Sunday, 1 February 2015

DAR ES SALAAM: ILALA, SEGEREA NA UKONGA – MBIVU NA MBICHI HIZI HAPA.

Na. Julius Mtatiro,Former CUF Deputy Secretary.
UTANGULIZI
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ipo kati ya Latitudo 6 na 7 kusini mwa Ikweta na kati ya Longitudo 39 na 40 Mashariki, ina eneo la kilomita za mraba 210 ambapo zaidi ya asilimia 75% ya eneo hilo ni eneo la mji. Manispaa hii imepakana na Manispaa za Kinondoni na Temeke kwa upande wa Kaskazini na Kusini, Mkoa wa Pwani kwa upande wa Magharibi na Bahari ya Hindi katika ukanda wa Pwani wenye urefu Kilomita 10 kwa upande wa Mashariki na hapa ndipo Ikulu ya Tanzania inapatikana.
Kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya iliyofanyika Agosti 2012, Ilala ina jumla ya wakazi wapatao 1,220,611, ambapo Wanaume ni 595,928 na wanawake ni 624,683
Manispaa ya Ilala ina Majimbo matatu (3) ya Uchaguzi ambayo ni Ilala lenye Kata 10, Ukonga lenye Kata 8, na Segerea lenye Kata 8.
Shughuli muhimu za kiuchumi katika Manispaa ya Ilala ni biashara, viwanda, kilimo na uvuvi pamoja na huduma za kiuchumi na kijamii. Pato la wastani la mkazi wa Manispaa ya Ilala ni sh.489, 204.00 kwa mwaka.

JIMBO LA ILALA
Kisiasa, jimbo hili limekuwa ngome ya Chama Cha Mapinduzi tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania. Katika chaguzi zote 1995, 2000, 2005 na 2010 – Ilala imeendelea kuipatia CCM ushindi mkubwa. Kwa ajili ya kuweka kumbukumbu vizuri tutaangalia chaguzi mbili zilizopita, ule wa mwaka 2005 na 2010. Katika Uchaguzi wa mwaka 2005 jumla ya vyama 11 viliweka wagombea ubunge kwenye jimbo la Ilala. Kati yao, ni wagombea wawili tu ndiyo walionesha ushindani. Wagombea tisa walipata jumla ya kura 2917 sawa na asilimia 5.9. Mgombea wa CUF wakati huo Omar Mnyanga Ahmad alipata kura 9,637 sawa na asilimia 19.6 na Azzan Zungu Mussa wa CCM aliibuka na ushindi mkubwa wa asilimia 74.5 uliotokana na kura 36,629.
Katika uchaguzi wa mwaka 2010, jimbo la Ilala lilishuhudia ukuaji wa upinzani. Mara hii idadi ya wapiga kura ilishuka na hata ushindi wa mbunge wa CCM aliyetetea kiti chake kwa mara ya pili ulikuwa mdogo. Vyama 11 viliweka wagombea ambapo CCM ikimsimamisha Azzan Zungu ilipata kura 25,940 sawa na asilimia 66.77 na CHADEMA ikaibuka katika nafasi ya pili ikiwa na kura 8,053 sawa na asilimia 20.73 huku CUF ikiwa nafasi ya tatu kwa kura 3,988 sawa na asilimia 10.27. Vyama vingine 8 vilipata jumla ya kura 472 sawa na asilimia 1.22. Uchaguzi huu ulishudia kuporomoka kwa ushindi wa Zungu kutoka asilimia 74.5 mwaka 2005 hadi 66.77 mwaka 2010.

Jimbo la Ilala linakabiliwa na tatizo kubwa la askari wa jiji kunyanyasa wamachinga, ukosefu wa miundombinu ya uhakika (barabara) na ukusanyaji kodi mkubwa ambao haulingani na maendeleo halisi wanayopata wananchi. Hata hivyo, kukosekana kwa mtandao wa uhakika wa vyama vya upinzani katika jimbo hili, ukaribu wa mbunge wa Ilala kwa vijana wa mjini, vyama vya wapinzani kutokujua wapiga kura halisi wa Ilala (Wengi wanafanya kazi na biashara Kariakoo na Ilala huku wakiishi nje ya jimbo hilo) huku CCM ikijua wapi itawapata wapiga kura hao, na kukosekana kwa mpinzani wa uhakika mwenye uzoefu na jimbo hilo – ni sababu ambazo zina faida kubwa kwa CCM. CCM wanataraji kumrudisha Azzan Zungu na hivyo jimbo la Ilala linaweza kuchukuliwa tena na CCM walau kwa ushindi wa asilimia 50 – 55, japokuwa akitokea mshindani imara kutoka vyama vya UKAWA atapunguza ushindi wa CCM kwa kiasi kikubwa.
JIMBO LA SEGEREA
Segerea imekuwa sehemu ya jimbo la Ukonga tangu uchaguzi Mkuu wa Mwaka 1995. Dr.Militon Makongoro Mahanga amekuwa mbunge wa jimbo la Ukonga (Segerea ikiwamo) kutokea mwaka 2000 hadi 2010. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilipotangaza kugawa baadhi ya majimbo kabla ya uchaguzi wa mwaka 2010, jimbo la Ukonga liligawanywa mara mbili na kuzaa jimbo la Segerea.
Katika Uchaguzi wa Mwaka 2005 ambao Segerea ilikuwa sehemu ya jimbo la Ukonga, Makongoro Mahanga wa CCM alipata kura 126,955 sawa na asilimia 62.7 ya kura zote za jimbo la Ukonga la wakati huo (likijumuisha Segerea), alifuatiwa na Bethuel Pori Heko wa CUF aliyepata kura 51,519 sawa na asilimia 25.4 na wa tatu alikuwa Jacob Chacha Florence wa CHADEMA aliyepata kura 12,297 sawa na asilimia 3.8. Wagombea wengine 12 waliotokana na vyama 12 ambavyo havijatajwa hapa – walipata jumla ya kura 11,833 sawa na asilimia 5.9 ya kura zote. Jumla ya vyama 15 vilisimamisha wagombea.
Mwaka 2010 wakati jimbo la Ukonga lilipogawanywa na Segerea kuzaliwa, Makongoro Mahanga wa CCM alikuja kugombea Segerea na alishinda kura za maoni ndani ya chama chake, safari hii ikionekana angekuwa na kazi nyepesi kwa sababu jimbo la Segerea lina kata chache tu. Uchaguzi wa mwaka 2010 ulikuwa mgumu sana kwa Makongoro Mahanga na CCM.
Matokeo ya mwisho yaliyotangazwa yanaonesha alijipatia ushindi mwembamba mno wa asilimia 41.7 dhidi ya asilimia 37.49 za CHADEMA na asilimia 17.94 za CUF. Asilimia hizo zilitokana na kura 43,554 za CCM, kura 39,150 za CHADEMA na kura 18,737 za CUF, ambapo CCM ilimsimamisha Makongoro Mahanga, CHADEMA ikamuweka Fred Tungu Mpendazoe na CUF ikimsimamisha Kimangale Ayoub Musa.
Ndio kusema, kama UKAWA ingekuwepo mwaka 2010, kura za CHADEMA na CUF zingetosha kuipa UKAWA ushindi wa asilimia 55.94 na kuipita CCM kwa asilimia 14.24. Hivyo, jimbo la Segerea kwa mwaka huu 2015 lina kila sababu ya kwenda chini ya vyama vya UKAWA ikiwa vitasimamisha mgombea mmoja na awe mtu anayefahamika kama ilivyokuwa kwa Mpendazoe mwaka 2010. Japokuwa taarifa zilizopo ni kuwa, Bwana Mpendazoe hatagombea tena katika uchaguzi wa mwaka huu 2015.
Dr. Militoni Makongoro Mahanga bado anaweza kurejeshwa na CCM kwa sababu ya uzoefu wake na hata mtandao wake ndani ya CCM, lakini ikiwa atasimama tena au ataletwa mgombea mpya, jambo hili halitakuwa kitisho kikubwa kwa UKAWA ikiwa wataweka mtu anayeuzika. Kwa kifupi, jimbo la Segerea ni kati ya maeneo ambayo CCM ina wakati mgumu sana kutokana na kuchokwa kwa chama chenyewe na hata Mgombea waliyenaye, sababu kuu zikiwa kushindwa kukidhi haja ya maendeleo ya wananchi kama ambayo walitegemea.
JIMBO LA UKONGA
Hili ndilo jimbo mama ambalo taarifa zake zimeelezewa katika sehemu ya uchambuzi wa jimbo la Segerea, kwa sababu miaka ya 2000 – 2010 jimbo hili liliijumuisha Segerea kama sehemu yake kabla ya kugawanywa na Segerea kujitenda. Kwa sababu hiyo, Uchambuzi juu ya jimbo la Ukonga utaanzia mwaka 2010 kwa kuzingatia kuwa miaka ya nyuma imekwishaelezwa.
Katika uchaguzi wa Mwaka 2010 baada ya Makongoro Mahanga kugombea Segerea, jimbo mama la Ukonga lilibaki peke yake na hivyo kufanya uchaguzi Mkuu kama lilivyo (bila kuhusisha Segerea). Jumla ya vyama 12 viliweka wagombea katika jimbo hili na mvutano mkubwa ulijitokeza kati ya CCM na CHADEMA ambapo mgombea mpya wa CCM Eugen Mwaiposa Elishiringa alijizolea kura 28,000 sawa na asilimia 53.07 ya kura zote huku Binagi James Chacha wa CHADEMA akipata kura 17,059 sawa na asilimia 32.34 ya kura zilizopigwa. Mgombea wa CUF Heko Bethuel Pori alijipatia kura 5,220 sawa na asilimia 9.89. Wagombea wengine kutoka vyama 9 walipata jumla ya kura 1,470 sawa na asilimia 2.8 ya kura zote.
Joto la siasa katika jimbo hili limekwishapanda sana kwa sababu Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa analihitaji jimbo hilo kwa udi na uvumba. Pamoja na kutofanya vizuri katika nafasi yake ya umeya ukizingatia kuwa Ilala imeendelea kuwa na matatizo makubwa ya wazi yasiyotatulika (Mfano: Masoko kuwa machafu kupita kiasi huku makampuni ya ushuru yanachukua mabilioni ya pess kinyemela), bado Silaa ambaye ana nafasi kubwa ya kupitishwa na CCM – atakuwa karata muhimu sana kwao.
Vyama vya UKAWA ili kulipata jimbo la Ukonga vitapaswa kupata mgombea kijana (Chini ya Miaka 40) mwenye sifa na mvuto kuliko Jerru Silaa na tena awe mtu mwenye uzoefu na umaarufu wa kutosha kupambana na Silaa wa CCM. Jimbo la Ukonga litakuwa gumu kwa pande zote UKAWA na CCM na upande wowote ambao utajipanga kimkakati, atalichukua.
Tukutane jumamosi ijayo kwa majimbo ya Temeke na Kigamboni.
(Mwandishi ana uzoefu mkubwa wa masuala ya uongozi wa kisiasa ndani ya Tanzania. Ana shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na hivi sasa ni mwanafunzi wa fani ya sheria (L LB) – 0787536759, juliusmtatiro@yahoo.com).

No comments: