Wednesday, 15 April 2015

TANZANIA KUFUNGUA UBALOZI KUWAIT

Mazungumzo ya ushirikiano yakiendelea

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kufungua Ubalozi nchini Kuwait kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha wa 2014/2015. 
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) alipokutana na Mtukufu Sheikh Sabah Al-Khalid Al-Sabah, Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait nchini Kuwait siku ya Jumanne tarehe 14 Aprili, 2015. Katika mazungumzo yao viongozi hao wawili walisifu ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili ambao ni wa kidugu na unalenga kuwanufaisha wananchi wa nchi hizi.

“Kwa kufungua ofisi za Ubalozi, Kuwait ushirikiano huu wa kidugu utaongezeka kwenye nyanja zote muhimu na utazaa matunda yatakayo wanufaisha watu wetu, kwa nchi hizi mbili” alisisitiza Waziri Membe katika mazungumzo yake na kiongozi huyo.Kwa upande wa Kuwait, Serikali yao ilifungua ubalozi nchini Tanzania Februari 2015 na Mhe. Jassem Ibrahim Al Najem kuwa Balozi wake wa kwanza nchini Tanzania, mwenye makazi yake Jijini Dar es salaam.Aidha, kwa sasa Tanzania inawakilishwa nchini Kuwait kupitia Ubalozi wake uliopo Riyadh, Saudi Arabia.Katika mkutano huo, Mtukufu Sabah Al-Khalid Al Sabah alisifu jitihada za Tanzania kwenye kulinda na kuleta amani Barani Afrika hasusan kwenye maeneo yenye migogoro. Alisema kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania sio tu kwenye maeneo muhimu ya maendeleo lakini pia hata kwenye ulinzi wa amani kwani ndio changamoto kubwa inayoikabili dunia kwa sasa. Kuhusu misaada Barani Afrika, viongozi hao walijadili suala la uratibu wa misaada mbalimbali ya Serikali ya Kuwait Barani humo ambapo waliangalia uwezekano wa kuanzisha kituo maalum nchini Tanzania kwa ajili ya kusimamia shughuli za uratibu wa misaada hiyo.

Kwa sasa Serikali ya Kuwait kupitia Mfuko wake wa Maendeleo – Kuwait Fund- imetoa Dola za Kimarekani Bilioni moja kwenye Umoja wa Afrika kwa ajili ya usalama wa chakula Barani Afrika.Awali Waziri Membe alikutana na Mhe. Abdulwahab A. Al-Bader, Mkurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait na kumshukuru kwa misaada mbalimbali ya kimaendeleo wanayoendelea kuitoa nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla.Aidha Waziri Membe alielezea kuwa maandalizi ya miradi mitano ya umwagiliaji nchini Tanzania ambayo inayofadhiliwa na mfuko huo yamekamilika, na kwamba sasa iko tayari kuanza. Aidha Waziri Membe na Mhe. Al-Bader walizungumzia uwezekano wa mfuko huo kuikopesha Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) ili iweze kuendesha shughuli zake kikamilifu.

Waziri Membe yuko nchini Kuwait kwa ziara ya siku moja na anatarajiwa kuondoka kesho kuelekea nchini Oman. Ujumbe wa Mhe. Membe nchini Kuwait unamjumuisha Bw. Peter Noni, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Uwekezaji Tanzania, Balozi Simba Yahya, Mkuregenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Bi. Mindi Kasiga, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje.

-Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es Salaam

15 Aprili 2015

No comments: