bila shaka zinamwacha mwanachi wa kawaida, mimi na wewe, tukiwa tumeleweshwa chakari na ukosaji wa msimamo wa viongozi hawa. Ni bayana kwamba kuruka rukia farasi huyu mara yule, kuchumbiana kisiasa, ufungaji ndoa wa chama hiki na kile, na kuvishana pete zenye misingi ya kikabila sio kwa manufaa ya taifa letu. Hizi ni sera na mbinu za kujinafsisha wenyewe badala ya kuweka masuala yanoyoikabili nchi yetu mbele ya maslahi yao. Kwao, maslahi ya akina yakhe, yaani umaskini tuuonao katika mitaa ya Kibera na Korogosho, mle vijijini na katika makao ya halaiki ya Wakenya walioadhiriwa na vurugu ya baada ya uchaguzi wa 2007/2008, sio suala muhimu kwao. Lililo muhimu kwao, ni takwimu iliotangazwa majuzi ya wapiga kura takriban 14,337,399 ambao waliojiandikisha kutumia haki zao za kikatiba kuwachagua viongozi wawapendao. Vigogo hawa wa miungano ya CORD, JUBILEE na PAMBAZUKO wanaelewa tu lugha moja: kwamba kati ya waliosajiriwa kupiga kura, dhuluthi kubwa itakuwa Wakenya kutoka jamii za Wakikukiyu, Wakalenjin, Waluhya, Wakamba na Wajaluo. Wanapofanya mishikamano hii kisiasa ya kujinafsisha wenyewe, kulenga kura za makabila haya makubwa kana kwamba, sisi tulioko katika makabila madogo madogo kama vile Wakisii, Wameru, Wasomali, Waturkana, Wateso, Wamasai, Wagabra, Warendille, Wabaorana, Mijikenda, Wadaasanachi, Wanyagatom, Wamursi, Wasurma, na wengineo hatuna mchango wowote wa kuichangia taifa letu. Tunawekwa kando. Tunawekwa chini ya jamvi, tusahaulike miaka mingine mitano, miaka hamsini tangu Kenya kumtimua Mkoroni. Cha kushangaza katika miungano hii ya kisiasa ni kwamba vigogo hawa wote hawajafikia kiwango cha kuyajadili masuala muhimu yanayowakabili wananchi na taifa letu. Wao wanajijadili wenyewe. Tunachokisikia kukisoma katika vyombo vya habari ni farakano na kutoelewana kwa vigogo hawa wenyewe pale maslahi yao ya kibinafsi yanapokuwa hatarini. Misimamo yao, masuala yao, itikadi zao, falsafa zao, ni wao wenyewe. baba na ndugu waliabudiwa tangu baada ya uhuru. Wao pia wataka kuabudiwa, kwa lazima, nipende nisipende.....tupende tusipende. Pengine Bi Martha Karua ana jambo analoielekeza kwetu: kwamba miungano ya ubinafsi wakujinafsisha binafsi haufai, hautufai. Unaendeleza chuki, unaitenganisha taifa na watu wetu. Kiongozi wa kweli na wa kuaminika ni yule anayeweka masuala na maslahi ya wananchi wa eneo lake na taifa letu katika safu ya kwanza. Taifa yetu inahitaji miradi ya kuzalisha kazi kwa vijana wetu, uelewano wa makabila yote, uimarishaji wa masoko ya bidhaa zetu, maji mazuri na salama, elimu bora kwa watoto wetu, miradi ya kuboresha nishati, utekelezaji wa katiba kikamilifu, usalama wa chakula, usalama wa wananchi na taifa, ukarabati wa barabara zote, na sera mwafaka za kigeni. Kuna yeyote anayefanya hivyo? Kuna yeyote anayeuza sera hizi katika kampeini zao? Ni nani anayeyashughulikia masuala nyeti kama hayo? Hamna! Tuonacho ni mavazi wanayoyavaa ya marangi rangi kama wenda wazimu. Wanamuona mwananchi wa kawaida kama tarakimu tu, yaani nambari itakayomfanya yeye, familia yake, rafiki zake na kabila zao kuendelea kupeperusha bendera ya nchi kana kwamba hio ni haki yao. Wanachokigombania sio uongozi wala vyama, ila ni nani atayewalinda wasisukumwe kizimbani kwa kashfa na dhambi walizozifanyia nchi na wananchi. Unapowaona wakiwapigia madebe vigogo hawa sio kuwa wanawapenda: wanaangalia usalama wa mali waliojilimbikiza kwa njia isio halali, na kinyume cha sheria. Wanapozozana hadharini mbele ya vyombo vya habari, jioni jioni wanakutana katika Muthaiga Golf Club, Hilton Hotel, na mahoteli makubwa makubwa mengineo kutucheka sisi, kukucheka wewe: kutudhihaki na kutudharao sisi. Eti waache wakae vivo hivyo. Vigogo hawa wanautazama kiongozi kama mfadhili badala ya kuutazama kama mwakilishi na mtetezi wa umma. Badala ya wao kujadili namna ya kutatua kiini cha matatizo na changamoto zinazowakabili watu wetu, wanajijadili wao, tunawajadili wao. Kipindi hiki tulichonacho hivi sasa ni cha kuwachagua viongozi wenye maadili, sio wale wanaofoka maneno wasioyaamini. Wakati umepita wa viongozi na wawania kiti cha urais kutofanya kazi ya udaku, umbea, usalata, uraji milungura huku wakifikiria na kufuatilia kati yao ni nani hawara wa nani ili baada ya uchaguzi adhalilishwe uongozini. Wakati wakujineemesha, kuabudiwa kama miungu, ubinafsi wa kujinafsisha umefika ukingoni. Tuwang'oeni mamlakani. Kuuza kura kwa Sh200 ni kuuza haki yako, taifa lako na matumaini ya watoto wetu na vizazi vijavyo. Likatae

No comments: