Sunday, 1 February 2015

Pinda Hafai kuwa Rais wa Tanzania

Pinda

MIZENGO Pinda, waziri mkuu wa Jamhuri, hafai urais. Hapaswi kufikiriwa kuwa miongoni mwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaoweza kupendekezwa kuingia katika kinyang’anyiro hicho.
Kinachomuondoa Pinda katika mbio za kusaka urais, ni kauli zake za kibabe dhidi ya wananchi; kushindwa kusimamia serikali na lundo la kashfa linalomkabili. Waziri mmoja mwandamizi serikalini amesema, “ni hatari kwa taifa hili kukabidhiwa mwanasiasa anaina ya Mizengo Pinda.” Amesema, “Tumefika hapa kwa sababu ya udhaifu wa Pinda. Huyu bwana ameshindwa kusimamia serikali. Ni dhaifu anayetaka kuvitumia vyombo vya dola kulinda utawala wake.”

Akiongea kwa uchungu, waziri huyu amesema, “Tangu amekuwa waziri mkuu Pinda ameponyoka katika kashfa karibu nne huku walio chini yake wakitakiwa kujiuzulu.”Kashfa ambazo Pinda amenyoka, huku mawaziri wake wakiangamizwa kisiasa, ni pamoa na ukwapuaji mabilioni ya shilingi katika Akaunti ya Escrow na operesheni tokomeza.Pinda ndiye aliyeagiza jeshi la polisi kupiga raia kwa kile alichoita, “serikali imechoka kuvumilia.” Kauli ya Pinda ni kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayopiga marufuku katika Ibara ya 12 kwa mtu yeyote kuteswa ama kuadhibiwa kinyama na kumpa adhabu, ambazo zinamtesa mtu na kumdhalilisha.


Pinda aliliambia Bunge mjini Dodoma 20 Juni 2013, “…umeambiwa usifanye hiki, wewe ukaamua kukaidi, utapigwa tu.” Alikuwa akijibu swali la mmoja wa wabunge aliyetaka kujua “vitendo vya vyombo vya dola kupiga raia mkoani Mtwara.” Alisema, “Ukifanya fujo, utapigwa tu. Maana hakuna namna nyingine. Maana lazima wote tukubaliane kwamba, nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria.” Alisema, “Sasa kama wewe umekaidi, hutaki, unaona kwamba ni imara zaidi, wewe ndiyo jeuri zaidi, watakupiga tu. Na mimi nasema muwapige tu. kwa sababu hakuna namna nyingine. Maana tumechoka sasa.” Kuibuka kwa waziri huyo mwandamizi kudai Pinda amepoteza sifa ya kuwa rais; na kumtuhumu kuvitumia vyombo vya dola kulinda udhaifu wa serikali, kumekuja wiki moja tangu jeshi la polisi kumshambulia na kumdhalilisha mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba.

Prof. Lipumba alidhalilishwa wakati akielekea eneo la Zakhem, Mbagala, kuhutubia mkutano wa hadhara uliolenga kuwakumbuka mamia ya wafuasi na wanachama wa chama hicho, waliouawa na polisi Januari 26 na 27 mwaka 2001.“Kama mtu amechoka kuongoza, huomba kupumzika. Kutumia vyombo vya dola kulinda udhaifu wako, ni kutaka kuingiza nchi katika machafuko. Hakukubariki,” ameeleza waziri huyo ambaye ameomba kutotajwa jina lake. Pinda anatajwa kuwa miongoni mwa wanachama wa CCM walioamua kutafuta urais kufa au kupona. Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema, Pinda siyo kwamba hakuhusika na kashifa ya Escrow, bali aliondolewa kutokana na kuwapo maridhiano.

“Wabunge wa CCM waliapa kutounga mkono mapendekezo ya Bunge. Waliweka sharti la kuondolewa Pinda. Walifanya hivyo ili kulinda serikali na Jakaya Rais Kikwete,” ameeleza Lissu.Taarifa zinasema, wabunge hao wakiongozwa na Anne Kilango Malecela, walidai kuwa hawatapenda kumuona Rais Kikwete anakuwa na mawaziri wakuu watatu katika utawala wake wa miaka 10.“Katika makubaliano hayo, ndipo unaona hata katibu mkuu kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, naye anatolewa. Tuna ushahidi kwamba huyu bwana ndiye alikuwa anashinikiza fedha za Escrow kulipwa. Lakini tumeshindwa kumwajibisha kwa sababu ya tabia ya kulindana ya CCM,” ameeleza Lissu.

No comments: