Saturday 8 October 2016

JAJI MUTUNGI, AFUKUZWE KAZI, ASHITAKIWE!

Image result for Jaji Mutungi Pictures

Inashangaza na kusikitisha sana. Juzi Alhamisi tarehe 06 Oktoba 2016 Mwenyekiti wa CUF kwa tiketi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Prof. Lipumba aliripoti benki ya NMB katika tawi la Ilala na kuwasilisha nyaraka mbalimbali ili afunguliwe akaunti ya NMB yenye jina la THE CIVIC UNITED FRONT ili Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ianze kumpa ruzuku ya chama hicho katika juhudi za serikali kuivuruga CUF, UKAWA na harakati za kudai haki zilizoporwa Zanzibar.

Mshangao mkubwa ambao wafanyakazi mbalimbali wa benki ya NMB tawi la Ilala waliupata ni pale walipogundua kuwa nyaraka ambatanishi inayompa Lipumba nguvu ya kufungua akaunti hiyo ni Barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwenda kwa Meneja wa NMB tawi la Ilala (nakala ya barua hiyo tunayo). Barua hiyo ya Msajili wa Vyama kwenda NMB inamtambulisha Lipumba kama Mwenyekiti halali wa The Civic United Front (CUF) na kisha inamtaka meneja wa NMB amfungulie akaunti ya NMB yenye jina la THE CIVIC UNITED FRONT (CUF).

Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa Sura 258 (The Political Parties Act No. 5 of 1992) kwenye kifungu cha 15 (1), kila chama cha siasa kupitia BODI YAKE YA WADHAMINI kinapaswa kumiliki akaunti ya Benki na pesa zote zinazoingia katika chama kwa mujibu wa kifungu cha 13 cha sheria hiyo zinapaswa kuingizwa katika akaunti hiyo. Hili ni takwa la lazima la kisheria na si hiyari, yaani Bodi ya Wadhamini lazima ikae katika kikao na kuidhinisha ufunguaji wa akaunti yoyote ile na kisha kuandaa azimio/muhtasari ambao utapelekwa kwa Benki iliyochaguliwa. Muhtasari huo husainiwa na Katibu na Mwenyekiti wa Bodi ya chama husika pamoja na kuelekeza ni kina nani watakuwa watia saini wa akaunti hiyo n.k.

Cha kushangaza zaidi, maombi ya Lipumba kwa benki ya NMB yameambatanishwa na Barua ya Msajili na Muhtasari ulioambatanishwa kwenye Barua hiyo ni wa kughushi na haukusainiwa na Bodi ya Wadhamini ya CUF ambayo imesajiliwa RITA ikiongozwa na Ndugu. Abdallah Said Khatau – Mwenyekiti (Masasi), Ndugu. Ali Mbarouk Suleiman – Makamu Mwenyekiti (Zanzibar).

Nimesoma Katiba ya CUF ya mwaka 1992 toleo la 2014 katika kifungu cha 98 (1 – 6) na kujiridhisha kuwa Bodi ya Wadhamini ya CUF huteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama hicho ambalo halimuungi mkono Lipumba. Nimebaki na maswali, NMB watamfungulia Lipumba akaunti ya benki kwa kutumia maelekezo ya Msajili wa Vyama? Tokea lini Msajili wa Vyama akaiagiza benki fulani imfungulie aakaunti ya benki kiongozi wa chama cha siasa kwa kutumia jina la chama hicho? Je, NMB itamfungulia Lipumba akaunti ya benki bila kuwa na muhtasari wa bodi halali ya wadhamini ya CUF ambayo inaongozwa na Ndugu. Katau wa Tanzania Bara na ndugu. Mbarouk wa Zanzibar?


Kifungu cha 15 (2) cha Sheria ya Vyama vya Siasa Sura 258 (The Political Parties Act No. 5 of 1992) kinaeleza kuwa “Stahili zozote (fedha) zinazotoka serikalini kwenda kwa chama cha siasa, hazitalipwa ikiwa chama husika hakina akaunti ya benki inayozingatia masharti ya kifungu cha 15 (1)”. Kifungu hiki cha 15 (2) kina maana kuwa, Msajili wa vyama vya siasa anapigwa marufuku kuweka fedha za serikali katika akaunti ya chama cha siasa ambayo imefunguliwa bila kufuata masharti ya kifungu cha 15 (1) ambayo yanalazimisha kwamba ni lazima Bodi ya Wadhamini ya Chama ndiyo iidhinishe ufunguaji wa akaunti ya chama husika.

Nimekaa na kujiuliza maswali zaidi, Je, Jaji Mutungi anaweza kuidhinisha Lipumba awekewe fedha za ruzuku za CUF katika akaunti mpya ya NMB ambayo imefunguliwa bila kufuata matakwa ya sheria ya kifungu cha 15 (1) cha Sheria ya vyama vya siasa? Hivi huyu Jaji Mutungi ni Jaji wa Mahakama Kuu? Au ni Majanga? Kwa nini anayafanya yote haya na bila aibu kwa kukishughulikia chama kikubwa kama CUF na kwa kuvunja sheria huku akijiamini namna hii? Je, Jaji Mutungi ana maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu, John Pombe Magufuli kwamba aivuruge CUF hadi isambaratike kabisa? Na kama Magufuli hamtumi kwa nini anamuangalia akifanya upuuzi wa kiwango hiki?


Nimeendelea kuisoma katiba ya CUF katika kifungu cha 93(1) (i) na kugundua kuwa Katibu Mkuu wa CUF ndiye muwajibikaji wa mambo yote ya fedha na mali za Chama katika ngazi ya Taifa (Chief Acounting Officer) na hiyo peke yake (kwa mujibu wa Katiba ya CUF na ambayo Mutungi anasema lazima ilindwe na kufuatwa) inamaanisha kuwa hata kama Lipumba angelikuwa Mwenyekiti halali wa chama cha CUF (kwa mujibu wa Mutungi) kwa namna yoyote ile Lipumba hawezi kuwa na mamlaka ya kwenda benki kufungua akaunti ya benki vyovyote vile, na katika mstari huo huo, hata kama Jaji Mutungi ndiye angekuwa na mamlaka ya kuzielekeza benki zifungue akaunti za vyama vya siasa, bado angepaswa kuiandikia benki fulani ili ifungue akaunti ya chama kupitia kwa Katibu Mkuu wa chama, na siyo Mwenyekiti wa chama. Jaji Mutungi amepatwa na nini?


Ukiachilia mbali uvunjaji mkubwa wa Sheria wa Jaji Mutungi (kwa sababu yuko juu ya Sheria za nchi na kwa sababu anafanya kazi aliyotumwa na wakubwa wake), nitaishangaa sana Benki ya NMB ikiwa itathubutu kufungua akaunti ya The Civic United Front (CUF) bila kufuata matakwa ya Katiba ya CUF kifungu cha 93 (1) (i) ambacho kinamtambua Katibu Mkuu kama muwajibikaji namba moja wa masuala yote ya pesa.

Nitaishangaa sana Benki ya NMB ikiwa itakubali mbinyo wa serikali na dola na kupitisha maombi YASIYO NA AIBU ya ufunguaji wa akaunti nyingine ya CUF kupitia kwa Lipumba bila kuzingatia masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa kifungu cha 15 (1) na 15 (2) ambavyo vimeweka sharti la Bodi ya Wadhamini ya Chama husika kuidhinisha ufunguaji wa akaunti ya benki bila kusahau kuwa kifungu hicho hakitoi mamlaka yoyote kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuielekeza Benki imfungulie akaunti ya Benki kiongozi yeyote wa chama au chama chenyewe.


Nimefuatilia na kugundua kuwa maombi ya Lipumba na Msajili ya kufunguliwa akaunti ya Benki ya NMB yameidhinishwa na Meneja wa NMB tawi la Ilala siku ya Alhamisi lakini kwa sababu akaunti husika itatumiwa na taasisi imebidi Meneja husika ayapeleke maombi hayo Makao Makuu ya NMB ili yaidhinishwe ndipo akaunti hiyo ifunguliwe.

Nitapigwa na bumbuwazi mara 100 pale watendaji wa Makao Makuu ya NMB watakapoidhinisha ufunguaji wa akaunti kwa kuvunja sheria za nchi namna hii. Na akaunti hiyo ikifunguliwa hakutakuwa na jambo la zida zaidi ya kuifanya NMB ianze kushiriki katika miamala ya pesa kwa njia za kifisadi kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa. Hii itakuwa aibu ya karne kwa benki hii.


Na mwisho, nimekaa na kujiuliza mara mbilimbili. Hivi Msajili anapolazimisha Lipumba apewe pesa za Ruzuku za CUF anataka kumkomoa nani? Kwani Msajili hajui kuwa Kamati ya Utendaji yote ya CUF haiku upande wa Lipumba isipokuwa wajumbe wawili tu, Sakaya na Abdul? Ikiwa Lipumba anapewa fedha, nani watakaozisimamia kwa mujibu wa Katiba ya CUF ambayo imeeleza wazi kuwa masuala yote ya kusimamia utendaji wa chama na bajeti za chama yanafanywa na Ofisi ya Katibu Mkuu? Kwani Jaji Mutungi hajui kuwa wajumbe 43 kati ya 53 wa sasa wa Baraza Kuu la CUF wamemkataa Lipumba na hata kumvua uanachama?


Hizo Fedha za CUF ambazo Mutungi anataka kumpa Lipumba anadhani zitaidhinishwa ili kutumiwa na Baraza Kuu lipi, ikiwa Baraza Kuu la CUF lilishamkataa Lipumba? Kwani Msajili wa Vyama vya siasa hakumbuki kuwa Mkutano Mkuu wa CUF ulipiga kura 476 (76%) na kumuondoa Lipumba rasmi kwenye uongozi? Kwani Msajili wa vyama vya siasa hajui kuwa kati ya wabunge 43 wa CUF ni wawili tu ndiyo wako na Lipumba na waliobakia (41) wako upande wa chama hicho unaoongozwa na Maalim Seif na wenzake? Msajili wa vyama vya siasa anataka kumpa Lipumba pesa za CUF kama nani? Na Msajili amesahau kuwa hizo ni fedha za umma ambazo huwekwa mahali kwa kufuata katiba na sheria zilizopo na ambapo kuna vyombo vya kuzisimamia?


Nisaidieni kumshangaa Jaji Mutungi, nisaidieni kumuombea. Kwa nini Rais Magufuli anaangalia watendaji wake wakivunja Sheria na kufanya ubabe juu ya masuala ya kisheria? Kwa nini Rais Magufuli anaangalia na kutochukua hatua wakati taasisi za serikali na hata mabenki yetu yanajaribu kukubali kutumiwa kuanzisha michakato ya kifedha inayovunja sheria na ambayo ina madhara makubwa kwa ukuaji wa demokrasia katika  nchi..

Na. Abdallah Yusuph Juma, yabduljuma72@yahoo.com

No comments: