Friday 24 April 2015

DR. ASHA ROSE MIGIRO: NANI NI NANI URAIS CCM?


Kwa sababu nchi yetu inaelekea katika uchaguzi mkuu niliona panapaswa kuwa na utafiti wa kuchokoza mada juu ya watu wanaojipanga kugombea urais na wale wanaotajwa. Uchambuzi huu unapaswa kuwa chachu tu ya kuanzisha mjadala juu ya "watarajiwa mbalimbali". Yanayosemwa na uchambuzi huu ni sehemu ndogo tu ya mazuri na mabaya ya watarajiwa wetu, haya yatusaidie kuchokoza na sasa tumjadili mama yetu DR. ASHA ROSE MIGIRO. Tukimaliza watarajiwa kutoka CCM ambao ni zaidi ya 20 tutageukia kwa wale wa vyama vya upinzani kwa utaratibu huu huu.
HISTORIA YAKE: ASHA ROSE MIGIRO
Dk Asha Rose Migiro alizaliwa Julai 9, 1956 katika Wilaya ya Songea, Mkoa wa Ruvuma. Migiro alianza masomo katika Shule ya Msingi Mnazi Mmoja, Dar es Salaam mwaka 1963 hadi mwaka 1966. Akahamia Shule ya Msingi Korogwe, Tanga na kuendelea na elimu ya msingi mwaka 1967–1969.
Baadaye akajiunga kidato cha kwanza mpaka cha nne katika Shule ya Sekondari Weruweru mkoani Kilimanjaro mwaka 1970 mpaka 1973 na kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Korogwe mwaka 1974 -1975.
Migiro alikuwa mmoja wa wasichana waliofaulu vizuri Korogwe Sekondari na alipojiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1977 alichukua masomo ya sheria ambako alitunukiwa shahada yake (LLB) mwaka 1980.
Baada ya kukamilisha shahada yake ya kwanza, aliajiriwa UDSM kufundisha masomo ya sheria kama Mhadhiri Msaidizi. Alifanya kazi hiyo kwa miaka miwili kabla ya kuendelea tena na masomo ya juu ya sheria mwaka 1982–1984 hapohapo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na akatunukiwa shahada ya uzamili (LLM).
Kati ya mwaka 1985–1988, alifundisha UDSM. Mwaka 1988 alikwenda Chuo Kikuu cha Konstanz, Ujerumani ambako alisoma na kutunukiwa shahada ya uzamivu (PhD) katika masuala ya sheria mwaka 1992. Dk Migiro alirejea Tanzania akiwa Mhadhiri Mwandamizi na aliendelea kufundisha katika Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi mwaka 2000 alipoingia kwenye siasa.
Dk Migiro, akiwa UDSM kati ya mwaka 1992 – 1994 alikuwa Mkuu wa Idara ya Sheria za Katiba na Utawala. Kati ya mwaka 1994 – 1997 aliongoza Idara ya Sheria za Makosa ya Jinai (Idara zote zipo katika Kitivo cha Sheria UDSM). Anaongea vizuri Kiingereza, Kifaransa na Kijerumani na ni mke wa Profesa Cleophas Migiro na wana watoto wawili wa kike.

MBIO ZA UBUNGE
Tofauti na wanasiasa wengi ambao hufikia ngazi za juu za uongozi wa nchi kuanzia siasa katika nyadhifa za vyama vyao, Dk Migiro amekuwa na historia tofauti kidogo. Yeye ameanza siasa za kujijenga akitokea katika taaluma, akitazamwa na watu wengine kuwa ana uwezo wa kulisaidia taifa. Hata hivyo, tofauti na wanasiasa wengi ambao hupaswa kujisukuma wenyewe, yeye tunasema ‘alisukumwa.’
Mwaka 2000, ‘alisukumwa’ na Rais Benjamin Mkapa na baadaye akateuliwa kuwa waziri kwenye Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto. Alitumikia wadhifa huo hadi mwaka 2005 bila kubadilishwa akisimamia mambo mengi ya kisera na kimiundombinu, bila kusahau utekelezaji na upiganiaji wa haki za wanawake na watoto.
Wanasiasa wengi wanapoteuliwa kuingia bungeni kipindi kimoja, kijacho utawaona wakipambana majimboni ili kujiimarisha na kutosubiri kuteuliwa, kwa Migiro ilikuwa tofauti sana, hakwenda kuchukua jimbo la mtu na hivyo hakuwa mgombea.
Rais Jakaya Kikwete alipoingia madarakani mwaka 2005, alimteua Dk Migiro kuwa mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje, Januari 2006 na kuwa mwanamke wa kwanza kuwahi kushikilia wadhifa huo. Katika kipindi cha mwaka mmoja tu, alifanya kazi nyingi za kimataifa zilizomweka katika anga nyingine kisiasa.
Ilipotimu Januari 5, 2007, aliweka rekodi nyingine kubwa kimataifa; aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, akiwa mwanamke wa pili kushika wadhifa huo baada ya Louise Fréchette, mwanadiplomasia wa Canada aliyeongoza kuanzia Aprili 1997 hadi Aprili 2006. Migiro alichukua nafasi iliyoachwa na George Mark Malloch Brown wa Uingereza aliyeongoza kuanzia Aprili 2006 hadi Desemba 2006.
Migiro alishikilia wadhifa huo kwa miaka mitano, akifanya kazi kubwa kimataifa hadi Julai 2012 alipopumzishwa na nafasi yake kuchukuliwa na mwanadiplomasia wa Sweden, Jan Elliason.
Wakati anateuliwa kushikilia nafasi hii ya kimataifa, Ban Ki-moon alimtaja kama “….kiongozi anayeheshimika ambaye ameongoza maendeleo ya nchi masikini kwa miaka kadhaa kupitia huduma yake iliyotukuka na ameonyesha ujuzi wa usimamizi wa kipekee na uzoefu wa kutosha kwenye masuala ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi…”
Januari mwaka 2013, Dk Migiro aliteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Desemba 2013 aliteuliwa kuwa mbunge katika Bunge la Tanzania. Mwezi mmoja baadaye yaani Januari 2014 aliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria na Katiba, nafasi ambayo anatarajiwa kuendelea nayo hadi Oktoba mwaka huu.
MBIO ZA URAIS
Dk Migiro hakuwahi kutamka hadharani kuwa atagombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ila amekuwa akipigiwa chapuo sana.
Alipotua uwanja wa ndege mwaka 2012 akitokea Marekani, baada ya ‘kustaafu’ nafasi ya juu ya UN, waandishi wa habari walimuuliza kama atagombea urais naye aliwajibu; “….Hivi sasa tunajua Tanzania inaongozwa na Rais Kikwete… hakuna tena mtu mwingine, hivyo si vizuri kusema ninahitaji kugombea nafasi hiyo wakati muda bado, tuwe na subira”.
Wachambuzi wengi wanamweka Migiro kwenye orodha ya wateule ndani ya CCM kwa sababu ya haiba yake ambayo huenda wanasiasa wengi wakongwe ndani ya chama hicho hawajaifikia. Uzoefu wake kitaifa na kimataifa, taaluma na utulivu wake vinafanya aonekane kuwa anaweza kuteuliwa.
NGUVU YAKE
Dk Migiro ni zaidi ya mwanamke. Kwanza, ni msomi mahiri ambaye wanaume wengi wanakubali juhudi zake katika nyanja muhimu kwenye dunia ya sasa. Katika dunia ya sasa, ukiwa mwanamke, tena msomi unakuwa na nafasi ya kipekee ya kufanikiwa na kuungwa mkono kwa sababu ya dhana kwamba wanawake wanapaswa kupewa nafasi. Jambo hili linambeba Migiro.
Pili, ni mtu wa watu, tena wa kawaida sana. Ukiongea na wanafunzi aliowafundisha UDSM katika kipindi kirefu kilichopita, wanakueleza namna mama huyu alivyo na roho ya uwajibikaji na huruma. Mambo haya yanamfanya awe tofauti na wanasiasa wengi ambao hujawa kiburi na dharau baada ya kupewa nyadhifa fulani kubwa.
Uzoefu wake si jambo la kuchezea. Ni Watanzania wachache sana na wanasiasa wa kuhesabu nchini ambao wana uzoefu alionao. Ni mwana taaluma nguli akiwa amefanya tafiti juu ya masuala mengi, wakati huohuo akiwa na uzoefu wa masuala ya kibunge kwa miaka takribani minane; amekuwa na uzoefu wa utendaji wa serikali akishikilia dhamana kubwa kwa karibu muongo mmoja; na zaidi ya yote ameshikia nafasi ya pili kimamlaka katika chombo kinachoendesha dunia – UN. Huyu ni moto wa kuotea mbali kwani sifa hizi zinambeba kwa namna yoyote ile.
UDHAIFU WAKE
Migiro ni mpole sana. Kuna wanawake wengi sana katika siasa za Tanzania ambao wana “roho ya kike” lakini yanapokuja masuala magumu hubadilika na kuvaa “roho ya kiume” na kupambana nayo. Migiro hana kaliba hiyo. Tanzania ilipo hivi sasa inahitaji rais anayeweza kuwa mkali kila itakapohitajika na awe rafiki sana wa watu wakati itakapoonekana ni muhimu kufanya hivyo.
Jambo la pili linaloweza kumhukumu ni utendaji wake UN. Gazeti la “New York Times” la Marekani liliwahi kuandika kwamba UN ilihitaji kuteua mwanamke katika nafasi ile aliyoshikilia kwa miaka mitano, inawezekana kuwa alitafutwa mwanamke kwa sababu ya jinsia lakini si kwa maana ya sifa.
Baadhi ya duru zinaonyesha kuwa Migiro alishindwa kupambana na kasi ya majukumu ya UN, yakiwamo masuala ya kufanya uamuzi wa haraka na kuusimamia, lakini pia kuongoza majopo ya wataalamu wanaofanya tafiti wasioweza kuendeshwa kwa ubabaishaji. Mtandao wa Vox Media unaripoti kwamba “…vyanzo ndani ya UN vilieleza kuwa, utendaji wake usioridhisha na kushindwa kuendana na mazingira yenye mtanzuko na magumu ndivyo viliifanya UN isimwongezee mkataba mwingine”.
Mtandao huo unaendelea kusisitiza kuwa hata wakati anapewa nafasi hiyo muhimu na UN ilitokana na sababu za ukaribu wa Kikwete na Ban Ki-moon, ambao wamewahi kufanya kazi wote kwenye wizara za mambo ya nje za nchi zao.
Vox Media imeendelea kueleza kuwa Migiro hakuwahi kuwa mwanadiplomasia maarufu na alishindwa kumsaidia Ban Ki-moon kwa sababu hakuwa anasikilizwa, hasa ikizingatiwa kwamba hata uteuzi wake ulipingwa na baadhi ya wanadiplomasia mashuhuri.
Udhaifu mwingine mkubwa wa Migiro ni kusubiri atafuniwe mambo kila mara. Tatizo lililo dhahiri kwake katika mbio hizi za urais ni hiyo tabia yake ya kusubiri aambiwe na chama chake “anza harakati, chukua fomu n.k”. Anataka aendelee kubebwa kama ilivyokuwa katika nafasi zote alizoshikilia kisiasa – “kupewa”.
Pengine, alipaswa kujifunza kuwa yeye ni mwanamke wa mfano katika nchi. Alipaswa kusimama kidete na jamii imjue kuwa yu “mwanamke wa shoka”; uthubutu wa namna hiyo ungempa ujasiri wa kusimama hata katika jimbo fulani muhimu na kuwaangusha wanaume au wanawake wenzake. Migiro huyu angeweza kupanda ngazi na kuaminiwa zaidi kuliko ilivyo sasa, “kuaminiwa kwa kubebwa”.
NINI KINAWEZA KUMFANYA APITISHWE
Dhana ya kuwapa wanawake nafasi inaweza kuwa sababu kuu ya kupenya kwa Migiro kwenye chekecheo la CCM. Tukumbuke kuwa huu ni wakati wa wanawake kuachiwa nafasi ambazo zimeshikiliwa na wanaume kwa karne nenda rudi. Hii ni karata muhimu kwake.
Jambo jingine linaloweza kumvusha ni uzoefu wake wa taaluma na uongozi wa juu wa CCM. Amewahi kuongoza idara ya mambo ya nje ya chama chake na ukiachilia mbali uwaziri, taaluma yake na uzoefu wa mambo vinambeba kufikiriwa kwenye kikaango.
Kwa upande mwingine Migiro ni mwanamke anayependa kujiendeleza. Kitendo cha kutoka katika familia ya kawaida na kusoma hadi chuo kikuu na kuwa daktari katika miongo kadhaa iliyopita si jambo dogo.
Ni mwanamke anayeonekana kujiamini na anaweza kupigania ndoto zake hadi zikamilike.
Lakini, kama CCM inatafuta wagombea wasio na makundi na wanaoweza kuunganisha chama kwa dhana hiyo, Migiro ni mmoja wao.
Kutotumia muda kujijenga kumemfanya asiwe na makundi ndani ya chama chake na hiyo ni faida kwake kwani anafanyiwa tathmini kama mgombea “neutral”.
Pamoja na kuwa na miaka 59, Migiro anaonekana kuwa mtu wa kizazi cha sasa kwa maana ya mitizamo yake, tabia zake na hata marafiki zake. Nakumbuka wakati tuko Bunge la Katiba, ‘angenifuata na kusalimiana nami kwa sababu ananisikia na kuniona kwenye siasa, angeniuliza mambo mawili matatu na kucheka, tungegonga mikono kisha akaenda zake.’ Huyu ndiye Migiro na anaweza kabisa kuvaa viatu na mawazo ya vijana.
NINI KINAWEZA KUMWANGUSHA
Jambo la kwanza linaloweza kumwangusha katika safari ya kuusaka ukuu wa nchi ni hofu za kijinsia. Vyama vyote vikubwa vya siasa hapa nchini bado havijawaamini sana wanawake.
Ukiangalia hata kwenye nafasi za uongozi wa juu wa vyama, ni Chama Cha Wananchi (CUF) na NCCR Mageuzi tu, labda na sasa ACT Wazalendo, ndivyo vimethubutu kuwapa wanawake nafasi moja miongoni mwa nafasi tano za juu. Ndani ya CCM ndiyo kabisa, kwa sasa si rahisi mwanamke akapewa hata ukatibu mkuu wa chama, achilia mbali fursa ya kugombea urais. Mwaka 1995 alijitokeza Rose Lugendo, lakini jina lake lilikatwa mapema.
Pia, CCM ina hofu sana na vyama vya upinzani hususan Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na ikipiga hesabu inaona watangaza nia za urais walio tishio ndani ya Ukawa, wote ni wanaume, kwa hiyo ikimleta mwanamke anaweza kushindwa uchaguzi wa kitaifa kabla ya kura kupigwa kwa kuzingatia kuwa mitazamo ya Watanzania wengi bado “inamhukumu mwanamke” na haijamwamini sana kushikilia nafasi muhimu zaidi za maamuzi ya nchi.
Jambo la pili linaloweza kumwangusha ni kuwa na ushawishi mdogo kwa makundi ndani ya CCM. Pamoja na kuonekana kama mtu asiye na makundi, lakini haonekani kama anaweza kuyaunganisha makundi yaliyojijenga na kujengeka na kusaka urais kwa uhasama.
Kama atapitishwa CCM inahofia jambo hilo na linaweza kuchukuliwa kama kitisho kwa chama na majibu yanaweza kuwa ni kumtosa.
ASIPOPITISHWA (MPANGO B)
Migiro hajaonyesha nia ya kugombea ndani ya CCM, lakini ni ukweli ulio wazi kuwa yeye ni mmoja wa wanawake wachache na wanaoheshimika ndani ya CCM. Moja ya mipango yake inaweza ikawa ni kusubiri nafasi ya uteuzi na labda kupewa nafasi ya uwaziri tena ikiwa chama chake kitashinda.
Mpango mwingine unaoweza kumfanya atoe mchango wake kwenye jamii ya kimataifa ni kujihusisha na mambo ya kimataifa na usuluhishi wa migogoro mbalimbali hasa barani Afrika. Atatumia uzoefu wake wa UN na ule wa kuongoza wizara ya mambo ya nje kutimiza wajibu huu. Jambo jingine analoweza kufanya ni kufundisha vyuo vikuu. Tanzania hivi sasa ina vyuo binafsi lukuki na havina walimu madhubuti hasa kwa fani kama sheria. Migiro anaweza kurudi darasani na akapumzika mbio za huku na kule ili kuzalisha vijana watakaolisaidia taifa letu.
HITIMISHO
Dk Migiro amefanya mambo mengi yanayoweza kumfanya awe mwarobaini ndani ya CCM, lakini hajajijenga ndani ya chama na amezungukwa na mazingira ya kuwa katika chama ambacho bado hakiwaamini wanawake katika wadhifa mkubwa kama “kugombea urais”, achilia mbali hata “ukatibu mkuu” wa chama. Itampasa kusubiri maamuzi magumu sana ya chama chake kuona kama ndoto anayootewa ya urais inaweza kutimia.
Hata hivyo, uzoefu katika mambo mengi ya kitaifa na kimataifa, usomi uliotukuka na ubobezi wa hali ya juu ukichanganya na utulivu wake katika kufanya maamuzi vinamweka katika orodha ya watu muhimu. Namtakia kila la heri katika safari yake.
KUHUSU MCHAMBUZI:
Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, ana uzoefu mkubwa wa uongozi wa kisiasa hapa Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi na Lugha, Shahada ya Sanaa “B.A” katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (L LB) – Anapatikana kupitia +255787536759,(juliusmtatiro@y ahoo.com) Uchambuzi na huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi). (Uchambuzi huu umechapishwa na Gazeti la Mwanchi la Jumatatu, 20 Aprili 2015).

No comments: