WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amesema amewashitaki wanasiasa wenzake, Edward Lowassa na Rostam Aziz, kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa vitendo vyao vya kifisadi.Akizungumza na Raia Mwema juzi Jumatatu, Sitta alisema tayari amewasilisha vielelezo vya ushahidi wake ndani ya chama hicho na anachosubiri kwa sasa ni majibu ya tuhuma zake hizo.“Tayari nimepeleka maelezo yangu kwenye chama kwa ajili ya kuchukua hatua. Haya mambo ninayoyazungumza kila siku si porojo bali ni ukweli na nina vielelezo vya kuthibitisha hayo na tayari nimevipeleka kwenye chama,” alisema Sitta, mwanasiasa mkongwe ambaye amewahi kuwa Spika wa Bunge la Tanzania.
Sitta hakutaka kuingia undani wa tuhuma alizozitoa kwa maelezo kwamba anasubiri kwanza chama kitoe majibu ya hoja zake.
Katika mazungumzo yake hayo na gazeti hili, Sitta alitamka kwamba ingawa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa na Rostam Aziz, Mbunge wa zamani wa Igunga na mfanyabiashara tajiri, ndiyo aliowataja kwa tuhuma za ufisadi, anafahamu pia mafisadi wengine walio ndani ya CCM lakini ameamua tu kuwataja hao kwa sasa.
Sitta alikuwa akijibu tuhuma za Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba, aliyezungumza na gazeti hili juzi Jumatatu na kudai kwamba chama hicho hakina mafisadi na kwamba wanaosema hivyo wanakivuruga chama badala ya kukijenga.
Katika maelezo yake, Makamba alisema; “Kama akina Lowassa wangekuwa mafisadi, wangekuwa tayari wamechukuliwa hatua na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) au vyombo vingine vya dola.
“Kama hawajachukuliwa hatua na bado ni viongozi halali waliopitishwa na chama kwenye nyadhifa zao, basi watu hao si mafisadi. Sitta anatakiwa awataje kwa majina mafisadi anaowasema badala ya kulitumia neno hilo kuzungumza kijumlajumla,” alisema.
Akizungumza kwa utulivu, Sitta alisema kisiasa, mtu haondokewi na tuhuma za ufisadi kwa vile tu hajakamatwa na vyombo vya dola au ushahidi dhidi ya tuhuma zake haujapatikana.
“Kwenye siasa, mtu kujulikana kama fisadi au si fisadi hakutokani na kutokamatwa na vyombo husika. Ni tabia ambayo mtu unaionyesha kwa jamii ndiyo inakuwa taswira yako.
“Ndiyo maana, Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba mke wa Kaisari hatakiwi kutuhumiwa kwa uchafu. Hata kama hakufanya makosa, kule kutuhumiwa tu ni kubaya.
“Kwa bahati nzuri, namfahamu vizuri Makamba. Nafahamu kwamba ni miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakipokea pesa kutoka kwa Lowassa na Rostam. Sasa anapokuja hadharani na kuwatetea mimi sioni cha ajabu.
“Watu kama akina Makamba ndiyo wamelea ufisadi katika nchi hii. Ninaposema Makamba ni mlezi wa mafisadi sisemi kwa bahati mbaya bali kwa sababu nafahamu misaada wanayompa,” alisema Sitta.
Akizungumzia suala la kukamatwa kwa mafisadi, Sitta alisema lina ugumu kwa sababu, kwa tabia, mafisadi ni watu wajanja na wanaofanya mambo yao katika usiri mkubwa na wana mahusiano na watu walio katika mfumo.
Alisema kama Tanzania haitakuwa tayari kupambana na mfumo uliopo ambao unalea mafisadi na ufisadi, itakuwa ngumu kupambana na rushwa ambayo alisema ndiyo adui mkuu wa nchi kwa sasa.
Hii si mara ya kwanza kwa wanasiasa kuweka hadharani tuhuma kati yao, mara ya kwanza ilikuwa kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kudai Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amewahi kupewa fedha na Mbunge wa Musoma Vijijini Nimrod Mkono ili pamoja na mambo mengine, kumhujumu aliyekuwa mgombea wa CHADEMA Musoma Vijijini katika Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Kutokana na tuhuma hizo, Zitto naye alikuwa mkali akisema anatumaini Mkono pia amemwambia Lissu kwamba Mbowe naye aliwahi kuchota mabilioni kadhaa kutoka Mkono, licha ya Mkono kutambuliwa na chama hicho kuwa ni fisadi.
Katika majibu yake kuhusu tuhuma hizo, Mbowe ambaye ametishia kumshitaki Zitto, alisema kuchukua fedha kutoka kwa yeyote akiwamo Rais Jakaya Kikwete au CCM si tatizo bali tatizo ni nia iliyopo kuhusu fedha unazochukua.
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/sitta-awashitaki-lowassa-rostam#sthash.RN2om5ej.dpuf
No comments:
Post a Comment